Pages

Subscribe:

Tuesday, August 29, 2017

Story: NILILALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI - 10

SITASAHAU NILIPOLALA NA MWANAMKE JUU YA KABURI (10)
Kufumba na kufumbua tulifika Singida. Kupika na kupakua tuliingia Tabora. Taratibu tukauacha mkoa huu wa Wanyamwezi, tukafika Kahama mkoani Shinyanga.
Tulifika wilayani hapo saa nne usiku. Ikabidi tulale kwani sheria hazikuturuhusu kusafiri muda ule. Abiria wachache walishuka, wakaenda...
kupumzika gesti. Wengi tulibaki ndani ya basi, tukalala tukiwa tumekaa.
Tuliamshwa na mlio wa honi, “boboooooooooh!” wote tulikuwa juu ya viti vyetu. Safari ikaendelea.
Mida ya saa nne asubuhi tuliifikia kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Kanembwa. Tuliwaona askari imara wakizungukazunguka kuhakikisha usalama wa kambi na taifa. Wengine walikimbia  mchakamchaka wakiimba nyimbo za kuwasahaulisha uchovu:
“Usimseme usimseme shori wangu! Usimseme,
“Usimseme usimseme shori wangu! Usimseme.” Kamanda aliimbisha. Kuruti wakaitika kwa morali.
Tuliiacha kambi, tukaingia eneo kubwa la wilaya ya Kibondo ambalo lilikuwa pori. Kwa muda wote huo, nikagundua uwepo wa binti mrembo pembeni yangu. Nilikaa upande wa kushoto, yeye akakaa dirishani. Nikaamua kumchombeza kujipima uwezo wa kurusha makombora bila fedha.
“Mrembo mamboooh!” nilimsabahi, akageuza shingo kunitazama, akanipandisha na kunishusha. Alipogundua nilikuwa kapuku asiye na bahati, akanipuuza. Hakujibu salamu, nami nikaamua kukaa kimya. Tukasafiri kimyakimya mimi na jirani yangu.
Gari liliendelea kuukata mwendo. Kama kawaida, miti ilirudi nyuma kwa kasi . barabara haikuwa na lami, hivyo vumbi lilitusabahi kwa shangwe. Wachache, walipiga chafya. Akina siye vumbi ni sehemu ya maisha, hatukujali.
Ilinyesha mvua ikakata. Tope kiasi likapunguza mwendo wa basi. Tulizama katika mashimo na vidimbwi, tukaibuka katika tambarare! Safari ikaendelea. Dereva akiendesha, abiria tukiendeshwa!
Tuliingia  katika pori nene. Mlio wa risasi ukatushtua. Nilipotazama mbele, niliona magogo yamepangwa katikati ya barabara. Pembeni upande wa kushoto walisimama wanamme watatu walioshiba misuli. Nao upande wa kulia, walisimama wengine wanne wenye vifua vya mazoezi, jumla yao wakawa saba. Na wote kwa pamoja walishika bunduki za kizamani aina ya ‘SAR’.
Ndani ya basi watu walianza kulia hovyo. Dada aliyenipuuza mwanzo akanishika bega kwa woga akinisalimia: “Shikamoo,” nami nikaitika, “Marahaba tumekwisha…”

Nini hatma ya watekaji hawa na safari ya Popo kusaka tiba? Tukutane

0 comments:

Post a Comment