Pages

Subscribe:

Wednesday, October 26, 2016

STORY: NILIACHA USISTER NIKAWA MCHAWI 04

Image result for SISTER AT THE CHURCH
ILIPO ISHIA:Nilianza kugundua ni kwa nini mama hupenda kwenda Kabuku na kupata jibu kwamba, kumbe kila anapokwenda ndiyo hupata nafasi ya kushiriki mambo na wachawi wenzake. “Wewe si nimekuuliza?” yule mwanamke alisema kwa ukali zaidi. SASA ENDELEA… 

“Ndiyo.” “Sasa mbona hujibu neno?” “Siko tayari.” Nilisikia kicheko kutoka kwa wachawi wengine ambacho sikukijua kilihusu kufurahia kukataa kwangu kutokuwa tayari au la! Ghafla nilishtuka na kujikuta niko chumbani, tena...
kitandani nimekaa. Jasho jembamba lilikuwa likinitoka huku nikihema kwa kasi. Nilikiangalia chumba chote kama ningemwona mama au bibi lakini hakukuwa na mtu. 

Nilianza kuwaza je, kilichonitokea dakika chache nyuma kilikuwa na ukweli au ndoto? Nikiwa nawaza hivyo, nilijiangalia na kubaini kwamba, sehemu kubwa ya mwili nilichafuka tena viungo vilikuwa na maumivu. Hapo ndipo nilipojua kuwa kumbe nilikuwa kwenye tukio la ukweli kabisa. Mfano, sehemu ya uso nilisikia maumivu na nilipojishika nikabaini nilichubuka. Kitendo hicho kiliumiza sana akili yangu. Nilichukua simu, nikaanza kujiuliza nimpigie baba kumsimulia yaliyonipata au nipambane mwenyewe nione mwisho wake? Jibu nililipata kwamba nitampigia kesho. Niliamka na kwenda bafuni kuoga. 

Mwili ulikuwa umechoka kama niliyetoka kulima shamba kwa jembe la mkono. **** Asubuhi niliamka nikiwa bado nimechoka sana. Kila nilipofikiria matukio ya siku iliyopita niliumia moyoni. Wenzangu waliniuliza kuhusu alama ye jeraha usoni nikawadanganya kwa kuwaambia kwamba nilijigonga usiku kwenye kitasa, wakanipa pole. 

Sikuwa na wazo la kumpigia simu baba, lakini nilishangaa yeye ndiye akanipigia: “Hujambo mwanangu?” “Sijambo baba, shikamoo na habari za huko nyumbani?” “Huku salama. Unaendeleaje wewe?” “Naendelea vizuri. Hajambo mama?” “Mama yako alikwenda Kabuku toka juzi.” “He! Hajarudi?” Niliposema ‘he hajarudi?’, palepale nikamwona bibi kasimama kwenye jiwe moja huku akinionesha mkono wa onyo kama ambaye hakupenda mazungumzo yangu na baba. 

Nilikimbiza mazungumzo hayo nikamuuliza kuhusu hali ya afya ya majirani zetu kule Tanga ambapo baba alisema wote wazima, ila kuna mtoto wa mzee mmoja anaitwa Nasibu Muree aliungua moto yuko Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo. Nilipomaliza kuagana na baba, niliambiwa kuna mgeni wangu. Kabla sijaenda niliuliza anakotokea mgeni huyo na jina lake. Nikaambiwa anaitwa Elizabeth. Elizabeth ninayemjua mimi ni mama yangu mzazi, sasa ni yeye kweli? Nilitembea haraka kuelekea kwa wanapofikia wageni, nikaulizia aliko huyo Elizabeth, kila mtu akaniambia alisimama hapa, mara alisimama kule. 

Hakuna aliyekuwa amejua vizuri alikoelekea. Niliuliza swali lingine. Je, mtu huyo yukoje kwa maana ya mtazamo. “Ni mwanamke mtu mzima. Mweupe kama wewe, kwenye pua upande wa kulia ana kidoti cheusi, anasema anatokea Tanga. Alisema mnafahamiana,” mtu mmoja alinijibu hivyo, nikashtuka kwa vile alama zote alizozisema ni za mama. Niliamua kurudi ndani ili nikaendelee na shughuli zangu kwani sikuwa tayari kuanza kupoteza muda kwa kujiuliza mambo ambayo hayakuwa ndani ya uwezo wangu. 

Kabla sijafika niliitwa tena: “Wewe Bena, karudi anakuita tena, kumbe alikwenda kutafuta kitambaa.” Nilirudi mbio, lakini ile nafika tu eti nikaambiwa kwamba, amezunguka nyuma ambako kuna ukuta, sasa amezungukaje? “Jamani sitarudi tena. Tena nasema huyo akija mkamateni ni mwanga.” “Bena mimi ni mwanga? Asante sana mwanangu.” Ni mama alisimama mbele yangu na kuniuliza huku akiwa amejishika kiuno. Nilishtuka na kusema: “Haa! Mama.” Akapotea na watu wakaniuliza mama yako yuko wapi? Sikuwa na jibu. 

Nilibaki nikitetemeka, mwili uliisha nguvu, nikaanguka. Nilipokuja kupata fahamu nilikuwa chumbani kwangu, wenzangu walinizunguka huku wakinipepea ili nipate hewa safi. Niliangaza kulia na kushoto nikiamini nitamwona mama lakini hakuwepo. “Jamani pole sana Benadeta, pole sana Bena,” wenzangu waliniambia. Niliwauliza nini kilinipata wakasema nilianguka ghafla baada ya kumwona mama yangu kwenye maono. “Nilimwona mama kwenye maono?” niliuliza kwa sauti ya juu kidogo nikishangaa. 

“Ilikuwa ni maono Bena kwa sababu hakuna mwingine aliyemwona zaidi yako.” “Si maono.” “Sasa ni nini Bena?” “Ule ni ushetani tena ni ushetani wa hali ya juu.” Niliwaambia alichoniambia mama baada ya kunitokea pale na ilivyokuwa usiku uliopita, walishtuka sana. Walianza kuomba huku wakilia kwamba kumbe niko katikati ya mateso mazito. Waliomba sana, ikafika mahali mmoja wao akasema jamani tunyamaze, wote wakanyamaza, kisha akauliza kama kuna mmoja wao anajua kukemea kwa jina la Yesu. 

Hapa naomba nifafanue kidogo, kukemea alikosema yule sista ni kama vile wanavyofanya walokole wakisema kwa jina la Yesu pepo toka kwa jina la Yesu nakuamuru pepo toka. “Mimi hapa naweza, nilishatoa mapepo sana,” alijibu sista mwingine ambaye alionekana ana ujasiri mpaka kusema vile. “Tunaomba ukemee tafadhali,” alisema sista aliyeomba huduma ya kukemea.

0 comments:

Post a Comment