Pages

Subscribe:

Saturday, October 15, 2016

STORY: NILIACHA USISTER NIKAWA MCHAWI 01

Image result for SISTER AT THE CHURCH
“Si jambo la kawaida kutokea, lakini nadhani asili ya mama yangu ilichangia sana kwani kidogodogo nilianza kushawishika na kuamini kwamba nitaingia kwenye shughuli yenye mamlaka kuu kuliko ya kumtumikia Mungu. “Kifupi naitwa Benadeta au Bena kama ambavyo nyumbani walizoea kuniita. Ni mtoto wa kwanza kuzaliwa kwenye familia yenye watoto kumi na mmoja.

“Nilizaliwa mwaka 1969, Mjesani, Tanga. Baba yangu alikuwa akifanya kazi Mamlaka ya Bandari Tanzania kituo cha Tanga. Mama alikuwa wa nyumbani, lakini mara nyingi alikuwa akisafiri kwenda kwa mama yake, Kabuku,” ndivyo alivyoanza...
kusimulia Bena.

 Anaendelea… Nilipomaliza elimu yangu ya kidato cha nne, baba aliniuliza nataka kufanya nini? Nikamjibu utawa (usista) ndiyo kitu kilichomo ndani ya moyo wangu. Alishtuka sana kwani mimi ndiyo nilikuwa mtoto wake wa kwanza, sasa aliamini baada ya masomo ningeanza kufanya kazi na kuisaidia familia lakini maneno yangu yakawa siyo. “Bena una maana unataka kuwa upande wa kufanya kazi za Mungu?” aliniuliza baba nikamjibu haswa. Alikaa kimya kwa muda akionesha kutafakari, lakini mwisho akasema atanipa jibu jioni mama akiwepo. Siku hiyo mama alikwenda Kabuku kwa mama yake mzazi, yaani bibi yangu. 

Lakini palepale nikamuuliza baba ni kwa nini mama amekuwa na safari za Kabuku kila mara? Akajibu si kwa mama yake! Nilimwambia hata kama ni kwa mama yake lakini si kwenda kila wakati. Yeye kwa wiki alikuwa anakwenda Kabuku mara nne. Nilikwenda chumbani kwangu. Ile nafika tu, nilishtuka. Nilihisi kama nimemwona bibi kitandani akiniangalia kwa uso wa hasira. Nilitoka mbio huku nikipiga kelele, baba akasikia maana na yeye alikwenda chumbani kwake, akaja sebuleni huku akiniuliza kuna nini. “Nimemwona bibi.” “Wapi?” “Kitandani baba.

” Baba alinipita kwa kasi mpaka chumbani kwangu, lakini alipotoka akaniuliza: “Mbona sijamuona? We ulimuona akifanya nini?” “Amekaa kitandani.” “Ulisalimiana naye?” “Jamani baba, nitasalimiana na bibi wakati sikumwona akiingia, si yupo Kabuku!” Naamini baba alihisi swali lake kwangu limejikanganya, akanyamaza lakini akisema kuwa hajamuona, huenda ni mawazo yangu kwa sababu tulitoka kumzungumzia muda mfupi uliopita.” Basi, muda ulikwenda huku nikiwa namsubiri mama kwa shauku ili nimsikie baba angenijibu nini kuhusu mtazamo wangu wa kufanya shughuli ya kumtumikia Mungu.

Ilikuwa saa kumi na mbili na nusu jioni, mlango mkubwa ulisukumwa, akaingia mama, nyuma yake alifuatia bibi, nikashtuka na kukimbilia chumbani kwangu. Mama akaja mbio mpaka chumbani na kuniambia: “Hiyo tabia yako ni mbaya sana Bena. Wewe hutakiwi kuuliza maswali mengi. Mimi ni mama yako, yule ni bibi yako. Hata wewe unapaswa kujua mimi naendeleaje?” Sikumwelewa kabisa mama kwamba alikuwa na maana gani kusema vile. Kila nilipojaribu kukumbuka maneno yake yanaunga kutoka wapi, sikupata jibu lolote. 

“Baba yako yuko wapi?” aliniuliza mama, nikamjibu sifahamu lakini hakutoka muda mrefu sana. Mama akafungua mlango na kutoka chumbani, nikabaki peke yangu. Swali kubwa akilini mwangu ni je mimi na mama kuna ugomvi gani ulitokea? “We Bena,” mama aliita kwa sauti ya juu akiwa jikoni. “Abee.” “Njoo haraka sana.” Nilikwenda jikoni. Nilimkuta mama amekaa na bibi. Walikuwa wakikata nyama, bibi ameshika kama anakata. “Shikamoo bibi,” nilimsalimia huku nikifanya ishara ya kupiga magoti.

 Bibi hakuitika wala hakuniangalia, alikaza macho kwenye nyama inayokatwa. “Nenda kachote mchele uchambue,” mama aliniambia. Kusema ule ukweli nilijisikia vibaya sana moyoni kwani nilivyojua mimi, mama aliniita ili nimsalimie bibi lakini badala yake kumbe aliniita ili anitume na bibi alivyokaa kimya bila kuitika nikajua yeye angesema chochote. Nilitoka kwenda kuchota mchele, kwenye korido nikapishana na baba akiingia. 

“Mama amerudi?” “Ndiyo baba, tena amerudi na bibi.” Niliuona uso wa baba kama umeshtuka. Lakini sikujua alishtuka kwa kitendo cha bibi kuja au kulikuwa na lingine. Akapitiliza kwenda hadi jikoni ambako walikuwepo mama na bibi. Saa tatu na nusu usiku, nakumbuka nilikuwa chumbani kwangu nataka kulala, mama aliniita. Nikatoka, nikamkuta amesimama. “Baba yako anakuita.”

 Tuliongozana na mama hadi sebuleni ambako nilimkuta baba amekaa. “Bena,” baba aliita nikiwa nakaa. “Abee baba.” “Nimeongea na mama yako kuhusu ule mpango wako, kimsingi hata yeye amekubali kwamba ukawe sista.” Kabla sijasema asante, nilimsikia bibi chumbani aliko akicheka sana. Mama, baba wakashtuka.

0 comments:

Post a Comment