Pages

Subscribe:

Friday, September 15, 2017

Story: SIKU SABA KUZIMU (Sehemu Ya 23) - 23


ILIPOISHIA:
“Mzimu? Mzimu gani wakati sasa hivi ni mchana?”
“Nilikuwa nimelala nikatokewa na mzimu wa marehemu Jamal!”
“Mh! Au unaanza kuchanganyikiwa mwenzetu? Jamal gani unayemzungumzia?”

SASA ENDELEA
“Nimeota kabisa naongea na Jamal wakati ameshafariki. Ninachosema ni kweli kabisa, wala siyo kwamba nimeanza kuchanganyikiwa,” Shenaiza alizidi...
kusisitiza lakini hakuna aliyemuamini.

Tangu aende kuchukuliwa kwa nguvu na walinzi wa baba yake na kurejeshwa kwenye makazi ya siri ya familia yao, Kurasini, alikuwa ni kama amechanganyikiwa. Muda mwingi alikuwa ni mtu wa kulia na kuijutia nafsi yake huku akimlaumu baba yake kwamba alikuwa akimuonea kwa yote aliyokuwa akimfanyia.

Alipokuwa akizidi kusumbua, daktari maalum wa familia hiyo, alikuwa akipewa kazi ya kumdunga dawa za usingizi zilizomfanya alale muda mrefu. Hali hiyo ilimfanya kwa kiasi kikubwa akose hata nafasi ya kufuatilia kilichokuwa kinaendelea kuhusu Jamal, kitu pekee alichokuwa anakijua akilini mwake, ni kwamba kijana huyo alikuwa amefariki dunia baada ya lile tukio ambalo yeye ndiye aliyekuwa chanzo.

“Muiteni dokta.”
“No! I dont need any more sedatives please, im not out of my mind,” (Hapana! Sihitaji tena kuchomwa dawa za usingizi, mimi sijachanganyikiwa) alipiga kelele Shenaiza lakini haikusaidia kitu, muda mfupi baadaye, daktari wao aliingia akiwa na bomba la sindano na kichupa cha dawa mkononi kilichokuwa na maandishi yaliyosomeka Diazepam, akiwa ameongozana na wanaume wawili wenye miili mikubwa.

Shenaiza alijaribu kufurukuta lakini wapi! Akashikiliwa kwa nguvu na wale wanaume, daktari akatoa pamba iliyokuwa imepakwa ‘spirit’, akamsafisha sehemu ya ndani ya mkono wake, mahali kwenye mishipa ya damu na taratibu akazamisha sindano kwenye mshipa wake na kuisukumia ile dawa ndani, muda mfupi baadaye, Shenaiza alianza kuzungumza maneno yasiyoeleweka na kupitiwa na usingizi mzito.

Wakati yote hayo yakiendelea, nilikuwa nikishuhudia kila kitu, bado nikiwa katika hali ileile ambayo hakuna mtu ambaye aliniona ingawa mimi nilikuwa na uwezo wa kuona kila kitu. Kile kitendo cha kushuhudia Shenaiza akifanyiwa ukatili ule, kilinisikitisha sana ndani ya moyo wangu na kunifanya nianze kumtazama Shenaiza kwa sura tofauti kabisa.

Nisiseme uongo, baada ya mfululizo wa matukio yale, mpaka lile la mwisho ambalo liliyabadilisha kabisa maisha yangu na kunifanya nisieleweke kama mimi ni binadamu au maiti, nilikuwa nikimchukia sana kwa kuona kwamba yeye ndiye aliyeniingiza kwenye mtego huo kwa makusudi.

Hata hivyo, kwa kile nilichokishuhudia, nilianza kuamini kwamba huenda haikuwa dhamira ya Shenaiza kuniingiza kwenye matatizo makubwa kiasi kile, nikajikuta nikimuonea huruma na kuwalaani wale waliokuwa wakimfanyia kitendo kile.

Nilijikuta nikiwasonya kwa nguvu. Cha ajabu, ilionesha kwamba walisikia nilivyowasonya kwani wote waliokuwa ndani ya kile chumba, wakiwemo wale ndugu zake Shenaiza waliokuwa wamefanana naye sana, yule daktari na wale walinzi, waligeuka na kuanza kutazama huku na kule.

“Nimesikia kama mtu amesonya, au masikio yangu yamesikia vibaya,” aliuliza mmoja, kila mmoja wao akajibu kwamba na yeye amesikia lakini wakawa hawajui ni nani aliyefanya kitendo hicho. Japokuwa nilikuwa palepale jirani yao, kwenye moja ya kona za chumba hicho, hakuna aliyeniona, baadaye nikawaona wakianza kutoka mmoja baada ya mwingine, kila mmoja akionesha kuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake.

Nilichojifunza, katika maisha ya kawaida, ukijiona upo katika mazingira ambayo hakuna mtu lakini ghafla ukasikia mtu anakusonya kwa sauti lakini ukigeuka humuoni yeyote, jua kwamba eneo hilo hauko peke yako. Kuna mtu au watu wengine wanakuona na pengine hawafurahishwi na unachokifanya.

Ukiwa na akili, inabidi urekebishe kile unachokifanya kwa sababu unaweza kupata matatizo ambayo hakuna anayeweza kuyaelezea, hapa ndipo lile neno ‘katika mazingira ya kutatanisha’ linapotumika. Kwamba unafanya tukio au unapatwa na tukio ambalo katika akili ya kawaida, hakuna anayeweza kuelewa nini hasa kilichotokea.

Basi niliendelea kusimama palepale nikimtazama Shenaiza ambaye tayari alishapitiwa na usingizi mzito, nikawa na shauku kubwa ya kutaka kujua mambo mengi yaliyokuwa yamejificha nyuma ya maisha yake.

“Jamal! Jamal! Jamaaaal!” nilisikia sauti nzito, nene ya kutetemeka ikiliita jina langu kwa nguvu, kabla hata sijajibu chochote, nilishangaa nikichukuliwa pale na kitu kama kimbunga kikali, sekunde chache tu baadaye, nilijikuta nikiwa tena kulekule nilikokuwa mwanzo, giza nene likiwa limetawala kila upande lakini tofauti na awali, nilihisi kama nimesimama juu ya kokoto.

Ile sauti iliyoniita haikusikika tena, ila kwa mbali nikawa nasikia muungurumo kama wa treni likija kwa kasi kubwa pale nilipokuwepo. Muungurumo ulizidi kuongezeka, nikawa nageuka huku na kule kutazama ulikokuwa unatokea lakini sikuona chochote, nikahisi nikiendelea kusimama palepale huenda nikagongwa na treni hilo.

Nilipopiga hatua moja mbele, nilikanyaga kitu kama reli, nikagundua kwamba kumbe nilikuwa kwenye njia ya treni hilo ambalo sikuelewa ni la aina gani kwa sababu ninachojua mimi, treni huwa zinakuwa na taa na huwa haziendi kwa mwendo kasi kiasi hicho.

Ilibidi nichangamke, nikakimbia hatua kadhaa lakini kila nilipokuwa napita, bado nilikuwa nikikanyaga reli, ghafla nikasikia mlio mkali wa honi uliofuatiwa na mwanga mkali wa taa, ni hapo ndipo nilipogundua kuwa treni hilo lilikuwa limenikaribia mno na lilikuwa likija usawa wangu kabisa kiasi kwamba kama nisingefanya chochote kujiokoa, lingenigonga na kunisagasaga.

Cha ajabu zaidi, baada ya kunipigia honi na kunimulika, miguu yangu iliganda palepale nilipokuwa nimesimama, sikuweza hata kutingishika, nikawa nimeganda kama sanamu huku hofu kubwa ikiwa imenijaa moyoni, ilibidi nifumbe macho kwani nilijua huo ndiyo mwisho wa maisha yangu.

Nilisikia kelele za vyuma vikikwaruzana, nadhani ni matairi ya treni na reli baada ya kufunga breki kali, nikasikia nikipulizwa na upepo mkali na kudondokea mita chache mbele, nilipofumbua macho, lile treni lilikuwa limesimama mita chache kutoka pale nilipokuwa nimeangukia, ile taa ikiwa imezimwa lakin likiendelea kunguruma kwa nguvu.

“Panda twende,” ilisikika sauti nzito ya mwanaume, nilipoinua macho yangu, nilimuona mzee mmoja akiwa amekaa sehemu ya dereva, akawa ananipungia mikono akiniashiria nifanye vile alivyoniambia.

Harakaharaka niliinuka, nikalisogelea lile treni ambalo lilikuwa na joto kali, nadhani ni kwa sababu ya kasi liliyokuwa nayo, yule mzee akanionesha niendelee kuelekea nyuma mpaka sehemu ya kupandia, nilifanya hivyo lakini kutokana na giza nene lililokuwepo nilishindwa hata kuona sehemu ya kuelekea, nikashtukia nikishikwa mkono na mtu ambaye wala sikumuona, akanisukumia kwenye ngazi, nikapanda na kuingia ndani ya treni hilo.

Kilichonipa moyo, ndani ya treni hakukuwa na giza kama kule nje, kulikuwa na taa ndogo iliyokuwa na mwanga hafifu uliofanya angalau nione ndani ya lile treni kulivyokuwa. Treni hiyo ilikuwa chakavu sana, kuanzia viti vyake, sakafu na kila kitu ndani yake.

Kulikuwa na abiria kadhaa ambao wote walikuwa wameinamisha vichwa vyao kuonesha kwamba walikuwa wamelala, niliamini kwamba huenda watakuwa wametoka safari ya mbali sana ndiyo maana walichoka vile.

Muda huohuo, treni iliondoka kwa kasi kubwa, kelele za vyuma na muungurumo zikawa zinasikika kwa nguvu huku moshi mwingi ukiingia kupitia madirishani, nilitamani kuuliza tulikuwa tunaelekea wapi lakini hakukuwa na wa kumuuliza. 

Nilitamani hata kumuona yule mtu aliyenishika na kunisaidia kupanda lakini pia sikumuona, watu wote walikuwa kimya kabisa, nyuso zao wakiwa wameziinamisha.

Treni ilizidi kushika kasi, ikafika kipindi nikawa nahisi kwamba haikanyagi kwenye reli bali inapaa angani kwa jinsi ilivyokuwa ikienda kasi. Ghafla, nilipogeuka huku na kule, nilishtuka kugundua kwamba nilikuwa nimebaki peke yangu kwenye treni hilo, sikukumbuka kama kuna sehemu lilisimama, nikawa najiuliza wale abiria wengine wameenda wapi?
Je, nini kitafuatia? Usikose

0 comments:

Post a Comment