SEHEMU YA KWANZA
Nilikuwa nimeongozana na mke wangu tukitokea dukani eneo
lile la ugenini. Nikiwa ‘busy’ kwenye simu yangu huku nikiongea na mke
wangu ambaye alikuwa nyuma yangu akinisemesha hili na lile.
Mara nikagundua hali isiyo ya kawaida, mke wangu alikuwa kimya ghafla. Nikageuka haraka kutaka kujua nini kilimfanya awe kimya namna ile, lakini cha ajabu sikumuona mke wangu. “Khaaa...
Uamuzi nilioufikia haraka ni kurudi nyuma kujaribu kumtafuta huku nikimpigia simu kwa maana nakumbuka alitoka nyumbani na simu yake. Kitu
cha ajabu simu yake iliita nyuma yangu baada ya kuwa nimetembea hatua
chache tu. Niligeuka nikaufuata muito ule wa simu ambao nilikuwa
nikiujua kuwa ni wa simu ya mke wangu.
Kweli ilikuwa simu ya mke wangu ikiwa pale chini ikiendelea kuita.
Nilishikwa na bumbuwazi kwa sekunde chache nisijue hata cha kufanya, kisha nikaiokota ile simu na kuanza upya safari ya kurudi eneo lile la madukani kujaribu kuona kama naweza kumuona mke wangu.
Nilitembea huku nikiangaza huku na huko nikiamini pengine ningemuona mke
wangu lakini mpaka nafika eneo lile la maduka sikuwa nimemuona.
Nikajaribu kuvuka eneo lile na kuangalia maeneo ya mbele zaidi ila sikumuona. Akili ikaniambia labda atakuwa amekwenda nyumbani, nikakimbia mpaka nyumbani ila mlango ulikuwa umefungwa kama ambavyo tuliuacha, mke wangu hakuwepo na funguo alikuwa nazo yeye. Sikuwa na sehemu nyingine ya kumuangalia kwa maana tulikuwa hata hatujazoeana na majirani.
Moja kwa moja nikaenda mpaka duka lile ambalo tulikuwa tumenunua bidhaa
dakika chache zilizopita kwani ndilo duka pekee ambalo tulikuwa
tukinunua kwa muda wote wa siku tatu tangu tuhamie mji ule. Hata muuzaji
wa duka lile tulikuwa tumeanza kuzoeana hivyo sikuwa na mtu mwingine wa
kumfuata wakati ule zaidi yake.
“Samahani Mangi” Nilianza kumsemesha mara baada ya mteja aliyekuwa akimuhudumia
kuondoka.
“Samahani Mangi” Nilianza kumsemesha mara baada ya mteja aliyekuwa akimuhudumia
kuondoka.
“Aisee mke wangu hajafika hapa?” niliuliza nikilingojea jibu kwa hamu huku nikitamani awe na chochote cha kusema ambacho kingesaidia kumpata mke wangu kwa maana hofu kubwa ilikuwa imeniingia tayari.
Mangi alionekana kunishangaa kidodgo kisha akauliza “Wewe si umeondoka
hapa na mke wako hata dakika kumi hazijaisha?” kufika hapo nikachoka
kabisa na kujikuta nikikaa kwenye benchi ambalo lilikuwa nnje pale
dukani. Mwili wangu ulikuwa ukitetemeka kiasi ambacho kilimshangaza
Mangi ambaye wakati huo alikuwa akijaribu kunisemesha lakini hata
sikumbuki alikuwa anaongea nini kwa maana akili yangu hata haikuwa pale
na wala sijui ilikuwa wapi.
Kugutuka nilimuona Mangi akiwa amesimama mbele yangu pamoja na watu wengine ambao walionekena kuwa wenyeji wa eneo lile wakitaka kujua nini kilikuwa kimetokea.
Usikose Sehemu ya Pili.
0 comments:
Post a Comment