Mzee aliletewa tumbaku aliyoagiza. Ilikuwa tumbaku ya tozo. Akaiweka katika kiko kilichokuwa na kaa dogo la moto, akavuta mikupuo miwili haraka, nikakohoa kwa ule moshi wake.
“Navuta mimi unakohoa wewe! Bwana mdogo acha uchuro,” mzee alisema akinikazia macho. Sikumjibu, niliachia...
tabasamu jembamba.
“CHIMOTA S. SAMIKE,” mzee alianza kusimulia, “alikuwa mjukuu wa mzee Samike. Samike ni mzee mchawi haijapata kutokea. Inasemekana alizaliwa na uchawi wake mkononi. Alijaaliwa kuwa na mjukuu mmoja tu, ambaye alipatikana kutoka kwa binti yake wa pekee aliyebahatika kumzaa enzi za ujana wake. Haijulikani hasa baba wa Chimota alikuwa nani kwani mara baada ya binti kupata ujauzito, kichaa cha ghafla kilimvaa akawa haelewi la Kaskazini wala la Magharibi.”
“Kwa nini Samike hakumtibu binti yake? Umesema alikuwa mchawi haijapata kutokea,” niliuliza.
“Acha ujinga. Mchawi si mganga.” Alinikata mdomo. Nikagundua jambo, mzee hakupenda maswali na endapo ningeendeleza udadisi huo, hapana shaka mambo yangeenda segemnege.
Baada ya kimya kifupi, mzee akaendelea kusimulia: “Binti alipojifungua, akakata kamba zake za uzuzu, kisha huyoo akatokomea kusikojulikana. Inasemekana alipigwa ‘kipapai’ na maadui wa mzee Samike, wakamchukua kumuonyesha wao walikuwa walozi waliobobea zaidi. Lilikuwa kasheshe la wachawi wakipambana kuonyeshana umwamba.
Samike akabaki na kitoto kidogo kisichomfahamu mama. Mzee aliishi peke yake katika nyumba ya ukiwa. Pamoja na maisha hayo, alijitahidi kumhudumia Chimota. Chimota akanenepa kwa ule unywaji wa maziwa ya ng’ombe na upendo wa babu.
Hata hivyo, kisicho riziki hakiliki. Wachawi walikuja kumuumiza zaidi mzee Samike. Waliyakatisha maisha ya Chimota akiwa na miezi saba tu. Samike alisikitishwa sana na mkasa huo. Alitegemea mtoto yule ndiye angekuja kuwa mrithi wa mikoba yake ya ulozi.
Mzee Samike kwa sababu ya uchawi wake, alikwishatengwa na jamii. Watu wote walimwogopa na hawakuthubutu kwenda msibani. Japo alisimama juu ya paa la nyumba kutangaza kwa sauti kuwa alifiwa na mjukuu, watu waliziba masikio, msiba wakaupa kisogo.
0 comments:
Post a Comment