Thursday, October 20, 2016
STORY: NILIACHA USISTER NIKAWA MCHAWI 03
ILIPO ISHIA: Bibi alicheka kama vile aliyekuwa akisema moyoni kwamba kupajua pale hapakuwa suala lenye utata kwake. Hakunijibu badala yake alininyooshea mkono kwa ishara kwamba niamke kitandani. Kabla sijaamka nilimwamkia shikamoo, lakini bibi akatingisha kichwa kukataa shikamoo yangu SASA ENDELEA…
“Bibi umekuja kwa wema au ubaya?” nilimuuliza, nikamwona anabadilika sura ghafla, meno yakawa marefu kama vijiko, macho yakatoka kwa usawa wa kikombe cha kahawa, midomo ikapanuka na kuwa kama...
bakuli ndogo. Sasa bibi akawa ananifuata pale kitandani huku akiwa ameinua mikono. Nilipiga kalele kwa kusema: “Bibi unaniua.” Ghafla nikashtuka na kukaa kitandani.
Cha ajabu jasho jembamba lilinitoka, moyo ulinienda mbio mpaka nikajishika kifuani kama kujipima. “Hii ni nini? Kwa nini nimemuona bibi katika hali ile?” nilijiuliza mwenyewe lakini sikupata jibu. Nikiwa bado nimekaa nikasali sala ya Bikira Maria. Nilipofika sehemu ya kusema ‘Maria Mtakatifu Mama wa Mungu’ mlango wangu ukagongwa. Niliacha kusali, nikatoka kitandani kwenda kufungua mlango. Sikumwona mtu wala sikusikia ishara ya mtu kutembea kutoka katika eneo hilo.
Nilirudi ndani, moyoni nilidhamiria kwamba, kama mlango utagongwa tena sitashuka kitandani kufungua. Sikupata usingizi, nilibaki natafakari maana ya ile ndoto ya kumwona bibi. Nilijipa moyo kwamba huenda ni ndoto tu kwa sababu ya kazi nilizofanya siku hiyo kama Biblia inavyosema ‘ndoto huja baada ya shughuli nyingi’. Niliutafuta usingizi kwa nguvu zangu zote lakini wapi, sikuupata. Ilifika mahali niliamua kukaa kitandani nikiwa nimeegemea ukuta, lakini ghafla nikashikwa na usingizi wa kulazimishwa na nguvu nyingine si yangu, nikaangukia kitandani puu! Nilijikuta nikielea kwenye shimo refu sana kwa kwenda chini.
Nilikuwa nikishuka polepole wakati mwingine kwa kasi hadi nikafika mwisho na kuanguka. Nilimwona tena bibi. Safari hii alikuwa kwenye kundi la watu wa ajabu. Watu hao walikuwa wanawake kwa wanaume, wote walivaa viguo vilivyositiri sehemu za siri tu. Wanawake walishindwa hata kujiziba kwenye matiti. Mimi nilikuwa katikati, wao walinizunguka wakicheza ngoma ambayo mpigaji wake sikuweza kumwona. Ngoma hiyo ilichezwa kwa dakika kama saba, ikasimama.
Mwanamke mmoja, mweusi wa kutengeneza, nadhani alijipaka masizi usoni, ndiye aliyefungua kinywa na kusema: “Bibi Adam, huyu ndiye maana mara mbili nzima umetuletea mtu ambaye siye.” “Huyo ndiyo mwenyewe, lakini siku hizi eti na yeye anajifanya ni mtu wa Mungu,” alisema bibi. Wakati huo nilikuwa najaribu kumwangalia kila mtu aliyekuwa pale, sikumfahamu hata mmoja lakini kwa vile ilikuwa usiku na pia eneo lenyewe lilikuwa na vumbi kwa sababu ya kule kucheza ngoma. “Anamjua Mungu kweli, Mungu gani?” aliuliza yule mwanamke. “Muulize mwenyewe,” alijibu bibi.
Ni kweli bibi mtaani kwake pale Kabuku alikuwa akijulikana kwa jina la bibi Adam. “Wewe binti wewe. Unajua ni mtoto sana kumjua Mungu, Mungu yupi kwanza?” yule mwanamke aliniuliza. “Mungu aliyeumba mbingu na nchi.” Watu wote wakacheka maana wakati naulizwa walikaa kimya kusikiliza majibu yangu. Mwanamke mwingine alichomoka kutoka aliposimama na kuja mbio kwangu huku akisema: “Ndiyo maana nilisema kuna mwanangu amepotea, ndiyo huyu sasa. Anaitwa Benadeta.” Nilishtuka sana kwani mwanamke mwenyewe alikuwa mama yangu mzazi, mama Bena. Mtaani aliitwa hivyo kwa kufupisha jina langu. “Ha! Mama, ni wewe? Hata wewe unaungana na bibi?” nilimuuliza, lakini mama akasonya msonyo mrefu sana kama wa sekunde kumi nzima tena uliokuwa ukisikika kwa nguvu.
Akaondoka kurudi alikosimama huku akiniangalia kwa macho ya dharau. “Ina maana hapa nipo na wachawi?” “Ina maana mama ni mchawi?” “Bibi naye ni mchawi?” Nilivuta picha na kukumbuka mazingira fulani ya nyuma kule nyumbani kwamba siku moja nikiwa na baba nilimuuliza ni kwa nini mama anapenda kila mara kwenda Kabuku kwa bibi, matokeo yake nilipokwenda chumbani niliona taswira ya bibi kitandani kwangu. Nakumbuka nilipomweleza baba alisema ni mawazo yangu tu lakini si kweli kwamba niliona taswira ya bibi.
Lakini pia nikakumbuka siku baba aliponiita sebuleni akiwa na mama na kuniambia wamezungumza wamekubaliana mimi nikasomee usista, kabla sijasema asante bibi alicheka sana chumbani mpaka mama akaenda. Si hayo tu, nilikumbuka pia jinsi mama alivyoonesha kunichukua siku hiyo bibi akiwa nyumbani tena nikiwa sijafanya kosa lolote. Picha iliyonijia ni kwamba, bibi kweli ni mchawi, mama pia. Na uchawi wao ni wa kiwango cha juu. Wanaweza kujua nini kinaendelea mtu alipo hata kama ni mbali. Nisingeiona taswira ya bibi chumbani kwangu kama nisingemuuliza baba swali lile la kwa nini mama anakwenda Kabuku kila mara.
Pia, niliuona uwezo wao wa kichawi ni mkubwa kwa vile bibi alivyonitokea chumbani wakati hajawahi kufika hata mara moja. “Sasa sisi tumekuita hapa tunataka kukupa uwezo wa kushiriki kazi za huyo Mungu. Kama utakubali utashangaa mwenyewe, utakuwa mkubwa kuliko wenzako, utamudu kufanya miujiza kuliko padri wako, waumini watakupenda sana,” alisema yule mwanamke, akaniuliza kama niko tayari kwa hilo au la! Nilibaki nimewatumbulia macho kwa zamu, yule mwanamke aliyesimama jirani yangu na wale wengine waliokuwa mbali, akiwemo mama.
“Benadeta,” mama aliniita kwa sauti ya juu. “Abe mama.” “Si unaulizwa wewe, uko tayari au hauko tayari, unachotakiwa ni kutoa jibu moja tu tena bila maelezo.” Badala ya kuwaza kutoa jibu niliwaza kitu kingine, kwamba muda ule mama kama alikuwa pale, baba alikuwa na nani nyumbani! Au mama aliaga anakwenda Kabuku kwa mama yake? Nikaanza kugundua ni kwa nini anapenda kwenda Kabuku na kupata jibu kwamba, huenda kila anapokwenda Kabuku, ndiyo wanapata nafasi ya kushiriki mambo na wachawi wenzao. “Wewe si nimekuuliza?” yule mwanamke alisema kwa ukali zaidi.
Labels:
HABARI & UDAKU,
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment