Pages

Subscribe:

Friday, July 15, 2016

HADITHI: NYUMA YA MACHOZI (sehemu ya kumi na nne) 14


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:Baada ya kukubaliana Kinape aliondoka na kumwacha Kilole akifurahia mpango wake umekwenda kama alivyopanga. Aliamini jioni akirudi cha kwanza kitakuwa kuvunja uchumba wake na Happy kisha mengine yangefuata ya kumdhibiti Deus ili abaki na Kinape.


SASA ENDELEA...
Deus akiwa ofisini kwake akipitia ripoti ya uchunguzi wa wauzaji sugu wa madawa ya kulevya, simu toka kwa sekretari wake iliita. Alipokea mkono mmoja, mwingine ukiwa bado umeshikilia kwenye...
kalatasi ya ripoti.
“Haloo, ofisi ya kuzuia madaya ya kulevya hapa, nazungumza na nani?”
“Msamalia mwema.”

“Ndiyo Msamalia mwema, nikusaidie nini?”
“Mkuu, ndege ya shirika la Swiss air, inayoingia saa kumi na moja jijini Dar kuna dada mmoja mwenye umbile la kati maji ya kunde nywele za kipilipili, amevalia gauni fupi jekundu chini viatu virefu na kwapani atabeba mkoba wa rangi sawa na nguo zake.

”Pia anaweza kuwa miwani ya rangi hiyo hiyo kama atakuwa ameivaa kama ataivua basi chukueni vigezo nilivyo waeleza. Dada huyu ana dawa za kulevya mkamateni na kumpekua.”
“Samahani unazungumza toka wapi?” “Si muhimu kujua zaidi ya kufuatilia taarifa niliyokupa, asante.” “Haloo...haloo...”
Deus alichelewa simu ilikuwa imekatwa. Alinyanyuka na kutoka hadi kwa sekretari kuulizia simu inatoka wapi.

“Haloo Happy, simu inatoka wapi?”
“Namba zinaonesha inatoka Itary.”
“Asante,” Deus alijibu na kurudi ofisini kwake. Alijikuta akijiuliza aliyetuma taarifa na kujiita msamalia mwema alichokisema kina ukweli au ndiyo kutaka kuwasumbua. Lakini hakutaka kuipuuza taarifa ile, aliwaita vijana wake na kuwapa habari zile na kuwaeleza wafuatilie ndege ile kama kweli yupo huyo mwanamke basi akamatwe na kupekuliwa.

Kwa vile ilikuwa imebakia saa moja kabla ya ndege kuingia, aliwahimiza vijana wake kufika eneo husika kabla ndege haijafika. Baada ya kuwapa majukumu vijana wake aliendelea kupitia ripoti ya wauza dawa za kulevya sugu.
*****
Majira ya saa kumi ndege ya shirika la ndege la Swiss air iliwasiri uwanja wa ndege wa mwalimu JK Nyerere. Vijana wa Deus alikuwa katika kona yao kama kawaida. Baada ya ndege kusimama na mlango kufunguliwa waliteremka abiria mmoja mmoja waliokuwa katika mistari.

Dada mmoja maji ya kunde mwenye nywele fupi gauni jekundu fupi lililoishia juu kidogo ya magoti na viatu virefu alikuwa mmoja ya abiria katika ile ndege. Baada ya kutoka kwenye mlango wa ndege hakuteremka haraka aliangalia mandhali ya Tanzania kisha alivaa miwani yake nyekundu na kuteremka taratibu kwenye ngazi za ndege na kuelekea kwenye ukaguzi.

Vijana wa Deus hawakupata shida ya kumuona yule binti aliyeonekana mrembo tena bado mbichi. Walitegemea kusikia chochote kutoka sehemu aliyopitia, lakini alipita salama. Hawakuwa na haraka ya kumkamata walisubiri kuona yupo na nani pia mizigo yake.
Baada ya kutoka chumba cha usafiri alielekea kwenye gari aina ya Ranger Rover ‘Vogue’ ya rangi nyeusi iliyokuwa umepaki pembeni. Alipokaribia mlango ulifunguliwa, kabla hajaingia kikosi cha kuzuia dawa za kulevya kilifika na kujitambulisha kisha walimweka chini ya ulinzi msichana yule ambaye hakuonesha wasiwasi.

“Jamani vipi?” aliuliza huku akitoa miwani usoni. “Sisi ni askari wa kikosi cha kuzuia dawa za kulevya, tuna wasiwasi na wewe.”
“Mna wasiwasi gani?” “Tunaomba ufike kituoni kwa ajili ya upekuzi.” “Mbona mnanishangaza, ina maana wakaguzi wa kiwanjani hawafai?” Aliuliza kwa kuwashangaa askari wale.

“Samahani tunaomba ufuate maelekezo yetu.”
Wakati huo gari lao lilisimama pembeni yao na kumuomba aingine ndani ya gari. Kabla ya kuondoka yule msichana aliwaomba vitu vyake vitangulie nyumbani.
“Jamani vitu vyangu si hivi ngoja nivifungue hapahapa ili muone nimeweka wapi hayo madawa ya kulevya,” Alisema yule msichana huku akifungua pochi yake na kuvimwaga vyote vilivyokuwa ndani ya pochi kisha alitaka kufungua brif case ili vitu vilivyomo ndani avimwage chini waone kuna nini. Lakini walimkataza asifanye vile kwa vile kuna sehemu zake.

“Dada kwani tatizo lako nini, wewe twende ofisini, sisi tumetumwa tukukamate mengine anajua mkuu wetu, ingekuwa hatukutumwa wala tusingekusumbua,” askari mmoja alisema.
“Lakini kumbukeni nimechoka natakiwa kupumzika.”
“Tunajua, lakini sisi tumetumwa, hatuwezi kurudi mikono mitupu wakati mtu tuliyetumwa tumemuona.”

“Nani anayenifahamu na kuwatuma mje mnikamate, kumbukeni nitashitaki kwa kunidhalilisha,” binti yule alitishia. “Hatujakudhalilisha kwa vile hakuna mtu anayejua kinachoendelea hapa, zaidi ya wewe kumwaga vitu vyako bila kukuambia.”
“Basi turudini chumba cha ukaguzi uwanja wa ndege ili mnikague, ili niwahi nyumbani kuna mtu nimeahidiana kukutana naye.”
“Dada kuwa mwelewa, si wewe umevaa gauni jekundu?” Askari mmoja alimuuliza akisoma karatasi bila kumtazama.

 “Ndiyo.”
“Pochi yako nyekundu?”
“Ndiyo.”
“Miwani nyekundu?” “Ndiyo,”
“Na viatu vyako virefu?”
“Ndiyo.”
“Nywele zako za kipilipili?”
“Ndiyo.”
“Rangi maji ya kunde?”
“Ndiyo.”
“Sasa dada haya tumeyajulia wapi sisi?”
“Hata mimi nashangaa sijui nani anataka kunichafua?”
“Ungekuwa na tofauti na hii iliyoandikwa kwenye karatasi tusinge kugusa lakini kila kilichoandikwa kwenye karatasi unacho kwa asilimia mia,” walimweleza huku akimpa karatasi iliyokuwa na maelezo yote.

Askari walikuwa na uhakika kwa pale hakukuwa na ushahidi wowote kuwa yule dada kaingia na dawa za kulevya. Hata kama ilikuwa biashara yake siku ile walikuwa wamechemsha.

“Mmh! Sina jinsi twendeni lakini mnanipotezea muda bure,” alijitetea yule msichana aliyeonekana kujiamini katika mazungumzo yake.
Kama isingekuwa amri toka kwa mkubwa, waliona hakuna haja ya kumpoteza muda wake bure wangemuachia. Lakini vigezo vyote walivyoelezwa na mkuu wao Mr Deus ndivyo alivyokuwa navyo kwa asilimia mia. Hivyo hawakuwa na budi kumpeleka kwa mkuu wao. Walimuingiza kwenye gari na kumpeleka makao makuu kwa ajili ya upekuzi. Kabla ya kuondoka aliomba mkoba wake ambao hauna kitu utangulie nyumbani.

“Sasa kaka zangu kwa vile mkoba wangu hauna kitu naomba basi utangulie nyumbani.”
“Dada yetu haturuhusiwi kupoteza ushahidi wowote uliokuja nao, vyote vinatakiwa ili kukamilisha ushahidi.”
“Hakuna tatizo,” alijibu kwa kujiamini kitu kilichowafanya askari waamini hana kosa.
“Sasa Teddy itabidi nikufuate?” Dereva wa Ranger Rover alimuuliza mgeni wake.
“Noo Danny, tangulia nyumbani nitakuja sasa hivi kwa vile nakwenda kukamilisha walichotumwa na mkuu wao. Lakini kwa upande wangu sina tatizo lolote.”
Maneno ya kujiamini ya msichana yule yalikuwa na nguvu kubwa ya askari kumuachia lakini kwa vile walikuwa wakitimiza agizo la mkubwa wao hawakuwa na budi kumpeleka.

Walimuingiza kwenye gari na kumpeleka makao makuu kwa ajili ya kutimiza wajibu wa kazi. Walipofika walimpitisha chumba cha upekezi na kufanya upekuzi wote wa awali ambao haukuonesha dawa za kulevya. Taarifa alipelekewa mkuu wao Mr Deus.
“Mkuu hana kitu chochote.” “Mmempekuwa vizuri?”
“Ndiyo mkuu.”

“Mmetumia vifaa vya kisasa?”
“Vyote mkuu.”
“Mmempa chakula kigumu?”
“Kila kitu ujuacho tumekifanya lakini hatukumkuta na dawa.”
“Sasa aliyenipigia simu alikuwa na maana gani?”
“Kwani taarifa zimetoka wapi?” “Kwa msamalia mwema mmoja toka Itaria.”
“Ni kweli dada huyu anatoka Itaria.”
“Ina maana alikuwa anatudanganya?”
“Mkuu, huenda kweli anashughulika na biashara hii, lakini huenda njia aliyotumia si ile ambayo mtu aliyetutumia taarifa anaijua.”
“Inawezekana.”
“Lakini mmemuonaje?”
“Kwa kweli haoneshi wasiwasi zaidi ya kulalamikia muda wake.”
“Sasa fanyeni hivi mfuatilie mpaka atakapofikia fanyeni dolia usiku kucha ili tupate kujua kama kasingiziwa au ndiyo kazi yake.”
“Tutafanya hivyo mkuu.”
“Basi kamwachieni aende.” Kabla kijana wake hajaondoka alikumbuka kitu kimoja na kumwita.
“John hebu rudi kwanza.”
“Ndiyo mkuu.”
“Hebu mleteni hapa kabla ya kuwachia kuna maswali mawili matatu nataka kumuuliza.”
“Hakuna tatizo mkuu.”
John alitoka baada ya muda alirudi na yule msichana aliyekuwa mrembo kwenye macho ya mwanaume.
“Shikamoo,” yule msichana alimsalimia Mr Deus. “Marahaba, hujambo?”
”Sijambo mkuu.”
“Karibu ukae,” alimwambia huku akimuonesha sehemu ya kukaa.
“Asante,” Alijibu huku akikaa kwenye kiti. Baada ya ukimya mfupi Mr Deus alituliza macho kwa binti yule ambaye alikuwa ameinama chini. “Unaitwa nani?”
“Thereza Mayunga.”
“Ni Mtanzania?”

“Ni Mtanzania mwenye uraia wa Itaria.”
“Naomba Paspoti yako.” Teddy alifungua mkoba wake na kutoa paspoti na kumkabidhi Mr Deus, aliipokea na kuisoma kwa muda kisha alimrudishia.
“Okay, Wazazi wako wapo wapi?”
“Kwa kweli siwajui, ila niliambiwa niliibiwa nikiwa na umri wa miaka mitano na mwanamke mmoja aliyekuwa akikaa Itaria ambaye alinifanya mwanaye mpaka alipokaribia kufa ndipo aliponieleza kuwa wazazi wangu wapo Tanzania ila hakujua wapo wapi. Pamoja na kuniiba bado jina langu na la baba yangu hakulibadilisha.”
“Una shughulika na nini?”

“Ni mfanya biashara wa vitu mchanganyiko.”
“Hapa Dar unafikia wapi na kwa nani?”
“Nafikia Masaki kwa ndugu wa marehemu mume wangu.”
“Mumeo alikuwa Mtanzania?”
“Ndiyo.” “Okay, unaweza kwe...” Mr Deus kauli yake ilikatwa na mlio wa simu ulioingia kwenye simu yake. “Samahani,” alisema huku akipokea simu. “Bila samahani,” alijibu Teddy. Mr Deus alipokea simu na kuzungumza kwa sauti ya chini. “Eeh.”
“Mkuu simu ile ya Italia.”
“Okay, nipe nizungumze naye.”
“Haloo.”
“Haloo mkuu.” “Ndiyo.”
“Mmemuona?”
“Hebu subiri kidogo,” Mr Deus alisema huku akimuomba yule msichana amsubiri nje mara moja. “Hakuna tatizo,” alijibu yule binti huku akinyanyuka na kutoka nje. Baada ya kutoka Mr Deus alirudi hewani.
“Ehe! Msamalia mwema.”
“Nauliza mmemuona?”
“Ndiyo.”
”Mmepata hayo madawa?”
“Hatujayapata.”
“Nilijua hamuwezi kupata kitu.”
“Sasa kama ulijua hatupati kitu kwa nini umetusumbua?”Mr Deusi aliuliza kwa sauti hya ukali kidogo. “Siyo kuwasumbua, niligundua nilifanya kosa katika maelezo ya kuyapata hayo madawa, ndiyo maana nimepiga tena simu haraka.”
“Kwa hiyo tutakuwa basi tumechemsha.”
“Bado hamjachemsha.”
“Tusaidie jinsi ya kuyapata.”
“Mkoba wake mwekundu anao?”
"Ndiyo."
Itaendelea

0 comments:

Post a Comment