Pages

Subscribe:

Thursday, April 6, 2017

Story: SI KITU BILA PENZI LAKO - 13



Mara baada ya Patrick kujisikia nafuu, akaruhusiwa kutoka hospitalini ambako Gibson na mkewe wakamchukua na kwenda nae jijini Dar es Salaam. Gibson na mkewe walitaka kumpa Patrick kila kitu alichokihitaji katika maisha yake.

Kila mwezi mchungaji Smith pamoja na mkewe, Bi Rachel walikuwa wakimtumia fedha Gibson kiasi cha zaidi ya shilingi milioni mbili kwa ajili ya kumtunza Patrick ambaye kadri...

siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo alivyozidi kubadilika.

Patrick akaonekana kuwa na afya tena, mwili wake ulikuwa umeongezeka kupita kiasi. Japokuwa alikuwa na mawazo juu ya baba yake na mama yake lakini alijitahidi kukaa na vijana wenzie kwa ajili ya kuongea mambo tofauti tofauti hali iliyomtoa katika msongo mkubwa wa mawazo.


Siku ya Krismasi ilipofikia, matokeo ya darasa la saba yakatolewa. Patrick alikuwa amefanya vizuri kuliko wote katika shule ambayo alikuwa amemalizia elimu ya msingi. Alama zake nyingi alizozipata ndizo ambazo zilimfanya kujiunga na shule ya Sekondari ya wavulana ya Kibaha.


Kila siku alionekana kuwa na furaha, hatua ya yeye kuchaguliwa na kujiunga na shule hiyo kulimpa furaha mno. Kila siku aliziona ndoto zake za kuwa mwanasheria zikianza kutimia. Ila pamoja na hayo yote, alitamani baba yake na mama yake wawe mahali hapo kwa ajili ya kuyaona mafanikio yake.


Maandalizi yakaanza kufanyika, Patrick akanunuliwa kila kitu kilichohitajika shuleni. Mavazi mazuri, begi kubwa la nguo pamoja na mahitaji yake mengine yalikuwa yamewekwa tayari kwa ajili ya kwenda shule na kuanza kidato cha kwanza.
Masomo yalipoanza, Patrick alionekana kuwa tofauti na wanafunzi wengine. Shuleni alikuwa akionekana mpweke kupita kawaida. Kusoma kwake likawa ni jambo gumu ambalo lilipelekea kufeli masomo yake kuliko mwanafunzi yeyote aliyekuwa akisoma shuleni hapo.


Muda mwingi Patrick alikuwa akiutumia kwa kuchora picha mbalimbali za viongozi wa nchi hii. Uchoraji wa Patrick ukamsisimua kila mtu aliyeziangalia picha zake. Hakukuwa na utofauti wowote kama ungeonyeshwa picha ambayo ilipigwa na kamera na picha ambayo aliichora Patrick.


Alionekana kuwa na uwezo mkubwa wa uchoraji ambao aliiwakilisha shule yake katika kila mashindano ya uchoraji yalipofanyika. Jina lake likaanza kujulikana katika shule zote, kipaji chake cha uchoraji kilionekana kumvutia kila mtu.


Waandishi wa habari wakaanza kumiminika katika shule ya Sekondari ya Kibaha kwa ajili ya kuziangalia picha ambazo zilikuwa zimechorwa na Patrick. Kila mwandishi alitaka Patrick afanye kazi pamoja nao kwa ajili ya kuchora picha mbalimbali ambazo zingekuwa zikichapishwa magazetini.


Waandishi wa habari kwa kuyawakilisha magazeti yao, wakaamua kuweka mikataba na Patrick ya kuchora picha kadhaa na kuzichapa katika magazeti yao. Kila mtu ambaye aliyanunua magazeti yale na kuziangalia picha zile, alishindwa kuamini kama picha zile zilikuwa zimechorwa.


Jina a Patrick likaaanza kukua, akaanza kushika kiasi kikubwa cha fedha mkononi mwake. Masomo akawa ameyasahau kabisa hali iliyomfanya kufeli kupita kawaida. Kila mtihani ambao ulikuwa ukifayika shuleni, Patrick alifeli vibaya.
“Kwa hiyo tumfanye nini?” mwalimu wa taaluma aliwauliza walimu wenzake katika mkutano wa walimu uliofanyika shuleni hapo.


“Tumuiteni na kumuonya. Najua atabadilika,” mwalimu mkuu aliwaambia.
Patrick aliitwa na kuonywa. Aliambiwa asome sana na mambo ya kuchora ayafanye baadae. Alikubali lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote yaliyotokea. Kila siku Patrick alikuwa akiendelea kuchora zaidi na zaidi huku picha zake akiziuza katika magazeti mbalimbali.


“Haina jinsi. Ni lazima tumsimamishe shule,” mwalimu wa taaluma alisema.
Hiyo ndio ilikuwa hatua ambayo ilichukuliwa, Patrick akasimamishwa shule. Patrick alijiona kupewa uhuru mkubwa zaidi. Kila siku nyumbani alikuwa akichora picha, hakujali elimu hata mara moja japokuwa alikuwa amewekewa kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti yake na kiasi hicho kilikuwa kikiongezeka kadri miezi ilivyokuwa ikisonga mbele.


Baada ya mwezi kumalizika, Patrick akaruhusiwa tena kurudi shuleni. hakuwa na mabadiliko yoyote yale, bado alikuwa akiendelea kuchora, tena wakati huu alikuwa ameongeza kasi zaidi.


Aliwachora walimu mbalimbali shuleni hapo, picha ambazo walimu hao walizichukua na kuziweka katika flemu na kuzitundika ukutani. Picha zile zilionekana kuwa na uhalisia kabisa, hazikuonekana kuwa na utofauti wowote na zile za kupigwa kwa kamera.


Bado maendeleo yalikuwa mabaya. Patrick hakuwahi kupata alama zaidi ya kumi katika mitihani yake yote. Kitu ambacho alikuwa akiking’ang’ania katika maisha yake kilikuwa ni kipaji cha uchoraji ambacho aliamini kuwa kingeweza kumtoa katika maisha yake.


“Ni lazima tumfukuze shule. Ni kweli anaipa shule zawadi mbalimbali za uchoraji, ila hapa amekuja kusoma na si kuchora. Kwa sababu maendeleo yake hayaridhishi, basi ni lazima tumfukuze shule,” mwalimu mkuu aliwaambia walimu wenzake.


Hivyo ndivyo ilivyokubaliwa. Patrick akafukuzwa shuleni hapo. Gibson na Beatrice hawakutaka kumsema Patrck kutokana na maisha ambayo alikuwa amepitia. Kutokana na kutotaka kusoma na badala yake kutaka kuchora, Gibson akaamua kumpigia simu mchungaji Smith ambaye aionekana kusikitishwa na kile ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha ya Patick.
“Unasema kweli amefukuzwa shule?”
“Ndio”
Mchungaji Smith na mkewe hawakuwa na jinsi, wakaanza kuyakabidhi maisha ya Patrick mikononi mwa Mungu. Tayari wakaona roho ya kutotaka maendeleo ilikuwa imemkumba hali iliyompelekea kutotaka kusoma kabisa. Kila siku walikuwa wakifanya maombi ili Mungu ambadilishe Patrick na kuigeukia Elimu.


“Hali imeongezeka mchungaji. Patrick bado anaendelea kuchora na si kusoma. Yaani tunashindwa kujua tufanye nini,” sauti ya Gibson ilisikika simuni.


Patrick alionekana kushindikana kabisa. Kila siku alikuwa mtu wa kuchora tu, hakutaka kusoma kabisa. Maisha ya nyuma ambayo alikuwa amepitia ndio ambayo yalikuwa yameondoa hamu yake ya kusoma kabisa. Hakuona kama kulikuwa na sababu ya kuendelea kusoma na wakati alikuwa akiishi katika hali ya mawazo mengi.


Waandishi wa habari wakazidi kumiminika zaidi. Picha alizokuwa akizichora Patrick zilionekana kumchanganya kila aliyekuwa akiziangalia. Patrick akawa na jina kubwa kwa watu wote ambao walikuwa wakimzunguka, katika vyombo vingi vya habari hasa vya magazeti, Patrick alikuwa akijulikana vilivyo.
“Kwa hiyo hataki kusoma kabisa?” mchungaji Smith aliuliza.
“Ndio.”
“Nakuja Tanzania kwa ajili yake. Nitamchukua na kumleta huku ili nimpeleke katika shule yenye vipaji mbalimbali,” mchungaji Smith alimwambia Gibson na simu kukatwa.


Moja kwa moja Gibson akampa taarifa zile Patrick. Akafurahia sana. Hakufurahi kwa sababu alikuwa akielekea Marekani siku si nyingi, bali alikuwa akifurahi kwa sababu alikuwa akipelekwa katika shule ya kukuza vipaji, huko hakukuwa na masomo tena kama jinsi ambavyo ilivyokuwa Tanzania.


Baada ya wiki moja mchungaji Smith akaingia nchini Tanzania. Akapata muda wa kuongea na Patrick huku Gibson akiwa mkalimani wake. Mipango ya Patrick kusafirishwa ikaanza. Kila kitu kilipokuwa tayari, Patrick alikuwa katika ndege ya Shirika la Ndege la American Airlines wakielekea Marekani.


Kitendo cha kupanda ndege kilimpa faraja kupita kiasi. Hakuamini kama muda huo alikuwa amepanda ndege, usafiri ambao hakuwa akiufikiria hata siku moja kuwa angeutumia. Moyo wake ulikuwa na furaha kupita kawaida, ila kila alipokuwa akimfikiria Victoria, furaha ikatoweka kwani alijua kwamba alikuwa akienda kuishi mbali na Victoria.


Walitumia zaidi ya masaa ishirini na nane angani pamoja na kubadilisha ndege jijini Uholanzi na ndipo ndege ikaanza kutua katika uwanja wa ndege wa JFK uliokuwa katika jiji kubwa la kibiashara la New York.


Mara baada ya ndege kusimama, abiria wakaanza kuteremka. Patrick alibaki akiangalia majengo marefu ambayo yalikuwa yakionekana vizuri machoni mwake. Baridi ambalo lilikuwa likimpiga ndilo ambalo lilimfanya kuanza kupiga hatua kuelekea kule katika jengo la uwanja ule.


Kila kitu ambacho Patrick alikuwa akikiangalia kwa wakati huo alibaki akishangaa tu. Idadi kubwa ya majengo marefu pamoja na usafi mkubwa uliokuwa ukinekana ulimfanya kubaki na mshangao. Kila wakati alikuwa akiangalia katika kila kona, hakuonekana kujisikia huru kabisa, alionekana kuogopa kupita kiasi.


Mara baada ya mizigo kukaguliwa, moja kwa moja wakaanza kutoka nje ya jengo lile ambako Bi Rachel alikuwa uwanjani pale na kuwapokea.
Wote wakaingia garini na dereva kushikilia usukani. Muda wote Patrick alikuwa akiagalia nje dirishani. Bado mambo mengi mageni yalikuwa yakionekana machoni mwake.


Moja kwa moja dereva akachukua barabara ya St’ Johnson 23 ambayo ilikuwa ikielekea katika upande wa Magharibi wa jiji hilo huku lengo lae likiwa ni kufika katika Jiji la Brookyn.


Baada ya kufika umbali wa kilometa moja, dereva akakata kona kushoto na kuchukua barabara ya Alexander 35 ambayo bado ilikuwa ikiendelea na uboreshaji wa kuongeza barabara ya njia saba. 


Maneno makubwa yaliyosomeka ‘WELCOME IN BROOKLYN CITY’ yalikuwa yakionekana katika bango kubwa lililokuwa mbele katika njia kubwa lililokuwa limewekwa katika maghorofa makubwa mawili.


Safari yao iliendelea zaidi na zaidi, barabara nyingi zilikuwa zikionekana njiani ambako wakaamua kuchukua barabara moja ambayo ilikuwa ikiwapeleka mpaka katika mji mdogo wa Port Elizabeth. Baada ya dakika kadhaa, gari likasimama nje ya nyumba moja kubwa na ya kifahari.


Nyumba ilionekana kuwa kubwa sana. Geti likajifungua na gari kuingia. Magari zaidi ya kumi na mbili yalikuwa yakionekana yakiwa yamepakiwa pembeni. Bwawa kubwa la kuogelea lilikuwa likionekana machoni mwa Patrick.


Patrick alibaki akishangaa, hakuamini kama duniani kulikuwa na nyumba kubwa namna ile. Sanamu kubwa ya Yesu akiwa msalabani ilikuwa ikionekana pembeni kabisa na nyumba ile. Akaanza kukazia macho katika eneo moja ambalo lilikuwa na miti kadhaa, wanyama walikuwa wakionekana huku neno ‘Zoo’ likionekana vizuri.


Wote wakateremka, Patrick akakaribishwa katika nyumba hiyo, maneno mbalimbali yalikuwa yakionekana yakiwa yameandikwa ukutani. Maneno hayo yote yalikuwa ni mistari kadhaa ambayo ilikuwa imeandikwa katika Biblia. Patrick akashtuka mara baada ya kuangalia huku na kule na kugundua kwamba kulikuwa na kamera katika maeneo mengi ya nyumba ile.


Hapo ndipo ambapo maisha ya Patrick yalipoanza kwa mara nyingine. Taratibu akaanza kujifunza lugha ngeni ya kingereza na baada ya mwezi mmoja, akaweza kuifahamu lugha hiyo. Patrick akazoeleka na kila mtu katika nyumba hiyo, muda wote alikuwa akionekana kuwa na furaha kupita kiasi.


Mwezi mwingine ulipofikia, Patrick akaandikishwa katika shule ambayo ilikuwa ikikuza vipaji mbalimbali iliyoitwa Vanguard ambayo ilikuwa katika jiji la Florida. Mara ya kwanza alikuwa mgeni kabisa, kila mtu kwake alionekana mpya.
Kila siku alikuwa akikaa peke yake mpaka pale msichana wa kizungu, Vanessa alipoanza urafiki nae. Kila siku Vanessa alikuwa karibu na Patrick, walisoma wote huku hata wakati wa mapumziko wakienda kula chakula pamoja.


Kutokana na umaarufu aliokuwa nao mchungaji wa Kimataifa, Smith, Patrick alikuwa akiheshimiwa sana shuleni hapo. Patrick alionekana kuwa mchangamfu sana kwa Vanessa hali ambayo ilimfanya kupata marafiki wengi ambao walisikia juu ya uchangamfu wa Patrick kutoka kwa Vanessa.


Kila mwanafunzi shuleni hapo alikuwa akitaka kukaa karibu na Patrick huku wengine wakijiuliza juu ya kipaji ambacho alikuwa nacho kilichomfanya kuletwa katika shule hiyo. Hakuwa akielekea katika vikundi vya nyimbo wala michezo yoyote, muda wote alikuwa darasani tu.


“What do you got? What is your talent, Patrick?” (una nini? Kipaji chako ni nini, Patrick?) Vanessa alimuuliza Patrick ambaye hakujibu kitu zaidi ya kutabasamu tu.
“What do you think? (unafikiria nini?)”
“Nothing. Are you a singer? Actor? Pleaseee Patrick..tell me (Sifikirii kitu. Wewe ni muimbaji? Muigizaji? Tafadhari Patrick..naomba uniambie)” Vanessa alimwambia Patrick.


“Do you real want to know Van? (Kweli unataka kujua Van?)” Patrick aliuliza huku akimwangalia Vanessa kwa uso uliojaa tabasamu.
“Yeah” Vanessa alijibu.


Patrick akachukua begi lake ambalo lilikuwa na madaftari kadhaa na kuliweka mezani. Akalifungua huku Vanessa akitaka kujua Patick alitaka kumuonyeshea kitu gani. Patrick akatoa bahasha moja na kisha kumkabidhi Vanessa.


Vanessa akaifungua bahasha ile, akakutana na karatasi kubwa ambayo akaitoa na macho yake kutua katika picha moja. Vanessa akaonekana kushtuka, macho yake yakaongezeka kwa ukubwa kutokana na kuwa na mshangao mkubwa.


“Where did u get my picture? (Umeipata wapi picha yangu?)” Vanessa aliuliza huku akishangaa. Maswali yakaanza kumiminika kichwani mwake, kamwe hakuwahi kumuonyeshea wala kumpa Patrick picha yoyote ile, kitendo cha Patrick kuwa na picha yake kilionekana kumshtua.


“I drew it (Niliichora)” Patrick alitoa jibu lililomshangaza Vanessa.
“What......? “
“I drew it yesterday (Niliichora jana)” Vanessa akabaki kuwa na mshangao, hakuamini hata kidogo kama picha ile ilikuwa imechorwa.


Mara akainuka kutoka katika kiti kile na kuanza kuelekea nje huku akiruka ruka. Kila mwanafunzi alibaki akimshangaa Vanessa ambaye akaanza kuipitisha picha ile kwa kila mwanafunzi ambaye alikutana nae huku jina la Patrick likitajwa mara kwa mara kutoka kichwani mwake.


Ni ndani ya dakika thelathini, kila mwanafunzi alikuwa amejua ni kitu gani ambacho alikuwa amekifanya Patrick. Kwa wanafunzi ambao hawakuwa wakimfahamu Patrick kwa kumwangalia zaidi ya kumsikia wakataka kumuona kwa macho yao. Picha ambayo alikuwa ameichora ilionekana kumdatisha kila mtu. Hakukuwa na mtu ambaye aliamni kama picha ile ilikuwa imechorwa.


Wanafunzi wengi pamoja na walimu wakaanza kuelekea katika darasa lile huku wakiongozana na Vanessa ambaye alionekana kuwa na furaha kupita kiasi. Walipofika darasani, Patrick hakuwepo, alikuwa amekwishaondoka.


“Where is Patrick? (Patrick yuko wapi?)” Mwalimu mmoja kati ya walimu wanne waliokuja darasani mule pamoja na wanafunzi wasiopungua hamsini aliwauliza wanafunzi ambao waliwakuta katika darasa lile.
“He left (Aliondoka)” Mwanafunzi mmoja alijibu.


Simulizi zitakujia hapa hapa kila siku kuanzia saa tatu asubuhi mpaka saa nne asubuhi na ukipitwa na story basi nenda hapo juu kwenye menyu kisha bofya mahali palipo andikwa LOVE & STORY. Pia waweza kudownload Application yetu kwa kubofya neno DOWNLOAD hapo chini ufuate na maelekezo ili uweze kupata story na updates mbalimbali kwa muda muafaka na kwa urahisi zaidi.
 

Tukutane tena kesho muda kama huu.. ahsante


Download

0 comments:

Post a Comment