Kila nilipogeuka nyuma, nilimuona mtu wa ajabu akizidi kunikaribia. Nikaongeza mbio ili kujiweka salama. Hata hivyo, kwa sababu ya kukimbia kupita kiasi, mapafu...
yakashindwa kufanya kazi yake. Nikadondoka kwa kishindo kama furushi, “Puuuh!” fahamu zikapotea.
Nilishtuka asubuhi nikajikuta nikiwa chumbani kwangu. Haya yalikuwa maajabu mengine kwani sikutambua ni nani aliniweka mule ilhali muda uliopita nilikuwa katika tukio la kufukuzwa na yule adui yangu.
Sikutaka kubaki mjini tena, nikaamua liwalo na liwe, lazima niende Kigoma kumtafuta Mzee Samike. Nililisogelea kabati chakavu lililojaa vumbi. Panya mkubwa akakimbia kuelekea juu zaidi ukutani ambako alifahamu nisingeweza kumfikia. Sikupata muda wa kumtafakari, nikafungua zipu ndogo ya begi nikatoa kiasi cha fedha ambacho niliamini kingeweza kunifikisha Kigoma na kunisadia katika gharama ndogondogo.
Nilimaliza kujiandaa. Nikatoka nikiwa na fulana nyeusi, suruali ya jinsi, viatu vikubwa na kiasi cha fedha kufanikisha safari ya kusaka tiba.
Jua halikuonyesha dalili ya kuchomoza, lilipakatwa na mawingu mazito yaliyoifunika dunia. Wingu lile nililiona kama turubai lililoweka matanga. Kama si msiba wangu, ulikuwa msiba wa nani? Sikupata jibu.
Nilitembea kwa hatua za kuruta wa jeshi, ‘chap chap’ mpaka nikafika stendi. Hapo nilipokelewa na wapiga debe wengi ambao kila mmoja alinivutia kwake kama ilivyo kwa mwamba ngoma.
Sikumsikiliza yeyote. Nilikwenda mpaka ndani ya ofisi ya basi nililotaka, nikakata tiketi, kisha nikazama ndani ya chombo cha usafiri.
Nilipokaa juu ya siti, nikapitiwa na usingizi mzito. Kwa muda wa siku kadhaa sikulala vya kutosha. Asili ya maumbile ikanikwapua mzima-mzima. Nikalala kama dume la konokono.
Nilishtuka gari likiwa Dodoma. Nikajinyoosha kinyonge tayari kuendelea na safari. Gari ilikwenda kwa mwendo wa kistaarabu. Dereva alikuwa mzee na alizishika sheria zote za barabarani. Kweli utu uzima dawa!
0 comments:
Post a Comment