Sunday, September 10, 2017
Story: SIKU SABA KUZIMU (Sehemu ya 21) - 21
ILIPOISHIA:
Nikiwa naendelea kulia, nilipaliwa na mate, hali iliyofanya nikohoe mfululizo, ajabu zaidi, na ule mwili wangu pale kitandani ukakohoa, madaktari wakazidi kupigwa na butwaa, wakawa wanatazamana wakiwa ni kama hawaamini kilichokuwa kinatokea.
SASA ENDELEA
“Amerejewa na fahamu zake, amezinduka,” alisema daktari mmoja kwa sauti, nikaona pilikapilika zimeanza tena kupamba moto mle wodini. Daktari mmoja akaja...
kunipima mapigo ya moyo huku akiwatazama wenzake, nikamuona akitingisha kichwa.
Niliendelea kupewa matibabu ya uhakika, kila mmoja akawa anachakarika kwa nafasi yake. Nilimuona daktari mmoja akifungua mlango na kutoka nje, akasogea mpaka pale akina Raya walipokuwa wamekusanyika.
Nikamuona akizungumza nao mambo fulani, ghafla nikamuona Raya akimrukia mwilini kwa furaha, akamkumbatia kwa nguvu kisha akainua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu.
Japokuwa sikuwa nimesikia walichokuwa wanakizungumza, niliamini kwamba lazima yule daktari atakuwa ameenda kuwaambia kwamba sikuwa nimekufa kama wanavyofikiria. Nilijikuta nikisisimka sana, yale machozi yaliyokuwa yananitoka yakaacha, nikawa namtazama Raya alivyofurahi kama mwendawazimu.
Nilijikuta nikitabasamu kwa jinsi maichana huyo alivyokuwa amefurahi, nikamuona akimkumbatia kila mtu kwa furaha, huku tabasamu likichanua kwenye uso wake uliokuwa umeloweshwa na machozi. Kumbe vile nilivyokuwa nikitabasamu mwenyewe, hata ule mwili wangu pale kitandani ulikuwa ukitabasamu, nikawaona madaktari wote wakipeana mikono kama ishara ya kupongezana.
Ama kweli hii dunia ina maajabu, nilisema mwanzo na sitaacha kusisitiza, hii dunia ina mambo mengi sana ambayo kwa akili za kawaida ni vigumu sana kuyaelewa. Najua bado kuna watu wengi hawaelewi au hawaamini ninachokisema lakini napenda tu kuwaambia watu kwamba maisha yana siri kubwa sana.
Ni wale tu ambao wako tayari kujifunza vitu vipya kila siku wanaoweza kuendana na kasi halisi ya maisha. Ukitazama kwa juujuu, unaweza kuona kama maisha au uhai wa mtu ni jambo jepesi sana lakini haipo hivyo. Ukiijua thamani halisi ya maisha na uhai, kamwe huwezi kumtendea ubaya binadamu mwenzako, huwezi kuyakatisha maisha ya mtu wala huwezi kuwadharau wengine.
Basi wakati watu wote wakionesha kufurahishwa na maendeleo yangu pale kitandani, mimi mwenyewe nilikuwa nikijihisi hali tofauti kabisa. Japokuwa nilikuwa nimefungwa bandeji kubwa kwenye lile jeraha langu kubwa kifuani na mara kwa mara lilikuwa likisafishwa na kuwekwa dawa nyingine, huku katika ulimwengu wa peke yangu sikuwa nikihisi maumivu hata kidogo.
Hata watu walivyokuwa wakihangaika, nilibaki kuwashangaa tu kwa sababu sikuwa najihisi kama naumwa sehemu yoyote na hata pale walipokuwa wanasema kwamba nimekufa, mwenyewe bado nilikuwa na akili zangu timamu na nilikuwa naelewa kila kitu kilichokuwa kinaendelea.
Katika ukuaji wangu, nimewahi kusikia kwamba mtu anapokufa, anakuwa anaendelea kuishi kwa siku kadhaa, na hata siku ya mazishi yake, huwa mwenyewe anashuhudia anavyozikwa, anaangalia nani analia sana, nani halii, nani anafurahia kifo chake na watu wangapi wamehudhuria kwenye mazishi yake.
Kabla sijatokewa na mkasa huu, na mimi nilikuwa mgumu sana kuamini lakini leo naamini kwamba kumbe hata wafu huwa wanaishi, kwa hiyo usimtendee mtu ubaya ukiamini kwamba akishakufa huo ndiyo mwisho wake, unajidanganya!
Hata katika vitabu mbalimbali vya dini, vinaeleza kwamba kuna maisha baada ya kifo, natamani sana kila mtu awe anaishi maisha yake akielewa kwamba kuna maisha baada ya kifo!
Nikiwa bado nimesimama palepale nikijitazama mwili wangu pale kitandani na watu wote waliokuwa ndani ya wodi hiyo, kwa mara nyingine nilijikuta nikishikwa tena mkono na kuvutwa kwa nguvu na mtu ambaye sikumuona.
Safari hii alikuwa na nguvu pengine kuliko hata mara ile ya kwanza, kufumba na kufumbua nikajikuta nimerudishwa tena kule nilikokuwa mwanzo lakini tofauti yake, safari hii giza halikuwa nene sana wala hakukuwa na milio ya wanyama wa kutisha.
Jambo ambalo bado lilikuwa likifanana, ni kwamba kila nilichokuwa nikikiwaza moyoni, kilikuwa kikisikika kwa sauti ya mwangwi utafikiri nimekitamka mdomoni. Yule mtu hakunisemesha chochote, akaniacha mahali ambapo sipajui kisha akayeyuka kama upepo.
“Jamal! Nisamehe Jamal,” niliisikia sauti ambayo niliitambua kwamba ni ya Shenaiza ikinizungumzisha kwa mbali, ikawa inasikika kwa mwangwi kama sauti nyingine. Nilishtuka sana, kilichonishtua ni kugundua kwamba Shenaiza naye alikuwepo kwenye mazingira yale ya ajabu na kutisha kuliko kawaida.
“Nimekusamehe Shenaiza ila nataka kuufahamu ukweli wako,” nilitamka lakini kama ilivyokuwa mwanzo, sauti haikutoka kabisa, nikashusha pumzi ndefu na kuanza kuzungumzia moyoni, nikarudia maneno yaleyale, kweli sauti ikatoka.
“Mimi sina ubaya wowote na wewe Jamal, haya yote ameyasababisha baba yangu.”
“Baba yako amesababisha kivipi? Na hapa nilipo ni wapi? Nimefikaje?”
“Sijui chochote Jamal, mi nahisi kama nipo ndotoni ila nasikia wewe ulishakufa,” alisema Shenaiza na muda huohuo, nikajikuta nimehama pale nilipokuwepo na kutokezea sehemu nyingine tofauti kabisa. Nilijikuta nimetokezea kwenye chumba cha kifahari, kilichokuwa na kitanda kikubwa na vitu vingine vya thamani.
Juu ya kitanda hicho, alikuwa amelala msichana mrembo ambaye bila hata kuuliza, niligundua kuwa ni Shenaiza. Nilishindwa kuelewa pale ni wapi na imekuwaje nifike pale, pia nikawa najiuliza kuhusu kauli ya Shenaiza kwamba eti mimi nimekufa. Kama Shenaiza amelala, niliyekuwa nazungumza naye ni nani? Au ndiyo maana alisema anahisi kama yupo ndotoni?
“Shenaiza!” nilimuita lakini sauti haikutoka, nikamuita moyoni! Cha ajabu aliitika, nikamuona japokuwa alikuwa amelala, midomo yake ilikuwa ikichezacheza kuonesha kwamba ni yeye ndiye aliyekuwa akizungumza.
“Unasema baba yako ndiyo anahusika na haya yote, hebu niambie kivipi.”
“Siwezi kukwambia chochote Jamal kwa sababu wewe umeshakufa, ila kaa ukielewa kwamba baba yangu siyo mtu mzuri hata kidogo.”
“Nataka uniambia ukweli, ilikuwa ukaipata namba yangu na kuanza kuwasiliana na mimi wakati ukijua kabisa unanisababishia matatizo na kwa sababu gani unang’ang’ania kusema nimekufa?”
”Hayo hayana maana tena Jamal, nakuomba unisamehe kwa kukusababishia kifo.”
“Kifo? Mimi sijafa Shenaiza.”
“Najua naongea na mzimu wako Jamal, nakuomba sana msamaha, siku ya mazishi yako nitajitahidi kufika nikuage, nilikupenda sana lakini ndiyo hivyo tena, Mungu amekuchukua kipindi ambacho hata sijakufaidi, najisikia vibaya sana Jamal.”
“Unazungumza nini? Mimi sijafa Shenaiza! Sijafaaa,” nilisema kwa sauti kubwa huku nikimtingisha pale kitandani azinduke usingizini, ghafla nikashangaa msichana huyo akikurupuka usingizini na kupiga kelele kwa nguvu!
“Mzimuuu! Mzimu wa Jamal umenifuata, nisaidieni nakufaaa!” alisema Shenaiza na kuendelea kupiga kelele, muda mfupi baadaye, mlango wa chumba chake ukafunguliwa, wakaingia wanawake wawili ambao walikuwa wamefanana naye, wakamshika huku na kule na kuanza kumuuliza kilichotokea.
“Umepatwa na nini?”
“Nimetokewa na mzimu.”
“Mzimu? Mzimu gani wakati sasa hivi ni mchana?”
“Nilikuwa nimelala nikatokewa na mzimu wa marehemu Jamal!”
“Mh! Au unaanza kuchanganyikiwa mwenzetu? Jamal gani unayemzungumzia?”
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue
Labels:
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment