Pages

Subscribe:

Monday, June 20, 2016

HADITHI: NYUMA YA MACHOZI (sehemu ya saba) 07


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
Kilole alijiuliza atawezaje kumsogeza karibu Kinape ambaye tayari ameisha jitangaza kuwa ana rafiki wa kike ambaye wakati wowote atatambulishwa kwao. Kila alipokuwa Kinape peke yake alitamani kuzungumza naye ili kumweleza jinsi gani anavyoteseka juu yake. Japo hakutaka kuachana na mumewe lakini shida yake wawe karibu ili kukumbushia mapenzi yao ya zamani ambayo aliamini hakuna mwanaume mwingine wenye kumpa raha kama Kinape.
SASA ENDELEA...

Wakati huo Deus mambo yake yalizidi kuwa mazuri kutokana na kuingiza kipato kikubwa kutokana na takrima ya kazi yake. Aliweza kumpa siri nyingi rafiki yake kipenzi jinsi anavyoweza...
kupata pesa nyingi nje ya kipato chake cha kawaida. Deus alijikuta akimuamini sana Kinape kwa kumweleza mambo mengi kuhusu uwezo wake wa kipesa na madaraka yake kazini. “Kinape nipo kwenye kitengo cha hatari sana ukiwa mnoko huchelewi kufa, hivyo inabidi uume na kupuliza. 

Kitengo cha kudhibiti madawa ya kulevya ni kitengo hatari sana vigogo ndiyo wahusika wakuu kama utakamata mizigo yao huchelewi kuhamishwa au kutengenezewa zengwe litakalo kulaza pabaya hata kukumaliza kabisa.” “Kwa hiyo vigogo hawakamatwi?” Kinape alimuuliza Deus. “Utaanzia wapi, nyuma yako kuna wakubwa wanakula kupitia mgongo huo huo, sasa wewe jitie kiherehere.” “Kwa hiyo matumizi ya dawa ya kulevya kwisha ni vigumu?” “Ni vigumu lazima tuseme ukweli.” “Sasa kitengo hicho kazi yake nini?” “Kudhibiti dawa za kulevya.” “Lakini mbona wengine mnawakamata?” “Hao ukiona hivyo hawana mikono ya wakubwa.” “Kwa hiyo unapata posho nene toka kwa hao vigogo?” “Kweli rafiki yangu, nisingeweza kuwa vitu hivi kwa muda mfupi.” 

“Alafu unafahamika sana na watu wazito, huwezi kuamini siku ile uliponituma niende kwenye kampuni ile nilipokelewa kama mfalme. Nje niliacha watu wakisota kuomba kazi hata jioni baada ya kazi nilipewa gari la kunirudisha nyumbani, wote pale wanajua Paroko ni ndugu yangu wa damu.” “Hao ndio watu tunaokula nao mjini, waswahili wanasema sema na watu uvae viatu.” ******* Wakati Deus akiuweka wazi uwezo wake wa pesa na njia zinazoingilia, Kilole alikuwa katika wakati mgumu kuhakikisha Kinape kabla ya kuhama mule ndani basi awe ameisha mrudisha katika himaya yake. Siku moja Deus alisafiri kikazi na kuwaacha ndani ya nyumba mkewe, Kinape na mfanyakazi wa ndani. Kilole aliamini ile ni nafasi pekee ya kumsogeza Kinape karibu, Lakini siku hiyo jioni ilikuwa chungu kwa Kilole baada ya Kinape kuja na mpenzi wake nyumbani kumtambulisha. 

 Roho ilimuuma kwa kuamini Kinape amefanya vile ili kumlingishia yeye, alipofika na rafiki yake wa kike Kinape alimtambulisha kwa Kilole. “Shemu huyu ndiye ubavu wangu kama nilivyowataarifu, nilipanga leo awakute wote, lakini kwa vile Swahibu amesafiri nimeonelea si vibaya hata wewe kuwa muwakilishi hata siku akija asionekane mgeni.” “Karibu sana mgeni,” alimkaribisha kinafiki lakini moyoni alikuwa na donge zito. “Asante nimekaribia,” mgeni alijibu huku akijilaza kwenye kifua cha Kinape kama katumwa. “Shemu usione Kinape natakata sababu ya mtoto huyu, kwao wamemlea akalelewa, sifa ziende kwa wazazi wake.” 

“Mmmh! Kama hivyo hongera.” Siku ile walishinda pale na jioni alimsindikiza nyumbani kwao, aliporudi alimkuta Kilole hayupo katika hali ya kawaida kitu kilichomshtua Kinape. “Vipi shemu mbona upo hivyo, maana naona ghafla umekosa raha au unamkumbuka mzee mbona ni leo tu?” “Kwanza Kinape jina hilo unaloniita silipendi sema hujui tu.” “Jina gani?” “La shemeji.” “Aah, sasa wewe ni nani kama siyo shemeji yangu.” “Niite mpenzi au jina langu.” “Eti?” Kinape alishtuka. “Umesikia sana napenda uniite mpenzi mahawala hawaachani.” “Lakini kwangu wanaachana.”

“Kinape kumbuka bado nakupenda.” “Hata mimi nakupenda,” Kinape alimjibu Kilole. “Sasa kwa nini unanionesha mwanamke wako mbele yangu?” “Jamani kuna ubaya gani nami kuwa na wangu mbona mimi sijakuzuia kunionesha kuwa ni mke wa Deus?” “Kinape sikia, kama nilivyokueleza kuwa mimi nilikubali kuolewa kwa shinikizo, lakini nakuhakikishia bado nakupenda na upendo wangu hautakufa milele.” “Sawa, sikatai lakini sasa hivi nitaendelea kukuheshimu kama shemeji yangu na si mpenzi wangu.” “Hilo najua endelea kuniheshimu kama shemeji yako, lakini Deus akiwa mbali utabaki kuwa mpenzi wangu. Nitahakikisha kutokana na uwezo wa mume wangu kukuwezesha kipesa kisha nitaachana naye ili tuishi pamoja.” “Kilole hilo halitawezekana hata siku moja,” Kinape alimjibu huku akimkazia macho.

“Litawezekana, kwa vile wewe ndiye mwanaume aliye moyoni mwangu, hakuna mwingine zaidi yako.” “Kilole siwezi kumtendea unyama rafiki yangu kwa ajili ya tamaa zako za mwili, pia siwezi kukorofishana na rafiki yangu kwa ajili yako, sitaki nionekane mwizi wa fadhira kukosa nuksani kwa ajili ya starehe za muda.” “Kama hutaki tumfanye hivyo basi tufanye penzi la siri.” “Kilole hakuna siri katika mapenzi.”
“Lipo kama wenyewe tukiitunza siri hiyo.” “Haitawezekana, Kilole mshukuru Mungu kwa kukupa mume wenye uwezo pia mwenye mapenzi ya dhati na wewe. Kwa nini unataka kuichezea shilingi kwenye tundu la choo?” “Kumbuka wewe ndiye uliyenionjesha tamu ya dunia.” 

“Ni kweli, lakini kisicho riziki hakiliki, haukuwa riziki yangu ndiyo maana ameolewa na mwingine.” “Kama ulijua hivyo mbona ulinilaumu?” “Nilikulaumu kwa haki kwa vile ulivunja ahadi yetu, lakini uliponieleza umeozwa kwa shinikizo la wazazi wako nilikuelewa.” “Kinape nimekubali, basi naomba kwa leo tu ili nipoze machungu ya moyo wangu, usiponipa nitateseka na nitakuwa radhi kuachika na kurudi nyumbani.” “Kilole kwa nini hukusema mapema mpaka umesikia nina mwanamke ndiyo yazuke haya?” “Nilikuwa natafuta nafasi ili nikueleze, kumtambulisha mpenzio ilikuwa kama kuniwahi kuzieleza hisia zangu.” 

“Nimekuelewa, lakini nakuomba chonde heshimu ndoa yako, kumbuka bomu unalotaka kulitega litatusambaratisha na kijiji tutashindwa kurudi.” “Kinape nakuhakikishia hata Deus akijua hawezi kufanya lolote kwa vile nina siri zake nyingi chafu.” “Lakini kipi unachokikosa kwa mumeo?” “Mapenzi yako, ilinionjesha sasa hivi siyapati.” “Kilole bora lawama kuliko fedheha, nakuhakikishia siwezi kushea mapenzi na rafiki yangu na ukizidi kunilazimisha nitahama hapa. Kuanzia leo nione kama mbingu na ardhi,” Kinape alisema kwa kujiamini bila mzaha. “Wapii? Kinape nakuhakikishia lazima utakuwa mpenzi wangu.” “Labda kwa nguvu za giza.” “Walaa, situmii mizizi wala hirizi wenye hila ni wanawake bwana.” 

 “Tutaona, na sasa naomba unione kama kituo cha polisi kwa muuza unga, Kilole nimeteseka sana kutafuta maisha, mwanga unaonekana unataka kunipeleka wapi, nitawaeleza nini wazazi wangu.” “Wee, maliza yote lakini mwisho wa siku utabakia kuwa mpenzi wangu, kumbuka wewe ndiye uliyenirubuni na kupoteza sifa za usichana wangu, leo hii eti nikuone kama kituo cha polisi na mvuta bangi. Kwa taarifa yako mimi nakuona kama jalala na siku zote ndilo kimbilio la mimi nzi.” “Haya tutaona.” “Si upo, ipo siku utakubaliana na mimi ninachokisema, haiwezekani nitunze mimi wengine wafaidi utamu. Kumbuka Kinape nimekuwa na wewe katika mazingira magumu na uliniahidi ipo siku nitafaidi raha. Leo hii umepata unanikataa.” “Sijakukataa, sasa hivi wewe ni mke wa mtu kuwa muelewa.” “Kwa hili siwezi kukuelewa mpaka naingia kaburini nakuapia ukinikataa nitajiua.”

“Umefika mbali, lakini mbona una maisha mazuri mumeo anakuhudumia kila kitu kwa nini unataka kulipiga teke fuko la pesa.” “Kama unataka suruhu tufanye penzi la siri, nakuhakikishia kumheshimu mume wangu wala sitamdharau.” “Kilole najua hutanielewa nakuomba umkemee shetani wa uzinzi.” “Kinape uniniambia hivyo? Leo hii unajua kukutamani ni kuwa na shetani wa uzinzi kama ungejua hivyo usingenihalibia usichana wangu kumbuka nilikueleza mpaka utakaponioa au zawadi kwa mwanaume yeyote atakayenioa. Lakini ulinidanganya kuwa utanioa mbona hukunioa?” Kilole alizugumza huku akilia kwa hasira. 

“Kilole naomba unisikilize tena unisikilize kwa makini, kabla ya kuja mama yangu alilijua hili na kunieleza nisiwe na wewe karibu hivi akisikia nimefukuzwa na Deus kwa sababu yako nitakuwa mgeni wa nani. Kumbuka sasa hivi wazazi wangu wanaishi maisha ya raha kwa ajili ya Deus huoni kujiingiza katika mapenzi na wewe itakuwa sawa kukata tawi nililokalia?” “Kinape usiwe mwingi wa nahau, Deus hajui lolote kuhusu uhusiano wetu kwa hiyo itatupa nafasi ya kufanya mambo yetu kwa siri bila kujua.” “Kilole narudia tena sitafanya na wala sitegemei kufanya tuheshimiane na kuanzia leo humu ndani nahama nitakuja akiwepo Deus tu.” “Na akikuuliza kwa nini umehama utamjibu nini?” “Nitajua nitakacho mjibu lakini hakitahusiana na wewe.”

 “Kinape naomba uje unizike, ukiondoka jiandae kusikia msiba wangu.” “Kwa hilo sitakutenga nitahudhuria mazishi yako.” “Yaani upo tayari nife unaniona?” “Kwa hili nipo radhi ufe, nina imani hata bila kuwa na mimi bado utaendelea kufurahia maisha. Kusema utajiua kwa ajili yangu ni uongo mkubwa, kama ungekuwa na mapenzi na mimi usingeolewa.” “Nikueleze mara ngapi nililazimishwa lakini mapenzi yangu yote kwako.” “Nimekuelewa, basi endelea na mumeo.” “Upo tayari nife?” “Kwa hili nipo tayari, sipo tayari kujigeuza nyoka mdogo nimekuwa nammeza mfugaji kwa ajili ya tamaa zako za mwili.” “Kinape nimekuelewa, ila nakuomba kitu kimoja endelea kuniita shemeji na mimi nitakuheshimu kama rafiki ya mume wangu. Nakuahidi sitakutamkia tena maneno ya mapenzi. 

Nakuomba unisamehe kwa yote yaliyojitokeza, nina imani ukiondoka lazima siri itavuja naweza kukosa Bara na Pwani. “Kinape nisamehe sana, ni mapenzi mazito kwako, lakini nakuhakikishia nitarudia tena nisamehe sana,” Kilole alisema kwa sauti iliyoambatana na kilio. “Nimekusamehe Kilole, tuiheshimu safina hii tunayosafiri pamoja, lolote baya tukilitenda itakuwa sawa na kuitoboa kwenye kina kirefu tutazama wote.” “Nimekuelewa Kinape, nakuomba unisamehe sana.” 

“Nimekusamehe, asante kwa kunielewa.” Walikubaliana kuendelea na taratibu zilizokuwepo za kuheshimiana kama mtu na shemeji yake na si wapenzi. Kilole baada ya kugonga mwamba alikuwa na mpango mzito moyoni mwake wa kikakikisha anampata Kinape bila mwenyewe kujua. Wakiwa katikati ya mazungumzo simu ya Kinape iliita, alipoangalia aliona ni ya mpenzi wake. “Haloo sweet.” “Haloo darling.” “Niambie mpenzi wangu.” “Vipi upo tayari?” “Ooh, sorry nilikuwa na mazungumzo na shemeji kidogo yamechukua muda ngoja nijimwagie maji.” “Fanya haraka nakuja sasa hivi.” Baada ya kusema vile alielekea chumbani kwake kubadili nguo akaoge ili atoke na mpenzi wake. Usiku wa siku ile walipanga kwenda kwenye kumbi za starehe, Kinape toka awe na mpenzi wake mpya amekuwa akionjeshwa raha za duniani ambazo hakuwahi kuziota. 

Alipokuwa akielekea chumbani kwake, Kilole alimsindikiza kwa macho huku moyoni akisema “nitakomesha jeuri yake.” Akiwa bado yupo katika hali ya uvivu kutokana na maneno ya Kinape yaliyomkata maini. Alishtushwa na sauti ya Happy mpenzi wa Kinape akiwa katika vazi la kutokea jioni. “Aah, dada kumbe upo sebuleni, ina maana husikii hodi yangu?” “Aah! Kumbe ni wewe nilikuwa mbali kimawazo.” “Dada, shemeji kuondoka asubuhi tu umekuwa hivyo, je, akimaliza wiki?” “Wee acha mdogo wangu, nawe utaolewa utayaona.” “Ahaa! Umeishafika?” Kinape alisema akiwa anatoka bafuni. “Niliona unachelewa nikaamua nikufuate, si unajua mtu chake.” “Na kweli mdogo wangu,” Kilole alijibu huku roho ikimuuma. “Hongera umependeza,” Kinape alimsifia Happy. 

“Nawe nataka upendeze kama mimi, vaa nguo nilizokununulia.” “Hakuna tatizo dear nipe nusu dakika.” “Aah, wapi nakuja huko huko.” Waliongozana wote hadi chumbani huku Happy akiwa amemkumbatia Kinape. Kilole alijua Kinape amefanya vile kumuumiza roho, lakini aliapa kumshikisha adabu huku akipanga mpango kabambe wa kusambaratisha penzi lile. Baada ya muda walitoka wakiwa wameongozana katika mtembeo wa mapenzi mazito. Kilole aliwasindikiza kwa macho huku roho ikizidi kumuuma jinsi walivyopendana. Alijua maisha yale hakuna sehemu ya kuyapata zaidi ya kuwa na Kinape. 

Toka aolewe na Deus hakuwahi kwenda sehemu za starehe zaidi ya kwenda kwenye dhifa ya kiserikali. Lakini mashoga zake walimweleza raha wanazozipata wanapokwenda kwenye kumbi za starehe hata kwenye vikundi vya taarabu. Moyoni alijisemea: Leo mjanja lakini ipo siku utanijua mimi na yeye nani zaidi.”
Itaendelea..

0 comments:

Post a Comment