Thursday, July 7, 2016
HADITHI: NYUMA YA MACHOZI (sehemu ya kumi na tatu) 13
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:“Wakati najiandaa kupika.”
“Basi amka twende hospitali.”
“Nimemeza dawa kidogo kichwa kimeanza kutulia.”
“Kwa maana hiyo hujapika?”
“Nipike saa ngapi mume wangu, ungeniona nilivyokuwa ungenikimbiza hospitali.”
SASA ENDELEA...
“Lakini si umekunywa dawa ya kutuliza kwa nini tusiende hospitali?”
“Mume wangu huwezi kuamini kuja kwako kama umenipa dawa, sasa hivi sijambo kabisa.” “Mmh! Basi kama ni hivyo, jiandae baadaye twende...
tukachukue take a way.”
Baada ya kutengeneza uongo wake na kufanikiwa bado moyo wake bado uliendelea ulimuuma kila alipomuwaza Kinape na kibaya zaidi habari za kujitambulisha kwao na Happy alimueleza mbele ya mumewe.
“Samahani shemeji.”
“Samahani ya nini?”
“Sikukueleza mapema kuwa naitakwenda kujitambulisha nyumbani kwao na Happy, pia kesho nakwenda kijijini kumtambulisha mwenzangu.”
“Mmh! Safari njema,” (moyoni alijisemea tutaona si muda mrefu jeuri yako itakwisha)
***
Siku ya pili Kilole alikuwa na wakati mgumu kufikisha ujumbe kwa Kinape ili kuzuia asiweze kwenda kijijini kumtambulisha mchumba wake. Lakini juhudi zake zilikuwa bure, baada ya kuondoka na katika gari moja na mumewe. Roho ilimuuma sana kwa hila za Kinape za kumkwepa kwa kuondoka na mumewe kwenye gari moja. Alijifikiria kupiga simu kumzuia Kinape na kumweleza ukweli juu ya picha zile, lakini alisita kwa kuhofia mabadiliko yoyote yatakayo tokea kwa Kinape lazima mumewe angemtilia wasiwasi na pengine siri kutoka nje kabla ya kutimiza lengo lake.
Aliamua kumsubiri akirudi na kuingia anga zake ndipo amlipue. Kinape bila kujua kuna mpango kabambe wa kuvunja mipango yake ya kumuoa Happy. Utambulisho ulikwenda vizuri, familia ya Kinape kumpokea kwa bashasha mchumba wa mtoto wake huku wakimuahidi kumpa ushirikiano mkubwa kufanikisha ndoa ya mtoto wao.
Baada ya utambulisho walirudi mjini kujipanga kwa ajili ya maandalizi ya harusi ambayo Deus alimuahidi Kinape kuyasimamia kwa asilimia mia. Kinape aliutumia muda mwingi kumkwepa Kilole kwa kurudi muda ambao atakuwa amewasiliana na Deus kama yupo nyumbani. Hata walipokutana kwa bahati mbaya hakutaka kuzungumza kwa muda mrefu kwa kisingizio cha Deus yupo.
Moyoni Kilole alijiapiza hata kumfuata Kinape ofisini na kumweleza uchafu ule kwa kuugeuza upande wa pili kana kwamba Kinape ndiye aliyefanya mchezo ule.
Alipanga kufanya vile kabla mipango ya harusi haijaanza, lakini aliamua kuonesha kama halikumuuma baada ya kutumia nguvu bila mafanikio. Siku moja akiwa anaendelea na kazi zake alishangaa kumuona Kinape akirudi mchana ghafla huku akionekana ana wasiwasi mwingi.
“Vipi Kinape mbona leo mchana?”
“Kuna vitu nilisahau kuondoka navyo asubuhi, hivyo nimerudi kuvichukua,” alisema huku akielekea chumbani kwake.
Kilole alimsindikiza kwa macho huku akijiuliza aitumieje nafasi adimu kama ile, wazo la haraka lilimjia aanza kujiliza ili kuonesha kuna kitu kimempata na Kinape akiuliza basi afumue mzinga wa nyuki. Kinape wakati anatoka alishangaa kumkuta Kilole akilia kilio cha kwikwi.
“Shemu vipi?” Alimuuliza huku akimsogelea.
“Siamini kama unaweza kunifanya uliyonifanyia, sawa hunitaki kwa nini unataka kunivunjia ndoa yangu?”
“Kilole mbona sikuelewi!” Kinape alishangaa kusikia habari zile.
“Kinape nimekufanya nini?”
“Subiri usiondoke uone unyama ulionifanyia, nikiachika utapata faida gani?” Kilole alisema kwa sauti ya kilio.
“Mbona sikuelewi nimekufanyia nini?” Kinape alizidi kushangaa.
“Nimekuambia subiri halafu uniambie kama ulichokifanya ni haki.”
“Fanya haraka nimeomba ruhusu mara moja nifuate kalatasi hizi.”
Kilole alikwenda chumbani na kuchukua picha chafu walizopiga wakifanya mapenzi na kumpelekea Kinape aliyekuwa amesimama wima akimsubiri huku akionesha wasiwasi.
Alipofika alimpa baadhi ya picha na zingine kuziacha ndani, Kinape alipokea bahasha ya picha na kuanza kutoa picha moja, alishtuka kuziona picha zilizoonesha wakifanya mapenzi na Kilole.
“Ha! Hizi nini?” Kinape alishtuka huku akiendelea kuchambua picha.
“Nikuulize wewe, kwa nini umeamua kunidhalilisha kiasi hiki, kumbe ulikuwa na lako jambo, hebu fikiria picha hizi zimfikie mume wangu mimi nitakuwa mgeni wa nani?” Kilole aliangua kilio cha uongo na kuzidi kumchanganya Kinape.
“Wewe hizi picha umezitoa wapi?” Kinape aliuliza huku jasho la hofu likimtoka.
“Kuna mtu kazileta anasema kaziiba kwa jamaa mmoja ambaye amekula naye njama ili kunidhalilisha,” Kilole alisisitiza kama kweli.
“Nioneshe huyo aliyeleta picha hizi aeleze kazitoa kwa nani na huyo mwenye picha aseme kama mimi ndiye nilifanya mpango huu. Haki ya nani, leo ndiyo naziona hizi picha, sijui lolote maskini wa Mungu,” Kinape alizidi kujitetea.
“Kinape umebadilika baada ya kunivua nguo, shukurani yako kunidhalilisha, kwa taarifa yako najua kabisa nipo uchi pengine si mmoja aliyeziona kuna wengi. Pia wasiwasi wangu huenda zingine zimebaki na hizi ni baadhi ya hizo picha.
“Kwa maana hiyo bora nimweleze ukweli mume wangu na kumuonesha hizi picha nijue moja, anisamehe kwa kumuomba msamaha au aamue atakacho amua kwa vile siwezi kumlilia mtu. Inawezekana kabisa ulifanya makusudi ili niachike baada ya kuona nilikusaliti.”
“Kilole sijui nikueleza kitu gani ili unielewe, haki ya nani sijui lolote kuhusiana na hizi picha, pia nakuomba usimuoneshe mumeo wala kumueleza tulivyo hujumu ndoa yake, ni hatari si unajua jamaa ana bastora anaweza kuniua.”
“Naweza nisimwambie na kukaa kimya, kumbuka nimetoa laki tano ili nipewe hizi picha, kama zipo zingine wanashindwa nini kumuuzia mume wangu. Akijua uchafu wetu sura zetu tutaziweka wapi?” “Yaani nichechanganyikiwa hata sijui nikwambie nini.”
“Kinape hii ni hatari.”
“Kweli ni hatari tena kubwa, hivi Deus anavyoniamini nitamwambia nini akiona hizi picha?”
“Ndiyo maana nikaona bora nijisalimishe kwa mume wangu sina jinsi, kama picha hizi zikimfikia tumekwisha.”
“Mmh! Yaani hata sijui nani kafanya mchazo mchafu kama huu?”
“Unajua kila kitu lakini unanizunguka, kwani Kinape hapa jiji wapo wangapi?”
“Siwezi kujua labda wapo wengi.”
“Ina maana hiyo Kinape pia ni ndugu yake Deus.”
“Mmh! Yaani aliyeleta kasema hivyo?”
“Tena inasemekana umempa laki tatu, ndio maana kataka laki tano ili anipe picha.”
“Yaani, nimechanganyikiwa hata nguvu zimeniisha,” Kinape alisema huku akiketi kwenye kochi baada ya nguvu kumwisha ghafla.
“Kinape nilikuwa na maamuzi mawili?”
”Yapi hayo?”
“Moja la kujisalimisha kwa mume wangu, la pili kumuwahi Deus kabla picha hazijamfikia.”
“Utamuwahi vipi?”
”Ikiwezekana hata kumuua huoni hili likifika kwa wazazi litakuwa baya zaidi.”
“Mmh! Tumefika mbali sana huo si mpango mzuri.” Kinape alipinga mpango ule.
“Basi kama hatuwezi tumwambie.” “Bado huo si uamuzi sahihi.”
“Sasa tufanye nini?” “Tutafute njia nyingine zaidi ya hii.”
“Mimi nina siri za mume wangu kama tutazifikisha Takuru lazima atafungwa.”
“Sasa wewe utabaki na nani?”
“Na wewe.”
”Na Happy?”
“Kwa ulichokifanya heri niwe na wewe kwa vile siwezi tena kurudi kijijini.”
“Hapana, basi tutafute njia nyingine.”
”Hiyo nyingine nipe wewe.”
“Sina.”
“Basi wacha ninywe sumu ili ufurahi siwezi kuona nahukumiwa kwa kosa la kwako.
” Kilole alimtishia Kinape.
“Usinywe sumu bado tunaweza kujipanga kuhakikisha tunamdhibiti.”
“Nakupa siku moja kuhakikisha unapata ufumbuzi bila hivyo nitakacho amua tusilaumiane.” “Lakini naomba usimwambie kwanza Deus,” Kinape alijikuta akichanganyikiwa baada ya kukosa jibu la tatizo lililokuwa mbele yake.
“Ni wewe wa kunifanya nisimwambie, nataka kabla habari hizi hazimfikia tuwe tumekwishajua tumefanya nini.” “Nimekuelewa, yaani hata kazini sirudi nguvu zimeniisha,” Kinape alichanganyikiwa. “Kinape wewe mwanaume unatakiwa kuonesha unaweza kukabiliana na chochote kinachotokea mbele yako. Mbona mimi niliyetendewa sijachanganyikiwa zaidi ya kupanga mikakati ya kujiokoa na janga hili.”
“Najua huwezi kunielewa sijui lolote kuhusiana na hizi picha, kwa kweli zimenichanganya sana.” “Kwa kusema hivyo ina maana nimezipiga mimi?”
“Hapana sina maana hivyo, ila nimechanganyikiwa sijui hata nani aliyefanya mchezo mchafu kama huu.”
“Ndiyo tunatakiwa tutafute njia ya kujiepusha, kumbuka hili ni bomu likipasuka hakuna atakayepona.”
“Basi inawezekana alipoondoka aliweka mpelelezi ili atufuatilie.”
“Atufuatilie kwani anajua chochote kuhusiana na penzi letu la zamani?”
“Inawezekana kuna mtu anayetujua alipotuona tupo pamoja alimweleza na kuamua kufanya upalelezi.”
“Aweke asiweke lazima tutumie njia ya kumdhibiti kabla hajafanya lolote.”
“Sasa tutamdhibiti vipi?” “Kwa nini tusimuwekee sumu afe,” Kilole alisema bila wasiwasi. “Kilole mbona mpango huo ni mbaya!”
“Unafikiri tukimchelewesha akigundua lazima atatuua kwa risasi.”
“Tukimuua tutakosa fadhira hata Mungu atatulaani, tutafute njia nyingine ya kumdhibiti, ngoja nitoke nikirudi nitakupa jibu ila nakuomba chonde usimueleze Deus chochote kuhusiana na habari hii.”
“Siwezi hata mimi natamani kuishi maisha marefu.”
Baada ya kukubaliana Kinape aliondoka na kumwacha Kilole akifurahia mpango wake umekwenda kama alivyopanga. Aliamini jioni akirudi cha kwanza kitakuwa kuvunja uchumba wake na Happy kisha mengine yangefuata ya kumdhibiti Deus ili abaki na Kinape.
Itaendelea
Labels:
HABARI & UDAKU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment