Mavoko ameungana na Diamond mwenyewe pamoja na wasanii waliosainishwa awali, Harmonize na Raymond. Pia katika utambulisho wa label hiyo ulioendana sambamba na kumtangaza Mavoko kama msanii wake mpya, Queen Darleen, dada yake Diamond naye... alitambulishwa rasmi kama sehemu ya roaster ya wasanii wa Wasafi Records.
Haya ni mambo matano ambayo nimeyabaini kwenye hatua hiyo:
1. NI ISHARA NYINGINE KUWA MUZIKI WETU UMEKUA
Pale tasnia ya muziki inapokuwa na record label za uhakika, ni ishara kuwa muziki umekua sana na unazidi kuwa rasmi. WCB wanaelekea kuanza kufanya mambo tuliyokuwa tukiyasikia kwenye nchi zilizoendelea tu. Nigeria ndipo wanapotupigia bao. Wana utitiri wa label zenye uwezo wa kugharamia mambo mengi kwa msanii na akafanikiwa kutengenezwa na kubwa mkubwa.
Utambulisho wa Mavoko uliandaliwa katika ukubwa ambao unaonesha kuwa WCB ipo serious na biashara ya muziki. Ndiyo maana, Katibu Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA, Godfrey Mngereza ameipongeza label hiyo.
“Ni vizuri sana tunapowaona wasanii watanzania wanawekeza katika industry ya muziki, kwa hatua hii inaondoa ile dhana kwamba wanaoweza kuwekeza kwenye muziki ni watu toka nje, kwahiyo ni hatua kubwa sana, ni hatua ya msingi sana ambayo Diamond na timu yake yote wameipiga katika kuonyesha dhahiri kwamba kila kitu kinawezekana,” alisema Mngereza Alhamis hii.
“Huu ni mfano kwamba ameingia hatua nyingine ya kuwa na label. Msanii kuwa na label ni hatua ya juu sana katika industry ya sanaa, kwahiyo kwa vyovyote vile tuweze kumpongeza Diamond, na serikali ipo na inatoa support kwa asilimia mia. Kwa Diamond na mameneja wake, lakini na team nzima ya Diamond, kwamba wanachokifanya, si kwa manufaa yao tu, lakini ni kwa manufaa ya maendeleo ya tasnia nzima ya sanaa na taifa kwa ujumla,” alisisitiza.
2. RICH MAVOKO AMECHUKUA UAMUZI MUHIMU MAISHANI MWAKE
January 29 niliandika makala kuhusu iwapo Rich Mavoko kusainishwa kwenye label ya Wasafi kunaweza kuwa kitu sahihi. Kwa mtazamo wangu, huu ni uamuzi muhimu zaidi ambao Rich Mavoko amewahi kuufanya kwenye maisha yake. Kwa kujiunga na label ya Diamond, hitmaker huyo ni sawa na mmea uliokuwa umeathirika na ukame na kisha kupata matone ya mvua na hivyo kuchipuka zaidi.
Mavoko sasa ana maisha mapya, uhakika zaidi katika muziki kwa kuwa kwenye label ya kwanza kubwa Tanzania inayofanya kazi zake kama label zilizopo kwenye nchi za wenzetu. WCB kupitia Diamond si label yenye wasiwasi wa vitu vidogo tena kama bajeti ya kufanya video nzuri, studio, photoshoot, wapiga picha na vitu vingine ambayo wasanii wengi vinawaumiza kichwa.
Mavoko anarudi tena kwenye chati, kwenye midomo ya watu, mtandaoni na kwenye vyombo vya habari, na muda si mrefu anarejea tena kuwa miongoni mwa wasanii wanaopiga show nyingi zaidi Tanzania. Hilo liko wazi hasa ukiangalia mabadiliko waliyonayo Harmonize na Raymond tangu wawe chini ya label hiyo ambao kwa sasa wana msululu wa show zinazolipa.
Ni kama vile kila anachokigusa Diamond hugeuka kuwa dhahabu. Hakuna shaka tutashuhudia Mavoko akigota vilele ambavyo kama angeamua kujaribu mwenyewe ingekuwa safari ndefu na yenye mitihani mingi.
3. KWA DIAMOND BIASHARA KWANZA, USHINDANI BAADAYE
Unapomuona msanii akichukua vijana wenzake kuwasaidia ilhali akiujua uwezo wao kuwa ni wa kuotea mbali, basi hapo ni wazi kuwa anafikiria biashara zaidi kuliko ushindani. Label ni biashara maarufu sana kwenye muziki – in fact ndicho kiini cha muziki wa Marekani. Kwa wenzetu, ni ndoto kwa msanii kutoka mwenyewe bila kupitia record label na wale waliofanikiwa hivyo ni wa kuwahesababu.
Label nyingi kama Def Jam, Warner Music, Universal Music, Sony Music, Atlantic Records ni makampuni yenye uwekezaji wa mabilioni ya dola za watu ambao hata hawatajwi kwenye vyombo vya habari. Kwahiyo pale ambapo msanii anayeendelea kustruggle kwenye muziki lakini akaamua kuwasaini wasanii wenzake, hahofii tena ushindani. Mawazo ya msanii kama huyu ni ya kiujasiriamali zaidi. Na kwa mkataba wa miaka kumi aliosaini Mavoko WCB, pande zote zitaneemeka na huo ni uwekezaji usio na shaka kabisa.
4. MAVOKO NA DIAMOND WANA CHEMISTRY
Mimi ni mmoja wa watu ambao nimeshangazwa na jinsi Rich Mavoko na Diamond wametengeneza chemistry halisi ndani ya muda mfupi. Sina uhakika, lakini sijawahi kusikia iwapo waliwahi kuwa marafiki huko nyuma. Na nakumbuka kuna wakati kulikuwepona ushindani mkubwa katika ya wawili hawa kiasi ambacho kulizaliwa hadi tension ambayo mara nyingi kwa wasanii wengi zimewahi hata kusababisha uadui.
Na hiyo ndiyo ilikuwa shaka kubwa ya watu wengi tangu tetesi za Mavoko kusainishwa WCB zilipoanza kuvuma. Wengi walikuwa na wasiwasi kuwa fahari huyu ataweza kuwa chini ya fahari mwenzake? Picha na video zinaongea jumbe maelfu kuwa wawili hao wana upendo halisi wao kwa wao na Diamond ni kama mzazi anayejivunia kuwa na Mavoko.
Video aliyoipost Diamond ya sherehe ya kumkaribisha staa huyo WCB ikimuonesha akiimba wimbo Ibaki Story, ni kithibitisho kuwa mastaa hao wana chemistry ya nguvu.
5. MAVOKO ANA FURAHA
Naamini moyo wa Rich Mavoko una furaha kubwa sasa. Hicho ni cha muhimu zaidi kuliko hata matarajio mengine makubwa aliyonayo. Tena, video zinaonesha jinsi alivyofurahia kujiunga na himaya hiyo. Support anayopewa na timu nzima ya WCB sasa ni ishara tosha kuwa yupo kwenye mikono salama.
0 comments:
Post a Comment