Pages

Subscribe:

Wednesday, July 19, 2017

STORY: KAHABA KUTOKA CHINA (Sehemu Ya Tatu) 03

Related image
Katika kipindi chote ambacho Peter alikuwa chuoni nchini Afrika Kusini kichwa chake kilikuwa kikimfikiria Rose, msichana ambaye alitokea kumpenda kuliko msichana yeyote maishani mwake. Kila alipomkumbuka, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa kasi huku akianza kujisikia amani moyoni.

Katika kipindi hicho, Peter alikuwa katika mapenzi ya dhati, hakuona sababu yoyote ile ya kuchukua msichana yeyote chuoni hapo na wakati kulikuwa na msichana ambaye...
aliandaliwa kwa ajili yake nchini Tanzania.

Wasichana wengi wazuri wa Kizulu na Xhosa walitamani kuwa na naye lakini Peter hakuwa rahisi kutekwa na wasichana hao, Kwake, ndani ya moyo wake kulikuwa na msichana mmoja tu, Rose ambaye aliingia moyoni, akavuta kiti na kutulia.
 
Hakuwa na habari na wasichana wengine, japokuwa mara nyingi walimtega lakini hiyo haikuwa sababu iliyomfanya Peter kuwafuata na kumtoa Rose moyoni mwake.

Rose alikuwa kila kitu ndani ya moyo wake, alikuwa kama malkia mpya ambaye aliingia ndani ya moyo wake na kuanzisha utawala wa kimapenzi. Katika kila kitu ambacho alikuwa akikifanya, bado alimuamini sana baba yake, Bwana Edward ambaye alimuachia kazi ya kuweza kuongea na baba yake Rose, Bwana Shedrack kuhusu msichana huyo.

“Usijali. Kila kitu kinakwenda safi kabisa. Unasubiriwa wewe tu,” alisema Bwana Edward.
“Kwa hiyo kila kitu safi?”
“Yeah! Si unajua wazee tunajuana bwana. Tunajua namna ya kuongea kiutu uzima. Wewe maliza chuo na kisha njoo!” alisema Bwana Edward.
“Sawasawa. Umenifanya niione miaka miwili kuwa mingi. Kama kila kitu kipo freshi, nitakuja na kufunga naye ndoa,” alisema Peter huku akionekana kuwa mwenye furaha.

“Usijali. Unasubiriwa wewe tu.”
Presha ilizidi kuongezeka moyoni mwa Peter, mawazo juu ya Rose yakaongezeka zaidi na zaidi. Hakuamini kama kazi ambayo alimuachia baba yake ilikuwa imefanyika kwa urahisi sana tofauti na jinsi alivyokuwa akifikiria kabla. Muda mwingi chuoni alionekana kuwa na furaha, kitendo cha kufanyiwa kazi yake kilimpa furaha kupita kawaida.

Mwaka wa kwanza ukakatika chuoni, hakutaka kurudi nchini Tanzania kwa sababu alikuwa na mambo mengi ya kufanya. Akabaki nchini Afrika Kusini mpaka mwaka wa pili kuingia. Katika kipindi hicho bado mawazo yake juu ya Rose hayakuweza kumtoka hata kidogo, alikuwa akiendelea kumfikiria msichana huyo.

Miezi ikaendelea kukatika mpaka kufikia kipindi ambacho alitakiwa kufanya mitihani yake ya mwisho. Alijitahidi sana kusoma, moyo wake ulikuwa umegawanyika katika vyumba viwili. Nusu ulikuwa ukifikiria kuhusiana na masomo na nusu ulikuwa ukimfikiria Rose. Mitihani ilipokwisha, akaanza kujiandaa na safari yakurudi nchini Tanzania.

Ndani ya ndege, aliiona ndege hiyo ikichelewa kufika nchini Tanzania. Alitamani yeye ndiye angekuwa rubani aiendesha ndege hiyo kwa kasi zaidi na kuingia nchini Tanzania. Hakukuwa na kitu alichokipanga kwa wakati huo zaidi ya kufika nchini Tanzania na kufunga ndoa na Rose ambaye aliamini kwamba uzuri wa msichana huyo ulikuwa umeongezeka maradufu.

Mpaka ndege inakanyaga ardhi ya Tanzania, mapigo ya moyo wake yalidunda mno, hamu ya kumtia machoni Rose ilikuwa imemkaba kupita kawaida. Kwa mwendo wa harakaharaka akashuka kwenye ndege ile na kuanza kuelekea katika jengo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kuchukua mzigo wake.
“Nimewakumbuka sana,” alisema Peter baada ya kuwaona wazazi wake, akawakumbatia.

“Karibu tena nchini Tanzania,” alisema Bwana Edward.
“Nimekwishakaribia. Nilidhani mngekuja na Rose kuja kunipokea,” alisema Peter wakati wakiingia ndani ya gari.

“Usijali. Hatukutaka kumtaarifu kwani tulitaka kumfanyia sapraizi,” alisema Bwana Edward na kuwasha gari na kuondoka mahali hapo.
Kila kitu kikaonekana kukamilikia. Walipofika nyumbani, Bwana Edward hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kuanza kuwasiliana na Bwana Shedrack na kumwambia kwamba kijana wake tayari alikuwa amekwishaingia nchini Tanzania na hivyo alitaka kuonana naye.

“Hilo si tatizo. Tunaweza kuonana,” alisikika Bwana Shedrack kwenye simu.
“Sawa. Nije hapohapo nyumbani kwako au?”
“Vyovyote vile lakini kama tukionana sehemu yoyote tulivu ya vinywaji itakuwa bora zaidi,” alisema Bwana Shedrack.

Wakapanga sehemu ya kukutania, walipoonana kila mmoja alionekana kuwa na furaha, wakakubaliana kwamba ilikuwa ni lazima vijana wao wafunge ndoa na hatimae kuishi pamoja kama mume na mke na kuufanya urafiki wao kuwa karibu zaidi ya ndugu.

Walichokiona ambacho kilikuwa bora zaidi ni kumtaka Peter kuja nyumbani ili aweze kuonana na Rose kama hatua mojawapo ya wawili hao kuzoena na mambo mengine kuendelea.

Hilo halikuwa tatizo kwa Peter, siku iliyofuata, wakati wa mchana akaenda nyumbani kwa mzee Shedrack kama alivyoambiwa.
Alipofika nyumbani hapo, akapiga honi, mlinzi akafungua geti dogo, akatoka nje na kumhoji Peter maswali kadhaa kabla ya kumruhusu. Peter akajitambulisha, geti kubwa likafunguliwa na kuliingiza gari lake na kuliegesha.

Peter akateremka, katika kipindi hicho, mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa kasi kupita kawaida, akaanza kuufuata mlango wa kuingilia sebuleni na kuanza kuugonga.

Mlango ukafunguliwa na John, kwa sababu alikuwa akifahamiana na John, wakaanza kuongea kwa furaha na kuingia ndani. Macho ya Peter hayakutulia, japokuwa John alikuwepo mahali hapo huku akiongea naye maneno mengi lakini macho yake yalikuwa na kiu ya kumuona Rose tu.

“Rose yupo?” aliuliza Peter.
“Yupo. Nimuite umsalimie?”
“Itakuwa vizuri sana.”

John hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuelekea chumbani kwa Rose kwa ajili ya kumuita msichana huyo. Peter alibaki akiwa na presha kubwa, hakuamini kwamba mara baada ya kusubiri kwa miaka miwili siku hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kumtia machoni Rose kwa mara nyingine tena. Alibaki kochini kwa dakika kadhaa, John akarudi mahali hapo huku akiongozana na Rose.

Mapigo ya moyo ya Peter yakaongezeka kasi zaidi, mzunguko wake wa damu ukawa mkubwa kupita kawaida. Peter akajihisi kipindi chochote kile angezimia kwa presha mara baada ya kumtia machoni Rose.

Ule uzuri aliokuwanao katika kipindi cha nyuma ukaonekana kuongezeka maradufu, hakuamini kama Rose alikuwa akionekana kuwa mrembo namna ile.

Miguu yake ikawa mizito kusimama, macho yake hayakuweza kutoka usoni mwa Rose, lipsi za mdomo wake zikaanza kuchezacheza huku kwa mbali akiuhisi mwili wake kuanza kutokwa na kijasho chembamba cha wasiwasi.

“Habari yako,” Rose alimsalimia Peter ambaye bado alikuwa akimwangalia huku akionekana kuwa na mshangao.
“Nzuri. Karibu Rose,” Peter alimwambia Rose.

Rose, msichana aliyekuwa akimfikiria kwa takribani miaka miwili leo hii alikuwa mbele yake, msichana ambaye alikuwa akimpa nafasi kubwa moyoni mwake leo hii alikuwa amekaa mbele yake huku akimwangalia.

Muda wote Peter alionekana kuwa na furaha, hakuamini kama yule Rose ambaye alikuwa akimfikiria kwa kipindi kirefu leo alikuwa mbele yake. Wakati mwingine alijiona kuwa na uhitaji wa kumfuata Rose na kumkumbatia kwa dakika kadhaa japo aanze kulihisi joto la mwili wake.

“Rose,” aliita Peter bila kupenda.
“Abeeee.”
“Nimekukumbuka sana,” alisema Peter ambaye alibaki kimya kwa muda.
John akahisi kitu, muonekano ambao alikuwa nao Peter ulionekana kuwa muonekano mwingine kabisa, alichokifanya ni kuinuka na kuelekea chumbani.

“Umekuwa mzuri maradufu,” alisema Peter, muda huo Rose alibaki kimya.
Peter akaona kwamba kama angeongea maneno matupu ilikuwa ni sawa na kutwanga maji kwenye kitu huku ukisubiria yasagike. Alichokifanya ni kuinuka pale kochini na kisha kuanza kumsogelea Rose katika kochi lile na kukaa karibu yake. Alipoupeleka mkono na kumgusa tu, Peter akajihisi akisisimka kupita kawaida.

“Rose…!” Peter aliita kwa sauti ya chini.
“Abee” Rose aliitikia.
“Nakupenda,” Peter alimwambia Rose.
“Nafahamu.”
“Ninahitaji kukuoa na kuwa mke wangu wa ndoa hapo baadaye,” Peter alimwambia Rose huku akiwa ameushika mkono wake.
“Kunioa?”
“Ndiyo!”
“Sidhani!”
“Kwa nini tena?”
“Nahisi sistahili kuolewa!”
“Kwa nini?”
“Basi tu!”
“Hapana Rose. Nimekuwa nikikusubiria kwa miaka miwili mpaka sasa, nimekuwa nikiwakataa wasichana wengine kwa ajili yako, hebu fikiria muda wangu nilioupoteza kwa ajili yako Rose,” Peter alimwambia Rose.
“Najua.”

“Sasa kwa nini hutaki nikuoe?”
“Unakumbuka nilikwambia nini kipindi cha nyuma?”
“Hapana.”
“Nilikwambia kwamba sikutaki.”
“Rose…pleaseeee.”
“Huo ndiyo ukweli. Mbaya zaidi sina hata ndoto za kuolewa na mwanaume yeyote yule,” Rose alimwambia Peter na kusimama kutoka kochini pale na kisha kuanza kuondoka.
“Rose…Rose…Rose…” Peter aliita lakini Rose hakusimama wala kugeuka, akapotea machoni mwake.

Peter aliumia, aliumia zaidi ya maumivu ambayo aliumia katika maisha yake ya nyuma. Hakuamini kwamba kwa miaka miwili ambayo alikuwa ameipoteza kwa ajili ya kumsubiria msichana huyo leo hii alikuwa akimwambia kwamba hakuwa akimpenda na wala hakuwa na ndoto za kuolewa na mwanaume yeyote yule.

Peter alijihisi kuchanganyikiwa, bila kutegemea akayahisi macho yake yakianza kulengwa na machozi na baada ya dakika kadhaa machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake. Maneno ya Rose yalikuwa yamemchoma moyo wake, alipata maumivu ambayo hakuwa akiyafikiria kabla.

Hapo ndipo akaanza kushikwa na shaka kwamba inawezekana Bwana Shedrack hakuwa ameongea na binti yake zaidi ya kumtaka Peter mwenyewe kufika mahali hapo na kuongea naye.

Alichokifanya ni kusimama na kutoka nje. Katika kipindi hicho, safari yake ilikuwa ni kuelekea katika kambi ya jeshi ya Lugalo kwa ajili ya kuonana na Bwana Shedrack na kumuuliza kile kilichotokea kwani kama angekuwa ameongea naye kabla basi msichana huyo asingeweza kumkataa kiasi kile.

Peter akaanza kuondoka. Akaingia ndani ya gari lake na kuliondoa mahali hapo. Bado moyo wake ulikuwa na maumivu makali mno. Hakuamini kwamba kweli msichana Rose alimkataa namna ile huku akimwambia dhahiri kwamba hakufikiria kuolewa na mwanaume yeyote yule.

“Kwa hiyo hatoolewa? Kwa nini aliniambia hivyo? Baba yake alimkataza au anataka kuwa sista?” alijiuliza Peter huku akiendesha gari lake.
Hakujua kwamba nyuma ya kila kitu kulikuwa na mtu mmoja tu ambaye alifanya kila kitu kutowezekana kwa wakati huo. Peter hakujua kwamba kwa kila kitu kilichoendelea kulikuwa na mtu aliyeitwa Irene, mtu ambaye alikuwa amepigilia msumali wa mwisho katika moyo wa Rose wa kumkataa kila mwanaume ambaye angemfuata.

Kauli ya Rose kwamba hakuwa tayari kuolewa na mwauame yeyote haikueleweka kwa Peter, hakuelewa kama kauli ile ilimaanisha kwamba hakuwa tayari kuolewa na mwanaume yeyote yule bali alikuwa tayari kuolewa na mwanamke, hasa Irene ambaye alikuwa amemuingiza katika ulimwengu mpya wa mapenzi.
Je, nini kitaendelea?

0 comments:

Post a Comment