UKITAJA listi ya wasanii wa kike wanaofanya vizuri kwa sasa kimataifa basi Vanessa Mdee ‘Vee Money’ linakuwa jina namba moja.Vanessa, 27, ambaye ameanza muziki ‘juzi’ sasa anaonekana kama mkongwe na kuwapita baadhi ya wasanii wa kike ambao amewakuta kwenye ‘gemu’.
kutajwa kama ‘nominees’ ni sifa kubwa kwake na taifa kwa ujumla.
Kwa sasa ametajwa kwenye Tuzo za AFRIMMA za Marekani, akiwania kipengele cha Mwanamke Bora wa Afrika Mashariki wa Mwaka na Mtetezi wa Haki za Binadamu (Best Female of East Africa and Humanitarian of The Year), pia Tuzo za AFEA (Africa Entertainment Awards), kwenye kipengele cha Msanii Bora wa Kike. Ili kumpigia kura ewe shabiki wake unatakiwa kuingia kwenye mitandao ya waandaaji na kufuata maelekezo.
Championi linakuletea mahojiano iliyofanya naye:
Championi: Unafikiri nini sababu ya wewe kukosa tuzo ya MTV MAMA 2015?
Vee Money: Hakuna sababu lakini niseme tu pengine muda wangu ulikuwa bado haujafika ndiyo maana imetokea hivyo, kikubwa ni kwamba Watanzania waendelee kunisapoti katika kazi zangu na tuzo zingine ambazo nimechaguliwa tena kuwania kwa sasa. Najipanga mwakani kwani kutakuwa na nafasi nyingine.
Championi: Umewezaje kupenya kwa haraka katika gemu ya muziki hadi kujulikana kimataifa?
Vee Money: Hapo asante zangu nyingi sana zinahusika kwenye ‘social media’ mbalimbali, ambazo kwa upande wangu zimenisaidia sana na ‘networks’ zote nilizonazo hususan ndani na nje zimenifanya nifike hapa nilipo.
Championi: Nani alikushonea gauni ulilovaa kwenye Tuzo za MTV?
Vee Money: Aaah! ha, ha, (anacheka kidogo....kisha anajibu) unajua bhana kuna mbunifu wangu mmoja hivi kutoka ‘Sauz’ ndio mara nyingi amekuwa akiniandalia nguo zangu za mitoko ya hapa na pale.
Championi: Mbali na kazi uliyofanya na K.O ya Wimbo wa No Body But Me, kuna kazi nyingine ya kimataifa ambayo unategemea kuiachia hivi karibuni?
Vee Money: Yap! Zipo nyingi sana. Sitapenda kuzitaja kwa sasa kwa sababu muda muafaka haujafika lakini wapenzi wa kazi zangu waelewe kuwa nimefanya kazi na Shayedee pamoja na B. Black kutoka Ghana, muda wowote mambo yatakuwa sawa.
Championi: Hivi karibuni ulisaini mkataba na Jarida la Essence, linalohusu mambo ya urembo, je, zaidi ya fedha ulizopata kuna kingine umepata?
Vee Money: Faida zipo nyingi sana lakini siwezi kuweka wazi. Unajua Essence ni jarida kubwa sana Marekani, linahusika na mambo ya urembo na mvuto wa wanawake wa Kiafrika. Sasa unaweza ‘kuimagine’ nina bahati kiasi gani, tangu mwaka 1978 hawakuwahi kukanyaga Afrika mpaka mwaka huu walipokuja na kunichukua mimi kuwawakilisha wasanii wote wa kike kutoka Afrika. Hiyo kwangu ni faida kubwa sana maana najitangaza zaidi.
Championi: Vipi kuhusu kampeni uliyofanya na One Compain, imezaa matunda gani?
Vee Money: Well, matunda yapo tena yaliyoiva kabisa, Ha! ha! haaa! (anacheka kidogo kisha anaendelea...) naomba watu waelewe kuwa bado kampeni hiyo ninaendelea nayo ukizingatia kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, huu ni mwaka wa wanawake.
Championi: Waeleze watu ambao hawafahamu kampeni hiyo inahusu nini na utaje baadhi ya wasanii ambao uko nao?
Vee Money: Aah! Inahusu uhamasishaji kwa nchi zinazoendelea kuandaa sheria ambazo zitawafanya wanawake kuwa na vipaumbele katika nyanja mbalimbali ili kujikimu kimaisha. Wasanii ambao wapo ni pamoja na Yemi Alade, Waje pamoja na Victoria Kimani, ambao tulifanya nao Wimbo wa Strong Girl.
Lakini jambo lingine ambalo watu wanatakiwa kufahamu kuhusu mafanikio, watu zaidi ya milioni moja wamesaini mswada ambao umeenda makao makuu ya umoja wa mataifa, nafikiri kufikia mwakani kutakuwa na matokeo mengine mazuri zaidi.
Championi: Unawezaje kufanya mambo mengi katika muda muafaka bila upande mmoja kuuathirika upande mwingine?
Vee Money: Nidhamu ni jambo la msingi sana, naheshimu kila ninachokifanya tena hasa muda ambao natakiwa kufanya ili mambo yangu yanaenda poa.
Championi: Unawashauri nini wasanii ambao wanatamani kufika hapo ulipo?
Vee Money: Juhudi na kuheshimu wanachofanya ndiyo mambo ya muhimu sana kuzingatia, bila hivyo mafanikio watayasikia tu kwa watu wengine.
Championi: Msanii gani wa kike unampenda Bongo na kwa nini?
Vee Money: Ninampenda sana Jide (Judith Wambura) kwa kweli, kwa sababu ni mfano tosha wa kuigwa na wanamuziki wa kike wa Kitanzania, na kubwa zaidi amefungua njia na kututambulisha vema kimataifa, lakini pia uwepo wake mpaka leo unaonyesha ni jinsi gani kazi zake zina ubora usiopotea, so kupitia yeye kuna mengi tunaweza kujifunza na tukapata mafanikio makubwa.
Championi: Unapenda siasa, kama ndiyo chama gani?
Vee Money: Yes! Napenda siasa lakini siwezi sema ni chama gani na kikubwa zaidi kuelekea mwaka wa uchaguzi, nikiwa kama msanii ambaye ni kioo cha jamii, ninaiombea nchi yangu ifanye uchaguzi wenye amani na upendo kwa manufaa ya kupata viongozi bora na siyo bora viongozi.
0 comments:
Post a Comment