Monday, April 3, 2017
STORY: NILIFANYA MAPENZI NA MAITI 20 ILI NITAJIRIKE-26 [FINAL EPISODE]
Nilikuwa nimedhamiria kutoa roho za watu na niliamini kusingekuwa na mtu ambaye angenitisha kwa lolote lile. Niligundua kwamba kupitia ajali kungekuwa na damu nyingi sana ambayo ingepatikana huko.
Nilijitahidi na kununua mabasi kumi ambayo niliyapa majina ya Highway. Nilikuwa na lengo la kuteketeza roho za watu wengi na ndiyo maana nikayapa majina hayo nikiwa na maana...
ya njiapanda.
Nilihakikisha kunapatikana huduma bora ndani ya mabasi hayo ili yawe kivutio kwa kila abiria ambaye angeingia humo kwa mara ya kwanza. Kweli nikafanya hivyo na kupitia nguvu za giza, watu wengi waliyapenda mabasi yetu kutokana na huduma bora iliyokuwa ikipatikana humo.
Matajiri wengine ambao tulikuwa wote katika dini ile walishangaa kwa uamuzi wangu huo kwani haikuwa biashara iliyokuwa ikiingiza kiasi kikubwa cha fedha kipindi hicho. Waliamini kwamba kama ningekuwa na biashara katika machimbo ya madini basi ningeingiza kiasi kikubwa cha fedha kuliko kipindi hicho.
Sikutaka kuzungumza kitu, nilijua nina maana gani hivyo nikawaambia kwamba wasubiri. Nilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kipindi hicho, fedha ziliendelea kuingia huku utajiri wangu ukizidi kuongezeka kila siku.
Nilikuwa mtu wa kusafiri huku na kule, nilitumia fedha kadiri nilivyoweza, katika kipindi hicho bado nilikuwa kwenye uhusiano na mpenzi wangu, Majeed. Mtoto wetu aliendelea kukua, alikuwa nusuu jini na nusuu binadamu, wakati mwingine hakuwa akila chakula cha kawaida, chakula chake kikubwa kilikuwa damu.
Miezi ikakatika mpaka kufika ile miezi ambayo niliambiwa kwamba ilikuwa zamu yangu kutoa kafara. Damu za watu wanne zilikuwa zikihitajika kipindi hicho. Hilo halikuwa tatizo kwani kulikuwa na mabasi yangu yaliyokuwa yakifanya safari kuelekea mikoani.
Siku ambayo nilitakiwa kuchinja kafara hizo ikawadia na hivyo kuelekea kanisani. Kama kawaida yetu tulifika huko saa sita uziku na kuingia huku tukiwa watupu na ndani kupewa mavazi makubwa kama kanzu fulani yaliyokuwa na rangi nyekundu, rangi iliyokuwa ikivalia siku ya kutoa kafara kama siku hiyo.
Ibada ilianza na kila mmoja alikuwa makini kumsikiliza kiongozi wetu aliyekuwa mbele kabisa. Siku hiyo ilikuwa maalumu kwa ajili ya utoaji huo hivyo kuitwa na kwenda mbele.
Nikawekewa kioo huku nikipewa uwezo ambao sikuwa nao kabla. Niliambiwa nikiangalie kioo hicho kwa umakini mkubwa kwani kuna kitu kilitakiwa kuonekana katika kioo hicho.
Nikafanya hivyo na ghafla nikaanza kuliona moja ya basi langu likiwa safarini kuelekea Dodoma. Ndani kulikuwa na abiria sitini, wakubwa kwa wadogo, nikaambiwa kwamba nilitakiwa kulipindua hilo basi hivyo nilitakiwa kwenda sehemu ya tukio.
Kumbuka kwamba muda huo ulikuwa ni saa sita usiku, kile nilichokuwa nikikiona si muda huo ila ni kile ambacho kingetokea siku inayofuatia. Nikaanza kuzungumza maneno fulani ambayo katika hali ya kawaida kuyaelewa ni vigumu sana, ghafla nikajikuta nikiwa nimesimama katika barabara ya lami maeneo ya Mvomero.
Nilisimama hapo, hakukuwa na watu, kulikuwa na ukimya mkubwa na mara chache sana mabasi yalipita lakini nilitakiwa kuachana nayo kwani sikuwa pale kwa ajili ya mabasi hayo bali basi langu ambalo lingepita muda mchache ujao.
Baada ya dakika kadhaa, kweli nikasikia muungurumo wa basi langu, unaweza kujiuliza ni kwa namna gani niliweza kugundua kwamba basi hilo lilikuwa langu.
Nilikuwa katika mazingira ya ulimwengu mwingine kabisa, hivyo nilikuwa na nguvu kubwa ya kugundua kitu hicho. Nikaanza kuliona basi hilo kwa mbali likija kwa kasi mbele yangu.
Nilichokifanya ni kunyoosha mkono wangu mbele kama mtu aliyekuwa akilitaka basi hilo lisimame. Dereva ambaye alikuwa akiendesha akaanza kuliona jiwe kubwa likiwa limesimama katikakati ya barabara hivyo kutaka kulikwepa.
Basi likamshinda na hapohapo basi lile likaelekea pembeni ambapo likabimbilika, watu walipiga kelele tu. Baada ya mwendo fulani likasimama huku mataili yakiwa juu.
Nilichokifanya ni kulifuata na kisha kuchungulia ndani ambapo watu waliumia vibaya, wale watu wanne ambao niliwakusudia walikuwa wamekufa huku damu zikiwatoka hivyo kuwafuata na kisha kukinga damu kwa ndoo kubwa niliyokuwa nayo, nilipomaliza, huyo nikaondoka zangu na kurudi kule kanisani.
Kila mmoja akaanza kushangilia, kilichotokea, wao wenyewe hawakuamini, nilionekana kuwa kama shujaa, kuangusha mabasi ilikuwa kazi kubwa ambayo wengi waliishindwa, na hiyo ilifanyika sanasana kuzimu na sii duniani, sasa ilikuwaje mpaka nikafanikiwa kuliangusha basi hilo na kuchukua damu?
Ibada iliendelea huku kila mmoja akisifia na baada ya ibda kumalizika, nikatoka kanisani na wenzangu kulifuata gari langu. Nilipolifikia, nikaufungua mlango na kuingia ndani.
“Unaendeleaje?” nilisikia sauti kutoka humo ndani ya gari, nilishtuka sana, nikageuka na kuangalia alikuwa nani.
Huwezi amini, alikuwa Majeed, alikuwa ndani ya gari langu kiti cha nyuma.
Nilimwangalia usoni, siku hiyo alionekana kuwa tofauti kabisa, alikuwa amevimba macho hali iliyoonyesha kwamba kipindi kirefu alikuwa amelia.
“Nzuri! Kuna nini jamani?” nilimuuliza.
“Maamuzi unayotaka kuyafanya, naomba uachane nayo mpenzi,” aliniambia huku akiniangalia.
“Maamuzi! Maamuzi gani?” nilimuuliza huku nikimwangalia kwani sikuwa nimepanga kufanya maamuzi yoyote mabaya.
“Hayo unayotaka kuyafanya!”
“Yapi tena?”
Hakunijibu swali hilo, alibaki kimya na kuendelea kuulia. Kwa kweli alinichanganya sana na sikujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Nilimuona akifungua mlango na kuanza kuondoka.
Sikutaka kubaki garini, nami nikateremka na kumfuata kule alipokuwa akielekea. Bado kichwa changu hakikuwa sawa, maneno aliyoniambia yalinichanganya sana. Alipofika sehemu fulani, akakata kona, nikapiga hatua za haraka sana, nilipofika na mimi kukata kona, sikuweza kumuona kabisa.
****
Hakika nilichanganyikiwa, sikujua Majeed alimaanisha nini kwani manano yake yalinichangaya sana, nilijua kulikuwa na kitu na nilitaka kufahamu, nilitamani kumuuliza ili aniambie kile kilichokuwa kikiendelea lakini sikupata nafasi hiyo kwani sikuweza kumuona tena.
Nilichokifanya ni kurudi nyumbani, nilitulia kitandani huku nikiwa na mawazo lukuki kuhusu yeye. Ilipofika usiku wa saa sita, nikaanza kuhisi mwili ukiwa kwenye uchovu wa ajabu na ghafla nikajikuta nikilala usingizi mzito.
Sikujua ni nani alinichukua, nilijikuta nikiwa nimesimama juu ya mlima mmoja mkubwa, ulikuwa ukitisha sana, mbele yangu, nilikuwa nikiwaona watu wengi, wakubwa kwa wadogo ambao walivalia mavazi meupe kabisa.
Nilibaki nikiwaangalia, walikuwa wakiimba kwa sauti kubwa, sikumbuki ni nyimbo gani walizokuwa wakiimba. Nilipopelekwa mahali hapo nilikuwa na hofu tele lakini kitu cha ajabu baada ya kuwaona watu hao, hofu yote iliyokuwa moyoni mwangu ikatoweka.
Nilijiuliza juu ya mahali hapo, sikupata jibu. Nilibaki nikijiuliza sana, sikujua sababu ya mimi kuletwa mahali hapo. Nilibaki nikiwaangalia watu wale huku na mimi nikitamani kuungana nao na kuimba pamoja nao.
Nyuso zao zilikuwa kwenye tabasamu pana, jinsi walivyoimba na kucheza, nilijisikia furaha sana na ninadiriki kusema kwamba sikuwahi kuwaona watu wakiimba kwa furaha, kwa nguvu kama walivyokuwa wakiimba watu hao.
Wakati nikiwa ninawaangalia, ghafla machozi yakaanza kunitoka, moyo wangu ukawa na uchungu mkubwa, nilijiona kuwa mkosaji mkubwa, niliyaona maisha yangu niliyokuwa nikiishi kuwa maisha ya shida, yenye mateso sana.
Nilihisi moyo wangu ukiwa mzito sana, nilijiona kuwa kama mtu aliyebeba mzigo mkubwa ambaye alihitaji msaada kutoka kwa mtu fulani kuutua mzigo mkubwa ambao hakika ulinielemea.
Wakati nikiwaangalia watu hao waliokuwa wakiimba kwa sauti za shangwe, ghafla akatokea mwanaume mmoja katika mlima ule. Akanisogelea pale nilipokuwa, nilipoyapeleka macho yangu usoni mwake, alikuwa ni mzuri wa sura.
Uzuri wa sura yake sikuwahi kuuona kabla, ulikuwa ni mara elfu moja ya uzuri aliokuwa nao Majeed. Akatoa tabasamu, lile tabasamu lake likaufanya moyo wangu kusikia furaha ya ajabu, alionekana kuwa mwanaume mwenye nguvu fulani na alifika mahali hapo kwa sababu fulani.
Alichokifanya kabla ya kuzungumza chochote kile ni kuiinua mikono yake juu, ghafla nikaona giza lote lililokuwa katika mlima ule likipotea na nuru ya ajabu kutokea.
Hakika niliogopa sana na kuona kila kitu kilichotokea kuwa muujiza mkubwa.
Akanisogelea na kisha kuniambia nikae chini pamoja naye, nikafanya hivyo. Muda wote alikuwa na tabasamu pana tu, sikujua sababu iliyomfanya kuwa katika hali ile, nilimshangaa mno.
“Neema ya Mungu hutokea mara moja tu,” alianza kwa kuniambia maneno hayo ambayo katika ulimwengu wa kawaida, nisingeweza kuyaelewa, ila kwa kuwa alinipa uweza fulani, nikayaelewa.
“Shetani ni muongo, yeye ni baba wa uongo, ameandaliwa moto wa milele yeye na malaika wake wa giza, hataki kwenda huko peke yake na ndiyo maana kila siku amekuwa akiwatafuta watu wa kwenda naye. Bahati mbaya zaidi, hata wewe alikukamata kutokana na tamaa ulizokuwa nazo,” aliniambia huku akiniangalia. Katika hali nisiyoitegemea, machozi ya uchungu yakaanza kunitoka.
Naomba niwaambie wazi kwamba uchungu ninaouzungumzia hapo ni uchungu haswa. Nilihisi maumivu ambayo sikuwahi kuyasikia kabla. Niliumia sana na kuzijutia njia zangu nilizopitia katika maisha yangu yote.
“Kwa nini nimeletwa hapa?” niliuliza swali ambalo mimi mwenyewe sikutegemea kuliuliza.
“Kwa sababu unahitaji ukombozi!”
“Kutoka wapi?”
“Kwa Mungu aliye hai!” alinijibu.
“Wewe ni nani?” nilimuuliza.
Hakunijibu, alichokifanya ni kunishika mkono, ngozi yake ilikuwa laini sana kama ya mtoto mdogo. Akaniambia kwamba kuna sehemu alitaka kunipeleka, nikakubaliana naye na kuondoka mahali hapo.
Hatukutembea, nilishangaa sana, tulikuwa tukipiga hatua lakini tukawa tunatembea angani, yaani kwa kifupi ni kama watu waliokuwa wakipaa. Alinipeleka katika mji mmoja, ulikuwa ni wa ajabu sana, ulikuwa na majengo mengi, yote yalikuwa ni ya dhahabu iliyoonekana kuwa tofauti na dhahabu ya huku tulipo, ilionekana kuwa ya gharama sana.
“Huu ni mji mtakatifu niliowaandalia watu wangu,” aliniambia huku akiachia tabasamu pana.
Nilifurahi, kulikuwa na watu wengi huko, wote walilingana kimo. Nilibaki nikiwaangalia kwa mshangao mkubwa. Tuliendelea kwenda mpaka tulipofika katika sehemu moja kulipokuwa na mlango mmoja mkubwa, akaniambia tuingie humo, nikasema sawa.
Mlango ukajifungua, huko, tukakutana na mji mwingine kabisa, mji wenye uzuri wa ajabu. Kulikuwa na wanyama wengi, nilishangaa kuona simba akiwa pamoja na swala, amani ilionekana kutawala kila sehemu, nilishangaa kwani haikuwa kawaida kabisa.
“Hapa ni wapi?” nilimuuliza.
“Hapa ndiyo sehemu niliyowaandalia watu wangu,” alinijibu huku tabasamu pana likiwa usoni mwake.
“Watu wako?”
“Ndiyo! Watu wote ambao watatenda mema watakuja huku, watakaa meza na baba na kunywa na kula naye, hakutokuwa na machozi, huku hakutokuwa na maumivu milele, itakuwa ni shangwe milele na milele,” aliniambia, maneno yake yakaufanya moyo wangu kujisikia vizuri kabisa, furaha ambayo sikuwahi kuipata tangu nizaliwe.
Nakumbuka siku hiyo tulitembea sana lakini hatukuchoka hata kidogo. Bado moyo wangu ulikuwa na hamu kubwa ya kuendelea kutembea katika mji ule mkubwa ulionishangaza sana.
Hakukuwa na magari wala pikipiki kwani kutembea kwake ilikuwa ni rahisi kufika sehemu husika, yaani ni kama kufumba na kufumbua tu tayari ulikuwa umefika.
Tulitembea mpaka tulipofika katika sehemu ambayo kulikuwa na miti mingi.
Nilishangaa sana kwani nilipoitazama, matawi ya miti ile ilikuwa ikiinama kila wakati kitu kilichonifanya nistaajabu na kumuuliza yule niliyekuwa naye.
“Mbona miti hii inainama kwa pamoja na kuinuka, hii inamaanisha nini?’ nilimuuliza.
“Kila kitu chenye uhai kinamsifu na kumuabudu Mungu! Binadamu usipomsifu na kumuabudu Mungu, basi jua hata miti itamuabudu na kumsifu, hata mawe yatapaza sauti na kumwabudu yeye aliye juu,” alinijibu.
Tuliendelea kutembea mpaka tulipolifikia geti jingine, akaniangalia na kuachia tabasamu pana. Kwa kweli nilishangaa sana kwani tabasamu lile lilikuja na upendo mkubwa sana, moyo wangu ulijisikia kuwa na amani kuliko siku yoyote ile katika maisha yangu.
Wakati akiwa anaachia tabasamu hilo, ghafla akabadilika, sijajua ni kitu gani kilitokea lakini akaonekana kuwa na huzuni ghafla. Nilishangaa. Ninaposema huzuni, alionekana kuwa nayo sana kiasi kwamba nilihisi kwamba hakukuwa na mtu duniani aliyekuwa na huzuni kama yeye. Hapohapo akaanza kutokwa na machozi.
“Kuna nini tena?” nilimuuliza huku nikimwangalia.
“Mungu aliandaa sehemu hii kwa ajili ya watu aliowaumba kwa mfano wake, ila kinachosikitisha, watu wanaokwenda upande wa pili ni wengi sana ikiwemo wewe mwenyewe. Hili limekuwa likimuumiza kila mmoja, ibilisi amewateka watu kwa starehe za kidunia na mambo mengine maovu,” alisema huku akiniangalia, machozi yaliyokuwa yakimbubujika yalikuwa mengi mno na sikuwahi kumuona mtu aliyekuwa akibubujikwa kwa machozi mengi kama alivyokuwa yeye.
“Huo upande wa pili ni wapi?” nilimuuliza.
“Unataka kupaona?”
“Ndiyo! Ninataka kuangalia kila kitu kinachoendelea huko,” nilimwambia.
Ndugu yangu, ninasimulia haya ambayo niliyaona kwa macho yangu, sikuhadithiwa na mtu yeyote yule. Mwanaume yule akanishika mkono na kisha kuondoka mahali hapo, tulipoelekea ilikuwa ni sehemu yenye kutisha sana.
Naweza kusema ilikuwa ni ya kutisha kuliko sehemu yoyote ile duniani. Kulikuwa na giza kubwa, mwili wangu ulikuwa ukiweweseka mno na wakati mwingine nilihisi kama ningekufa.
Sehemu hiyo ilitisha, kulikuwa na giza la ajabu na joto lililokuwa mahali hapo siwezi kulisimulia hata kidogo. Hapo tuliposimama tulikuwa tukisikia sauti nzito ya moto uliokuwa ukiwaka ambao sikujua ulikuwa wapi.
Akaniambia tusogee mbele zaidi, nikamwambia kwamba nilikuwa nasikia joto kali sana, alichonifanya ni kutoa tabasamu na ghafla lile joto lote nililokuwa nikilisikia, likatoweka mwilini mwangu na kuwa katika hali ya kawaida.
Tulitembea mpaka tulipofika katika sehemu moja ambapo mbele yetu kulikuwa na shimo kubwa sana, huko nilikuwa nasikia sauti za watu wengi wakilia, sauti zao zilikuwa kubwa ambazo sikuwahi kuzisikia sehemu yoyote ile.
Ndani ya lile shimo kulikuwa na moto mkubwa uliokuwa ukiwaka na ulifanana kama ujiuji fulani wenye kuunguza sana ambao ulifanana na ule uliotumika kuyeyushia vyuma ila ulionekana kuwa mkali mara elfu moja ya ule ujiuji wa kuyeyushia vyuma. Mwanaume yule akaniambia tuingie kule chini tuone jinsi kulivyo.
“Sitaki! Naomba niondoke, naomba niondoke,” nilimwambia huku nikianza kulia.
“Ila ninataka nikuonyeshee katika upande wa pili, uone sehemu ambayo yule ibilisi atatupwa na watu wake,” aliniambia kwa sauti ya kipole sana.
“Naomba niondoke, sitaki kuingia humo,” nilimwambia kwa sauti kubwa, nilianza kuogopa, sikuwa tayari kuingia ndani ya shimo hilo, niliyoyaona yalionekana kutosha, yalinitisha na nilitaka kuondoka shimoni mule.
Akaniangalia huku uso wake ukiwa umelowanishwa kwa machozi kiasi kwamba nilimuonea huruma, bila kupenda wala kulazimishwa nikakubaliana naye na kisha kushuka chini ndani ya shimo lile. Ndugu zangu, niliyoyaona humo, yalitisha sana.
Niliwaona watu bilioni kwa mabilioni wakiwa wanalia. Nilisikia kwamba watu watakuwa wakilia na kusaga meno, sikujua walimaanisha nini lakini nilipowaona watu hao, kweli walikuwa wakilia na kusaga meno.
Moto mkali, zaidi ya moto wowote ule niliowahi kuuona duniani ulikuwa ukiwaunguza, kulikuwa na wanyama fulani kama dragons ambao kazi zao ilikuwa ni kuwang’ata watu waliokuwa humo shimoni ambao walikuwa wamefungwa minyororo.
“Nisaidie…nisaidie..naomba nisaidie nirudi duniani, sitorudia tena, sitorudia tena,” niliwasikia watu wengi wakimwambia mwanaume yule niliyekuwa naye lakini yeye alichokijibu ni kwamba ‘Neema hiyo walikuwa nayo duniani, hakika isingewarudia tena’.
Tukaendelea kutembea huku na kule. Unaposikia motoni, inakupasa kuogopa kwani ni sehemu inayotisha kupita kawaida. Nilikuwa nikiogopa kila tulipokuwa tukipita mule.
Nililia, wakati mwingine nilikuwa nikisimama na kukipiga kifua changu kwani niliyoyaona yalinitisha sana. Mwanaume yule akaniambia kwamba anataka kunionyeshea watu ambao nilikuwa nawafahamu kabisa ambao walikuwa ndani ya hilo shimo.
Nikamwambia sawa, anionyeshee hivyo kuanza kuelekea sehemu iliyokuwa na vyumba vingi kama jela na kila mmoja alikuwa kwenye chumba chake akiteswa.
Tukafika katika chumba kimoja, kwa nje kiliandikwa jina, nililisoma jina lile, aliyekuwa ndani ya chumba kile aliitwa Saidi Ramadhani. Lilikuwa jina la baba yangu. Nikahisi mwili wangu ukipigwa shoti.
Mlango wa chumba kile ukafunguliwa na kuingia ndani, mtu niliyemuona akilia mbele yangu alikuwa baba yangu, alikuwa kwenye mateso makali mno, alilia huku akiomba msamaha lakini hakuachwa.
Minyororo ilimfunga, alifungwa mikono na miguu yake, kulikuwa na jitu la kutisha lililokuwa likimpa mateso makubwa kwa kumchapa kwa fimbo ya moto huku wakati mwingine likimuuma, na kumbuka kwamba katika chumba kile kulikuwa na moto mkali ulioendelea kumuunguza.
Jitu hilo halikuishia kumchapa tu bali lilikuwa likimwambia mambo yote mabaya aliyokuwa akiyafanya alipokuwa duniani, maneno hayo ya dhihaka ndiyo yaliyomuongezea maumivu moyoni mwake.
“Si ulikuwa mtenda dhambi, si ulikuwa unajifanya hujui kuhusu Mungu, si ulikuwa ukiabudu vitu vya duniani, sasa viite vikuokoe, viite vikutoe humu….hahahaha,” nililisikika jitu hilo likimwambia baba yangu, maneno ya kumkejeli kwa kile alichokuwa amekifanya duniani, niliumia, nilimuonea huruma sana, kwani alipokuwa duniani, hakuitaka neema ya Mungu japokuwa ilikuwa muda wote.
“Zakia…Zakia…niokoe mwanangu, ninateswa, nishike mkono Zakia. Mateso yamenizidi, nina kiu, naomba ukaniletee hata tone moja la maji ninywe, nisaidie Zakia,” alisema baba yangu huku akiniangalia, alikuwa akilia, kilio kikubwa ambacho sikuwahi kumuona mtu akilia namna hiyo.
“Zakia mwanangu, naomba uende ukawaambia watu uliowaacha huko duniani kwamba jehanamu ipo, moto upo, waambie wasipotoke hata mara moja,” nilimsikia baba yangu akiniambia maneno hayo tena kwa kunisisitiza sana.
Nilitembea humo ndani ya jehanamu huku moyo wangu ukiwa kwenye majonzi makubwa, sikuacha kulia, kila wakati nilikuwa nikilia sana kwani mbali na baba yangu, pia niliwaona watu wengi waliokuwa wakiteseka huko, tena nilikuwa nikiwafahamu sana.
Sikumbuki tulikaa huko kwa muda gani ila baada ya muda fulani nikaambiwa kwamba ni lazima nirudi duniani na kuja kuzungumza kile nilichokutana nacho kule nilipokwenda pasipo kuongeza au kupunguza kitu chochote kile.
“Naomba niulize swali,” nilimwambia mwanaume yule.
“Uliza.”
“Nakumbuka nilipokwenda Marekani, kwenye lile kanisa kulikuwa na kuandika namba 666 lakini nilipoingiza mkono wangu, sikuandikwa kitu ambacho haikuwa kawaida,” nilisema.
“Ulichaguliwa tangu kipindi cha nyuma kwamba ulitakiwa kuwa huku. Watu wote wanaopigwa chapa ya mnyama ya 666 huwa haitoki katika maisha yao na hiyo ndiyo huwa tiketi ya kwenda kuzimu. Kwako, ile ilikuwa ni neema ambayo haiwapati watu wengi,” aliniambia.
Nilizungumza naye kwa machache, aliponiambia niondoke tayari kwa kurudi duniani, nilishangaa kujikuta nikiwa ndani ya kanisa moja lililokuwa Mwenge, jijini Dar es Salaam.
Sikujua nilikuwa vipi ndani ya hilo kanisa lakini muda wote nilikuwa nikilia sana, machozi yalikuwa yamenitoka kupita kawaida na watu wote walikuwa wakiniangalia.
Wakati nikishangaa mahali hapo, nikasikia sauti ikianiambia kuwa pale ndiyo sehemu nilipotakiwa kumuabudu Mungu, kwa kweli nilishangaa sana. Nikaitwa mbele ya kanisa, watu wote walikuwa wakiniangalia, kitu cha kwanza kabisa ni kuuliza pale nilifikikaje?
Wakaniambia kwamba waliniona nikiingia, tena nilishuka kutoka kwenye daladala na kuingia humo kanisani na kutulia huku nikilia mfululizo. Siku hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wa utajiri wangu.
Niliamua kuokoka, sikuwa na jinsi. Nilikuwa Muislamu jina tu, tangu nizaliwe, sikuwahi kwenda msikitini kuswali, sikumbuki kama katika maisha yangu niliwahi kushika Kitabu Kitakatifu cha Qur-aan na kusoma, sikuwahi kupiga hata magoti kuswali kwa Allah, sasa nilipojikuta ndani ya kanisa hilo, sikuwa na jinsi. Nikaamua kuokoka.
Hiyo ndiyo ilikuwa historia ya maisha yangu, jinsi Nilivyofanya Mapenzi na Maiti 20 Nitajirike. Siku hiyo niliporudi nyumbani kwangu, kitu cha ajabu sana, sikupafahamu nyumbani hapo.
Nilikumbuka kabisa kwamba nilikuwa nikiishi Kijotonyama tena nilinunua nyumba kubwa na ya kifahari ila tatizo sikuweza kupafahamu nilipokuwa nikiishi. Nilichanganyikiwa sana lakini sikuwa na la kufanya.
Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa utajiri wangu, sikukumbuka tena kuhusu biashara zangu, nilichokifanya ni kurudi kanisani na kuzungumza kile kilichokuwa kimetokea katika maisha yangu tangu mwanzo mpaka kipindi hicho.
“Huo haukuwa utajiri, ulihisi ni tajiri lakini si utajiri,” aliniambia mchungaji.
Baada ya hapo, sikuonana tena na Majeed, hapo ndipo nilipokumbuka kwamba siku ya mwisho mwanaume huyo alionekana kuhuzinika kwa sababu alijua kile kilichokuwa kikienda kutokea.
Majeed hakurudi, nikawa naishi kwa mama Veronika, mmoja wa wanawake waliokuwa wakisali hapo kanisani ambapo baada ya miaka miwili nikaolewa na mume wangu ambaye nipo naye mpaka sasa na kumzalia watoto wawili.
Asanteni kwa kuifuatilia historia ya maisha yangu tangu mwanzo mpaka hapa ilipoishia. Naamini mmejifunza, kwa yale mazuri, yachukueni ila kwa yale mabaya, naomba muyaache na si ya kuyafuata hata mara moja.
MWISHO
Labels:
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment