Wednesday, August 23, 2017
Story: KAHABA KUTOKA CHINA (Sehemu Ya 14) - 14
Peter akaondoka hospitalini hapo huku akiwa na mawazo lukuki, hakuwa na uhakika wa kumpata Rose na hatimae kumchukua mtoto wake lakini kwa sababu baba yake alikuwa akimhitaji mjukuu wake, hakuwa na jinsi, alitakiwa kumtafuta kila siku bila kukata tamaa na hatimae kumpata. Endapo angemtafuta hivi hivi aliona hilo kuwa zoezi gumu, alichokifikiria mahali hapo ni kuingia gharama tu ya kutumia fedha.
Moja kwa moja akaingia ndani ya gari lake, hakutaka kuelekea nyumbani kwa wakati huo, safari yake ilikuwa...
ni kwenda Kinondoni B kwa ajili ya kuanza kazi kubwa iliyokuwa mbele yake. Kila alipokuwa akifikiria ukubwa wa Kinondoni B, akaonekana kukata tamaa lakini akajipa moyo kwamba ilikuwa ni lazima afanikishe kile alichokuwa akikihitaji.
Hiyo ikawa siku ya kwanza kwa Peter kufanya kazi yake, alimtafuta Rose kwa kuulizia sehemu nyingi lakini huko kote hakuweza kufanikiwa hata mara moja, kila aliyekuwa akimuulizia hakuwa akimfahamu. Siku ya pili ikaingia, bado alikuwa akiendelea kumtafuta, siku ya tatu mpaka mwezi mzima unakwisha bado Peter hakufanikiwa kumpata Rose.
Moyoni akaonekana kukata tamaa, huku akionekana kutaka kuiacha kazi hiyo kukawa na wazo moja ambalo lilimjia kichwani, wazo la kuitumia moja ya picha za Rose kumtafutia. Wazo hilo halikupata kipingamizi chochote kile kichwani mwake, alichokifanya ni kuelekea nyumbani kwa Bwana Shedrack na kisha kuanza kuongea na kuhusiana na kile kilichomleta.
“Ninahitaji picha ya Rose” Peter alimwambia Bwana Shedrack.
“Bado tu unamtafuta huyu malaya?” Bwana Shedrack alimuuliza huku akionekana kumshangaa.
“Nina kazi nae kwanza. Au wewe hauna shida ya kumuona mjukuu wako?” Peter aliuliza.
“Ninayo shida lakini kwa alichokifanya sijakipenda kabisa”
“Basi sawa. Naomba picha yake yoyote ambayo unaona itanisaidia katika kazi yangu” Peter alimwambia Bwana Shedrack.
Bwana Shedrack akainuka mahali hapo na kuelekea ndani, katika chumba alichokuwa akikitumia Rose na baada ya dakika kadhaa akarudi huku akiwa na albamu iliyokuwa imesheheni picha mbalimbali. Peter akaichukua albamu ile na kisha kuanza kuziangalia picha mbalimbali. Picha zile zikaonekana kumkumbusha kipindi cha nyumba kabisa, kipindi ambacho alikuwa pamoja na Rose wakiyafurahia maisha.
“Acha niende na hii” Peter alimwambia Bwana Shedrack huku akichukua picha ambayo aliiona kumfaa kumtafutia Rose na kisha kuondoka mahali hapo.
Kwa kutumia picha aliamini kwamba lisingekuwa jambo gumu kumtafuta Rose, aliona kwamba picha ile ingeweza kumsaidia kumpata Rose kwa urahisi sana kuliko vile alivyokuwa akifanya vya kumuuliza sehemu moja hadi nyingine. Alipofika Kinondoni B, moja kwa moja akaanza kazi yake ya kumuulizia Rose. Picha ikaonekana kuwa msaada mkubwa sana kwani kwa mtu wa tano tu kumuulizia kuhusu Rose, alikuwa akimfahamu vilivyo.
“Uliposema Rose ulinichanganya sana” Kijana mmoja alimwambia Peter.
“Kwa sababu gani?”
“Mimi ninamfahamu kama mama Lydia” Kijana yule alimwambia Petr ambaye akaonyesha tabasamu kubwa.
“Anaishi wapi?”
“Duh! Kwa sasa hivi sijui anaishi wapi. Alikwishahama zamani sana” Kijana yule alimwambia Peter.
“Alihamia wapi?”
“Mmmh! Wala sijui”
“Ila alikuwa akikaa wapi?”
“Nyumba ile pale yenye genge nje” Kijana yule alimwambia Peter.
“Kwa hiyo hakuna hata mtu anayefahamu alihamia wapi?”
“Labda umuulize Bi Fatuma anaweza kujua”
“Nitampata vipi huyo Bi Fatuma?”
“Anaishi ndani ya nyumba ile ile” Kijana yule alimwambia Peter.
Peter hakutaka kupoteza muda, hapo hapo akaanza kuelekea katika nyumba ile na kisha kumuulizia Bi Fatuma kwa wanawake ambao walikuwa nje ya nyumba hiyo. Wanawake wale wakamtaka kuingia ndani, Peter akaingia na moja kwa moja kupelekwa katika chumba alichokuwepo Bi Fatuma ambaye alikuwa amelala huku akiumwa.
“Shikamoo” Peter alimsalimia Bi Fatuma ambaye alikuwa amelala kitandani, alikuwa mgonjwa.
“Marahaba. Hujambo?”
“Sijambo” Peter aliitikia.
Bi Fatuma alionekana kuwa mgonjwa mahali hapo, alikuwa akionekana mnyonge kupita kawaida. Akajitahidi kuinuka katika kitanda alichokuwa amelala na kisha kukaa kitako. Akaanza kumwangalia Peter usoni, kijana ambaye alikuwa mbele ya macho yake alionekana kuwa mgeni kabisa, hakuwa akikukumbuka kama aliwahi kumuona sehemu yoyote kabla ya siku hiyo.
“Karibu” Bi Fatuma alimkaribisha Peter.
“Mimi ninaitwa Peter. Nimetokea Mwenge” Peter alijitambulisha.
“Ok! Nikusaide nini Peter?”
“Kwanza pole kwa kuumwa” Peter alimwambia Bi Fatuma.
Kitu cha kwanza Peter akaanza kuiangalia hali ya Bi Fatuma, mwanamke yule alionekana kuwa mwanamke aliyekuwa akiishi katika maisha ya dhiki, ule ukaonekana kuwa kama udhaifu mkubwa sana ambao Peter alitakiwa kucheza nao katika kipindi hicho. Hapo ndipo Peter alipoanza kuelezea kile ambacho kilikuwa kimemleta mahali pale.
Bi Fatuma alipolisikia jina la Rose, kumbukumbu zake zikarudi nyuma kabisa katika kipindi ambacho Rose alimwambia mengi kuhusiana na Peter. Japokuwa ulikuwa umepita muda mrefu sana lakini Bi fatuma akaonekana kukumbuka mengi, yule Peter ambaye alikuwa akimsikia, leo hii alikuwa mbele yake akimuulizia Rose.
Peter aliposema kwamba alikuwa akitaka kufahamu sehemu ambayo Rose alikuwa akiishi katika kipindi hicho, Bi Fatuma akaonekana kuwa mgumu kumwambia Peter kile ambacho alikuwa akikitaka katika kipindi hicho. Kila alipokuwa akimuomba zaidi na zaidi Bi Fatuma hakuwa radhi kusema mahali ambapo Rose alikuwepo katika kipindi hicho.
Peter akagundua kwamba kama angeendelea kumuulizia Rose kama vile alivyokuwa akiendelea kumuulizia asingepata kile ambacho alikuwa akikihitaji, alichokifanya ni kuutumia udhaifu ambao alikuwa nao Bi Fatuma, Kwanza akaingiza mkono mfukoni na kisha kutoa kiasi cha shilinngi elfu hamsini na kisha kumgawia.
“Ya nini yote hii?”
“Kwa ajili ya dawa na mambo mengine”
“Asante sana. Allah akujalie maisha mema” Bi Fatuma alimwambia Peter.
“Nafanya hivi kwa sababu nilisikia kwamba Rose alikuwa akikaa mahali hapa. Nafanya hivi kama kurudisha wema japokuwa hautofikia wema wote huo uliomfanyia Rose” Peter alimwambia Bi Fatuma.
Peter hakutaka kukaa sana mahali hapo, kitu ambacho alikuwa akikitaka ni kucheza na akili ya Bi Fatuma tu mpaka ambapo angeweza kumwambia kile ambacho alikuwa akikihitaji kwa wakati huo. Kuanzia siku hiyo Peter akajifanya kuuleta wema wake kwa Bi Fatuma, Kila siku alikuwa akifika mahali hapo na kumjulia hali huku akimletea matunda pamoja na kumwachia kiasi fulani cha fedha. Bi Fatuma akaonekana kutokuamini kwamba kijana huyo ambaye alikuwa amekuja ndani ya nyumba yake ndiye ambaye alikuwa akimfanyia mambo yote hayo na wakati hawakuwa wakijuana kabisa.
“Ila kwa nini unanifanyia haya?” Bi Fatuma alimuuliza Peter.
“Ninafanya haya kwa sababu uliweza kukaa na Rose mahali hapa, wema ambao ulimfanyia Rose basi na mimi natakiwa kuufanya japo kwa theluthi tu” Peter alimwambia Bi Fatuma.
Bi Fatuma akaonekana kujisahau kabisa, fedha pamoja na matunzo ambayo alikuwa akipewa na Peter yakaonekana kumlevya kabisa. Hata alipokuja kupona, msaada wa fedha haukuisha kabisa, kila siku alikuwa akizipokea fedha za Peter ambaye wala hakuonekana kuwa na lengo baya, kila kitu ambacho alikuwa akikifanya alikifanya kisomi.
Wiki ya kwanza ikapita, mwanzo wa wiki ya pili akaingizia kile ambacho alikuwa akikihitaji, tayari katika kipindi hicho Peter alionekana kuwa mwema kwa Bi Fatuma, kila alipokuwa akifikiria wema ambao alikuwa amemfanyia katika kipindi hicho, Bi Fatuma akaona lisingekuwa jambo jema kama angekataa kumwambia Peter kile ambacho alikuwa akikihitaji katika kipindi hicho.
“Rose anaishi Masaki kwa sasa. Katika nyumba ya mwanamke mmoja wa kichina” Bi Fatuma alimwambia Peter.
“Sasa kwa nini alimua kuhama hapa?”
“Yule mwanamke alionekana kuvutiwa nae”
“Kivipi?”
Hapo ndipo Bi Fatuma alipoanza kuelezea toka siku ya kwanza ambayo alikuwa ameonana na Rose mahali hapo, maisha ambayo alikuwa akiishi pamoja na hali ambayo alikuwa nayo. Bi Fatuma hakutaka kuficha kitu chochote kile, msaada mkubwa ambao alikuwa ameuonyesha Peter katika maisha yake ukaonekana kubadilisha kila kitu. Peter alikuwa makini kumsikiliza, alimsokiliza mpaka stori yake ilipokwisha.
“Kwa hiyo alijifungua salama?” Peter alimuuliza
“Ndio”
“Na ulishawahi kuwasiliana nae hivi karibuni?”
“Yeah! Huwa ninawasiliana nae”
“Mtoto wake yupo vipi? Mzurieeeee?”
“Ni mzuri. Ila nafikiri hakuwa wako” Bi fatuma alimwambia Peter maneno ambayo yalionekana kumshtua.
“Hakuwa wangu?” Peter aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Nafikiri”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Yeye ndivyo alivyosema”
“Atakuwa anatania tu” Peter alisema.
Peter hakutaka kuendelea kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kumwachia Bi fatuma kiasi cha shilingi laki moja na kisha kuondoka. Katika kipindi hicho alikuwa akitaka kufika Masaki, sehemu ambayo Rose alikuwa akiishi. Ndani ya gari, kichwa chake kilikuwa kikiyafikiria maneno ya Bi fatuma ambaye alisema kwamba mtoto ambaye alizaliwa hakuwa wake. Maneno yale yalionekana kumchanganya kupita kawaida, ilikuwaje mtoto asiwe wake na wakati yeye ndiye ambaye alifanya mapenzi na Rose katika kipindi ambacho alikuwa katika siku ya kupata ujauzito? Kila alichokuwa akijiuliza, alikosa jibu kabisa.
Peter aliendesha gari mpaka alipoingia Masaki ambapo akaanza kwenda katika sehemu ambayo alikuwa ameelekezwa. Kutokana na mitaa kupangika vizuri, wala hakupata tabu, akafika katika eneo lililokuwa na nyumba ambayo alikuwa ameelekezwa. Akaanza kuiangalia nyumba ile, alipoona ameridhika, akaondoka na kwenda mbali kidogo, akalipaki gari lake na kisha kuanza kurudi katika nyumba ile kwa miguu. Akagonga geti, mlinzi akalifungua.
“Nikusaidie nini?” Mlinzi alimuuliza Peter.
“Samahani. Namuulizia mama Lydia”
“Yupo. Nikuitie?”
“Hapana. Nimekuja kumuulizia kwa sababu alisema nimletee nguo za watoto ila sikuja nazo. Ngoja niende dukani nikamletee kwanza. Nilikuwa nataka kupata uhakika kama yupo, si unajua huwezi kubeba mzigo halafu ukaja hapa mwenyewe hayupo, inakuwa sio ishu” Peter alimwambia mlinzi.
“Hiyo sawa kabisa. Ni bora upate uhakika kwanza. Hebu sogea kidogo gari liiingie” Mlinzi alimwambia Peter katika kipindi ambacho gari dogo lilikuwa likitaka kuingia ndani ya nyumba ile.
Peter akainama na kisha kuanza kuchungulia garini, ndani ya gari kulikuwa na dereva pamoja na watoto wawili, mmoja alikuwa wa kichina na mwingine mweusi. Peter akatabasamu, kwa jinsi alivyokuwa akimwangalia mtoto yule mweusi, alikuwa amefanana sana na Rose, akapata uhakika kwamba yule ndiye alikuwa Lydia, mtoto ambaye aliamini kwamba ni wake.
“Samahani” Peter alimwambia mlinzi ambaye alikuwa akifunga geti baada ya gari kuingia.
“Bila samahani”
“Yule si ndio Lydia mwenyewe?”
“Ndio”
“Kumbe amekuwa mkubwa vile! Ameshaanza kusoma sasa hivi?” Peter aliuliza huku akionekana kutabasamu.
“Yeah! Anasoma shule ya St’ Marrys ila kwa mchana anakwenda shule ya kichina ipo hapo Posta” Mlinzi alimwambia Peter.
“Shule ya Kichina? Itakuwaje asome kichina na wakati yeye mtanzania?”
“Mama yake ndivyo alivyoamua ili kuweka ukaribu kati yake na yule mtoto wa kichina, Lee” Mlinzi alimwambia Peter.
“Basi poa kaka. Ngoja nielekee dukani nikalete hizo nguo” Peter alimwambia mlinzi na kisha kuondoka mahali hapo.
Mambo mengi ambayo alikuwa akitamani kuyafahamu akawa amekwishayafahamu na katika kipindi hicho kitu kilichokuwa kimebakia ni utekelezaji tu. Muonekano wake katika kipindi hicho ulionekana kuwa wa furaha kupita kawaida, hakuamini kama Bi Fatuma pamoja na mlinzi wangeweza kumuonyeshea ushirikiano ule ambao walikuwa wamemuonyeshea katika kipindi hicho. Alikuwa amekwishafahamu mengi na katika kipindi hicho alikuwa akitaka kitu kimoja tu, kumteka mtoto Lydia na kisha kumpeleka kwa baba yake ili aweze kumuona mjukuu wake hata kabla hajafa.
Kila kitu abacho alikuwa akikihitaji kwa wakati huo kilikuwa kimekamilika na utekelezaji ndio ambao ulikuwa ukihitajika kufanyika katika kipindi hicho. Peter alionekana kuwa na furaha kwa kuona kwamba kila kitu kingekuwa kama kilivyotakiwa kuwa katika muda si mrefu kutoka wakati huo. Kitu ambacho aliamua kukifanya ni kumtafuta rafiki wake wa muda mwingi, Ezekiel, kijana ambaye alikutana nae nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kusaidiana nae katika kazi hiyo.
Ezekiel alikuwa kijana ambaye aliondoka kuelekea nchini Afrika Kusini miaka ya nyuma kwa ajili ya kujitafutia maisha. Alipofika huko, maisha yakawa tofauti na mategemeo yake, kila kitu ambacho aliambiwa kwamba kilikuwa kikipatikana katika ardhi ya Afrika Kusini, hakuweza kukipata, maisha mazuri ambayo alikuwa akiyasikia midomoni mwa watu yalikuwa tofauti ya maisha ambayo alikutana nayo nchini Afrika Kusini.
Badala ya kupata maisha ya raha na faraja, maisha yakawa magumu zaidi, kama walivyokuwa wakifanya Watanzania wengi waliokuwa wakielekea Afrika Kusini, nae akajikuta akianza kuuza pipi, sigara pamoja na kuosha magari. Maisha yakaonekana kubadilika mpaka pale alipokutana na Peter ambaye akaahidi kumsaidia kurudi nchini Tanzania kuendelea na maisha yake kama kawaida.
Katika kipindi kirefu, Peter ndiye alikuwa mtu wake wa karibu ambaye alikuwa akimsaidia mambo mengi. Pamoja na kuwa alijiunga na kundi la vijana wa kihuni kutoka Soweto, kutumia sana bunduki katika kipindi cha uporaji lakini katika kipindi hicho akaamua kubadilika. Peter akampangia chumba kizuri na kumsaidia kila kitu ambacho alikuwa akikihitaji mpaka pale ambapo alitakiwa kurudi nchini Tanzania huku Peter akiendelea kumsaidia kwa kila kitu.
Katika maisha yake, Peter ndiye alionekana kuwa mwokozi wake na hata katika kipindi ambacho Peter alikuwa akihitaji msaada, Ezekiel hakuwa na tatizo, aliahidi kumsaidia kwa moyo mmoja bila malipo yoyote yale. Hiyo ikaonekana kuwa faraja kwa Peter ambaye akamuelezea namna ambavyo mambo yalitakiwa kuwa na hatimae mchezo mzima kutarajiwa kufanyika.
“Kwanza inabidi tumteke katika kipindi ambacho atakuwa akitoka shuleni. Unaonaje hapo?” Peter alitoa wazo na kisha kuuliza.
“Hilo si tatizo. Shule yenyewe unaijua?”
“Nimesikia tu kwamba ipo maeneo ya Posta, ni shule ya kichina” Peter alimjibu Ezekiel.
“Hapa itatubidi yufanye vitu kisomi, kitu cha kwanza yatupasa kuifahamu shule yenyewe ili siku ya tukio tusiweze kupata tabu” Ezekiel alimwambia Peter.
Siku hiyo hawakutaka kuendelea kubaki nyumbani, wazo ambalo alilitoa Ezekiel likaonekana kuwa muhimu sana na ambalo lilitakiwa kuchukuliwa hatua mara moja. Walichokifanya ni kuondoka mahali hapo mpaka Posta ambapo kwa msaada wa kuulizia ulizia wakaelekezwa mahali ambapo shule ya kichina ya Sheng Shung ilipokuwa.
Wakaanza kuelekea huko mpaka pale ambapo wakakutana na shule hiyo ambayo ilikuwa na sehemu ambayo kulikuwa na maandishi makubwa yaliyosomeka Sheng Shung huku maneno mengine ya chini yakiwa yameandikwa kwa lugha ya Kichina.
Walichokifanya, wakaanza kuangalia huku na kule, mlinzi alionekana kuwa Mtanzania jambo ambalo likawafanya kujiaminisha sana, wakaanza kuelekea getini.
“Mambo vipi!” Wote wakajikuta wakimsalimia mlinzi.
“Poa” Mlinzi alijibu huku akivuta sigara. Alichokifanya Ezekiel ni kutoa sigara yake.
“Naomba moto” Ezekiel alimwambia mlinzi ambaye akampa sigara yake na kisha kuiwasha.
“Nina maswali kadhaa naomba kuuliza ila kama nitakukosea naomba unisamehe. Si unajua sisi Watanzania maswali mengi” Peter alimwambia mlinzi yule.
“Swali kuhusu nini?” Mlinzi alimuuliza.
“Kuhusu shule hii ya hawa wachina” Peter alijibu huku Ezekiel akijifanya kuwa bize kuvuta sigara yake.
“Hivi shule hii wanafundisha kichina tu?” Lilikuwa swali la kwanza ambalo lilitoka kwa Peter.
“Yeah! Ni kichina tu. Wanachukua watoto wenye miaka mitano mpaka kumi na nne” Mlinzi alijibu.
“Mmmh! Sasa lugha yenyewe Kichina, hivi kuna watoto wa kibongo kweli wanasoma hapa?” Peter aliuliza huku akijifanya kushangaa.
“Yupo mmoja tu. Tena nae sijui imekuwaje. Hakuna mwanafunzi mweusi zaidi ya huyo” Mlinzi aliwaambia.
“Ok! Hapo nimekusoma. Na vipi kuhusu ratiba yao ya kuingia na kutoka?” Peter alimuuliza mlinzi.
“Ratiba ni kwamba wanaingia mchana saa sita na kutoka saa tisa” Mlinzi alimjibu.
“Ok! Usichoke na mawswali yangu kaka. Unajua kwa namna moja au nyingine jua kwamba unanisaidia pia” Peter alimwambia mlinzi.
“Usijali. Kazi ya ulinzi si lazima uhakikishe magari hayaibwi, huwa kuulizwa maswali kuhusu shule hii na kuyajibu ni jukumu letu pia” Mlinzi alimwambia Peter.
“Asante sana kaka. Na vipi kuhusu usafiri wa shule. Upo?”
“Yeah! Kuna basi la shule kwa wale ambao hawaji kuchukuliwa na magari ya wazazi wao”
“Hapo nimekusoma kaka. Sasa kama mimi nina mtoto wangu nataka aje kusoma hapa, ataruhusiwa au hadi nami ningekuwa mchina?”
“Anaruhusiwa hakuna tatizo”
“Nashukuru sana kaka. Asane sana” Peter alimwambia mlinzi.
“Msijali. Karibuni tena”
Peter na Ezekiel wakaondoka mahali hapo, tayari wakapata kitu kingine ambacho kingewaongoza vizuri katika kulitekeleza lile walilotaka kulitekeleza, walichokifanya ni kulifuata gari lao ambalo walikuwa wamelipaki mbali kidogo na kisha kuondoka kuelekea nyumbani.
Kila walichokuwa wakikitaka wakawa wamekwishakipata na kilichokuwa kimeakia ni kufanya utekaji tu. Wakakaa chini na kuanza kupanga namna ambayo walitakiwa kufanya kwa wakati huo. Kila kitu ambacho walikuwa wakikipanga kikaonekana kuwa kamili na kama kungetokea na sababu ambayo ingezuia kitu hicho kisifanyike basi kusingekuwa na jinsi, ila kuhusu mipango, ilikuwa ikienda vizuri.
“Hapa ni kucheza na hisia tu” Peter alimwambia Ezekiel.
“Kivipi?”
“Unavyoona wanaweza kutumia barabara gani kesho kutwa?” Peter alimuuliza Ezekiel.
“Ally Hassani Mwinyi”
“Sawasawa. Nadhani wakitoka na barabara ile wakakwenda njia kwa moja hadi daraja la Salenda, wataonganisha moja kwa moja mpaka makao makuu ya Mult Choice, baada ya hapo watakwenda mpaka katika shule ya msingi ya Msasani na kisha kukata kulia ile barabara ya kuelekea Bamaga. Nimekusea hapo?” Peter alitoa maelezo na kisha kuuliza.
“Kiasi upo sahihi”
“Ok! Ile ndio njia ambayo nina uhakika watakuwa wakiitumia na hii ni kwa sababu kwa kule Msasani kuna wanafunzi wengi wa Kichina wanaishi huko, katika ile mijumba yao mikubwa” Peter alimwambia Ezekiel.
“Sawa. Nimekubaliana na wewe. Sasa mchezo ufanyikie wapi?” Ezekiel alimuuliza Peter.
“General Tyre. Unaonaje?”
“Hakuna noma. Ila kwa nini tusiufanyie Macho?”
“Macho noma. Pale kuna bajaji nyingi, bodaboda za kumwaga kwa ajili ya watu wanaotaka kuelekea Coco Beach hivyo tunaweza kupata wakati mgumu. Cha msingi tuweke mitego yetu pale General Tyre, isipotiki basi ni lazima iende hapo Macho” Peter alimwambia Ezekiel.
“Hakuna noma. Hiyo kazi ndogo sana” Ezekiel alijibu.
Walichokifanya ni kutaka kuwa na uhakika kwamba kama vile walivyokuwa wakidhania ilikuwa ndivyo au sivyo. Siku iliyofuata wakaanza kuelekea shuleni katika kipindi ambacho wanafunzi walipokuwa wanatoka na kisha kuanza kulifuatilia basi la shule. Walikuwa wakilifuatilia kwa ukaribu sana, njia zote ambazo walifikiri kwamba zingetumika na ndizo zilizotumika jambo ambalo likaonekana kuwafariji sana kwa kuona kwamba mipango yao ingekwenda kama walivyopanga.
“Daah! Kuna mtihani mwingine ambao hatukuutegemea” Peter alimwambia Ezekiel.
“Mtihani gani?”
“Yule mtoto hatumii gari la shule. Hutumia gari binafsi” Peter alimwambia Ezekiel.
“Daah! Sasa hiyo si ndio nzuri zaidi. Tutalifuatilia hilo gari, tena nadhani litakuwa likipita njia za mkato. Ndio zuri hilo” Ezekiel alimwambia Peter.
“Kama ndio hivyo poa. Kesho ndio siku ya kazi, kuhusu bunduki hakuna tatizo, nitachukua bunduki ya baba na kisha kwenda kuifanya hiyo kazi. Tutakachotakiwa ni kusikilizia kwanza kama atatumia gari la nyumbani au la shule” Peter alimwambia Ezekiel.
“Hakuna tatizo”
Mpaka kufika kipindi hicho kila kitu kilikuwa kimepangwa na kupangika. Ramani zilikuwa vichwani mwao. Siku iliyofuatia, saa nane na nusu walikuwa mbali kidogo na shule ile lakini sehemu ambayo walikuwa wakiona vizuri mazingira ya shule. Siku hiyo ikaonekana kuwa ya tofauti na siku nyingine, gari ambalo lilikuwa likimfuata Lee na Lydia siku hilo halikuonekana mahali hapo, japokuwa walikuwa mbali, wakamuona mwanafunzi mweusi, Lydia akiingia ndani ya basi lile la shule pamoja na wanafunzi wengine. Lilipotoka, wakaanza kulifuatilia.
Ulikuwa ni mzunguko mrefu sana ambao basi lile la shule lilikuwa likitumia kuwashusha wanafunzi. Peter na ezekiel walikuwa wakiendelea kulifuatilia kama kawaida. Hawakuonekana kukata tamaa, japokuwa kuna sehemu basi lile lilikuwa likisimama sehemu nyingi ambazo wangeweza kwenda na kufanya utekaji lakini hawakutaka kufanya hivyo mpaka kufikia sehemu ambayo walipanga kufanyia tukio.
Safari iliendelea zaidi na zaidi, basi lile lilipofika Bamaga ya Msasani, wakalipita na kisha kuelekea mbele huku lengo lao likiwa ni kufika General Tyre na kisha kulisubiria basi hilo. Walipofika General Tyre, Peter akasimamisha gari na kisha kutoka nje huku bunduki ikiwa kiunoni mwake. Ezekiel hakutaka kubaki garini, nae akatoka na ksha kulisubiria basi lile ambapo baada ya sekunde chache likaanza kuonekana kwa mbali likisogea kule walipokuwa.
“Nalisimamisha. Dereva akilisimamisha tu, unaamuru mlango ufunguliwe” Peter alimwambia Ezekiel huku wakijiandaa kulisimamisha basi lile.
Basi lilipofika karibu, Peter akajaribu kulisimamisha lakini dereva wa basi lile hakusimama jambo ambalo likaonekana kuwa kasirisha kupita kawaida. Kwa haraka sana wakalifuata gari lao na kisha kuingia ndani na kuanza kulifuatilia. Walilifuatilia mpaka liliposimama maeneo ya Macho ambapo kulionekana kuwa na foleni ndogo.
Kwa haraka haraka Peter na Ezekiel wakashuka kutoka garini mwao na kisha kulisogelea basi lile na kumtaka utingo afungue mlango lakini akaonekana kugoma.
Peter hakutaka kuchelewa, akaanza kuelekea upande wa dereva, akausogelea mlango na kisha kumuonyeshea bunduki, kitendo cha dereva kuiona bunduki ile, tayari akaona kwamba kama wasingetii kile walichoamuriwa basi damu zingemwagika mahali pale.
“Fungua mlango Ally” Dereva alimwambia utingo wake na hivyo kuufungua mlango.
Kwa mwendo wa kasi, Peter akaingia ndani ya basi lile, watoto wote wakabaki kimya.
Peter hakutaka kuchelewa, alichokfanya ni kumsogelea Lydia ambaye alikuwa akimwangalia na kisha kumchukua na kuondoka nae. Lee ambaye alikuwa kimya akaanza kulia, kitendo cha kumuona ndugu yake, Lydia akichukuliwa kilionekana kumkasirisha, akataka kumfuata Peter lakini utingo akamzuia.
Peter akatoka nje na Lydia ambaye alikuwa akilia sana, akamuingiza ndani ya gari na kisha kuanza kuelekea katika barabara ile ya CCBRT, walipofikia ukingoni, wakakata kona kulia, wakachukua barabara ya vumbi ambayo ilitokea katika barabara ya Ally Hassan Mwinyi na kutokomea kusipojulikana huku wakiwaacha watu waliokuwa pale Macho kutokuelewa kama kulikuwa na utekaji ambao ulikuwa umefanyika mahali pale kutokana na uharaka ambao ulifanywa katika kutekeleza kitendo kile.
Swali ambalo lilitoka kwa Mpelelezi Deogratius Mariga likamfanya Rose kunyamaza kwa muda na kuanza kufikiria jambo. Si kwamba katika kipindi hicho hakumfahamu mwanaume ambaye alikuwa amezaa nae mtoto Lydia, alikuwa akimkumbuka sana ila hapo alionekana kama kupigwa bumbuwazi kwa kuulizwa swali ambalo hakulitegemea.
“Baba yake ni kijana fulani anaitwa Joshua” Rose alijibu na kisha kunyamaza.
“Mara yako ya mwisho kukutana nae ilikuwa lini?” Mariga aliendelea kuuliza maswali.
“Miaka mitano iliyopita” Rose alitoa jibu ambalo likamfanya kila mtu kushtuka.
“Miaka mitano iliyopita?”
“Ndio”
“Mbona kipindi kirefu sana?” Mpelelezi Zemba akaingilia kwa kuuliza swali.
Hapo ndipo ambapo Rose akaamua kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake ya nyuma. Hakutaka kuficha kitu chochote kile, kila kitu ambacho alikuwa akielezea, machozi yalikuwa yakimtoka, historia ya maisha yake hasa ile ya usagaji ilionekana kumuwekea doa kubwa moyoni mwake. Alipomaliza, kila mmoja akashusha pumzi ndefu.
“Umepata kitu chochote hapo?” Mpelelezi Zemba alimuuliza Mariga.
“Kidogo. Inawezekana huyo baba yake atakuwa amehusika katika utekaji” Mariga alijibu.
“Yeah! Inawezekana lakini kama nina mashaka kidogo” Zemba alijibu.
“Mashaka gani tena?”
“Hivi baba anaweza akamteka mtoto kweli?” Zemba aliuliza.
“Inategemea”
“Hebu subiri. Naomba nikuulize kitu kimoja Rose. Uliwahi kupigana na huyo kijana, Joshua?” Zemba alimuuliza Rose.
“Hapana”
“Hata kutoleana maneno mabaya?”
“Hapana”
“Duh! Mbona kazi inaonekana kuwa kubwa sana” Mariga alisema huku akionekana kukata tamaa.
Waliendelea na mahojiano zaidi na zaidi, mpaka saa moja linakatika, kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba Joshua ndiye mtu ambaye alikuwa amehusika katika utekaji wa mtoto Lydia. Walichokifanya ni kusimama na kisha kuaga huku wakiahidi kurudi siku inayofuatia. Wakaondoka sebuleni hapo na kisha kuingia ndani ya gari lao.
“Hebu subiri” Mariga alimwambia Zemba
“Kuna nini tena?”
“Kuna kitu nimehisi”
“Kitu gani?”
“Kuhusu mtu wa upande wa pili”
“Yupi?”
“Huyo Peter”
“Kuna kipi umehisi?”
“Hauoni kwamba nae anaweza kuwa amehusika?”
“Mmh! Sidhani. Lakini hakuna tatizo. Tukamhoji maswali kadhaa kuhusu huyo mtu kwanza” Zemba alimwambia Mariga na kisha wote kuanza kurudi ndani ya nyumba ile.
Awamu ya pili ya maswali ikaanza tena mahali hapo, katika awamu hii maswali mengi yalikuwa yakihusiana na Peter tu. Katika kila neno ambalo alikuwa akiongea kuhusiana na Peter, kila mmoja akaanza kutengeneza kitu chake kichwani mwake. Mpaka wanamaliza dakika ishirini za mahojiano, kila kitu kikaonekana kuwa wazi na wala hakukuhitaji maswali zaidi.
“Kila kitu kipo tayari. Mtekaji kashajulikana” Mariga alimwambia Zemba.
“Nani kamteka mtoto wangu?” Rose aliuliza.
“Peter”
“Peter?”
“Ndio”
“Mmejuaje?”
“Alikuwa akijua kwamba mtoto ni wake, si ndio hivyo?”
“Ndio”
“Katika sifa zote ulizotuambia kuhusu yeye, maelezo ya mlinzi wa getini wa nyumba hii, mlinzi wa shule ile ya Sheng Shung pamoja na dereva, ameonekana kuwa na alama hizo hizo. Au nimekosea Zemba?” Mariga alisema na kumuuliza Zemba.
“Haujakosea. Mtekaji atakuwa huyu huyu” Zemba alisema.
“Sasa kwa nini kamteka mtoto wangu?” Rose aliuliza huku akianza kulia tena.
“Ni kwa sababu anajua kwamba mtoto ni wake na hajamuona kipindi kirefu. Hilo tu” Mariga alimjibu Rose.
Hakukuwa na cha kuchelewa, kila kitu kikaonekana kuwa wazi kwa wakati huo na ukweli ulikuwa umekwishajulikana kwamba Peter ndiye ambaye alikuwa amehusika na utekaji ule, kwa maana hiyo walitakiwa kumtafuta. Kilichofanyika ni kupiga simu katika kituo cha polisi cha Mwenge na kisha kuwapata taarifa juu ya Peter ambaye alikuwa akihisiwa kuhusika katika utekaji wa mtoto Lydia, utekaji ambao ulianza kuvuma sana jijini Dar es Salaam.
“Mkifika na kumkuta, kitu cha kwanza muwekeni chini ya ulinzi kwa mahojiano maalumu” Mpelelezi Mariga alimwambia polisi ambaye alipokea simu kituoni.
“Hakuna tatizo”
“Cha msingi ngoja tusubiri hapa hapa ili kama itatokea wamempata na kumuweka chini ya ulinzi twende na Rose mpaka huko” Mariga alimwambia Zemba na kisha wote kutulia kochini wakisubiri wapigiwe simu.
Lydia alikuwa akiendelea kulia ndani ya gari lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alionekana kujali kitu chochote kile, kitu ambacho walikuwa wakikijali katika kipindi hicho ni kuelekea katika hospitali ya Mikocheni B kwa ajili ya kumuonyeshea Bwana Edward mjukuu wake ambaye alikuwa akitaka kumona kila siku.
Muda wote Ezekiel alikuwa amemkamata Lydia vilivyo katika siti za nyuma. Huku Peter akiendesha gari lile. Peter hakuonekana kuzijali kelele za Lydia kwa kuamini kwamba kuna kipindi kingefika, kipindi ambacho mtoto huyo angenyamaza kabisa na wao kuendelea na mambo mengine. Japokuwa kutoka Masaki mpaka Mikocheni B hakukuwa na umbali mkubwa lakini kutokana na foleni za hapa na pale walieza kutumia muda wa dakika arobaini na tano na ndipo gari lile likaanza kuingia katika eneo la hospitali ile.
Bado Lydia hakuwa amenyamaza, alikuwa akiendelea kulia kama kawaida. Hawakutaka kuteremka, moja ya sheria za hospitalini hapo ilikuwa ni kutokupiga kelele, hawakutaka Lydia aendelee kupiga kelele za kilio na wakati walikuwa na uhitaji wa kuingia ndani ya hospitali ile katika muda huo wa saa kumi, muda ambao ulikuwa ni wa kuwaona wagonjwa.
Lydia alilia mpaka akanyamaza, wakateremka na kisha kuanza kuelekea ndani ya hospitali ile huku Peter akiwa amembeba mikononi mwake. Moja kwa moja wakaelekea katika kile chumba alicholazwa Bwana Edward, walipofika, hata mama yake, Bi Stella alikuwepo ndani ya chumba hicho akiwa amekuja kumjulia hali mume wake.
“Baba….” Peter alimuita baba yake ambaye alikuwa amelala kitandani pale.
“Mjukuu wangu. Mjukuu wangu yupo wapi?” Bwana Edward alimuuliza Peter.
“Huyu hapa. Nimekuja nae baba kama nilivyokuahidi” Peter alimwambia baba yake, Bwana Edward.
Japokuwa alikuwa mgonjwa aliyeonekana kuzidiwa, akayageuza macho yake pembeni na kisha kuanza kumwangalia mtoto ambaye alikuwa amesimamishwa pembeni yake, mtoto ambaye alikuwa akiangalia kwa macho yaliyokuwa na uoga.
“Hatimae nimemuona mjukuu wangu. Nimemuona mjukuu wangu Peter” Bwana Edward alimwambia Peter huku kwa mbali maachozi yakianza kumlenga.
Bwana Edward akaonekana kuwa mwingi wa furaha, hakuamini kwamba katika kipindi hicho alikuwa amefanikiwa kumuona mtoto ambaye aliamini kwamba alikuwa mjukuu wake, kwa tabu sana akauinua mkono wake na kisha kuupeleka shavuni mwa Lydia na kisha kuanza kulishika shika shavu lake, moyo wake ulikuwa na furaha kupita kawaida.
Peter nae akaonekana kuridhika, kila alipokuwa akimwangalia Lydia, moyoni mwake alikuwa akijisikia amani kupita kawaida, hakuamini kwamba mara baada ya miaka mitano kupita siku hiyo ilikuwa ni siku nyingine ya kumuona mtoto wake, mtoto aliytoka katika kiuno chake.
“Lydia. Nyamaza Lydia. Mimi ni baba yako” Peter alimwambia Lydia ambaye alikuwa akianza kulia tena.
“Nataka kurudi kwa mama yangu” Lydia alimwambia Peter.
“Utarudi. Mimi ni baba yako Lydia…mimi ni baba yako” Peter alimwambia Lydia ambaye hakuonekana kuelewa zaidi ya kuendelea kulilia kurudi kwa mama yake.
“Nimeridhika. Kwa sasa hivi nipo tayari hata kufa. Nimeridhika kumuona mjukuu wangu” Bwana Edward alimwambia Peter huku akionekana kukata tamaa kitandani pale.
Hawakutaka kuondoka mahali pale, kwa Peter, alikuwa akijisikia faraja moyoni mwake, kitendo cha kumuona Lydia ambaye aliamini kwamba ni mtoto wake kilikuwa kimempa faraja kubwa kupita kawaida. Muda wote alikuwa amemshika Lydia, hakutaka aondoke mikononi mwake, alikuwa akitamani kuwa pamoja nae katika kipindi chote.
Huku wakiendelea kuwa katika furaha kubwa juu ya uwepo wa Lydia mahali hapo, mara mlango ukafunguliwa, dokta mkuu pamoja na polisi wanne wenye bunduki wakaingia ndani ya chumba hicho. Kitu cha kwanza wakawaweka wote chini ya ulinzi.
“Mpo chini ya ulinzi” Polisi mmoja aliwaambia huku akiwa amewanyooshea bunduki.
“Chini ya ulinzi! Kwa kosa gani?” Peter aliuliza huku akijifanya kushangaa.
“Utekaji”
“Utekaji? Hapana, sijamteka, huyu ni mtoto wangu, nilichokifanya ni kumchukua na si kumteka. Toka lini baba akamteka mtoto wake?” Peter alijibu na kisha kuwauliza swali ambalo likaonekana kuwa kama dharau kwa polisi wale.
Polisi wakaonekana kuwa na hasira, majibu ya Peter yakawafanya kuvimba kwa hasira kupita kawaida, wakawafuata mahali pale walipokuwa na kisha kumfunga pingu pamoja na Ezekiel na kisha kuondoka nao mahali hapo kuelekea kituoni. Bi Stella akabaki akilia tu, hakuamini kama mtoto wake ambaye alikuwa anampenda kwa wakati huo alikuwa amewekwa chini ya ulinzi wa polisi na kupelekwa polisi huku akitakiwa kufikishwa mahakamani siku za usoni kutokana na kukabiliwa na kesi ya utekaji.
Polisi hawakuondoka bila Lydia, nae wakamchukua na kisha kuelekea nae kituoni. Wakawapigia simu mpelezi Mariga na Zemba na kuwaambia kwamba walikuwa wamekwishampata mtoto pamoja na watuhumiwa kwa hivyo mama wa mtoto huyo alitakiwa kufika kituoni kwa ajili ya kumchukua mtoto wake na mambo mengine kufuata.
Katika kipindi chote hicho Peter alikuwa akilalamika tu kwamba hakuwa amemteka Lydia kwa sababu asingeweza kumteka mtoto wake mwenyewe. Polisi hawakutaka kumuelewa kabisa, walichokuwa wakikifanya ni kuendelea kumpeleka katika kituo cha polisi kwa ajiliya maelezo mengine.
Wala hawakuchukua muda mrefu, wakafika katika kituo cha Osterbay ambapo huko ndipo walipotaka ahifadhiwe kabla ya mambo mengine kuendelea zaidi. Polisi wote wakaonekana kufurahia, hawakuamini kama kazi ya kumkamata peter ilikuwa ni rahisi namna ile, walibaki wakipongezanana tu.
“Huyu atakuwa anajifunza utekaji” Polisi mmoja aliwaambia wenzake huku akicheka kidharau.
“Hahaha! Kwa nini?” Polisi mwingine aliuliza.
“Mtu unafanya utekaji hata masaa mawili hayajapita, umekamatwa. Huyu atakuwa akijifunza utekaji” Polisi yule alijibu.
Peter na Ezekiel waliendelea kubaki kituoni hapo mpaka saa kumi na mbili kipindi ambacho Rose akafika mahali hapo akiwa pamoja na wale wapelelezi na Bi Lucy. Kitu cha kwanza ambacho alikuwa akikitaka mahali hapo ni kuona mtoto wake tu, Lydia akaletwa, akamchukua na kumbeba huku akilia.
“Huyo kijana mwenyewe yupo wapi?” Rose alimuuliza polisi aliyekuwa pale kaunta.
“Yupo ndani. Anasubiria kesi yake”
“Naweza kumuona?”
“Subiri kwanza” Polisi yule alimwambia na kisyha kuingia kwenye chumba kimoja.
Rose alibaki mahali pale huku akimwangalia mtoto ake, Lydia. Hakuamini kwamba Lydia alikuwa amepatikana baada ya kutekwa ndani ya muda mchache. Kila alipokuwa akimwangalia, alikuwa akijisikia kulia kwa furaha.
Katika kipindi hicho hasira za Rose zilikuwa kwa Peter, mapenzi yote ambayo alikuwa nayo juu ya Peter katika kipindi hicho hayakuwepo tena, alikuwa akimchukia sana na chuki yake ilizidi zaidi mara baada ya kumteka mtoto wake. Rose alikuwa akitaa kuongea na Peter kwa sababu alikuwa akitaka kumwambia ukweli juu ya mtoto Lydia ili asiwe anajiwekea uhakika kwamba Lydia alikuwa mtoto wake kama alivyokuwa akijipa uhakika huo kila siku.
“Subiri kwanza” Polisi yule alimwambia Rose mara baada ya kurudi kutoka katika chumba kile.
Wala haukupita muda mrefu, ni ndani ya dakika kadhaa, polisi ambaye alionekana kuwa kiongozi wa kituo kile akatokea mahali hapo, akaanza kumwangalia Rose, uso wake ukaonyesha tabasamu kubwa. Kwa sababu Rose alikuwa akitaka kuongea nae kidogo hakutaka maongezi yafanyikie mahali hapo, akamwambia kuelekea katika chumba kile pamoja na Bi Lucy.
“Unataka kuongea nae? Kuhusu nini?” Polisi yule, Bwana Pawasa aliuliza.
“Kuna mambo fulani nataka kumwambia” Rose alijibu.
“Mambo gani?”
“Kama kumpa taarifa”
“Juu ya nini tena? Yaani unataka kuongea kwa amani na mtekaji wa mtoto wako?”
“Yeah! Nimeomba mkuu”
“Hakuna tatizo. Ila utatakiwa kuongea nae mbele yetu” Bwana Pawasa alimwambia Rose ambaye akakubaliana nae.
Polisi mmoja akagizwa kwenda kumfungulia Peter mlango wa sero na kwamba alikuwa akihitajika mahali hapo. Peter akatoka huku akionekana kukasirika, akapelekwa katika chumba kile, macho yake yalipogongana na macho ya Rose, akaonekana kutoa tabasamu kubwa.
Miaka mitano ilikuwa imepita tangu kipindi cha mwisho kabisa kuuona uso wa mwanamke huyo ambaye alikuwa amesimama mbele yake, mapenzi ambayo alikuwa nayo katika kipindi cha nyuma bado yalikuwepo moyoni mwake katika kipindi hicho. Kila alipokuwa akimwangalia Rose, Peter alikuwa na uhakika kwamba Rose ndiye ambaye angeongea ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea, yeye ndiye angeongea ukweli kwamba Lydia alikuwa mtoto wake na hivyo hakumteka, alikuwa amemchukua tu.
“Rose…!” Peter aliita huku akionekana kutokuamini.
“Kwa nini ulimteka mtoto wangu Peter?” Lilikuwa swali lililotoka kwa Rose huku uso wake ukionekana kuwa katika hali ya hasira.
“Sikumteka Lydia” Peter alimwambia Rose.
“Kumbe ulifanyajae?”
“Nilimchukua kama mtoto wangu”
“Hapana Peter, Rose si mtoto wako na kamwe hatokuwa mtoto wako” Rose alimwambia Peter.
“Lydia ni mtoto wangu Rose. Haukumbuki siku ile ambayo tulifanya mapenzi na kisha mimba kuingia. Haukumbuki kila kilichotokea kwetu ndani ya chumba changu na maneno ambayo uliniambia?” Peter aliuliza huku akionekana kuwa na uhakika kwamba Lydia alikuwa mtoto wake.
“Lydia sio mtoto wako Peter” Rose alimwambia Peter huku watu wengine wakiwa kimya ndani ya chumba kile.
“Ni mtoto wangu. Hata kama tutaachana na kuwa tofauti bado Lydia atakuwa mtoto wangu. Hautoweza kuubadilisha ukweli Rose” Peter alimwambia Rose.
“Ila kwa nini ulimteka Lydia?”
“Baba alitaka kumuona mjukuu wake kabla ya kufariki” Peter alijibu.
“Sasa ndio umchukue Lydia?”
“Ndio. Baba alikuwa akitaka kumuona mjukuu wake” Peter alimwambia Rose.
“Nisikilize Peter. Lydia si mtoto wako” Rose alimwambia Peter ambaye kwa mbali akaanza kutokwa na machozi.
“Si mtoto wangu?”
“Ndio”
“Kivipi?”
Swali hilo ndilo lililomfanya Rose kuanza kuhadithia kile ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake ya nyuma katika kipindi ambacho wavulana wengi walikuwa wakimfuatilia kwa kumtaka kuwa na mahusiano nae. Katika stori hiyo, aliongea mambo mengi sana ila hakutaka kugusia kuhusiana na usagaji, alimuelezea sana Joshua mpaka siku ambayo alifanya nae mapenzi na hatimae mbegu kuingia katika mfuko wake wa uzazi.
Kila mtu alikuwa ametegesha sikio akisikiliza kwa makini. Kadri Rose alivyokuwa akielelezea na ndivyo ambavyo Peter alivyozidi kutokwa na machozi zaidi na zaidi. Moyoni aliumiza, aliuhisi moyo wake kuchomwa na msumali uliokuwa na ncha kali tena uliokuwa wa moto kupita kawaida. Miguu yake ikapatwa na ganzi, akaihisi ikilegea na kisha kuchuchumaa huku machozi yakiwa yameloanisha sana mashavu yake.
“Haiwezekani Rose. Haiwezekani Rose” Peter alimwambia Rose huku akionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa amekisikia.
“Huo ndio ukweli Peter, sitaki kukudanganya. Lydia si mtoto wako. Ni mtoto wa Joshua” Rose alimwambia Peter.
“No…No…No Rose. Hapana. Lydia ni mtoto wangu. Hebu mwangalie alivyofanana na mimi. Hapana Rose, huyu ni mtoto wangu. Ni mtoto wangu” Peter alisema kwa sauti huku akilia kama mtoto.
“Huo ndio ukweli”
Kwa jinsi Peter alivyokuwa akionekana mahali pale, kila mtu aliyekuwa ndani ya chumba kile akaingiwa na huruma, hata Bi Lucy mwenyewe alijisikia maumivu, katika maisha yake hakuwahi kumuona mtu ambaye alikuwa akilia kwa uchungu kama alivyokuwa akifanya Peter. Rose akashindwa kuvumilia zaidi, nae alikuwa akizidi kutokwa na machozi. Akaanza kumfuata Peter, alipomfikia, akamkumbatia.
“Usilie Peter. Naomba usilie” Rose alimwambia Peter huku nae akilia.
“Umeniumiza Rose. Kwa nini haukuniambia kama mimba haikuwa yangu?”
“Nilihofia. Nilihofia kukuumiza na nilimhofia baba yangu”
“Hata kama Rose. Umeniumiza sana. Nimeingia katika matatizo kwa sababu ya kumteka mtoto ambaye si damu yangu, Baba yangu anakaribia kufariki, amemuona Lydia akaridhika kwa kuamini kwamba amemuona mjukuu wake. Mungu wangu! Kwa nini umenifanyia hivi Rose?” Peter alimwambia Rose na kumuuliza.
“Sikuwa na lengo la kukumiza Peter. Naomba unisamehe kwa kila kitu”
“Ni ngumu Rose. Ninachokiamini ni kwamba Lydia ni mtoto wangu. Hata kwa vipimo vya DNA, nipo tayari kupimwa lakini Lydia ni mtoto wangu” Peter alimwambia Rose.
“Kama unataka kupima, sawa. Hakuna tatizo. Nipo tayari upimaji ufanyike ili uamini zaidi” Rose alimwambia Peter.
Hayo ndio makubaliano ambayo yalikuwa yamefanyika mahali hapo kwamba ilikuwa ni lazima vipimo vya DNA vifanyike na hatimae ukweli ujulikane zaidi moyoni mwa Peter. Kwa Peter bado hakuwa akiamini kwamba Lydia hakuwa mtoto wake, kitu alichokuwa akikitaka ni kuufahamu ukweli na wala hakuwa tayari kumuacha Lydia aondoke na wakati kwa kiasi fulani alikuwa akiamini kwamba alikuwa mtoto wake.
“Kama mpo tayari hakuna tatizo. Ila kwanza itatakiwa kufanyika kitu kimoja” Bwana Pawasa aliwaambia.
“Kitu gani?” Rose aliuliza.
“Ni lazima tumpate huyo mtu ambaye unasema kwamba ni mzazi halali wa mtoto huyu”
“Joshua?”
“Ndio” Bwana Pawasa alijibu.
Labels:
HABARI & UDAKU,
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment