Pages

Subscribe:

Friday, December 23, 2016

JAY MOE AZIDI KUWABURUZA KIZAZI KIPYA



Juma ‘Jay Moe’ Mchopanga aka Mbakiaji, ni rapper mkongwe ambaye kama ng’ombe mzee, hazeeki maini. Kwa takriban miaka 15 ya career yake, Jay Moe hajawahi kuonekana kuhangaika kuonesha ujuzi wake kwenye hip hop.
 
Ni miongoni mwa wasanii wa zamani wenye hits nyingi ambazo licha ya kuwa na muda mrefu tangu zitoke, bado zinaweza kusikika na upya masikioni mwako. Nyimbo kama Bishoo, Mvua na Jua, Kama Unataka Demu, Maisha ya Boarding, Story 3, Famous ni miongoni mwa...
nyimbo zake classic zilizompa heshima. Huwezi kusahau hits zingine alizoshirikishwa kama Zeze ya TID, Kimya Kimya aliyofanya na marehemu Ngwair au Jirushe ya Ferooz.

Pamoja na ukongwe huo, Jay Moe amethibitisha mwaka huu kuwa anaweza kuwa rapper hatari katika kizazi cha trap na dab. Aliamua kuchukua risk iliyozaa matunda, kufanya muziki ambao rappers wenye heshima kama yeye wanaogopa kuufanya kwa kile wanachoamini wataonekana wanatapatapa. Wimbo wake Pesa ya Madafu ulimhamisha kutoka kwenye rap yake iliyozoeleka, hadi katika rap ya vijana wa leo, rap ya kizazi cha dab.

Jay Moe anasema aliamua kubadilika kiasi hicho kutokana na kukosolewa na watu kadhaa kwenye wimbo kabla ya huo, Hili Game ambao anasema alifanya makusudi kwa kuogopa kuja na ladha mpya kufuatia ukimya wake wa muda mrefu.

Anasema hiyo ilimpa sababu ya kuja na wimbo wenye usasa mwingi kwakuwa ni nyimbo ambazo anasikiliza pia. “Huko nyuma sikuwa na wimbo ambao ungeweza kuconnect watu wa jinsia tofauti na umri tofauti,” rapper huyo alikiambia kipindi cha Ngaz Kwa Ngaz cha Salama Jabir miezi kadhaa iliyopita.
“Kwasababu umekuwa ni wimbo ambao hata watoto wadogo nikipita tu wanaimba ‘pesa ya madafu.’

Na kiukweli kubadilika kwa Jay Moe kumekuwa na mafanikio makubwa kwasababu Pesa ya Madafu haikosi kwenye orodha ya nyimbo 10 za hip hop zilizotamba zaidi kwenye redio na TV mwaka huu.
Kubadilika kwake pia, kulikuwa na sababu za kiuchumi na kugoma kuendelea kushikilia misingi ya hip hop ambayo haina faida.

“Leo wakitajwa wasanii wakali wa hip hop hata watano Jay Moe atatajwa lakini wakitajwa wasanii watano wa hip hop wenye mafanikio Jay Moe hayupo,” alisema kwenye interview moja.
“Kwanini na mimi nisiwe kama Nay wa Mitego, kwanini mimi nisiwe kama AY na Profesa Jay wakati kipaji changu kinafaa niwe hivyo, zaidi ya hivyo. Wasanii wengi wa hip hop wanataka ku-maintain culture ambayo haipo tena. Wote tunakubali kuwa sasa hivi muziki biashara kwahiyo tukubali kufanya ule wa kibiashara ambao hatutokuwa na malalamiko ‘wasanii wa zamani tunabaniwa kwenye media’ sio kweli ni kwasababu hatujapeleka content ambayo media na wasikilizaji wanaitaka,” alisisitiza rapper huyo.
Jay Moe hajaishia kwenye Pesa ya Madafu, bali amekuja kuonesha kuwa amekimudu vizuri kizazi cha trap na dab kwenye wimbo alioshirikishwa na Songa – rapper mwingine aliyeamua kubadilisha muelekeo.
Mwendo Tu, ni wimbo mwingine wa trap ambao kutokana na ulivyo, umewaongezea wigo wa mashabiki hasa ‘teenagers’ na wasichana ambao haikuwa rahisi kuwapata kwa nyimbo walizokuwa wamezoea kufanya.

Nguvu ya wimbo huo imeongezeka zaidi kutokana na kuwa na video kali inayovutia macho ya kila mpenda vitu vizuri. Kwa mabadiliko hayo ya Jay Moe, ni wazi kuwa ana miaka mingi kwenye game na rappers wengi wapya watakuja na kuondoka na kumwacha akipeta kama na wao watashindwa kuwa vinyonga.

0 comments:

Post a Comment