Tuesday, July 19, 2016
HADITHI: NYUMA YA MACHOZI (sehemu ya kumi na tano) 15
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
“Siyo kuwasumbua, niligundua nilifanya kosa katika maelezo ya kuyapata hayo madawa, ndiyo maana nimepiga tena simu haraka.”
“Kwa hiyo tutakuwa basi tumechemsha.”
“Bado hamjachemsha.”
“Tusaidie jinsi ya kuyapata.”
“Mkoba wake mwekundu anao?”
“Ndiyo.”
SASA ENDELEA...
“Basi huo ndio wenye dawa hizo.”
“Mbona tumempekua hatujaona kitu?”
“Huyo dada ni muuzaji wa kimataifa wa dawa za kulevya, hata siku moja hamuwezi kumkamata kirahisi.”
“Tusaidie basi tujue ameficha wapi?”
“Huo mkoba wake umeshonwa maalumu kwa ajili ya kuvusha dawa za kulevya, una karatasi za lailoni ambazo haziwezi kuruhusu...
vipimo vyenu kuona ndani kuna kitu gani. Juu kuna manyoya hufanya mkoba huo mtu yeyote asiutilie wasiwasi. Kwa mtindo huo, umemfanya mwanamke huyu aendeleze biashara yake haramu ya dawa za kulevya bila kushikwa.”
“Kwa hiyo una maanisha mkoba alishonwa na dawa zake kabisa?”
“Ndiyo maana nikasema huyo dada ni muuzaji wa kimataifa, huzunguka sehemu zote bila kukamatwa na kumfanya aweze kujikusanyia fedha nyingi kila kukicha.”
“Una uhakika na unachokisema?”
“Kwa nini nimewapa picha jinsi alivyo na mmempata bila tatizo, kuna kitu nilichowaeleza akakataa?” “Mpaka sasa upo sahihi.”
“Basi pasueni mkoba wake mtanipa jibu, asante.”
Baada ya kusema vile alikata simu. Baada ya simu kukatwa, Deus alitumia dakika tano kutafakari maneno ya mtu aliyejiita msamalia mwema ili kutoa uamuzi ambayo kama utakwenda kinyume unaweza kumuhalibia sifa. Aliamuru yule mwanamke aingie, aliitwa na kuingia ndani na kukaa kwenye kiti. “Samahani,” alianza Mr Deus kumtaka radhi Teddy. “Bila samahani mkuu.”
“Naomba uniambie ukweli kuhusu sehemu ulipoficha dawa za kulevya.”
“Nimeeleza kila kitu, sasa mnataka nini? Sijui lolote juu ya dawa za kulevya nashangaa kunihusisha na biashara hatari kama hizo.”
“Naomba nifanye upekuzi kwenye mkoba wako.” “Huu hapa angalia,” Teddy alisema huku akiuweka mkoba wake juu ya meza.
“Kabla sijaupasua naomba uniambie ukweli juu ya kuficha dawa za kulevya.”
“Mkoba si huo hapo fanyeni muwezavyo utajua ukweli kuwa sihusiki japo kuwa watu wananipaka matope,” Teddy alisema kwa kujiamini. Mr Deus aliagiza kisu ili aupasue mkoba mbele yake, Kabla hajaupasua Teddy alimtaadhalisha.
“Kumbuka mkoba huu nimeununua pesa nyingi robo ya bajeti ya wizara moja kubwa katika serikali yako.” “Hiyo siyo juu yako.”
“Sema unataka shilingi ngapi ili usiharibu mkoba?”
“Sihitaji fedha yoyote zaidi ya kuupasua mkoba huu.” “Haya fanya uwezavyo lakini mwisho wa siku utaumbuka.”
Mr Deus hakumsikiliza alichukua kisu na kuanza kuupasua mkoba ili kupata uhakika kwa yale aliyoelekezwa na msamalia mwema. Alipoanza kuupasua mkoba Teddy aliomba asitishe zoezi. “Samahani mkuu.”
“Bila samahani,” Deus alijibu akiwa amesitisha zoezi la kuupasua mkoba.
“Naomba tuzungumze.” “Tutazungumza nikimaliza, fedha ya robo bajeti ya wizara hata mimi naweza kuilipa peke yangu wala usiwe na wasiwasi,” Mr Deus alijibu huku akinyanyua kisu kukididimiza kwenye mkoba.
“Naomba unisikilize kaka yangu,” Teddy alikuwa mpole ghafla.
“Juu ya nini?”
“Kuhusu huo mkoba.”
“Una nini?”
“Samahani kaka yangu naomba unisilize mdogo wako.”
Mr Deus aliacha kuuchana mkoba na kumgeukia Teddy aliyekuwa akitokwa na jasho japo ofisi ya Mr Deus ilikuwa na kiyoyozi kikali.
“Mhu! Unasemaje?”
“Najua nimepatikana, lakini naomba msaada wako?” “Umepatikana kivipi na unaomba msaada upi?”
“ Kila ulichoelezwa ni kweli?”
“Na nani?”
“Simjui, lakini inaonekana ananijua vizuri, sasa nifae kwa mvua nitakufaa kwa jua.” “Sijakuelewa,” Mr Deus alimshangaa Teddy.
“Ni kweli mfuko huu una dawa na kwa sasa nipo chini ya ulinzi na ukinifisha mahakamani nitafia gerezani, umri wangu bado mdogo. Nakuomba uniokoe kwa hili nipo radhi kukupa kiasi chochote ukitakacho hata ukiacha kazi unaweza kula miaka hamsini bila tatizo.”
“Lakini unajua dawa za kulevya ni haramu?” “Najua, na ndiyo maana nipo chini ya ulinzi.” “Sasa nikiwasikiliza wote tutamkamata nani?”
“Yaweza usione umuhimu wangu kwako leo, lakini kwangu mimi wewe ni mtu muhimu kama malaika mtoa roho aliyeahilisha kuchukua roho mama mzazi muda mfupi baada ya kujifungua.”
“Kwa ubinaadamu ni kweli nilitakiwa kukusaidia, lakini kwa vile ni dhamana niliyopewa na taifa sina budi kuwa na uso wa mbuzi.”
“Si kwamba nakulazimisha au nakufundisha kazi, hata hao wakubwa zako waliokutuma wanapokea mrungula. Amini usiamini kuna viongozi katika serikali yako hata viongozi wa dini mwenye heshima katika taifa hili wanaifanya biashara hii. Unaweza kunikamata na nikafungwa, lakini bado utakuwa umechota kikombe cha maji kwenye bahari hutapunguza kitu. “Nina imani msaada wako leo unaweza kukusaidia siku za mbele, mbegu ya wema siku zote haiozi.
Naomba unisaidie kwa leo nina imani nitakapotoka huwezi kujilaumu kwa msaada wako. Sema kiasi chochote ukitakacho hata kikipita fedha za mzigo huu nipo tayari kukupa tena muda huu.”
Kauli ile ilimfanya Deus alitulie kwa muda huku akiona sura ya yule binti ilivyoonesha kuomba msaada wake. Kila alilolizungumza alililona lina uzito kwake. Taratibu moyo ulilainika na kuona kuna umuhimu wa kumsikiliza yule msichana.
“Unajua binti unanipa wakati mgumu,” Deus alisema kwa sauti ya chini.
“Kivipi kaka yangu?”
“Unajua vijana wangu wakiona nakuachia wakati mimi ndiye kiongozi wao watanielewaje?”
“Sikiliza mkuu hakuna hata mmoja anayejua huku ndani kipi kinaendelea, wengi wanajua ni mazungumzo ya kawaida.”
“Mmh! Sasa kwa kesi nzito kama hii unanipa kiasi gani?”
“Chochote ukitakacho utakachokiona kinalingana na kosa hili.” “Kwa vile wewe ndiye uliyetangaza biashara kusema ili nione kama kinalingana na kosa lenyewe.”
“Lakini huu mzigo si utaniachia?”
“Itategemea na kiasi cha mzigo utakaotangaza.”
“Milioni 50.”
“Hailingani na kosa lako, kumbuka hapa nauza kazi naweza hata kufungwa maisha ikigundulika.”
“75.”
“Okay, nisikuumize sana nipe hizohizo.”
“Na mzigo wangu?”
“Utaondoka nao, nitapataje mzigo wangu?”
“Kama una kijana wako nimuagize aende sasa hivi akachukue mzigo mimi nikiwa hapa akipata utaniruhusu niondoke.”
“Itakuwaje?”
“Nampigia simu mtu ukisikia kisha unanipa mtu wako nimuelekeze akachukue.”
“Okay, fanya hivyo.”
Teddy alichukua simu yake iliyokuwa mezani na kubofya namba kisha alisema:
“Haloo Tonny.”
“Eeh, Teddy.”
“Andaa milioni 75 kuna mtu atakuja muda si mrefu.”
“Hakuna tatizo, nitamtambuaje?”
“Nitakujulisha.” Teddy alikata simu na kumgeukia Mr Deus aliyekuwa akishangazwa na uwezo wa kifedha aliokuwa nao binti yule.
Alikubaliana na kauli ya mtu aliyejiita msamalia mwema kuwa binti yule ni mfanya biashara mzoefu pia mwenye utajiri mkubwa.
“Basi mjulishe huyu mtu wako ili nimwelekeze akachukue mzigo.”
“Hakuna tatizo ngoja nimpigie ili nikupe umuelekeze,” Deus alisema huku akichukua simu na kumpigia rafiki yake Kinape afuatilie dili lile.
“Haloo Kinape upo wapi?”
“Ndiyo natoka kazini.”
“Hebu zungumza na dada huyu akuelekeze sehemu akakupe mzigo wangu.”
“Hakuna tatizo,” Deus alimpa simu Teddy ambaye alimuelekeza sehemu ya kukutana ampe mzigo huo. Baada ya maelekezo Teddy alimgeukia Deus na kumuuliza.
“Nina imani utaamini kwamba mimi si mtu wa kubabaisha.”
“Mpaka tutakapo maliza kazi.”
Mr Deus alinyanyua simu na kumwita secretary wake, baada ya muda alifika na kukakamaa kikakamavu mbele ya mkuu wake.
“Abee bosi.”
“Mletee mgeni kinywaji.”
“Sawa mkuu.” Aligeuka na kuondoka, baada ya muda alirudi na sahani iliyokuwa juisi ya paketi na glasi mbili. Aliweka juu ya meza na kuwawekea wote kisha aliwakaribisha.
“Karibuni Juisi dada.”
“Asante,” alijibu Teddy huku akichukua glasi ya juisi moyo wake ukiwa umeanza kutulia. “Lete stori,” Deus alivunja ukimya.
“Ninalo kaka yangu, nakuahidi si leo si kesho msaada wako hutaujutia.”
“Kwa nini mnakaa na fedha nyingi kiasi hicho ndani?”
“Kaka yangu kazi yenyewe bila ya kuwa na fedha za haraka unaozea gerezani.”
Wakati wa mazungumzo simu iliingia toka kwa secretary, alipokea na kuzugumza.
“Simu ya Italia mkuu.”
“Niachie.”
“Haloo.”
“Ndiyo msamalia mwema?”
“Vipi mzigo umeuona?” “Kazi umeisha tupa tuachie tuifanye,” Deus alijibu kwa jeuri kidogo.
“Mkuu sina maana ya kukufundisha kazi bali kufanikisha kukamatwa kwa huyo malaya.”
“Asante kazi inakwenda vizuri.” “Mmeziona?” “Hiyo si kazi yako.”
“Sawa mkubwa mara hii nimekuwa adui?” “Siyo adui tunashukuru kwa msaada wako mambo mengine ni siri ya ndani hatakiwi mtu mwingine kujua.”
“Nakutakia kazi njema.”
“Na wewe pia.”
Baada ya kukata simu Teddy aliyekuwa akifuatilia mazungumzo yale alijua mbaya wake bado alikuwa akimuandama kwa kufuatilia mpango wake.
“Samahani mkuu.”
“Bila samahani.” “Naomba nimjue huyo mtu.” “Hapana ni siri ya jeshi.”
“Kaka yangu nipo radhi kukuipa pesa ile mara mbili ili nimjue tu.” “Ukimjua?”
“Basi tu nitakaa naye mbali.”
“Kwa kweli amekataa kutaja jina lake zaidi ya kujiita msamalia mwema.”
“Anatokea wapi? “Italia.”
“Asante kwa msaada wako.”
Mara simu iliita, Teddy aliipokea na kusema: “Eeh! Tayari hebu mpe simu nizungumze naye,” Baada ya kupewa alizungumza:
“Eeh! Umefika?” “Ndiyo.” “Hebu zungumza na mkuu hapa,” alimpa simu azungumze na Kinape.
“Eeh! Kinape umefika?”
“Ndiyo.”
“Ni yeye,” Deus alimgeukia na kumwambia Teddy.
“Nipe simu.”
Baada ya kumpa alimwambia mtu wa upande wa pili.
“Tonny mpe mzigo mpe ulinzi mpaka atakapozifikisha salama.”
“Hakuna tatizo.” Teddy alikata simu na kumgeukia Mr Deus na kumuuliza:
“Utazipeleka wapi?”
“Nyumbani.”
“Naomba uzipeleke benki ni nyingi sana sitaki upoteze nguvu zako bure,” Teddy alimshauri Deusi.
“Sawa nitafanya hivyo.”
“Deus alipigia Kinape simu na kumweleza azipeleke benki katika akaunti ya Kinape yeye angezichukua baadaye.
Tonny alimsindikiza Kinape mpaka benki ambapo aliweka fedha yote aliyopewa kwenye akaunti yake. Baada ya kuweka alimpigia simu Deus kumjulisha.
“Mkubwa kazi imekwenda vizuri.”
“Amekupa zote?”
“Ndiyo.”
“Shilingi ngapi?”
“Milioni 75.”
“Ooh, vizuri umeshaziweka benki?”
“Ndiyo natoka sasa hivi.”
“Basi tutaonana baadaye nyumbani.” “Hakuna tatizo mkuu?” Deus baada ya kupata uhakika kwa Kinape alimgeukia Teddy aliyekuwa akiendelea kunywa juisi taratibu bila wasi kama hakuna kitu cha hatari kilikuwa mbele yake.
“Teddy,” alimwita.
“Abee.” “Nafikiri kila kitu kimekwenda vizuri.”
“Hakuna tatizo, naheshimu sana kazi yako pia muda wako.”
“Asante lakini kumbuka umeniweka katika wakati mgumu sana.”
“Kawaida tu kaka yangu, nakuapia ulichokifanya leo hutakijutia maishani kwako, huenda leo usione umuhimu wake lakini ipo siku utayakumbuka maneno yangu.”
Labels:
HABARI & UDAKU,
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment