Pages

Subscribe:

Wednesday, June 1, 2016

HADITHI: NYUMA YA MACHOZI 02

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Deusi aliipokea glasi na kuyanywa maji yote kwa mkupuo kisha aliiweka glasi juu ya meza. “Deusi.”
“Naam mkuu.”
“Kwanza pole sana.”
“Sijapoa mkuu.” “Kuna siri gani kati yako na mkeo?”
SASA ENDELEA...

“Kwa kweli sijui hata kitu kimoja, ni mwezi wa pili sasa, mke wangu ameujeruhi moyo wangu kwa kukosa uaminifu wa kubeba ujauzito usio kuwa wangu.”
“Mkeo ulimuoa kwa mapenzi yake au kwa kulazimishwa?” “Kwa kweli mke wangu nilichaguliwa na...

wazazi wangu nilipokwenda kijijini kuwatembelea. Mwanzo wa ndoa yetu alionesha mapenzi ya dhati kumbe nilikuwa nafuga nyoka, amekua sasa amenimeza. ” “Na Kinape ni nani?”
“Kinape alikuwa zaidi ya rafiki, tumesoma na kucheza pamoja kabla ya mimi kuendelea na masomo mpaka kupata kazi katika kitengo cha kuzuia dawa za kulevya.” “Na alifikaje kwako?”
“Ni historia ndefu”
******
Miaka minane iliyopita Deusi King’ole baada ya kuanza kazi kama mkuu wa kitengo cha kuzuia madawa ya kulevya. Miaka mitatu katika kazi yake alipata likizo iliyomfanya aende kijijini kwa wazazi wake. Katika watu wa karibu baada ya wazazi wake, walikuwa wazazi wa Kinape ambaye toka wakiwa shule ya msingi waliitwa pacha kutokana na ukaribu wao. Deus baada ya kufika kijijini na kupokewa na ndugu na jamaa ambao walimshangaa kumuona amerudi katika gari la kifahari, wengi walizoea kuliona gari kama lile kwa mbunge wao tu, alipokwenda kujijini kuwatembelea wapiga kura wake. Ilikuwa ni furaha hasa kwa wazazi wake ambao waliamini kazi ya kumsomesha mtoto wao ilikuwa imezaa matunda. Kitu kikubwa alichowaahidi wazazi wake kuhakikisha anayabadili maisha ya familia yake ikiwa pamoja na kuwajengea nyumba ya kisasa na kuwachimbia kisima cha maji. Baada ya kutulia alitaka kujua habari za rafiki yake Kinape.
“Jamani Kinape yupo?”
“Mmh! Nina siku sijamtia machoni,” mama Deusi alijibu.
“Nasikia sijui alikwenda mjini kutafuta kazi,” mdogo wake alisema.
“Sasa wewe mjini huko hukumuona?” Mzee King’ole aliuliza. “Baba mji ni mkubwa, mnaweza kukaa miaka kumi bila kuonana na mtu pengine mnakaa kitongoji kimoja.”
“Labda siku hizi, siku za nyuma watu tulikuwa tunajuana hata wageni walipoingia tuliwatambua.”
“Ni wakati huo baba, sasa hivi mji umepanuka.”
“Basi atakuwa hukohuko mjini.”
“Na yeye atarudi na gari?” Mdogo wake aliuliza.
“Siwezi kujua,” Deus alijibu kwa mkato.
“Lakini mzee Solomoni na mkewe si wapo?” Deus aliuliza.
“Wapo, waende wapi,” mzee King’ole alijibu.
“Basi ngoja nikawaone kabla ya kujipumzisha.”
“Haya baba,” mama Deus alijibu. Deus alinyanyuka ili aelekee kwa mzee Solomoni. “Kaka twende wote,” mdogo wake wa kike aliyekuwa anasoma kidato cha kwanza aliomba kuongozana na kaka yake.
“Hakuna tatizo,” alijibu huku akimshika mkono. Walikwenda hadi kwa mzee Solomoni, alimkuta mama Kinape akisuka ukiri. “Hodi hapa.”
“Karibu,” alijibu huku akiacha kusuka na kumtazama mgeni aliyekuwa amesimama mbele yake. “Shikamoo mama.” “Marahaba, karibu.”
“Asante.”
“Ndiyo baba,” ilionesha mama Kinape kamsahau Deus. “Mama unamjua huyu?” Salome mdogo wa Deus alimuuliza mama Kinape.
“Hata,” alijibu huku akijitahidi kumkazia macho.
“Si kaka Deusi huyu.”
“Deusi wa mjini?”
“Ndiyo.”
“Jamani, mwanangu mwenyewe nimemsahau, karibu baba tusameheane, macho ya uzee haya.”
“Kawaida, mama za hapa?”
“Hebu ngoja kwanza, Salome kamletee kiti kaka yako.” Salome alikwenda ndani na kurudi na kiti cha kukunja, alikiweka pembeni ya mama Kinape.
“Wee, Salome kiweke mbele nimuone vizuri,” Salome alifanya kama alivyo agizwa. Baada ya kukaa alianza kuzungumza: “Ndiyo, mama za siku?”
“Mmh! Hivyo hivyo tu baba, kila kukicha afadhari ya jana.”
“Ni kweli sasa hivi nasikia hata mvua zimegoma.”
“Kama unavyoona.”
“Baba yupo wapi?”
“Ametoka kidogo, ila achelewi, unavyomtaja pengine yupo njiani anarudi.”
“Na ndugu yangu?”
“Kinape?”
“Eeeh.”
“Mmh! Kakimbilia mjini.”
“Kufanya nini?”
“Mwanangu kwani wewe mjini unafanya nini?”
“Mimi nafanya kazi serikalini kutokana na elimu yangu.”
“Kwa kweli hatujui mjini anafanya kazi gani.”
“Anakaa wapi ili nikifika nimtafute?”
“Hatujajua ila yeye kasema atalala popote hata sokoni.”
“Mmh! Haya.”
“Vipi umeoa?”
“Bado.”
“Unasubiri nini?”
“Nilikuwa najipanga.”
“Deus wazazi wenu lini tutacheza na wajukuu?”
“Nina imani sasa hivi nitafuta machozi yenu.”
“Fanya hivyo, usiwe kama mwenzako kila siku kesi za watoto wa watu.”
“Sasa mama, wacha nikapumzike ndiyo nimefika nahitaji kupumzika.” “Hakuna tatizo, tuachie basi hata fedha ya unga.” Deus aliingiza mkono mfukoni na kutoa noti moja ya shilingi elfu kumi na kumkabidhi. Kabla hajaipokea alitokea mzee Solomoni na kusema: “Mheshimiwa nami usinisahau.”
“Aah, baba.” Deus alisema huku akimgeukia mzee Solomoni, Mzee Solomoni alishtuka kumuona Deus.
“Ha! Ni wewe Deus?”
“Ni mimi baba.”
“Umefika lini?”
“Leo.”
“Na lile gari la mbunge lililopaki kwenu?”
“Si gari la mbunge ni gari langu mwenyewe.”
“Ha! Ina maama na wewe siku hizi mbunge?”
“Hapana kuwa na gari kama lile halimaanishi mbunge, mtu yoyote anaweza kumiliki.”
“Kwa hiyo ni la kwako?”
“Ndiyo baba.”
“Hata hali yako inajionesha.”
“Kidogo kidogo.”
“Una habari gani?” Mzee Solomoni alisema huku akimtazama kwa makini Deus. “Nilikuja kuwajulia hali mara moja, ila nimesikitika kumkosa rafiki yangu kipenzi Kinape.”
“Yule rafiki yako mpumbavu, tena hana akili, amekimbia kilimo, ona jinsi tulivyochoka wazazi wake yeye anakimbilia mjini. Kibaya anapokwenda hana ndugu wala sehemu ya kufikia,” mzee Solomoni alisema kwa hasira.
“Lakini baba si kulalamika, ni kumuombea ili milango ya riziki ifunguke na kupata shughuli yoyote ya kumpatia kipato.”
“Kweli kabisa usemayo, kila siku baba yenu analalamika hajui kama ni laana kwa mtoto,” mama Kinape aliunga mkono.
“Wazazi wangu nakuahidini kitu kimoja, kwa vile mmesema yupo mjini nitamtafuta kila kona ili kuhakikisha nampata.”
“Litakuwa jambo la zuri.” Deus aliagana na wazazi wa Kinape ili arudi nyumbani, mzee Solomoni alikumbusha.
“Mwanangu na mimi mbona umenisahau?” Deus aliingiza mkono mfukoni na kutoa noti nyingine ya elfu kumi na kumkabidhi. “Asante sana mwanangu Mungu akizidishie.”
“Asante wazazi wangu, atuzidishie wote.” Deusi aliwaaga na kurudi nyumbani, njiani wakati wa kurudi walikutana na binti mmoja aliyekuwa amebeba chupa ya mafuta ya kula. “Shikamoo,” yule binti alimsabahi Deus.
“Marahaba.”
“Salome, mambo?”
“Poa, umemuona kaka yangu anayeishi mjini?”
“Kumbe ndiye huyu, shikamoo.”
“Jamani Kilole, mbona unataka kumchosha kaka yangu, shikamoo mara ngapi?”
“Jamani ya kwanza ya kutomjua, ya pili ya kumfahamu, kuna ubaya?”
“Hakuna ubaya, marahaba,” Deus aliitikia huku akitabasamu. “Karibu kwetu kaka.”
“Asante.”
“Haya nawahi nyumbani, Salome baadaye.”
“Haya.” Waliagana na Kilole kila mmoja aliendelea na safari yake, wakiwa wanarudi nyumbani Deus alijikuta akivutiwa na mchangamfu wa Kilole.
“Salome, Kilome mtoto wa nani?”
“Wa mzee Sikwera.”
“Mmh! Mbona huyu msichana simfahamu?”
“Kwani ulikuwa unapenda kutembea kijijini, mbona alikuwepo.” “Kumbe, rafiki yako?”
“Kiasi, vipi umemependa?”
“Basi tu kanivutia kwa uchangafu wake.”
“Hata mimi nampenda.”
“Ameolewa?”
“Mtu yupo kwao, atakuwa ameolewa vipi?”
“Kwa hiyo hajaolewa?”
“Hajaolewa.”
“Kama hajaolewa atakuwa na rafiki wa kiume?”
“Kaka swali hilo gumu.” Salome alificha siri ya Kilole kutokana na siku za nyuma kuwa na urafiki wa kimapenzi na Kinape rafiki kipenzi cha kaka yake. Kwa vile Kinape alikuwa na miezi sita toka aende mjini. Hakukuwa na haja ya kumzibia riziki kama kweli kaka yake anampenda.

0 comments:

Post a Comment