Wednesday, August 23, 2017
Story: SIKU SABA KUZIMU (Sehemu Ya Kumi) 10
Ilipoishia…
“Mungu wangu,” nilisema huku nikifikicha macho na kutazama vizuri, kuna muda nilikuwa nahisi kwamba huenda nipo ndotoni lakini haikuwa hivyo, sikuelewa pale kwangu nini kilisababisha watu wajae kiasi kile.
Endelea Nayo
Niliendelea kujiuliza maswali mengi bila kupata majibu. Wasiwasi wangu zaidi ulikuwa ni kuhusu Shenaiza, nilijiuliza au wale...
watu niliowaona usiku uliyopita walivamia na kubomoa geti langu hata kuingia ndani kwenda kumfanyia unyama ndio ikawa sababu ya watu wale kujaa, lakini bado hata swali hilo sikuweza kulipatia majibu ya moja kwa moja.
Huku moyo ukidunda niligeuza shingo yangu na kumtazama Raya, uso wake ni kama ulikuwa unaniuliza nini kinaendelea nyumbani kwangu! Bila kuzungumza jambo lolote niliyatoa macho yangu kwa Raya nikayarudisha kule ulipokuwa umati wa watu waliyokuwa kwenye hamaki kubwa huku minong’ono ikiwa imetawala.
Nilizidi kuwatazama hatimaye ukafika wakati uzalendo ukanishinda nikaanza kusikia msukumo kutoka ndani ya mwili wangu ukinitaka kwenda kushuhudia nini kilikuwa kimetokea nyumbani kwangu ili kama lipo la kukabiliana nalo nifanye hivyo.
Huo ndiyo uamuzi nilioufikia baada ya kuwaza na kuwazua, kwa ujasiri mkubwa huku miguu yangu ikitetemeka kwa woga nilianza kupiga hatua kwenda mbele, Raya naye alianza kunifuata nyuma bila kuzungumza jambo lolote lile mpaka tulipoufikia kabisa ule umati wa watu.
“Mungu wangu!” Nilijikuta nikitamka kwa hamaki kiasi kwamba watu wengi wakageuza macho yao na kuanza kunitazama.
Wala sikuwa na muda wa kujali juu ya nini walikifikiria juu yangu, macho yangu niliyatoa pima nikishangaa kilichokuwa kimetokea nyumbani kwangu, geti langu la chuma lilikuwa limebomolewa na kutupwa pembeni jambo lililonifanya nizidi kuingiwa na woga juu ya usalama wa Shenaiza.
Ilikuwa ngumu kuamini kila kilichokuwa kinatokea kama kilinitokea nikiwa kwenye ulimwengu wa kawaida, muda mwingi nilikuwa nikifikiri huenda nilikuwa naota na kuna muda ningeweza kushituka, lakini hilo lilikuwa ni jambo lisilowezekana maana kila kilichokuwa kinatokea kilikuwa katika ulimwengu wa kawaida kabisa.
Huku kila mtu akionekana kunishangaa nilizipiga hatua zisizo za taratibu sana kuelekea ndani ya nyumba yangu, lakini baada ya kuvuka tu eneo la mlango na kupiga hatua chache nilianza kuona michirizi ya damu ikitokea ndani sebuleni.
Mapigo ya moyo yalizidi kudunda kwa kasi zaidi maana tayari kutokana na hali halisi nilifahamu Shenaiza yalikuwa yamekwisha mkuta yakumkuta. Nilizidi kupiga hatua za kasi kuifuata ile michirizi ya damu, wakati huo Raya naye alikuwa nyuma yangu lakini pia baadhi ya watu waliokuwa wamefika pale kulishuhudia tukio hilo nao walikuwa wakinifuata mpaka tukaingia ndani kabisa.
Aisee, ilikuwa ni vigumu kuamini nilichokuwa ninakiona mbele yangu. Mwili wa Shenaiza ulikuwa katikati ya dimbwi la damu iliyokauka huku akiwa kimya kabisa! Kwa ujasiri ambao sikuelewa ulitokea wapi nilianza kusogea ili kumgusa na kufahamu kama alikuwa amekufa au la, lakini nilipoendelea kumsogelea watu waliokuwa nyuma yangu walinikataza kufanya hivyo.
“Kaka sikia, usithubutu kumgusa huyo mtu, jambo la kufanya tutoe taarifa polisi,” ilisikika sauati ya mtu moja ikizungumza. Niligeuka na kumtazama.
“Kweli kabisa, yanapotokea mauaji kama hukuwepo eneo la tukio hata kama mtu anakuhusu hutakiwi kumgusa.” Mtu mwingine aliongeza.
Nilibaki nimesimama huku nikihisi miguu yangu ikiishiwa nguvu bila kufahamu nifanye nini, Raya naye alinisogelea na kunitaka niwe imara juu ya kile kilichotokea. Akanisihi kuwasikiliza watu hao nini walikuwa wanasema na zaidi kujikaza kwa sababu mimi ni mwanaume na nilikuwa na kila sababu ya kuwa imara.
Sikuwa mbishi na kama walivyoshauri wale watu ndivyo ilivyofanyika, wao wenyewe waliamua kusaidia kutoa taarifa polisi na baada ya robo saa gari la polisi lilifika nyumbani kwangu pale, bila kupoteza muda askari waliovalia mipira mikononi waliingia mle ndani tulimokuwa, wakauliza nani mwenyeji, nikajitambulisha, wakanitaka kutoa maelezo mafupi juu ya kilichotokea.
Ukweli ni kwamba sikufahamu niseme nini. Kuhusu Shenaiza sikuwa nikimfahamu kabisa tofauti na kuwasiliana naye ndani ya siku chache kwenye simu, jambo lililonifanya hata kubabaika kwenye maelezo, wale askari wakaniambia nilitakiwa kuambatana nao polisi kwa ajili ya kutoa maelezo.
Hata hivyo jambo ambalo lilinishangaza mno baada ya wale askari kumgeuza Shenaiza waligundua kuwa hakuwa amekufa kama ambavyo sisi tulikuwa tukifikia. Moyo wake ulisikika ukidunda kwa mbali sana jambo ambalo kwa upande fulani nilinifanya kufurahi moyoni.
Walimbeba msichana huyo ambaye alikuwa amelowana chapachapa kwa damu, wakampeleka mpaka kwenye gari walilokuja nalo mahali pale, wakanitaka nami kupanda na kuambatana nao, Raya alipotaka naye kupanda ndani ya gari hilo walimkataza, ikabidi mimi nimwambia achukue usafiri mwingine na kulifuata gari lile la polisi ili aweze kufahamu ninapelekwa kwenye kitua gani jambo ambalo alitii.
Safari haikuwa ndefu sana na wala haikuchukua muda mrefu tayari tulikuwa tumekwishafika katika Kituo cha Polisi Osyterbay, bila kupoteza muda baada ya kuchukua kibali cha matibabu (PF3), gari lile la polisi liliondoka mahali pale na kuelekea hosipitali ambayo sikuifahamu kwa wakati huo, mimi ikabidi nibaki kwa ajili ya mahojiano.
Ukweli ni kwamba katika wakati wote huo nilikuwa kwenye hali mbaya sana. Nafsi yangu ilikuwa inajutia mno juu ya kumkubalia Shenaiza mawazo yake ya kumtorosha hospitali na kwenda naye nyumbani kwangu. Huo niliuona uamuzi wa kipuuzi usiyokuwa na mfano wake maana bila kufanya kwangu hivyo huenda nisingeingia kwenye matatizo hayo yote.
Hata hivyo sikuwa na namna zaidi ya kukubaliana na hali halisi iliyokuwa inaendelea, askari polisi wale waliniingiza katika chumba cha mahojiano na kuanza kunihoji juu ya kilichotokea mpaka Shenaiza akafikia katika hali kama ile aliyokuwa nayo, sikupenda kuficha juu ya ukweli niliokuwa ninaufahamu, zaidi niliwaeleza kuwa hata usiku uliyopita nilitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Kijitonyama maarufu kwa jina la Mabatini lakini sikuweza kupata msaada maana askari wote walikuwa kwenye doria.
Polisi wale walionyesha kushangazwa na jambo hilo, Mabatini kilikuwa kituo kikubwa ambacho ilikuwa si rahisi askari kukauka kabisa, kulionekana kuna uzembe fulani ulikuwa umefanyika, lakini hata hivyo maelezo yangu juu ya tukio na juu ya kumfahamu Shenaiza yalionekana kutowaridhisha wale askari polisi jambo lililofanya waniweke nyuma ya nondo.
Wakati hayo yote yanaendelea Raya alikuwa kituoni hapo na aliweza kupata taarifa za kila kitu kilichotokea, alijaribu kuwashawishi askari ili aweze kutoa dhamana lakini hawakumuelewa, walimwambia ilikuwa ni lazima nikae mahabusu pale wakati upelelezi wa tukio hilo ukiendelea.
Raya hakuwa na namna aliamua kuondoka kituoni kwenda kuwataarifu jamaa zangu wengine juu ya kilichokuwa kimetokea. Mimi nikiwa mahabusu hakuna kilichoendelea ndani ya akili yangu zaidi ya majuto, nilifahamu kabisa niliingia katika msala ambao sikuwa kabisa na hatia nao.
Saa zilikatika nikiwa bado nyuma ya nondo ambapo baadaye kama baada ya kupita saa tatu hivi au nne nilishangaa askari polisi akija kuniita, ambapo akanipeleka tena kwenye chumba cha mahojiano. Wakati huo nilikutana na sura mpya ambapo baada ya salamu askari huyo mwenye sura ya mkazo alianza kunihoji maswali.
Baada ya kumjibu jambo lililonishitua zaidi ni pale aliponiambia kuwa ilibainika Shenazia alikuwa ni mgonjwa aliyelazwa katika Hospitali ya Amana siku iliyopita na kutoroshwa, hoja ya msingi ilikuwa mimi nilimtoa wapi na utetezi wangu ni upi juu ya kuhusika kwenye tukio lililompata!
Labels:
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment