Tuesday, August 8, 2017
Story: SIKU SABA KUZIMU (Sehemu Ya Tatu) 03
ILIPOISHIA:
NILISHANGAA kugundua kwamba ukiachilia mbali meseji mbili za rafiki zangu, Justice na Prosper, nyingine zote zilikuwa zimetoka kwa yule msichana aliyekosea namba ya simu, nikashusha pumzi ndefu na kuanza kuzisoma, moja baada ya nyingine nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kuona ameandika nini.
SASA ENDELEA…
YA kwanza ilisomeka: “Samahani kaka Jamal naomba tuchati kama hutajali.” Nikaisoma na kuirudia zaidi ya mara mbili, sikuelewa maana ya yeye kuomba tuchati ni nini kwa sababu...
tayari nilishamwambia amekosea namba na mwenyewe akakiri hilo.
Hakuishia hapo, meseji nyingine ikasomeka: “Nina tatizo kubwa nilikuwa nahitaji mtu wa kumshirikisha ndiyo maana nikawa nimempigia simu ndugu yangu mmoja aitwaye Moses lakini baada ya kusikia sauti yako, naamini na wewe unaweza kuwa na busara na kunisaidia nini cha kufanya.”
“Mbona hunijibu?” ilisomeka meseji nyingine, nikawa naendelea kuzisoma moja baada ya nyingine ambapo msichana huyo alianza kulalamika kwamba nimemdharau ndiyo maana nilikuwa sitaki kujibu meseji zake, mwisho akaniambia nisimfikirie vibaya na kama ameniudhi anaomba nimsamehe.
Nilishusha pumzi ndefu baada ya kumaliza kusoma meseji zote, nikatafakari kwa kina nikiwa sijui lengo la msichana huyo ni nini hasa. Sina desturi ya kumdharau mtu hata mara moja, hasa anaponiambia ana matatizo. Huwa naamini kwamba hata kama huwezi kumsaidia mtu kwa namna nyingine, ushauri wa kimawazo unaweza kuwa msaada tosha kwake.
Ilibidi nichukue simu yangu na kupiga namba ya yule dada aliyeniambia kwamba anaitwa Shenaiza. Ilipoanza kuita tu, harakaharaka alipokea, nikamueleza kwa nini nilichelewa kujibu meseji zake.
“Nilikuwa na kazi naifanya ndiyo maana sijakujibu, nisamehe kwa hilo,” nilimwambia, harakaharaka akaniambia nisijali na anashukuru kwa kuwa nimempigia kwani tayari alishaanza kujisikia vibaya ndani ya nafsi yake. “Umeniambia una tatizo, naweza kukusikiliza tafadhali,” nilimuuliza kwa sauti ya kiungwana, nikamsikia akishusha pumzi ndefu kisha akaniuliza mahali nilipo.
“Nipo nyumbani, Mikocheni.”
“Mimi nipo Ilala, tunaweza kuonana tafadhali kama hutajali.”
“Mh!” niliguna, nilishindwa kuelewa msichana huyo anataka nini. Haikuwa kawaida yangu kuonana na watu nisiowajua, yaani dakika chache zilizopita mtu anakupigia simu na kukueleza kwamba amekosea namba, muda mfupi tena baadaye anakueleza kwamba ana shida muhimu na anataka kuonana na wewe? Nilijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
Nimewahi kusikia visa vya watu wengi hasa jijini Dar es Salaam ambao walitekwa na kwenda kufanyiwa vitu vibaya baada ya kutegeshewa wanawake. Wengi wanaamini ni wanaume wachache sana wanaoweza kuepuka kishawishi cha mwanamke anayekupigia simu na kuomba kuonana na wewe, hata kama hamfahamiani.
“Hapana, haitawezekana dada’angu, tuzungumze tu kwa simu, leo nina kazi sana,” nilimkatalia kijanja. Msichana huyo aliendelea kung’ang’ania akitaka kuonana na mimi lakini kwa sababu za kiusalama, niliendelea kushikilia msimamo wangu.
Alipoona nimekuwa mgumu, aliniomba basi nipange siku na mahali ambapo tutaonana kwa sababu anahisi kwamba huenda nina wasiwasi naye, nikamwambia asiwe na wasiwasi siku nitakayokuwa na nafasi nitamtaarifu.
“Ila naomba iwe haraka, nina tatizo kubwa mwenzio,” alisema huku sauti yake ikionyesha kwamba alikuwa na huzuni kali ndani ya moyo wake. Nilikata simu na kujilaza kitandani, nikashusha pumzi ndefu na kuendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
Kwa muda mfupi tu niliozungumza naye, tayari tulikuwa kama watu ambao tumefahamiana miaka mingi iliyopita. Sauti yake ilionyesha alikuwa na jambo zito ndani ya moyo wake lakini sikutaka kuwa mwepesi na kujiingiza kichwakichwa, nilikuwa tayari kutoa msaada wowote ambao angeuhitaji lakini pia nilihitaji kuwa na uhakika na maisha yangu.
Muda uliendelea kuyoyoma, kwa kuwa siku hiyo nilikuwa mapumziko nyumbani baada ya kazi za wiki nzima, niliutumia muda wangu mwingi kufanya usafi ndani kwangu, kufua nguo za kazini pamoja na za kushindia na baada ya kumaliza, nilirudi na kuendelea kutazama muvi. Jioni nilitoka na kwenda kwenye mgahawa uliokuwa jirani na pale nilipokuwa naishi, japokuwa nilikuwa nimekamilika kimaisha, nilikuwa mvivu sana kwenye suala zima la kupika kama walivyo vijana wengi ambao hawajaoa.
Kwa hiyo shughuli nyingine zote nilikuwa nikizifanya kwa mikono yangu isipokuwa jambo moja tu; kupika. Japokuwa nilikuwa na umri ambao ningeweza kuwa na msichana wa kunisaidia majukumu madogomadogo ya nyumbani, namaanisha mpenzi lakini nilikuwa nimeamua kuishi ‘single’ hasa kutokana na maumivu makubwa ya moyo niliyoyapata katika uhusiano wangu uliopita.
Tangu nilipoanza kuwa na akili za kikubwa, nilikuwa nimetoka na wasichana wawili tu, tena kwa nyakati tofauti lakini mambo niliyokutana nayo, yalinifanya nisitamani tena kuwa na mpenzi. Nikaamua kutuliza moyo mpaka umri wa kuoa utakapofika na huo ndiyo ulikuwa msimamo wangu.
Baada ya kupata chakula cha jioni, nilirudi nyumbani kwangu na kuendelea na mapumziko yangu. Majira ya kama saa tatu za usiku, yule msichana alinitumia tena ujumbe akinitakia usiku mwema, nami nikamjibu na tukawa tumeishia hapo kwa siku hiyo.
Kesho yake asubuhi, niliwahi kuamka na kuanza kujiandaa kuelekea kazini kama kawaida. Mahali nilipokuwa nafanya kazi, hapakuwa mbali sana na nyumbani kwangu kwa hiyo nilikuwa nikipanda daladala au wakati mwingine nikiwa na fedha za ziada, nakodi Bajaj au bodaboda.
Nilikuwa nikifanya kazi kwenye kampuni ya ukandarasi ya Collins Constructors & Civil Engineering, Mbezi Beach nikiwa kwenye kitengo cha usanifu wa ramani za majengo au kwa Kiingereza Architecture.
Sikuwa nimeanza kazi muda mrefu kwa sababu ndiyo kwanza nilikuwa nimehitimu masomo yangu ya chuo kikuu. Nikiwa kazini, niliendelea na majukumu yangu kama kawaida, ilipofika majira ya kama saa nne, muda ambao kwa kawaida huwa tunapumzika dakika chache kwa ajili ya kifungua kinywa, Shenaiza alinipigia simu kwa lengo la kunijulia hali, tukazungumza kawaida tu kisha akakata simu.
Niliendelea na kazi na kutokana na ubize wangu, sikushika tena simu mpaka saa kumi na moja jioni, muda ambao kwa kawaida huwa tunatoka kazini. Niliposhika simu yangu, nilikutana na ‘missed calls’ nyingi za Shenaiza na ujumbe mmoja ulionishtua sana moyo wangu. Aliniambia kwamba anahisi anakaribia kufa.
Ujumbe uliishia hivyo tu, nikashindwa kuelewa alikuwa anamaanisha nini? Ilibidi nimpigie, simu yake ikawa inaita tu bila kupokelewa. Nilipiga tena na tena lakini hakukuwa na majibu, nikapatwa na wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wangu.
Sikujua msichana huyo amepatwa na nini, nikajihisi kuwa na hatia kwa sababu pengine kama ningekubali kuonana naye jana yake alipotaka nifanye hivyo, ningeweza kuelewa nini kinachomsumbua na pengine ningeweza kumsaidia.
Niliondoka kazini nikiwa ni kama nimechanganyikiwa, sikuwa namjua Shenaiza lakini sijui kwa nini nilihisi kama matatizo yake yalikuwa yakinihusu sana. Nikiwa kwenye kituo cha daladala nikiendelea kusubiri usafiri, ujumbe mfupi uliingia kwenye simu yangu, ulisomeka:
“Mwenye simu hii amelazwa Hospitali ya Amana, Ilala. Hali yake ni mbaya, hawezi kuzungumza.”
Je, nini kitafuatia?
Labels:
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment