Pages

Subscribe:

Thursday, April 6, 2017

Story: FUTA MACHOZI MPENZI -- 02


ILIPOTOKA
Msichana mrembo, mwenye umbo matata, Pamela Ndanshau anakutana na Mzee Edward alipokuwa barabarani usiku wa manane. Mwanaume huyo anatokea kumpenda msichana huyo, anampa lifti na kumpeleka nyumbani kwao, Manzese.
Hajui historia ya msichana huyo, hajui kipindi kigumu anachopitia msichana huyo mrembo, anachokijua yeye ni kwamba msichana huyo anahitaji furaha, hivyo anachukua namba yake ya simu na kupanga kuzungumza naye.


SONGA NAYO

“Pamela! Upo wapi?” ilisikika sauti ya mwanaume kwenye simu, haikuwa sauti ya kawaida, ilikuwa ni sauti ya ukali. “Nyumbani baby!” alijibu...
Pamela kwa sauti ya upole.
“Jana ulikuwa wapi?”
“Nilikwenda kwa rafiki yangu Zaituni, si nilikwambia kama kuna sherehe ya siku yake ya kuzaliwa,” alijibu Pamela kwa sauti ya upole kabisa.
“Wewe mwanamke malaya sana. Mbona hukuniambia wakati unarudi? Au ulipitia kwa mabwana zako? Yaani wewe kila siku umalaya tu, hivi unaona sifa kuwa malaya kukitembeza kwa kila mtu?” aliuliza jamaa huyo kwa sauti ya ukali, alikasirika mno.
“Hapana mpenzi laki...” alisema Pamela lakini hata kabla hajamaliza sentensi yake, jamaa huyo akakata simu.


Moyo wake ulinyong’onyea, aliumia moyoni mwake, mwanaume aliyekuwa amempigia simu aliitwa Dickson. Huyo alikuwa mwanaume wake wa kwanza, hakuwahi kubadilisha mwanaume yeyote zaidi ya huyo.


Alimpenda sana Dickson, walikaa kwenye uhusiano kwa miaka zaidi ya mitano huku mwanaume huyo akiwa kila kitu kwake. Walipeana ahadi nyingi kwamba wangeona na kujenga familia pamoja, maneno hayo yalimchanganya Pamela na kuamua kumpa moyo wake Dickson.


Baada ya kukaa kwenye mahusiano kwa kipindi fulani, Pamela akapata ujauzito kitu ambacho hakumficha Dickson, akamwambia ukweli lakini tofauti na mategemeo yake, Dickson akamwambia kwamba ule ujauzito haukuwa wake, hivyo hakuutambua.


Pamela alihuzunika, hakuwa na mwanaume mwingine zaidi ya huyo, hakuwahi kumvulia nguo mwanaume yeyote na kufanya naye mapenzi, mwanaume ambaye aliwahi kumfanyia hivyo alikuwa Dickson tu na ndiye aliyempa mimba lakini mwisho wa siku mwanaume huyohuyo alimwambia kwamba mimba haikuwa yake.
Dickson akakaa na kujifikiria, akaona kwamba kwa kadiri muda unavyokwenda, mimba ile ingeongezeka na yeye hakuwa tayari kuzaa na Pamela, alichomwambia ni kutoa mimba ile.


“Nitakufa...” alisema Pamela.
“Hutoweza kufa! Wewe toa tu!”
“Sina hela, wewe mwenyewe si unajua tulivyo masikini!” alisema Pamela.
“Nitakupa hela.”
“Basi sawa!”


Wakakubaliana, baada ya siku mbili, tayari Dickson akapata kiasi cha fedha kilichohitajika na hatimaye mimba kutolewa. Hilo ndilo alilolitaka, hakumjali sana Pamela, kwake alikuwa mwanamke wa starehe, mapenzi yalikwisha moyoni mwake na kitu pekee kilichokuwa kimebaki ni mazoea tu.


Wakati yeye akichukulia mazoea katika mapenzi hayo, kwa Pamela ilikuwa balaa, moyo wake ulikufa na kuoza kwa Dickson, usiku hakulala vizuri, alichanganyikiwa kwa penzi lake na muda wote alikuwa akimuhitaji lakini mwanaume huyo hakujali.
Hakuwa anapokea simu, aliwasiliana na Pamela siku ambayo alihitaji kufanya hivyo. Mawazo yalimuendesha, mwili wake ukapungua kiasi kwamba kila mtu alimshangaa.
Siku ambazo Dickson alipojisikia kufanya mapenzi, aliwatafuta wanawake wake wengine, walipomwambia kwamba walikuwa kwenye siku zao, akamtafuta Pamela ambaye hakuwa na kinyongo, alimpenda sana Dickson hivyo kama kawaida akaitanua miguu yake tena.


Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake, yalimuumiza lakini hakuwa na jinsi, alitamani kuendelea kuwa na mwanaume huyo kwa sababu alimpenda kwa moyo wa dhati. Siku zikakatika mpaka alipopata mimba ya pili.


Alishangaa, hakujua iliingiaje na wakati alikuwa akitumia mpira, hakujua kama wakati wa kufanya mchezo huo, katikati Dickson alikuwa akiutoa mpira na kufanya bila mpira. Akili yake ilichanganyikiwa mno, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, alimwambia Dickson ambaye naye alibaki akishangaa tu, hakutaka kukubali kama hiyo ilikuwa mimba yake.


“Haiwezekani! Hii ni mara ya pili, utakuwa na mwanaume mwingine,” alisema Dickson huku akionekana kuchukia.


Hiyo mimba nayo ikatolewa, mwili wake ulichoka hata kabla hakuwa mke wa mtu. Huo ndiyo ukawa mwisho wa kuwa na Dickson, moyo wake ulimuuma lakini hakuwa na jinsi kwani alimpenda kupita kawaida.


Aliendelea kukaa nyumbani, baada ya mwaka mmoja, Dickson akamrudia tena, akamuomba msamaha, ilikuwa vigumu kwa msichana huyo kukubali lakini mwisho wa siku akaamua kumsamehe kwa sababu alimpenda, hivyo mapenzi kuanza tena.


Mpaka anakutana na mzee Edward, ilikuwa imepita wiki moja tangu kurudiana na Dickson, hakuwa na mapenzi makubwa kwa Dickson lakini alishindwa kumuacha kwa sababu tu alihisi moyo wake ukimpenda mno.
“Nilijua tu wewe malaya! Ulikwenda kutembea na mabwana zako huko halafu unamsingizia Zaituni,” alisema Dickson kwenye simu.
“Nisamehe mpenzi...”
“Hebu toka huko! Nisamehe inasaidia nini,” alisema Dickson na kukata simu.


Japokuwa mapenzi yalikuwa ni furaha lakini kwa Pamela yalikuwa ni sawa na kuishi kwenye tanuru la moto. Hakukuwa na siku ambayo aliyafurahia mapenzi aliyokuwa nayo kwa Dickson, kila siku alijiona akipitia katika maumivu makubwa lakini bado msimamo wake ulikuwa ni kumshikilia huyo Dickson ambaye hakuonekana kujali chochote kile.


Tangu alipomlalamikia na kukata simu, Dickson hakutaka kupiga tena, kwake, alijua kwamba Pamela hakuwa akipindua, hata kama angemkuta amelala na wanawake, bado msichana huyo angemsamehe na kufanya kile alichokitaka.


Mapenzi mazito ya Pamela yakawa kama fimbo ya kumchapia, hakujua msichana huyo alijisikiaje, hakujua ni kwa jinsi gani aliumia moyoni mwake, kitu alichokijali ni kwamba alipotaka penzi alipewa bila kinyongo chochote kile.


Wakati yeye akiringa, wakati akimuona Pamela hakuwa na thamani yoyote ile ndicho kipindi ambacho Mzee Edward akaingia kwa nguvu zote. Mzee huyo akatokea kumpenda Pamela, kwake alionekana kuwa msichana wa tofauti, mwenye uzuri wa ajabu ambao uliutikisa mtima wa moyo wake.


Baada ya kupewa namba ya simu, siku iliyofuata akampigia simu Pamela na kuzungumza naye. Hakutaka kumficha, alimwambia kwamba alimpenda na alitaka kumfanya mwanamke mwenye furaha kuliko wanawake wote aliowahi kuwa nao.
“Na mkeo je?” aliuliza Pamela.


“Mke wangu anaumwa sana Pamela. Sidhani kama atapona,” alijibu mzee huyo.
“Mmh! Sasa si ndiyo muda wa kumfariji!”
“Pamela! Siwezi kukuficha kitu chochote. Ninampenda sana mke wangu, nimekuwa naye tangu nilipokuwa masikini mpaka leo hii! Ninamthamini zaidi ya mtu yeyote katika dunia hii. Kila siku nimekuwa nikimlaumu Mungu kwa kumlaza mke wangu kitandani kwa mwaka mmoja na nusu. Kila nikimwangalia, nahisi atakufa, ninaumia kwa mawazo na ndiyo maana niliamua kutafuta msichana ambaye ataniondolea mawazo, ikitokea mke wangu akafa, basi nimuoe yeye,” alisema mzee huyo, wakati akiyazungumza hayo, sauti yake ilitoka na kwikwi kuonyesha kwamba aliumizwa na kilichokuwa kikiendelea.


“Pole sana mshikaji wangu,” alisema Pamela, jina hilo likamfurahisha mzee huyo, akaachia tabasamu pana.
“Nashukuru sana! Naomba nikuone leo,” alisema mzee huyo.
“Leo?”
“Ndiyo!”
“Mmh!”
“Kuna nini? Mbona unaguna jamani?
“Nitakwambia! Ngoja nicheki ratiba yangu,” alisema Pamela.
“Sawa. Nakupenda Pamela!”
“Ahsante!” alisema msichana huyo na kukata simu

Je, unajua nini kilitokea katika uhusiano wa watu hawa?
Je, Dickson atafanya nini baada ya kuona ameachwa?

0 comments:

Post a Comment