Pages

Subscribe:

Thursday, September 7, 2017

Story: NILILALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI - 17

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (17)
ILIPOISHIA…
Nadhani hata yeye pamoja na kutisha kwake na uajabuajabu aliokuwa nao, alishangaa kwa jinsi nilivyosimama kwa ujasiri. Alipofika akasimama na kutimua vumbi jingi. Nikamtazama usoni, uso wake ulitanda giza, lakini nilipoendelea kumtazama zaidi, sura yake ikaonekana. Sura ilipakwa unga mweupe usoni, meno ya pembeni yalikuwa marefu na alipopanua kinywa chake kilitisha kwa jinsi kilivyokuwa kipana.

Endelea...
Kama nilivyomtazama, naye alinitazama. Macho yake hayakuwa ya kawaida. Isingekuwa...
kukata tamaa na maisha ni lazima ningekimbia. Lakini niliamua kupumzika na purukushani za walimwengu. Nilisimama.

Nadhani alipenda sana kunikimbiza. Alipoona sikimbii, akaaanza kunitisha ili nikimbie apate raha yake ya kunifata mbiombio. Kwanza alitoa sauti za kutisha. Niliogopa lakini sikukimbia. Pili, aliunyanyua upanga wake wenye makali kuwili akawa anatisha kunikata. Niliogopa nikafunga macho ili upanga utue taratibu. Lakini hakunidhuru. Moyoni nikajipongeza kwa kuchukua maamuzi haya madhubuti.

Alifanya vimbwanga vingi nikabaki nimesimama nisiyekimbia kama alivyopenda. Naye kuona hivyo hakukubali kushindwa, akajibadili na kuwa chatu mkubwa. Loooh! Sikusimama, nilikimbia bila kukumbuka ule msimamo niliojiwekea. Nilichomoka kama punda wa Bruda. Nikakata kona ya Msamariamwema, kisha nikakunja barabara ya Mwendapole, nikanyooka katika viunga vya Mchopezo kisha vichochoro vya Hujuma, na bila kujitambua nilikuwa chumbani kwangu, nimejifunika shuka zito gubigubi, naogopa kila kitu, hata mapigo ya moyo yalipodunda nilishtuka nikidhani ni zile tambo za kukimbizwa na yule mnyama mbaya!

Kulikucha kwa shida. Nilipanga chumba kimoja na humo niliishi na kila kitu changu. Faida ya kuishi katika chumba kimoja unaona mali zako zote kila unapoamka. Mpangilio wa chumba ulikuwa wa hovyohovyo. Wadudu na wanyama ambao japo sikuwakaribisha walikuwa wakazi wa chumba hiki.

Mijusi wakubwa walitafuna wadudu wadogo. Basi ikawa vurumai ndani ya chumba changu mwenyewe.

Ilipita miezi mingi nikiishi maisha ya kufukuzwa na yule mtu wa ajabu. Sasa niliyazoea maisha yale ikawa sehemu ya mazoezi yangu ya kila siku. Alipotokea nilikimbia, akatimiza furaha yake ya kunifukuza bila huruma.

Hata hivyo, pamoja na mazoea hayo, maisha yangu yalibadilika. Niliathirika kisaikolojia nikawa mtu wa hofu muda wote. Hata niliposikia kishindo cha mtoto mdogo nilihisi mtu wa ajabu kafika, nikashituka kama niliyetoka usingizini. Kuna wakati nilikimbia bila sababu kwa hofu tu, kumbe yule mtu wa ajabu hakuwako. Hali hii ilinitesa na niliichukia, nikatamani tiba nisiweze kuipata.

Nakumbuka siku moja niliamua kwenda kanisani kufanyiwa maombi ya tatizo langu hili. Nilipokuwa njiani kueleka huko, mtu wa ajabu akatokea akiwa na hasira kuliko siku zote nilizowahi kumshuhudia. Siku hiyo alinikimbiza mpaka akanikamata, kisha akanikata kidogo mguu wangu kwa upanga wake na kusababisha damu kiasi ichuruzike. Toka siku hiyo, sikurudia tena njia hii.

Popo kakosa msaada wa tatizo lake, nini hitimisho la kukimbizwa siku zote? Tukutane kesho

0 comments:

Post a Comment