Sunday, August 27, 2017
Story: SIKU SABA KUZIMU (Sehemu Ya 13) - 13
ILIPOISHIA:
Ilibidi yule askari avunje ukimya na kurudia tena kumuuliza swali lile lakini badala ya kutoa majibu kama alivyokuwa akifanya kwa maswali yote, alikaa kimya huku machozi mengi yakimtoka na kulowanisha uso wake.
“Kijana hebu naomba utupishe mara moja, toka nje nitakuita,” alisema yule askari, ikabidi nitii, nikawaacha wenyewe wawili mle wodini.
SASA ENDELEA
Nilihisi kichwa changu kikipata moto, nilikuwa na shauku kubwa mno ya kutaka kuufahamu ukweli wa...
kilichokuwa kimemtokea Shenaiza. Lile swali la awali kwamba yeye ni nani, tayari nilishapata majibu kwa kiasi fulani lakini bado nilitaka kujua nini hasa kilichomtokea.
Mazungumzo kati ya Shenaiza na yule mpelelezi kule ndani yaliendelea kwa muda na baada ya kama dakika kumi na tano kupita, mlango ulifunguliwa na yule mpelelezi akatoka, akanionesha ishara kwamba niingie ndani.
Nikaenda ambapo nilimkuta Shenaiza akiwa anajifuta machozi, macho yake yakiwa yamebadilika rangi na kuwa mekundu sana.
“Come to me Jamal, you are my comfort,” (Njoo Jamal, wewe ndiyo faraja yangu) alisema Shenaiza kwa sauti ya chini, nikamsogelea pale kitandani na kumkumbatia, akanibusu shavuni na kuniomba radhi kwa kilichotokea.
“Unaniomba radhi kwa nini Shenaiza?”
“Najua hujajisikia vizuri kwa mimi kuzungumza kilichonitokea wakati wewe ukiwa nje, nilitamani na wewe usikie lakini naona kwa sasa siyo muda muafaka lakini nakuahidi kwamba muda mfupi ujao nitakueleza wala usijali,” alisema Shenaiza huku akiendelea kunibusu sehemu mbalimbali za mwili wangu.
Nilimtoa wasiwasi na kumtaka awe huru na mimi, akaniachia kisha nikakaa pembeni ya kitanda chake.
“Walitaka kuniua jana, yaani ni Mungu tu na naamini hata wao wanajua kwamba nimekufa, wamenipiga sana,” alisema Shenaiza na kuniambia anajisikia vibaya sana kuniingiza kwenye matatizo ambayo wala hayakuwa yakinihusu.
“Nakuomba sana nikishapata nafuu kidogo tu tuondoke, hata ikibidi kwenda kuishi hotelini mimi nitagharamia kila kitu maana wanaweza kurudi tena kule nyumbani kwako kwa sababu wanaamini kwamba nimeshakwambia kila kitu kinachoendelea.”
“Kwa hiyo unataka kusema wanaweza tena kurudi nyumbani kwangu?”
“Ndiyo! Wanaweza kurudi na kukudhuru bure wakati hauna hatia yoyote,” alisema Shenaiza, kauli ambayo ilinishangaza na kunijaza hofu kubwa moyoni. Kuna wakati nilikuwa najuta sana kwa kujiingiza kwenye mdomo wa mamba bila kujua.
Shenaiza aliendelea kuniongelesha mambo mbalimbali lakini wala akili yangu haikuwa pale, nilikuwa nikiwaza mambo tofauti kabisa. Baadaye nesi aliingia na kunieleza kwamba mgonjwa alikuwa anahitaji kupumzika kwa hiyo nitoke na kumuacha peke yake.
Shenaiza alikuwa mbishi kidogo lakini baadaye alikubali, akaomba kabla sijatoka nimbusu, nikamuinamia pale kitandani kwa lengo la kumbusu kwenye shavu lake lakini alinishika shingoni na kunivutia kwake, ndimi zetu zikagusana na kunifanya nipigwe na ganzi kwa sekunde kadhaa, aliponiachia, nilibaki nimeganda vilevile mpaka nesi aliponishtua.
“Inabidi uende nje kaka ili tumhudumie mkeo kisha apate muda wa kupumzika,” alisema yule nesi, nikashtuka kama mtu aliyekuwa usingizini, nikageuka na kumtazama Shenaiza pale kitandani, akanifinyia jicho lake moja na kunibusu kwa mbali, nikatoka mpaka nje huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wangu.
“Jamal! Uko salama mpenzi wangu? Nakupigia simu lakini sikupati mpaka imebidi nije huku,” alisema Raya ambaye aliponiona tu nikitoka wodini, alikuja na kunikumbatia kwa nguvu, akionesha kuwa na hofu kubwa na ukimya wangu.
Hata hivyo sikumtilia sana maanani, japokuwa nilitoka nikiwa natabasamu, nilipomuona nilikunja sura, nikaingiza mkono mfukoni na kutoa simu, nikagundua kuwa kumbe kweli ilikuwa imejizima bila mimi kufahamu, nikaiwasha na kusogea mpaka pembeni kulikokuwa na mabenchi, nikakaa. Raya naye akaja na kukaa pembeni yangu, akawa na shauku kubwa ya kutaka kusikia chochote kutoka kwangu.
“Niache kidogo Raya, akili yangu haijatulia kabisa, tutazungumza baadaye,” nilimjibu msichana huyo kwa kifupi, nikamuona akishusha pumzi ndefu na kutulia kimya. Maskini Raya! Alionesha kuwa na hisia nzito juu yangu lakini kwa bahati mbaya mwenzake nilikuwa namchukulia kawaida sana.
Sote tukiwa kimya kabisa, nilikumbuka kilichotokea kati yangu na Raya usiku na kujikuta nikishindwa kumeza chakula nilichotafuniwa, nikageuka na kumtazama usoni, naye akanitazama, nikagundua kwamba alikuwa akilengwalengwa na machozi.
“Najua hunipendi Jamal lakini hiyo isiwe sababu ya kuninyanyasa, nakupenda sana mwenzio kuliko mtu yeyote chini ya jua, naamini ipo siku utaujua ukweli,” alisema msichana huyo, nikarudia kumsisitiza kwamba aniache kidogo hayo mambo tutayajadili baadaye, safari hii nilizungumza kwa sauti ya chini nikiwa kama nambembeleza f’lani, nikamuona ametulia.
Nikiwa nimekaa pale, nilimuona yule askari mpelelezi akiwa na wenzake, nikamuomba Raya anisubiri hapohapo, nikainuka na kumfuata huku bado nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua alizungumza nini na Shenaiza.
Hata hivyo, licha ya kumfuata askari huyo na kumuomba anidokeze alichoelezwa na Samantha, alikataa katakata kwa maelezo kwamba atavuruga upelelezi, nikakosa cha kufanya. Nilirudi hadi pale nilipokuwa nimemuacha Raya, nikakaa pembeni yake huku nikiwa kimya kabisa.
“Nakushuru kwa jinsi ulivyojitoa kunisaidia katika haya matatizo yanayonikabili,” nilivunja ukimya na kumsemesha Raya, nikamuona akiinua uso wake ambao muda wote alikuwa ameuinamisha chini, akanitazama huku tabasamu hafifu likichanua kwenye uso wake.
“Usijali Jamal, nipo kwa ajili yako na kamwe sitakuacha peke yako hata iweje.”
“Yaani japokuwa ulikuwa unalia lakini macho yako yamezidi kuwa mazuri,” nilimtania Raya, akashindwa kujizua na kucheka kwa nguvu. Hakuna kitu alichokuwa anakipenda Raya kama kusikia kauli yoyote ya kumsifia kutoka kwangu. Ile huzuni aliyokuwa nayo, iliyeyuka kama theluji juani, akachangamka kabisa.
“Na leo si tutaenda kulala pamoja nyumbani kwetu?”
“Kwani wazazi wako bado hawajarudi?”
“Bado!”
“Ok, tutaangalia itakavyokuwa,” niliamua kumjibu hivyo Raya ili kumridhisha ingawa ukweli ni kwamba kauli hiyo haikuwa imetoka ndani ya moyo wangu. Wakati tukiendelea kuzungumza, niligundua jambo lisilo la kawaida.
Mita chache kutoka pale tulipokuwa tumekaa, kulikuwa na maegesho ya magari. Magari mengi yalikuwa yameegeshwa lakini miongoni mwa magari hayo, ndani ya gari moja kulionekana kuwa na watu zaidi ya mmoja ambao baadaye nilikuja kushtukia kwamba walikuwa wakitutazama sana mimi na Raya pale tulipokuwa tumekaa na zaidi walikuwa wakiniangalia mimi.
Nilipogeuka haraka na kuwatazama, macho yangu na yao yaligongana lakini wakazuga kwamba hawakuwa wakinitazama, wakawa wanaendelea na mazungumzo yao.
“Kwani nini wananitazama mimi?” nilijikuta nikizungumza kwa sauti, Raya akashtuka na kuniuliza nilikuwa namaanisha nini? Nikataka kumzuga lakini haikuwa rahisi, akafanikiwa kugundua kuwa nilikuwa nawatazama watu gani.
“Hata mimi nimewaona muda mrefu tu, tangu unatoka wodini walikuwa wakikutazama lakini sikuwatilia maanani.”
“Tuondoke!” nilisema huku nikiinuka pale nilipokuwa nimekaa kwani tayari kengele ya hatari ililia ndani ya kichwa changu, Raya naye akainuka, tukaanza kuelekea kwenye lango la kutokea nje ya hospitali hiyo lakini cha ajabu zaidi, tukiwa getini tunataka kutoka, nililiona lile gari nalo likija kule tulipokuwepo.
Je, nini kitafuatia? Usikose next
Labels:
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment