ILIPOISHIA
Nililala usingizi wa matumaini. Niliamini ni lazima
ningempata Samike. Nikiwa usingizini, niliota mseto wa ndoto za zamani
na mpya. Katika ndoto mpya iliongezeka sura ya askari. Nilikiota kichwa
chake. Nikawa kama naogelea katika ndoto za masufuria. Nilipoota kuhusu
kufukuzwa, nilipiga makelele. Kama kawaida yao, wazinzi wakashtuka
wakidhani ni fumanizi. Walipogundua ni mimi, kama ilivyo siku zote
wakanipuuza. Mchezo wa nyama ukaendelea.
Endelea nayo...
Niliamka nisiye na
matumaini. Nikawaza namna ya kumpata Mzee. sikupata jibu! Lilinijia wazo
la... kuanza upya msako. Nikalikubali wazo hilo. Baada ya kujiandaa,
nikaingia barabarani kumsaka mzee.
Kila mtu niliyekutana
naye nilimuuliza, “Umemuona Mzee katoka jela leo?” majibu yalikatisha
tamaa na kuvunja moyo. Hakuna aliyemwona Samike.
Nilirejea saa nne
usiku nikiwa nimechoka. Mbwa mchafu akabweka aliponiona. Hapo nikapata
sehemu ya kupoza hasira, nilimporomoshea matusi mazito yaliyomkata
mdomo, akabaki kimya!
Chumbani nililala
bila kusafisha kitanda. Nikiwa nusu kusinzia nusu kuamka, niliamua
kusitisha msako wa Samike. Nikaamua kurejea nyumbani ifikapo asubuhi.
Mtu yule wa ajabu aliyenikimbiza nikaapa kutokumkimbia tena. “Nitasimama
anichinje na upanga wake wenye makali kuwili,” niliwaza kishujaa.
Nilichoka kulala,
kuamka na kumtafuta mtu asiyepatikana. Zaidi, nilichoka kufukuzwa na
yule Ndondocha asiye na haya. Safari ya kurejea nyumbani Chisanza
haikuzuilika kwa gharama yoyote ile.
Nilikuwa miongoni mwa
abiria 75 waliopanda basi la Mwendakwao. Safari kurejea nilikotoka
iliwadia. Masaa yalikatika kama tulivyoukata mwendo. Kupunguza mawazo,
nikauchapa usingizi.
Nilishtuka basi
likiwa singida. Lilikuwa limesimama na watu wengi walishuka kuchukua
chakula. Kwa kuwa yalipita masaa mengi bila kula, nilishuka kuchukua
chochote.
‘Bobooooooh!’ honi
ilisikika. Watu wote tukaanza kukimbia kuingia ndani ya basi. Yalisimama
mabasi matatu, letu liliegesha katikati. Kila abiria alikuwa makini
katika kuchagua gari alilopanda vinginevyo angechanganya.
Niliingia ndani ya
basi langu nikakaa. Nilichukua siti ya mbele hivyo niliweza kuiona
safari kama alivyoiona dereva. Mbele yetu lilitangulia basi lililoitwa
‘Kinyonga.’ Nalo lilijaa abiria kama lilivyojaa letu.
Wakati gari la mbele
lilipoanza kuukata mwendo, mzee mmoja alichungulia dirishani.
Nilishtuka. Alikuwa na nywele nyeupe, sharubu nyeupe, na ndevu nyeupe.
Nikajikuta nikitamka kwa nguvu, “Samike!” hata hivyo nilichelewa. Gari
lilikwisha chochewa likaseleleka kwa kasi.
Nilipata matumaini.
Na niliwaza bila shaka basi lile lilikwenda Chisanza, hivyo ningempata
Mzee huyu niliyemtafuta kwa udi, manemane na uvumba.
Nilifarijika
nilipoliona basi alilopanda likiwa mbele na langu likiwa nyuma.
Nilifurahi jinsi nilivyokuwa na uhakika wa kusafiri njia moja na mtu
niliyemtafuta.
Hatimaye Popo kafanikiwa kumuona mzee! Atampata? Tukutane kesho…
Tuesday, September 5, 2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment