Pages

Subscribe:

Wednesday, September 6, 2017

Story: NILILALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI - 16

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (16)
 ILIPOISHIA
Nilifarijika nilipoliona basi alilopanda likiwa mbele na langu likiwa nyuma. Nilifurahi jinsi nilivyokuwa na uhakika wa kusafiri njia moja na mtu niliyemtafuta.

ENDELEA NAYO...
Hata hivyo, mambo yalianza kubadilika taratibu. Kuna wakati gari letu lililipita gari alilopanda mzee. Na kuna wakati gari lao lilikwenda mbele zaidi hata ...
nikashindwa kuliona. Mwisho, magari kadhaa yaliingia yakanifanya nisilione basi alilopanda Samike. Kilichoharibu zaidi nilipitiwa usingizi. Nikashindwa kutambua kama basi la Mzee lilikuwa mbela au nyuma. Taratibu nikaulaani mwendo kasi.


Basi lilifika Chisanza. Nikashuka haraka kwenda kukagua mabasi ambayo yalifika kabla ya basi langu. Nilikiona nilichokitafuta. Basi la ‘Kinyonga’ liliegeshwa nikagundua lilifika si chini ya masaa mawili yaliyopita. Nilijaribu kuchungulia ndani mwa basi nisione kitu.

Kwa masikitiko, niliikamata njia ya kurejea nyumbani. Nilifika nikakuta chumba kimejaa vumbi na mijusi wakubwa wakinitolea macho ya karibu mgeni. Sikujali chochote. Nikalala. Ilikuwa yapata saa nne usiku.

Asubuhi niliamua kwenda katika ‘mishemishe.’ Sikuwa na kazi maalumu. Chochote kilichopatikana kijiweni nilifanya. Nilifanya kazi nyingi kama: kuosha magari, kupara samaki, udalali, deiwaka na kazi zingine chungu nzima ilimradi mkono uende kinywani.

Nakumbuka siku hiyo nilipata tenda ya kuosha gari kubwa. Jamaa zangu kijiweni walihoji kuhusu kupotea kwangu. Niliwaficha kuwa nilikuwa naumwa, hivyo sikuweza kufika.

Baada ya kupiga kazi ya kuosha gari kubwa, nilipewa kiasi cha fedha kilichotosha kutengeneza tabasamu dogo usoni mwangu. Nisiye na mashaka  na kesho, nikaanza kurejea nyumbani. Ilikuwa ni mida ya saa moja na nusu usiku.

Wakati narejea nyumbani, nilipulizwa na upepo mkali hata shati langu likapepea. Nilipotazama pembeni nilimuona mtu wa ajabu akinisogelea. Siku zote niliishi maneno yangu. Niliamua kutimiza nilichopanga. Nitakimbia mpaka lini? Sikimbii, nataka aniuwe nipumzike! Kwa ujasiri nilisimama, nikamsubiri afike anichinje kama kuku.

Nadhani hata yeye pamoja na kutisha kwake na uajabuajabu aliokuwa nao, alishangaa kwa jinsi nilivyosimama kwa ujasiri. Alipofika akasimama na kutimua vumbi jingi. Nikamtazama usoni, uso wake ulitanda giza, lakini nilipoendelea kumtazama zaidi, sura yake ikaonekana. Sura ilipakwa unga mweupe usoni, meno ya pembeni yalikuwa marefu na alipopanua kinywa chake kilitisha kwa jinsi kilivyokuwa kipana.

Popo kaamua kupambana na mtu huyu wa ajabu... Nani atashinda? Tukutane kesho

0 comments:

Post a Comment