Pages

Subscribe:

Saturday, September 9, 2017

Story: NILILALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI - 18

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (18)

ILIPOISHIA
Nakumbuka siku moja niliamua kwenda kanisani kufanyiwa maombi ya tatizo langu hili. Nilipokuwa njiani kueleka huko, mtu wa ajabu akatokea akiwa na hasira kuliko siku zote nilizowahi kumshuhudia. Siku hiyo alinikimbiza mpaka akanikamata, kisha akanikata kidogo mguu wangu kwa upanga wake na kusababisha damu kiasi ichuruzike. Toka siku hiyo, sikurudia tena njia hii.

Endelea...
Asubuhi ya siku ya Jumamosi, ‘nilitupia’ shati la kaki na suruali nyeusi kisha chini nikavalia buti kubwa nyeusi nilizopewa na rafiki yangu mwanajeshi. Siku hiyo niliamua kwenda...
ufukweni kupumzisha akili kutokana na mikikimikiki ya kukimbizwa na maisha na kufukuzwa na mtu wa kutisha. Zimwi likujualo halikuli likakwisha, mtu wa ajabu alinitafuna taratibu na punde ningebaki mifupa!

Nilifika ufukweni. Mandhari yake yalipendeza. Kwa muda nikayasahau yale masahibu yangu ya siku zote. Katika jambo ambalo nilifurahi kuliona, ulikuwa ni ule ugonjwa wangu wa miaka mingi ulionipa mkasa wa kufukuzwa muda wote. Wanawake.

Walikuwako wengi. Nao kwa uchokozi walivalia nguo za ndani tu. wengi wakijitia kuogelea kama samaki. Wizi mtupu!

Kabla sijakaa, macho yangu yalitua kwa binti mmoja ambaye aliumbika haswaa. Nikageuza shingo kumtazama. Alivaa ‘bikini’ nyepesi ambayo haikuweza kuficha kilichokuwa ndani hata nikajiuliza alificha nini ilhali kila kitu kilionekana. Nyuma alifungasha mzigo mkubwa, faida yake ni kwamba, alipokaa hakukalia mifupa! Aliutambua urembo wake, ndiyo maana alitembea kwa maringo mithili ya twiga aliyeshiba nyasi.

Niliendelea kutembea huku nikimwangalia. Nikasahau kutazama mbele nilikokuwa naelekea. Ghafla, nilihisi nimekanyaga kitu laini kwa buti langu la kupewa. Nilipotazama, kumbe nimekanyaga makalio ya dada mmoja aliyekuwa amelala pembezoni mwa jamaa fulani mnyanyua vyuma. Dada akahamaki na kulalamika kwa uchungu. Jamaa kuona nimemzalilisha mwanamke wake, akanyanyuka na kunichapa kofi zito ambalo lilinifanya nifikiri tofauti. Sikuwa na muda wa kugombana, nikavumilia uchungu wa kofi na matusi ambayo niliendelea kuporomoshewa.

Nilikwenda mpaka sehemu iliyokuwa na kivuli, nikakaa nikipata upepo. Siku hii haikuwa nzuri kwangu. Wanawake wote walikuwa na mabwana zao. Si kwamba nilikwenda kuwinda wanawake, la hasha, lakini ilitia faraja kumuona mwanamke akiwa peke yake eneo kama lile.

Nikiendelea kupata upepo, nilivutiwa na mtumbwi mkubwa uliokuwa ukija ufukweni. Nilibashiri lazima mtumbwi ule ulikuwa wa mvuvi ambaye sasa alirudi na samaki wa kuuza. Niliendela kuutazama ukisogea taratibu ufukweni mpaka ulipofika.

Ndani ya mtumbwi alikuwamo mzee mmoja mwenye nywele nyeupe, nyusi nyeupe na ndevu nyeupe. Haikutosha kumuita mzee, lilikuwa pande la mzee. Nilifurahi nikatamka kwa sauti Samikeeeeeeeeeeh!

Itaendelea kesho…

0 comments:

Post a Comment