Pages

Subscribe:

Saturday, July 2, 2016

HADITHI: NYUMA YA MACHOZI (sehemu ya kumi na mbili) 12


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Kilichomshangaza ufunguo wa chumba chake alikuwanao mwenyewe. Alijikuta akishtuka na kujiuliza nani aliyechukua. Alikumbuka changudoa aliyelala naye na kuondoka akiwa amelala ndiye aliyechukua zile picha, alijiuliza amezichukua ili iweje.
Wasiwasi wake mkubwa ulikuwa kama zikivunja lazima Kilole atamuona hana manaa hata kumfanyia kitu kibaya.
Alipanga usiku akamtafute ili amrudishie picha zake, alichukua picha alizosafisha na kumpelekea Kilole.
SASA ENDELEA...

Kama alivyoelekezwa akitaka kupeleka picha alitakiwa amjulishe kwa simu ili azifuate mwenyewe kuliko kuingia ndani, kuondoa wasiwasi kwa Kinape. Jimmy alipofika alimpiga simu Kilole aliyekuwa...

amekaa sebuleni na Kinape wakitazama runinga.
Kilole baada ya kuona namba ya Jimmy aliikata simu na kuelekea chumbani bila Kinape kujua kinachoendelea. Alipofika chumbani alimpigia na kumuuliza:
“Vipi Jimmy?”
“Nimekwishafika.”
“Poa nakuja.”
Kilole alichukua upande wa kanga na kujitanda ili akirudi asionekane amebeba kitu, alipofika sebuleni Kinape alimuuliza:
“Vipi shemu?”
“Natoka kidogo.”
“Wapi tena?” “Nafika dukani.”
“Vipi utachelewa? Maana Happy kanipigia simu nimfuate ili nimpeleke hospitali hajisikii vizuri.”
“Sichelewi nisubiri, nafika dukani mara moja.”
“Hakuna tatizo.” Kilole alitoka nje na kwenda alipokuwa Jimmy, alipofika Jimmy alijitoa sehemu alipokuwa amesimama.
“Vipi tayari?”
“Tayari.”
“Poa.”
Kilole alichukua bahasha na kumpa fedha iliyobakia huku akiendelea kumsisitiza: “Jimmy nimekuamini kukupa kazi ya hatari, kama ukivujisha ishu hii ujue sitaona hatari kunyongwa kwa ajili yako. Nimekupa malipo mazuri ili kuhakikisha ufanyi uzembe wowote, au kuna kitu kimekwenda kinyume na mpango wetu?”
“Hapana.” 


Jimmy alijibu akiwa na wasiwasi wa picha zilizopotea katika mazingira ya kutatanisha. Akiwa katikati ya mawazo Kilole alimshtua:
“Vipi mbona kama kauli yangu imekushtua?”
“Ha..ha..pana,” Jimmy alibabaika. 


“Jimmy usiwe umefanya makosa tusije tukalaumiana, japo unaniona mwanamke kwenye hili nitakuwa zaidi ya mwanaume,” Kilole alizidi kusisitiza.
“Kilole mbona unanitisha kama uliona siwezi au huniamini kwa nini ulinipa kazi hii?”
“Si kwamba nakutisha maelezo yangu naona kama yamekubadili muonekano wako.”
“Wasiwasi wako tu, lakini nipo makini kuliko unavyofikiria.”
“Mmh! Sawa lakini zingatia hilo picha zote kwenye kamera umefuta?”
“Ndiyo.”
“Hebu nipe kamera nione.”
Jimmy alimpa kamera na kuangalia picha zilizokuwa zimebaki kwenye kamera hakuona picha ya tukio hata moja.
“Jimmy nakuamini najua huwezi kuniangusha.”
“Usihofu.”
Waliagana ili kumpumbaza Kinape alikwenda hadi dukani na kununua vitu vya kutafuna na kurudi navyo ndani. Alipofika sebuleni alimtupia bazoka Kinape na kumweleza:
“Unaweza kwenda lakini usichelewe.”
“Hakuna tatizo.”
Kinape alijibu huku akinyanyuka kujiandaa kwenda kwa mpenzi wake Happy bila kujua Kilole alimtoa kijanja ili apate nafasi ya kuangalia picha zake na kujipanga kumrudisha Kinape mikononi kwake na kuvunja penzi lao. 


Baada ya kuingia chumbani hakujiamini alijifungia kwa ndani na kuanza kupitia picha moja baada ya nyingine.
Zilikuwa picha alizozitalajia zenye kuonesha penzi la ushirikiano, picha zile zilimfanya atabasamu na kujikuta akiruka juu na kujitupa kitandani kuonesha alichokitaka ndicho kilichofanyika. Alijisemea kwa sauti ya chini: “Kinape kwisha habari yake.”
Aliziweka picha vizuri na kiendelea na shughuli zake moyoni akiwa na furaha tele.

Baada ya kumaliza semina ya kikazi Deus alirudi nyumbani Tanzania, uwanja wa ndege alipokewa na mkewe Kilole na mwanaye mpenzi Gift.
Pia alikuwepo rafiki yake kipenzi Kinape na mpenzi wake Happy. Baada ya kufika Kilole alijitupa kifuani kwa mume wake kuonesha kweli alikuwa amekosa mahaba yake.
“Jamani mume wangu baba Gift, karibu sana nyumbani, yaani siamini macho yangu,” alijiliza machozi ya uongo. 


“Mke wangu mbona hata wiki haikufika?”
“Basi hunipendi mume wangu, yaani nilivyoteseka unasema hivyo.”
“Basi mke wangu, mengine tutakwenda kuzungumzia nyumbani.”
Jinsi alivyokuwa akideka kwa mumewe Kinape alichekea moyoni na kuona jinsi mwanamke alivyo nyoka kwa kumdanganya mumewe anampenda kumbe anamla kisogo. “Mmh! Kinape za siku mbili tatu?”
“Nzuri tu best, za huko?”


“Eeh bwana nzuri tu, nimefurahi kuwakuta wote wazima, hii imenipa faraja kuwa wewe si rafiki bali ni ndugu wa damu kwa kuweza kuitunza familia yangu kipindi chote nilipokuwa mbali nayo.”
“Ni wajibu wangu kuilinda familia yako,” Kinape alisema huku moyoni ukiumia kwa kitendo cha kutembea na Kilole.
“Shemu vipi?” Alimgeukia Happy mpenzi wa Kinape.
“Safi, pole na safari shemu.”
“Asante, nina imani baada ya kurudi nitafanya kila niwezavyo kuhakikisha mnafunga ndoa.” 


“Nitashukuru shemeji maana ndugu yako amekuwa mzito.”
“Best, umekwisha kwenda kumtambulisha shemu nyumbani?” Deus alimuuliza Kinape. “Nilisubiri urudi baada ya kufika nina imani ni muda muafaka sasa kwenda kumtambulisha mpenzi wangu nyumbani.”
Kauli ile ilikuwa kichefuchefu moyoni mwa Kilole na kujisemea kimoyomoyo: “Tutaona mimi na huyu mjinga mwenzenu nani zaidi.”
Moyoni aliapa kulivunja penzi la Kinape na Happy kwa msaada wa zile picha.

Baada ya Deus kurudi, kutokana na makubaliano kati ya Kinape na Kilole heshima ilirudi na kuitana mtu na shemeji yake. Pamoja na makubaliano hayo Kilole alitamani siku moja moja amtoroke mumewe na kwenda chumba cha Kinape kupata penzi la hamu. Lakini mara zote Kinape alikuwa makini hasa usiku alijifungia kwa ndani na kuwasha muziki kama Kilole atamfuata atasingizia hakusikia. 


Ilikuwa kama alivyowaza usiku mmoja Kilole alimuacha mumewe amelala na kwenda kwa Kinape.
Lakini kikwazo kilikuwa mlango uliofungwa kwa ndani, alipojaribu kugonga kwa taratibu sauti ya mlango ilimezwa na sauti ya muziki uliokuwa ukilia chumbani. Kilole alikasirika na kujikuta akipandwa na hasira akiwa tayari kutumia turufu ya picha chafu ili kumtisha Kinape na kukubaliana na masharti yake.
“Kinape mbona jana ulifunga mlango kwa ndani?” Kilole alimuuliza kwa sauti ya chini baada ya kukutana kwenye korido la msalani.


“Lini ulikuta mlango upo wazi na ulikuwa na shida gani?”
“Hujui au ndiyo ushanichezea kisha uniache?”
“Lakini hii si sehemu ya mazungumzo haya, tulizungumza nini mumeo akirudi?”
”Kuzungumza nini, mbona ulifunga mlango?”
“Jamani, si chumbani kwangu?”
“Ilianza lini ina maana unaogopa kuibiwa.”
“Ni utaratibu wangu wa siku zote.”
”Kwa nini uliwasha muziki?”
“Sasa hayo ni maswali gani?”
“Najua ulifanya vile ili nikigonga usinisikie.”


“Lakini lawama za nini, ulinieleza utakuja nikakufanyia hivyo?”
“Basi baadaye..” Kilole alisema baada ya kusikia akiitwa na mumewe. Baada ya kuondoka Kilole kuitikia wito wa mumewe, Kinape alibakia amesimama na kuona aliyoyakataa ndiyo yameanza na siku zote penzi kikohozi huwa halina siri.
Aliamini njia ya kujiepusha na tatizo lile ni kuhama kisha kufanya mpango wa haraka kukaa na Happy. Alipanga siku ile ile azungumze na Deus kwenda kujitambulisha nyumbani kwao Happy ili siku inayofuata naye ampeleke kijijini kumtambulisha kwa wazazi wake kabla ya kupanga mipango ya ndoa. 


Aliamua jambo lile kulifanya kwa siri kuepuka vikwazo vya Kilole. Baada ya kufungua kinywa Kinape na Deus walitoka pamoja, njiani alimweleza dhamira yake ya kwenda kujitambulisha kwa kina Happy siku ile. “Mbona haraka sana?” Deus alimuuliza. “Nilipanga leo niende ila nilisahau kukujulisha, nataka kesho niende na Happy kijijini, isingekuwa vizuri kuanzia kwetu kabla ya mimi kujulikana kwao.”
“Hakuna tatizo, ni saa ngapi?”
“Saa mbili usiku.”
“Hakuna tatizo tutakwenda.” 



Waliagana kila mmoja aliendelea na shughuli zake, Kinape ilibidi asubuhi ile ile ampigie simu Happy kumjulisha kuwa usiku wana ugeni wa kujitambulisha. Japo ilimshtua kuona imekuwa ghafla, lakini ilikuwa habari njema aliyoisubiri kwa hamu kama tone la maji katika kiu kali.
Nafasi ile hakutaka kuipoteza kwa kufanya maandalizi ya kupokea ugeni wa mchumba wake. Maandalizi yalikwenda vizuri na kumsubiri ugeni wa usiku huku Happy akiona ndoto yake ya kuolewa na Kinape imeanza kuwa kweli.

Deus kama kawaida yake alikuwa hawezi kufanya jambo lililo kuwa nje na ratiba zake za kila siku bila ya kumtaarifu mkewe. Kwa vile walikubaliana na Kinape wakutanie mjini na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa mchumba wake. Aliamua kumjulisha mkewe baada ya kumaliza kazi zake majira ya saa moja na nusu usiku. Ujumbe ule ulimshtua Kilole kitu kilichomshangaza mumewe.
“Mbona umeshtuka hivyo?” Deus alimuuliza mkewe. 



“Nimeshtuka kwa vile jambo hilo mmelifanya kwa siri.”
“Kuna siri gani kama nimekupigia simu kukujulisha?” “Mbona hamkuniambia toka asubuhi.”
“Hili suala nimeambiwa asubuhi njiani na Kinape wakati nakwenda kazini.”
“Mmh! Sawa, nawatakia utambulisho mwema.”
“Hayo ndiyo maneno, na kesho wanakwenda kijijini kwa utambulisho wa upande wa pili.” 


“Atiii?” “Mbona umeshtuka tena?”
“Sasa mbona mambo mnafanya mambo kienyeji,” Kilole alikuja juu kwa hasira za kweli huku wivu ikimpanda.
“Mke wangu kwani tatizo nini, haya si maandalizi ya awali, mipango ya harusi ikianza wewe utakuwa na majukumu makubwa kuliko unavyodhani.”
“Mmh! Haya, basi endeleeni na maandalizi mema.” 


Baada ya kukata simu Kilole alijikuta moyo ukimuuma kwa kusikia habari zile, Alijiapiza kupitia picha zile lazima atahakikisha Kinape hamuoi Happy, alijikuta akipoteza furaha ya siku nzima na kujuta kupokea simu ya mumewe.
Baada ya kukata simu alikwenda chumbani na kurudia kuziangalia picha upya huku akiamini picha zile ndiyo suruhu ya kuangaika kwa Kinape. 


Alizirudisha kwenye bahasha na kuzificha sehemu yake. Utambulisho wa Kinape ulikwenda vizuri huku familia ya Happy akionesha furaha ya mtoto wao kupata mume.
Happy akiwa ndiye mtoto wa kwanza kuchumbiwa, baba yake mzazi aliwaahidi nyumba na gari kama zawadi kwa mtoto wake wa kwanza. Kinape naye aliwaahidi kumpeleka mchumba wake nyumbani kwao siku ya kesho yake. Walipewa baraka zote za familia za wazazi wa Happy kwenda kutambulishwa kijijini kwao.

Kilole alijikuta akikosa raha na kumfanya atangetange sebuleni kama kuku anayetaka kutaga, akitoka upande mmoja kwenda mwingine, nyumba aliiona chungu. Moyoni aliendelea kujiapiza juu ya kuhakikisha Kinape hamuoi Happy.
Alijikuta amesahau hata kupika chakula cha usiku kwa ajili ya kumfikiria Kinape. Honi ya gari ya mume wake ilimfanya akimbilie ndani na kujilaza kitandani kusingizia anaumwa ili asiulizwe chakula cha usiku.


Mume wake aliingia ndani alimkuta amejifunika shuka gubigubi.
“Vipi mke wangu?”
“Sijisikii vizuri.”
“Hali hii imeanza saa ngapi?”
“Wakati najiandaa kupika.”
“Basi amka twende hospitali.”
“Nimemeza dawa kidogo kichwa kimeanza kutulia.”
“Kwa maana hiyo hujapika?” “Nipike saa ngapi mume wangu, ungeniona nilivyokuwa ungenikimbiza hospitali.”


Itaendelea...

0 comments:

Post a Comment