Kwa wale ambao tuna nywele asilia a.k.a natural hair, tayari
tunafahamu changamoto kadhaa tunazokumbana nazo. Kwa wale mnaofikiria
kuanza kuwa na nywele asilia,karibuni sana tuendelee kujuzana namna ya
kutunza nywele zetu kama tulivyopewa na Mungu.
Je,unazifahamu nywele zako
vizuri? Una nywele za aina gani? Zina tabia gani? Zinataka nini?
1.Kuzikubali kama zilivyo na kuzipenda. Tatizo ni
kwamba hamjafahamiana vizuri yani wewe na nywele zako. Hata mimi
niligombana nazo sana huko nyuma kabla ya kuzielewa vizuri. Jenga ...
mahusiano mazuri tu na nywele zako,zielewe,ukifikia hapo utaanza
kuzipatia hata hazitakusumbua.
2.Usafi wa ngozi ya nywele na nywele zenyewe.
Nywele zenye afya huanzia kwenye ngozi safi ya nywele.Nafahamu
unataka nywele zako zisidumae kwa hiyo zioshe vizuri.Wakati uliopita
nilizungumzia kuziosha kwa product zilizo rafiki( ‘friendly’) .Ngozi
safi ya nywele itasababisha nywele kupata njia ya kujitokeza nje kwa
urahisi.Unapoziacha chafu,ule uchafu unaziba matundu ya nywele zako na
kuzuia njia,kama ambavyo matundu ya uso yakiziba unapata machunusi maana
uchafu unajaa basi kwa nywele hazitakua vizuri.
3.Linda unyevu wa nywele zako
Kila mtu akisikia kiu hunywa maji. Nywele zako zinahitaji kulindwa
zisisikie kiu. Unapoziosha,yale mafuta asilia ya kuzilinda huondoka na
uchafu.Nywele inabaki ikiwa na udhaifu fulani maana haiwezi hata
kushikilia hayo maji yaliyopo vizuri,na zikikauka zinakua kavu sana. Ni
vizuri kabla hazijakauka vizuri,ukazi-’condition’.Kwa nywele ambazo ni
nyepesi na chache,pia kuna product za kuzisaidia ziweze kutunza vizuri
unyevu na hivyo kuwa na afya nzuri.
4.Zifahamu nywele zako
Yani hapa ndo shule ilipolalia kabisaa maana ukizijua tu basi
utazihudumia kwa usahihi.Unatakiwa kuangalia namna gani nywele zako
zinanyonya unyevu.Unajuaje?
Chukua kikombe,kijaze maji safi.Ukipata glass itakuwa vizuri zaidi.
Chomoa unywele mmoja kichwani,hakikisha unatoka na kale kamzizi kake keupe keupe hivi.
Tumbukiza unywele wako kwenye glass yako ya maji hakikisha imeingia
yote.Kama ikizama hapo hapo na hainyanyuki tena,basi nywele zako
zinanyonya unyevu kwa haraka kabisa.Kama inachukua muda kuzama,au
haizami kabisa,nywele zako zinanyonya unyevu taratibu au zinanyonya kwa
shida.
(Wala usihofu,zipo namna ya kuzifanya zinyonye unyevu kwa
haraka,tutajuzana.)Ni kwamba ‘cuticle’ zake zimefunga haswa,ndio maana
unyevu au maji haviingii kwa haraka.
Kwa hiyo ukifanya ‘deep conditioner’ kwa kutumia joto kama la drier
lakini uwe moto mdogo sana au ufanye ‘hot oil treatment’ itakusaidia
‘cuticle’kufunguka na unyevu kupita.
Mbadala,unaweza baada ya kuosha suuza na maji ya uvuguvugu halafu weka mafuta ya kimiminika.Inasaidia sana.
Mimi nina aina gani?..Nina nywele zinazonyonya unyevu haraka.
5.Mafuta ya Kupaka kichwani.
Ni ya muhimu mnoo!.Nimefanya utafiti wa kina nimeona mafuta ya nazi
yanaweka afya nzuri kwa nywele aina nyingi hivyo na mimi nikaanza
kuyatumia.Kwangu mimi,mafuta ya nazi ya kutengeneza mwenyewe
yamenikubali sana.Japo huwa nanunua pia mafuta kama ya Zaituni
Olive(extra virgin) na ya Tea tree.
6.Kuzichambua vizuri kabla ya kuchana.
Uwe mkarimu na mwenye subira kwa nywele zako.Mimi zikijifunga huwa
nazichambua kwa mikono taratibu wakati mwingine nazilowesha na maji kwa
mbali halafu nachana kwa chanuo lenye mapana sio ambalo reli zake
zimebanana.sio kitana.Chanuo kubwa(wide toothed comb).
7.Usizisumbue mara kwa mara na usuke mitindo ya kuzitunza zikue.
Kama unataka zikue haraka,usizisumbue sana.Unaweza ukasuka mitindo
mizuri tu ukakaa nazo wiki nzima au kadri zitakavyodumu.Au upunguze
kuzichana mara kwa mara lakini utafute siku kama wikiendi ukae
uzichambue taratibu na vidole kuondoa mafundo.Kuchana mara kwa mara
zinapukutika,zinaanguka.Zitakua lakini sio kwa kasi ya kama ukizisuka
ukaziacha kwa muda.
8.Punguza matumizi ya vitu vya moto kwenye nywele zako kama pasi ya
nywele na vingine vya hivyo.Mimi dryer la nywele situmii zaidi ya mara
mbili kwa mwezi.Mara nyingi naziacha zikauke na hewa hata kama
nimezifunga rollers natoa kesho baada ya masaa 24.
Kwa leo naishia hapa.Tukutane tena wakati ujao kwenye kujuzana
zaidi.Unakaribishwa kwa maoni,ushauri na kupendekeza mada yoyote
izungumziwe kuhusu nywele asilia.
Mada ijayo tutazungumzia aina za nywele zilizopo humu duniani kwa ujumla.
Nakutakia mapenzi mema ya nywele zako,natumaini mmefahamiana kiasi sasa.
0 comments:
Post a Comment