“Tumeomba mara nyingi kukutana na Rais na tumekuwa tukiandika barua, lakini hatujibiwi chochote. Tunajua hizi ni njama tu za watu wachache wanaozuia tusionane na Rais,” alidai Mgoba.
Alidai kuwa wameandika barua nyingine na hivi karibuni Katibu wa Rais aliwapigia simu kuwa wafike Februari 10 ili waonane na Rais na walipofika, hawakufanikiwa kumuona Katibu huyo.
Akizungumzia sababu za kutaka kuonana na Rais, alidai ni kutaka kujua hatma yao ya kutopatiwa ajira kutokana na mafunzo ya kijeshi waliyoyapata. “Sisi tumepatiwa mafunzo ya kijeshi na sasa tupo uraiani kwa ajili gani? Hawa wote unaowaona ni askari tayari ” alidai.
Mkutano wao uliwakutanisha pamoja ili kuweka mikakati yao ikiwa ni pamoja na kufanya maandamano ifikapo Jumatatu kama serikali haijajibu, kama itawaajiri au hapana. Walidai endapo jibu halitapatikana, basi watafanya maandamano ya siku tatu mfululizo hadi ombi lao la kumwona Rais lifanikiwe.
Makamu Mwenyekiti, Paral Kiwango, alisema jambo hilo linaonekana kuwa na upendeleo mkubwa, kwani wenzao wa upande wa Zanzibar wote waliomaliza mafunzo ya JKT, wanapatiwa ajira. Alihoji iweje vijana wa Bara wametelekezwa?
“Wenzetu wa upande wa Zanzibar wakimaliza mafunzo wote wanaajiriwa, lakini sisi Tanzania Bara hakuna anayetujali na kututhamini,” alidai Kiwango.
Kwa upande wake, Katibu wao Liwus Emmaneul amesema kuna fursa nyingi za ajira hapa nchini kama vile TANAPA na sehemu zingine, ambazo wao wanaweza kufanya kazi; lakini wanaoajiriwa kule ni watu wengine wasiokuwa hata na ujuzi, huku wao wakitelekezwa na wakiomba ajira kule hawathaminiwi, kama watu wenye maadili na mafunzo.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipotafutwa ili atoe ufafanuzi juu ya maandamano hayo, simu yake ya mkononi iliita bila majibu.
0 comments:
Post a Comment