Sunday, January 3, 2016
Story: MKUKI MOYONI MWANGU 01
Kulikuwa na kila aina ya kelele hewani, miziki aina ya Vigodoro na Taarab ikipigwa mfululizo kiasi cha kumfanya hata mtu aliyemeza dawa ya usingizi asilale! Vyura nao walikuwa wakipiga kelele kutokea kwenye mto ulikuwa jirani tu na kibanda alichoishi Kevin Mdoe, kilichozungukwa na kila aina ya takataka kwani kilijengwa kwa mabati kando ya dampo.
Ni eneo la Tandale Taptap ndiko alikoishi, paliitwa hivyo kwa sababu ndiko yalikokuwa makao makuu ya pombe zote za kienyeji, kulikuwa na walevi wengi maeneo hayo lakini hapakuwa na...
baa hata moja zaidi ya vilabu vya pombe, kodi ya nyumba kwenye maeneo hayo ilikuwa elfu kumi kwa mwezi ndiyo maana Kevin aliweza kumudu kwa hali aliyokuwa nayo.
Ndani ya kibanda hicho cha chumba kimoja palijaa harufu kali na mbaya, ambayo haikuwa rahisi kwa binadamu yeyote kuivumilia, wengi walishindwa kuishi nyumba moja na Kevin sababu ya harufu hiyo. Alishapanga nyumba nyingi kabla ya hapo lakini aliishia kufukuzwa sababu wapangaji wenzake walilalamika.
Harufu hiyo ilikuwa ni ya mke wake Catarina David, aliyekuwa amelala kitandani kwa miaka mitano, mwili wake ukiwa umebaki mifupa na ngozi! Akiwa hajitambui kitandani, kila kitu alikifanya hapohapo, kuanzia haja kubwa hadi ndogo na hata kumuogesha kazi ambazo Kevin alizifanya.
Kwa mwanga wa kibatari cha mafuta ya taa walichotumia, Kevin aliziangalia picha walizozibandika ukutani zikimwonyesha Catarina akiwa katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa kuonyesha mitindo, picha moja iliandikwa kwa juu “World super model, Catarina from Tanzania” machozi yalimtoka Kevin alipomwangalia mke wake kitandani, macho yakiwa yameelekea darini kwenye kibanda kidogo kilichojaa buibui, haikuwa rahisi hata kidogo kuamini kuwa Catarina aliyekuwa amebaki mifupa na ngozi ndiye aliyewahi kuwa mrembo wa dunia, akikutana na watu maarufu wengi duniani huko Hollywood.
“Catarina! Catarina! Catarina!” alimwita lakini hakuitika wala kugeuza jicho lake kumwangalia.
Mwisho akanyoosha mkono na kuchukua redio yake ndogo iliyokuwa kando ya kitanda chini, akaiwasha na kubonyeza sehemu ya kanda, wimbo ambao Catarina aliupenda kuliko nyimbo nyingine zote enzi za uzima wake uitwao Careless whispers uliyoimbwa na George Michael ukaanza kupiga, alifanya hivyo siku zote akiamini ipo siku Catarina angeusikia wimbo huo na kurejewa na fahamu zake, jambo ambalo halikutokea.
Kevin hakuzaliwa masikini, alishauza kila kitu, akapoteza kazi na kulazimika kuhama Masaki ambako aliuza nyumba ya urithi ili tu amtibu mke wake, akazunguka na Catarina kila kona ya dunia kutafuta uzima lakini haikuwezekana, mwisho madaktari nchini India wakamwambia kwamba “She will finish the race in bed”
Kauli hiyo ilimaanisha Catarina angemalizia maisha yake yote yaliyobaki akiwa kitandani, Kevin alibubujikwa na machozi lakini hakuwa na la kufanya na asingeweza kumkimbia mwanamke aliyemtamkia mbele ya mchungaji kwamba alimpenda na angekuwa naye katika shida na raha.
“Mungu umenipa mtihani huu, unajua jinsi nitakavyoshinda!” aliwaza.
Je, nini kitaendelea? Endelea Kufuatilia kwenye blog hii kila J pili, J tano na J mosi
Labels:
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment