MAKAMPUNI 15 yaliyokwepa kodi baada ya kutorosha makontena
yao, yamejisalimisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini
yameshindwa kulipa kodi ndani ya siku saba za msamaha wa Rais John
Magufuli.
Kodi inayodaiwa kwa kampuni hizo ni Sh bilioni 3.75, hivyo
watachukuliwa hatua za kisheria kwa kukwepa kulipa kodi, ikiwa ni pamoja
na kufikishwa mahakamani.
Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA, Dk Philip Mpango alisema hayo
jana wakati akielezea makusanyo ya kodi ya makontena yaliyoondolewa
katika bandari kavu ya Azam, kinyume cha sheria pamoja na...
kumalizika kwa
siku saba alizotoa Rais Magufuli kwa wafanyabiashara hao kulipa kodi
waliyokwepa, bila kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria.
Dk Mpango alisema siku hizo saba zimefikia kikomo juzi,
hivyo hatua kali za kisheria kwa wafanyabiashara ambao hawakulipa kodi
katika kipindi hicho zinafuata hivyo wasubiri cha moto.
“Tumewasihi waje kulipa kwani huruma ya Rais sasa
imeisha... tulifanya uhakiki na kuthibitisha kuwa kampuni hizo zipo.
Wamekuja kulalamika lakini hakika hakuna atakayesamehewa kulipa na sasa
tunafuata mkondo wa sheria ili kuwafikisha mahakamani,” alisisitiza.
Wadaiwa
Alitaja kampuni hizo kuwa ni Ahmed Saleh Tawred anayedaiwa
Sh milioni 59.23; Cla Tokyo Limited Sh milioni 77.52; Farida Abdullah
Salem Sh milioni 75.33 na Juma Kassem Abdul Sh milioni 190.18.
Wengine ni Libas Fashion Sh milioni 52.94; Rushy Wheel Tyre
Center Co Ltd, Sh bilioni 1.8; Said Ahmad Hamdan Sh milioni 68.36; Said
Ahmed Said Sh milioni 68.73 na Salum Continental Co Ltd Sh milioni
151.17.
Pia yumo Salum Link Tyres Sh milioni 343.44; Simbo Yonah
Kimaro, Sh milioni 69.22; Snow Leopard Building Material Co Ltd Sh
milioni 93.97; Swaleh Mohamed Swaleh Sh milioni 34.68; Tybat Trading Co
Limited, Sh milioni 598.69 na Nasir Saleh Mazrui Sh milioni 70.10.
Alisema mpaka kufikia jana TRA walikuwa wamekusanya Sh
bilioni 10,643.004,948.46 kutoka kwa kampuni 28 ambapo kampuni 13
zimelipa kodi yote iliyokadiriwa, ambayo ni Sh 4,167,130,173.89 na Sh
2,303,637,554.57 kutoka kampuni 15 zilizolipa sehemu ya kodi
iliyokadiriwa.
Dk Mpango alisema Sh bilioni 4.17 zimelipwa na kampuni ya
Azam ICD, ikiwa ni dhamana ya kodi iliyokwepwa, hivyo atatakiwa kumaliza
kulipa kodi yote inayodaiwa kwa mujibu wa nafasi yake kama mwenye
dhamana.
Alisema wakati utekelezaji huo ukiendelea, ili kurahisisha
ukusanyaji wa kodi hiyo ya makontena yaliyoondolewa bandarini kinyume
cha sheria na taratibu za forodha, TRA imefungua akaunti maalumu katika
Benki Kuu yenye namba 9921169785 inayoitwa Commissioner for Customs and
Excise – Container Account.
Kwa mujibu wa Dk Mpango, mpaka sasa watumishi 36 wa TRA
wanaotuhumiwa kushiriki katika upotevu wa kodi kutokana na makontena
hayo kuondoshwa bandarini.
Watumishi wachongewa
Aidha, alisema TRA imepata taarifa zisizopungua 15 kutoka
kwa wananchi kuhusu mali za kifisadi na mwenendo mbaya wa baadhi ya
watumishi na walipakodi wanaokwepa kodi.
Aliwashukuru wananchi waliotoa taarifa na kuwaomba wengine
wajitokeze kutoa taarifa zaidi na mamlaka hiyo inawahakikishia kuwa
itawalinda.
Dk Mpango alisema wanaendelea kutekeleza maagizo ya Rais
katika ukusanyaji wa mapato, ikiwa ni pamoja na kupiga picha makontena
yote badala ya sampuli ya kontena ilivyo sasa na wanafanya utaratibu wa
kupata mashine za kupiga picha za nyongeza.
0 comments:
Post a Comment