Sunday, October 30, 2016
STORY: NILIACHA USISTER NIKAWA MCHAWI 6-7
ILIPO ISHIA: “Baba yako alianguka chooni, akatokwa mapovu kinywani, alipokimbizwa hospitali akaaga dunia kabla hata ya huduma, nimeshangaa sana. Muombee baba yako, kuna mkono wa mtu na huyo mtu mwenyewe atajulikana siku si nyingi.” “Eti mama ni kweli?” SASA ENDELEA…
Mama alibaki kimya, machozi yakimchuruzika. Nilihisi uchungu ambao sikuwahi kuupata tangu kuzaliwa. Nilimkazia macho mabaya mama. Kama angekuwa na rika langu ningemvaa mpaka chini. Niliwaza niondoke bila kumaliza msiba, lakini...
moyo mwingine ulikataa ukisema kwamba aliyekufa ni baba, mama hata kama hakutaka kunipa taarifa mapema lakini marehemu hahusiki.
Siku nne zilikatika, watu walishaondoka nyumbani kwenye msiba na tulibaki ndugu tu. Mimi, mama, wadogo zangu wawili, shangazi, baba mdogo, kaka zangu watatu wa baba mdogo, mjomba na mke wake, mdogo wake bibi anayeishi Segera, ndugu wengine na bibi ambaye nilimwona kama ndiye aliyemuua baba yangu. Kwa mila na desturi za kabila letu, tulikuwa tukilala chini kwa muda wote huo na kikomo kilitakiwa kuwa siku arobaini zikigota. Mimi nilikuwa nikilala sehemu ambayo kwa kulia kwangu alikuwa shangazi, kushoto kwangu ukuta, miguuni alilala bibi na wengine ambao ni ndugu.
asa kwa mila hizohizo za kuachana na kulala chini kwa siku arobaini ni kwamba, kama mtu anafanya kazi anaruhusiwa kwenda kazini, anaruhusiwa kuoga na kubadili nguo. Kama anaishi mbali na eneo la msiba na alipata ruhusa ya siku chache anaruhusiwa kuondoka na anakokwenda anaweza kulala kitandani kwa sababu hatakuwepo eneo la msiba. Usiku wa manane mmoja nilishtuka kutoka usingizini lakini sikuinuka, nilifumbua macho tu.
Ghafla nikamwona mama amesimama katika mlango mkubwa wa kutokea nje. Kwanza nilishangaa sana kwani alikuwa amevaa nguo nyeusi, huku sehemu za Pwani wanaita kaniki. Alijifunga kwa kuikatisha kwenye matiti. Nilijua pale mama alikuwa akiwanga kwa hiyo nilichofanya ni kukaa kimya kama sijaamka ili nione mwisho wake. Mara nikamwona na bibi naye akiamka. Lakini kwenye uamkaji wa bibi nilishangaa kwani nilimwona akiinuka huku akiendelea kubaki pale chini kwenye mkeka.
Bibi alifika mahali akasimama kabisa, lakini pale chini aliendelea kuwepo tena akiwa amelala. Alitembea hadi mlangoni kwa mama. Wakasimama sambamba wakiangalia mlango, mara wakageuka. Mama akaanza kutembea kwa kuinua mguu mmoja juu sana kisha unapotua ndiyo anainua mwingine, alitembea kwa mwendo wa kinyonga hadi tulipokuwa tumelala wengine. Alisimama jirani na mdogo wangu mmoja, akamwinamia na kuganda kwa dakika kama tatu hivi alipoinuka, alimpelekea mikono yule mdogo wangu kisha akaanza kuinuka mpaka akasimama. Alimchukua mpaka kwa bibi.
Halafu ikawa zamu ya bibi sasa, naye akatembea kama vilevile alivyokuwa akitembea mama, akaja mpaka katikati ya tulipolala. Hapo naomba ieleweke kwamba, wanaume walikuwa wamelala nje, wanawake tulilala sebuleni. Mpango ni kwamba, baada ya ndugu kupungua, wanaume watahamia sebuleni kulala, wanawake chumbani. Basi, bibi alikuwa amesimama katikati, pembeni yake kwa kulia alilala mdogo wake, kushoto alilala ndugu mwingine simkumbuki. Akamwinamia mdogo wake na akamfanyia kama vile mama alivyomfanyia mdogo wangu.
Bibi mdogo aliamka polepole mpaka akasimama. Naye akaanza kutembea na bibi mkubwa huyo ambaye ni mchawi mpaka mlangoni, bibi mdogo akaunganishwa na mdogo wangu. Baada ya hapo, bibi na mama waliwageuza wale wawili na kuwasukuma lakini si kwa kutumia nguvu sana. Nilishangaa sana kwani ilitokea elimu ambayo sikuwahi kuipata kabla ya siku hiyo. Kwani, baada tu ya kusukumwa, niliwaona wale waliosukumwa wakienda kwenye vyombo wakachukua ndoo za maji, wakafungua mlango wa uani, wakatoka.
Baada ya dakika tano walirejea wakiwa na maji kichwani, wakaingiza kwenye pipa wakatoka tena, baada ya muda walirudi na maji. Walifanya hivyo mpaka pipa likajaa. Hapo mama na bibi walikuwa wamesimama mlangoni huku wakionesha dalili ya kupuliza ndani ya sebule. Baada ya pipa kujaa, bibi alimpiga kofi mdogo wangu mama akampiga bibi mdogo, wote wakarudi kulala katika sehemu zao na wao pia wakarudi kulala. Kuna kitu nilikumbuka, jana yake asubuhi tulipoamka kuna mwanamke aliuliza maji ya kwenye pipa yalijazwa saa ngapi kwa sababu usiku mpaka tunalala, pipa lilikuwa halina kitu.
Mama akamjibu mwanamke yule ambaye alikuja na shangazi kwamba, eti yeye alidamka mapema akajaza, akapongezwa kumbe uchawi mtupu. Nilijiuliza kama binadamu amefikia hatua ya kufanya mambo ya muujiza kama ule, kuamsha usingizini wengine nao wakawa hawajui kuwa wameamshwa na kufanya kazi tena nzito kama ile ya kuchota maji kwenye ndoo mpaka pipa kujaa, basi ni uwezo mkubwa sana.
Sasa, nikawa najiuliza wale waliolala walilala kweli au uwezo wa dawa za kichawi? Niliamini ni dawa za kichawi na kwamba hazikunipata mimi kwa sababu namwogopa Mungu muda wote na namtumikia pia. Nje bado kulikuwa na gizagiza, haikuwa rahisi kujua ni muda gani labda kwa saa. Sikuwa na uwezo wa kuangalia saa kwani nilijua kitendo chochote kile cha kusimama kingewashtua wale wachawi wangu.
Labels:
HABARI & UDAKU,
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment