Pages

Subscribe:

Wednesday, April 5, 2017

KISA KAMILI CHA BINTI ALIYE JITUPA BAHARINI WAKATI AKIRUDISHWA ZANZIBAR

KISA cha binti mwenye umri wa miaka 16 (jina linahifadhiwa kutokana na miaka yake) kujitupa baharini akiwa katika boti ya Kilimanjaro V akitoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar juzi, kinaanzia kwenye mawasiliano yake na mvulana mmoja, kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, imefahamika.

Msichana huyo alikuwa akiwasiliana na mvulana huyo ambaye walifahamiana kupitia Facebook, kwa kutumia simu ya mkononi.
Mwandishi alifika Kikwajuni, nyumbani kwa msichana huyo ambaye ni... mwanafunzi wa kidato cha tatu (shule inahifadhiwa) na kuikuta familia yake ikiwa na majonzi, huku wakiwa hawaamini kilichotokea na binti huyo akiwa bado hai.

Akizungumza kwa huzuni, mama mdogo wa msichana huyo, Asha Saleh Mandhi, alisema palitokea mzozo baina yake na binti huyo baada ya kumkuta na simu ya mkononi wakati wazazi wake hawajamnunulia.

Alisema Jumatano iliyopita majira ya jioni akiwa nyumbani hapo na baada ya kupata taarifa kuwa mtoto wake wa kumlea anamiliki simu, alimwita na kumtaka aeleze amepewa na nani la sivyo atampeleka polisi akajieleze.

Alisema siku ya pili yake asubuhi, msichana huyo alitoroka nyumbani na ndipo alipotoa taarifa kituo cha polisi Madema kuwa amepotelewa na mtoto.

“Mimi ndiye ninayemlea huyu mtoto. Kwa kweli sijui amefikwa na mtihani gani kwa sababu hatujampa simu, lakini nashangaa tumemkuta na simu na hakutaka kumtaja aliyempa," Asha alisema.

"Kitendo cha kumuuliza ndicho kilichomfanya kukimbia na kwenda kusikojulikana.”

Mama mdogo huyo alisema baada ya kuwa ametoroka, aliichukua simu hiyo na kuangalia mawasiliano yake na ndipo alipofanikiwa kupata jina la kijana mmoja wa kiume ambaye alikuwa anawasiliana naye mara kwa mara. Hakumtaja.

Alisema baada ya kumpata kijana huyo kwa njia ya simu, aliulizwa anamfahamu vipi binti yao na kujibu kuwa wamejuana kupitia Fecbook, lakini hawajawahi kuonana kwa sababu yeye anaishi Dar es Salaam na binti anaishi Zanzibar.

Alisema alimpa taarifa kijana huyo kuwa binti yao ametoroka na haijulikani alikokwenda, hivyo kumwomba kusaidiana kuhakikisha wanampata akiwa salama.

“Kwa kweli huyo kijana alikubali kutoa ushirikiano na akawa anawasiliana na binti yetu na kumueleza kuwa yuko Dar es Salaam na amehifadhiwa na dereva teksi baada ya kukosa msaada wa eneo analotaka kwenda ambako ni kwa bibi yake anayeishi Mburahati, Dar es Salaam,” alisema.

Alisema aliwasiliana na dereva huyo ambaye alimueleza kuwa amesharipoti katika serikali ya mtaa katika eneo analoishi kuwa amemwokota binti huyo bandarini, Dar es Salaam baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kupata msaada.

Mama mdogo huyo alisema mama mzazi wa binti huyo anaishi Muscat, Oman na kwamba amemlea tangu akiwa mdogo.

Alisema walipata mshtuko baada ya kupata taarifa kuwa binti yao amejitupa baharini wakati akitokea Dar es Salaam baada ya kusakwa kwa siku kadhaa na hatimaye kupatikana.

MFANYAKAZI WA NDANI
Mmoja wa mashuhuda na mfanyakazi wa ndani katika nyumba anayoishi manusura huyo alisema wakati akiwa katika boti wakitokea Dar es Salaam juzi, walipata taarifa kuwa kuna mtu amejitupa baada ya kufika Chumbe, lakini hakujua kuwa aliyejitupa anamfamu.

“Baada ya kupata taarifa kuwa kuna mtu kajitupa baharini, tukaanza kupiga kelele na nilimwona akielea baharini, lakini nilijua ni mtoto wa kizungu bila kufahamu kuwa nilikuwa namfahamu,” alisema Hiyari Miraji Othman.

Alisema alikuja kufahamu kuwa anamfahamu manusura baada ya saa nne na kwamba hakutegemea angeweza kufanya kitendo hicho.

Alimwelezea msichana huyo kuwa ni mpole na mwenye nidhamu kwa kuwa amekuwa akimuona hivyo nyumbani kwao Kikwajuni kwa muda mrefu.

“Hapa kwao nakuja kila siku kwa sababu ndipo penye kibarua changu," alisema.


"Hapa huwa tunapika vyakula kwa ajili ya biashara na huwa namwona tabia zake ni mtoto mzuri anayejielewa.”

0 comments:

Post a Comment