Wednesday, October 19, 2016
STORY: NILIACHA USISTER NIKAWA MCHAWI 02
ILIPO ISHIA: “Nimeongea na mama yako kuhusu ule mpango wako, kimsingi hata yeye amekubali kwamba ukawe sista.” Kabla sijasema asante, nilimsikia bibi chumbani aliko akicheka sana. Mama, baba wakashtuka. SASA ENDELEA…
“Mama anacheka nini?” baba aliuliza. “Hata mimi sijui,” alisema mama huku akiondoka kwenda chumbani kwa bibi. Mimi moyo ulinilipuka, nikawa na wasiwasi, moyo wangu ukajaa hofu. Baba alinikazia macho kama aliyekuwa akiniambia endelea. Mara, mama alirejea na...
kukaa lakini baba hakumuuliza bibi alikuwa akicheka nini. Nilitoka kwenye kiti na kupiga magoti sakafuni huku nikisema asanteni wazazi wangu, nimefurahi kwani nitatimiza ndoto yangu ya miaka yote.
“Sawa mwanetu, sisi tunakupenda sana ndiyo maana tukaona tukubaliane na wewe kwa kuwa wewe ndiyo unajua maisha yako yatakavyokuwa,” alisema baba huku akisimama kuashiria kwamba alishamalizana na mimi. Baada ya kuondoka baba, nilimgeukia mama na kumuuliza kisa cha bibi kucheka chumbani kwake. “Hayakuhusu Bena, tena usimfuatilie mama yangu, ohooo,” mama alikuja juu huku akiinuka. Naamini hata baba alisikia kule alikokuwa amekwenda. Nilimshangaa sana mama, nilihisi amebadilika ghafla sana. Nilijikagua katika maeneo mbalimbali ili kujua nilikosea wapi lakini sikupata jibu. Kila eneo nilijiona niko sawa.
Basi, mipango ilifanyika, wazazi wangu walijipanga, baada ya miezi mitatu mbele nilikwenda kwenye chuo kimoja mkoani Ruvuma ambako mwaka wa kwanza ulikuwa wa majaribio, mwaka wa pili nilianza kuvaa kilemba nusu kichwa, miaka mingine miwili ilikuwa ya ukamilifu wa kiroho. Nilikaa pale kwa miaka minne, nilipomaliza nilipewa utumishi wa mwaka mmoja kulekule Ruvuma kwenye Mji wa Songea katika kanisa moja. Baadaye nilipelekwa Iringa ambako niliungana na masista wenzangu waliosomea mkoani Tanga na Mwanza.
Tanga walikuwa watatu, Mwanza wawili na mimi niliyetokea Songea na mwenzangu mmoja. Siku saba za kuanza utumishi wa pale, siku hiyo usiku kabla ya kulala tulisali kama ilivyo kawaida ya maelekezo ya vitabu vya Mungu na sheria za utawa katika mambo ya kiroho, lakini tulipomaliza tu mimi nilipatwa na hisia ya kuinua uso juu na kuutazama ukuta, nilishtuka kumwona njiwa ameng’ang’ania ukuta.
Nilihamaki na kusema jamani huyu njiwa kwenye ukuta ameingiaje? Wenzangu nao waligeukia ukutani ambako nilielekeza kidole, lakini wakanicheka na kusema nina uzingizi ndiyo maana naota ndoto nikiamini ni kweli. Wakati wenzangu wakinishangaa na kunikebehi kwa maneno hayo, yule njiwa pale ukutani hakuwepo! Hilo lilinishangaza zaidi. Nilibaki nimesimama nikishangaa, midomo ilikuwa wazi kwa mshangao huo, mwili ulitetemeka lakini wenzangu hawakujua. Ndipo mwenzangu mmoja anaitwa Sista Marieta akaniambia nikae chini kwanza. Baada ya kukaa, aliwaambia wengine kwamba amebaini nilichokisema kwamba nimeona njiwa ukutani ni kweli na wala si usingizi kama walivyonitania.
Sista mmoja anaitwa Anna-Maria akaniuliza kama tukio kama lile liliwahi kunitokea siku za nyuma, nikakataa lakini sijui kwa nini, kichwani mwangu nikahisi nachezewa ingawa sikumjua ni nani. Basi, tuliingia vyumbani kulala na mpaka kukakucha asubuhi bila kumwona tena yule njiwa au ajabu lingine lolote zaidi ya mawazo yangu tu kusumbuka kichwani kwamba ilikuwa nini. *** Miezi sita mbele, siku moja nilikuwa nafua. Ghafla mbele yangu akatua njiwa tena kama yuleyule. Nilishtuka sana, nikakimbia eneo hilo na kwenda kusimama mbali maana hapo nilipokuwa nafua nilikuwa peke yangu.
Nilikwenda kusimama mbali kidogo huku nikiwa nasali sala ya Salamu Maria kimoyomoyo, nilibaini kuwa yule njiwa alikuwa ana kikaratasi cheupe shingoni. Niliogopa zaidi, nikakimbilia ndani kuwaita wenzangu. Sista Marieta ndiye aliyekuwa mbele ya wote. Wote kwa pamoja tulikuwa tukisali, wengine walisali Baba Yetu, wengine Salamu Maria, wengine Atukuzwe Baba. Cha ajabu, hatukumkuta njiwa pale nje nilipokuwa nafua. Wenzangu wakanigeukia na kuniangalia kwa macho yenye kuniuliza yuko wapi huyo njiwa. Nilibaki nimeduwaa nisijue la kuwajibu.
Siku hiyo nilishinda sina raha, sina amani. Nilikumbuka sana nyumbani kwetu, Tanga. Nilimkumbuka baba, nilimkumbuka na mama, niliwakumbuka hata baadhi ya marafiki zangu niliokuwa nikisoma nao shule hasa sekondari. Kitu kimoja cha ajabu zaidi siku hiyo ni kwamba, baada ya kumaliza kufua sikuwahi kurudi chumbani. Nilifanya kazi nyingine za nje ikiwa ni pamoja na kuhudumu usafi kwenye nyumba ya padri. Saa kumi na mbili jioni nilikwenda chumbani na kukutana na kituko kingine. Kitandani nilikuta karatasi nyeupe imekunjwa mara moja.
Niliichukua, nilipoifungua nikakuata imeandikwa hivi; Kwako Bena, ni vizuri ukajitafakari ili ujue kama utumishi ulionao utaendelea kukufaa au uangalie maisha mengine. Mimi S. M. “Mh!” Nilijikuta nimeguna mwenyewe na kujiuliza kuhusu huyo S.M ni nani! Na kikaratasi kimeingiaje chumbani kwani mlango nilifunga. Nilipiga magoti, nikainua mikono juu nikimwomba Mungu anikimbizie mbali balaa lile. Lakini pia nilimwambia Mungu anijulishe huyo S. M ni nani. Sikuwaambia masista wenzangu kuhusu tukio hilo, niliamua kulifanya siri. Usiku wa siku hiyo niliwahi kupanda kitandani kulala, mwili haukuwa sawa kabisa. Kwanza nikiwa kitandani nilijisikia joto kali japokuwa mazingira ya mkoa wenyewe ni baridi na ulikuwa msimu wake, Julai.
Ghafla nilipitiwa na usingizi, kufumba na kufumbua bibi akasimama mbele yangu akiwa hana nguo hata moja! “Ha! Bibi, umepajuaje hapa nilipo?” Bibi alicheka kama vile aliyekuwa akisema moyoni kwamba kupajua pale halikuwa suala lenye utata kwake. Hakunijibu badala yake alininyooshea mkono kwa ishara kwamba niamke kitandani. Kabla sijaamka nilimwamkia shikamoo lakini bibi akatingisha kichwa kukataa shikamoo yangu.
Itaendelea
Labels:
HABARI & UDAKU,
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment