ILIPOISHIA:
ILIBIDI nisogee mpaka kwenye maegesho ya bodaboda nikiamini
pale itakuwa rahisi kuzungumza na dereva yeyote ili aniwahishe kabla ile
‘ambulance’ haijapotea kabisa. Nilipopiga hatua moja, nilijiona kuwa
mwepesi sana halafu tambo lilikuwa refu sana tofauti na kawaida.
Sehemu ambayo ningetembea hata hatua ishirini, nilipiga hatua mbili tu, nikawa nimeshafika pale kwenye bodaboda.
SASA ENDELEA HAPA CHINI…
“OYA mambo vipi mkubwa!” nilimsalimu dereva wa bodaboda aliyekuwa
pembeni yangu kwa bashasha kubwa lakini hakuniitikia, akawa anaendelea
kuifutafuta bodaboda yake.
Nilirudia kumsalimu lakini bado hakunijibu chochote na wala
hakuonyesha kama ananisikia. Nilimgusa begani lakini bado ilikuwa ni
kazi bure, aliendelea kufutafuta bodaboda yake, nikabaki nimepigwa na
butwaa.
Ilibidi nimsogelee dereva mwingine wa bodaboda, naye nikamsalimia kwa
bashasha lakini hakunijibu, nikarudia tena na tena lakini bado hali
ilikuwa ileile, nikaenda kwa watatu ambaye alikuwa akipiga stori na
wenzake, naye akaonyesha kutonisikia.
“Kwani imekuwaje? Mbona sielewi kinachoendelea?” nilijisemea huku
nikianza kutetemeka kwa hofu kubwa, mwisho niliamua kufanya jambo moja,
nilipaza sauti kwa nguvu nikiita ‘bodabodaaa!’ niliamini yeyote ambaye
atakuwa wa kwanza kuniona basi nitamchukua huyohuyo lakini wapi! Kila
mmoja aliendelea na mambo yake.
Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba huenda nilikuwa sionekani kwa macho
ya kawaida wala sauti yangu haisikiki licha ya ukweli kwamba mwenyewe
nilikuwa najisikia vizuri tu.
“Sasa nitafanyaje?” nilisema huku nikigeuka kuitazama ile
‘ambulance’, tayari ilishapotea kwenye upeo wa macho yangu lakini akili
zangu zilinituma kuamini kwamba lazima itakuwa imeupeleka mwili wangu
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Nataka nikashuhudie kila kitu kinachoendelea,” nilisema huku
nikianza kutafuta mbinu nyingine ya kunifikisha hospitalini hapo. Sijui
nilipata wapi akili hizo lakini nilijikuta tu nikiamua kuanza kutimua
mbio kuelekea kule ile ambulance ilikoelekea.
Nilipopiga hatua chache tu, nilijikuta nikiwa napaa angani kwa kasi
kubwa, nikawa naitazama mitaa ya jiji kutokea angani. Kuna wakati akili
zangu zilinituma kuamini kabisa kwamba nilikuwa kwenye ndoto ya kutisha
ambayo muda wowote itaisha lakini akili nyingine zikawa zinaniambia
kwamba siyo ndoto, kila kitu kilikuwa kikitokea kwa uhalisia.
Wakati ambulance ikiwasili kwenye geti kuu la kuingilia Muhimbili, na
mimi tayari nilikuwa nimeshafika eneo hilo, geti likafunguliwa na
likaingia moja kwa moja mpaka kwenye eneo la ‘emergency’ ambalo wagonjwa
wenye hali mbaya ndipo walipokuwa wanafikia.
Milango ya ambulance ilifunguliwa, manesi waliokuwa ndani ya ile
ambulance pamoja na wengine waliokuwa pale mapokezi, walisaidiana
kuushusha mwili wangu na kukimbizwa mpaka ndani, nikawa nashuhudia kila
kitu kilichokuwa kinaendelea.
Harakaharaka nilianza kupewa huduma ya kwanza, nikamuona nesi mmoja
akichukua mkasi na kukata shati nililokuwa nimevaa, nilipoliona jeraha
lililokuwa kifuani wangu, nilisisimka mno. Nilijiuliza iweje mtu
anifanyie ukatili mkubwa kiasi hicho, tena bila sababu ya msingi?
Japokuwa vitabu vya dini vinakataza kulipa kisasi, nilijikuta
nikipandwa na ari kubwa ya kulipa kisasi, nilikuwa nimejeruhiwa sana.
Niliwaona hata wale manesi akitetemeka kila walipokuwa wanalitazama
jeraha langu.
Kwa bahati nzuri, madaktari wa kiume waliingia, huwa naamini siku
zote kwamba sisi wanaume Mungu ametuumba na ujasiri mkubwa kuliko
wanawake. Wakaanza kunifanyia kile ambacho kitaalamu huwa kinaitwa ‘dressing’, yaani kusafisha jeraha kabla ya
kuanza kutibiwa. Muda mfupi baadaye, tayari nilikuwa nimesafishwa jeraha
hilo, nikahamishwa na kupelekwa chumba cha wagonjwa mahututi nikiwa
bado sijitambui huku madaktari na manesi wakiendelea kuhangaika
kudhibiti damu zilizokuwa zinaendelea kunitoka kwa wingi.
Nilipoingizwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, harakaharaka
niliunganishwa kwenye mashine ya kunisaidia kupumua huku dripu
ikitiririka kwa kasi kuingia kwenye mishipa yangu.
“He has lost a great deal of blood, he need an urgent transfusion,”
(Amepoteza damu nyingi sana, anahitaji kuongezewa damu haraka
iwezekanavyo) alisema daktari mmoja kwa Kiingereza, kwa kuwa na mimi
shule ilikuwepo kiasi chake kichwani, nilimuelewa vizuri.
Niendelee kusisitiza kwamba wakati haya yote yakitokea, katika
ulimwengu wa kawaida sikuwa na fahamu hata kidogo, nilikuwa nimefumba
macho na kulala pale kitandani kama maiti, nikiwa nimeunganishwa na
mashine ya kunisaidia kupumua lakini katika ulimwengu mwingine ambao
hata sijui niuiteje, nilikuwa nimesimama kwenye pembe moja ya ile wodi,
nikishuhudia kila kilichokuwa kinaendelea.
Kazi ya kuokoa maisha yangu iliendelea, madaktari na manesi wakawa
wanapishana huku na kule, huyu kabeba dawa, huyu kabeba chupa ya damu,
huyu mikasi na sindano, ilimradi kila mmoja alikuwa bize.
Nilijisikia ahueni kubwa ndani ya moyo wangu kuona watu ambao pengine
hata hawakuwa wakinijua, wakipigana kuokoa maisha yangu. Niliendelea
kuwatazama wanavyohangaika, kuna wakati machozi ya uchungu yalikuwa
yakinitoka kwa sababu ya kilichotokea, nikawa naendelea kujiuliza
maswali mengi yaliyokosa majibu.
Nilivuta kumbukumbu ya jinsi mambo yote yalivyoanza kutokea.
***
Januari 16, 2012
Mikocheni, Dar es Salaam.
“Haloo!”
“Haloo, nani mwenzangu.”
“Mh! Kwani namba yangu hujaisevu Moses, mbona una visa wewe.”
“Samahani, utakuwa umekosea namba, mimi siitwi Moses wala sikufahamu.”
“Ooh! Basi samahani kaka yangu nitakuwa nimechanganya namba. Samahani sana.”
“Usijali, kuwa makini,” yalikuwa ni mazungumzo kati yangu na mtu aliyepiga simu na kunifananisha.
Nilikata simu na kubonyeza kitufe kwenye rimoti ya runinga yangu
kubwa (flat screen) niliyokuwa nimekata sauti (mute) baada ya kuona simu
yangu inaita. Nikawa naendelea kutazama muvi kwani miongoni mwa vitu
nilivyokuwa navipenda, ilikuwa ni kutazama muvi, kuangalia mpira na
kusikiliza muziki, hasa muda ninaokuwa nyumbani baada ya kutoka kazini.
Haukupita muda mrefu, simu yangu ikawa inaita tena, nilikasirika kwa
sababu muvi ilikuwa imefika sehemu nzuri na sikutaka inipite hata sehemu
moja, safari hii nilibonyeza kitufe cha ‘pause’ kuisimamisha ili
isiendelee, nilipotazama namba ya mpigaji, ilikuwa ni ileile ya yule mtu
aliyedai kukosea namba.
“Samahani mpendwa najua nakusumbua, nimeangalia vizuri simu yangu na kugundua kuwa ni kweli nilikosea namba wakati nakupigia.”
“Usijali dada, tufanye yameisha.”
“Ahsante kwa kunisamehe kaka yangu, japo sikujui lakini unaonekana
mstaarabu sana. Mimi naitwa Shenaiza sijui mwenzangu unaitwa nani.”
“Naitwa Jamal au kwa kifupi Jay,” nilimjibu kwa kifupi kwa sababu niliona kama ananiletea stori zisizo na kichwa wala miguu.
“Ooh! Nimefurahi kukufahamu kaka Jamal. Unaishi wapi vile?”
“Mikocheni,” nilimjibu na safari hii niliamua kubonyeza tena rimoti,
muvi ikaendelea kwani niliona hana chochote cha maana cha kuniambia,
nikawa nimeiweka simu sikioni huku nikiendelea kuangalia muvi.
“Mbona kuna kelele kwani uko wapi?” alihoji msichana huyo lakini
sikumjibu chochote, naona baadaye alijishtukia mwenyewe, akaamua kukata
simu. Nikaiweka simu pembeni na kuendelea kutazama muvi.
Baadaye ilipoisha, nilichukua simu yangu na kugundua kuwa kulikuwa na
meseji nyingi zimeingia bila mwenyewe kushtukia, nikaanza kuzisoma moja
baada ya nyingine.
Nilishangaa kugundua kwamba ukiachilia mbali meseji mbili za rafiki
zangu, Justice na Prosper, nyingine zote zilikuwa zimetoka kwa yule
msichana aliyekosea namba ya simu, nikashusha pumzi ndefu na kuanza
kuzisoma, moja baada ya nyingine nikiwa
na shauku kubwa ya kutaka kuona ameandika nini.
Je, nini kitafuatia? Meseji zinahusu nini?
Tukutane tena Jumamosi
Thursday, August 3, 2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment