Pages

Subscribe:

Thursday, August 24, 2017

Story: SIKU SABA KUZIMU (Sehemu Ya 11) - 11


ILIPOISHIA:
Baada ya kumjibu jambo lililonishitua zaidi ni pale aliponiambia kuwa ilibainika Shenazia alikuwa ni mgonjwa aliyelazwa katika Hospitali ya Amana siku iliyopita na kutoroshwa, hoja ya msingi ilikuwa mimi nilimtoa wapi na utetezi wangu ni upi juu ya kuhusika kwenye tukio lililompata!

SONGA NAYO…
MACHO yalinitoka pima nikimtazama yule askari aliyekuwa amekaa mbele yangu akinihoji maswali mfululizo huku akiwa amenikazia macho. Nilijiuliza niseme nini hata askari huyo...
anielewe bila kupata majibu, ukweli ni kwamba japo moyoni nilifahamu sikuwa kabisa na hatia katika kila kilichokuwa kinaendelea juu ya Shenaiza lakini ilikuwa ni vigumu kuuelezea ulimwengu hata ukaniamini kuwa nilichosema ndicho kilikuwa kweli.

Moyoni nilizidi kugubikwa na majuto, nilifahamu fika hayo yote yaliyonitokea nilijitakia maana kama si ujinga wangu wa kumuamini msichana ambaye sikuwa ninafahamiana naye zaidi ya kuwa na mawasiliano naye kwenye simu nisingefika hapo nilipokuwa.

Huku hayo yote yakiendelea ndani ya akili yangu yule askari alizidi kunisisitiza kujibu maswali aliyokuwa ananiuliza, machozi yakinitiririka niliamua kufunguka kwa mara nyingine ukweli wote kuhusu mimi na Sheneiza. Kuanzia tulivyoanza kuwasiliana na hata nilivyopata taarifa kuwa amelazwa katika Hospitali ya Amana na yote yaliyoendelea baada ya hapo.

Askari yule alikuwa ananisikiliza kwa makini huku akiandika kwenye kitabu chake kidogo (diary), nafkiri mambo muhimu kutoka katika maelezo yangu niliyompa. Hakuacha kunihoji maswali kwa ajili ya kupata uhakika kwa yale niliyokuwa ninamuelezea baada ya saa zima la mahojiana alimuita askari polisi aliyekuwa zamu akamtaka kunirudisha nyuma ya nondo.

Siyo siri kila kitu ndani ya maisha yangu niliona kuwa kilikuwa kimebadilika na kuwa kigeni mana hata siku moja sikuwahi kufikiri ningeingia mahabusu hasa kwa sababu kama hiyo iliyonipeleka wakati huo.

Nikiwa katika chumba hicho cha mahabusu machozi yalikuwa yanazidi kunibubujika  mfururizo. Tofauti na mawazo niliyokuwa nayo  hali halisi ilikuwa inatisha, hakukuwa na hewa ya kutosha maana kidirisha pekee kilichokuwepo katika chumba hicho kilikuwa kidogo na kilikuwa juu, kila mmoja alikuwa anagombania aweze kupata hewa kwa kuwa karibu na dirisha.

“Eee Mungu, naomba uniokoe katika mtihani huu, ni mkubwa sana kwangu, nashindwa kuhimili, onyesha miujiza yako ili maisha yangu yasiishie pabaya,” niliwaza huku machozi yakiendelea kunibubujika.
“Wewe vipi mbona unalialia, humu kiumeni unatakiwa kujikaza,” nilisikia sauti ikiniambia kutoka pembeni yangu.
“Mtoto wa mama huyu, humu ndiyo ubayani, hakuna baba wala mama, suipojikaza utaolewa,” alisema mtu mwingine.

Niligeuza uso wangu na  kuwatazama kwa zamu hao waliokuwa wanazungumza, wote walionekana kuwa watu wa miraba minne tena wenye makovu mengi usoni, macho yangu yaliganda kwao kwa sekunde kadhaa kisha nikayatoa bila kujibu neno lolote lile.
Saa zikazidi kusonga mbele kwa tabu sana upande wangu nikiwa ndani ya chumba hicho cha mahabusu, majira ya mchana rafiki yangu Justice na Raya walifika katika kituo hicho cha polisi kufanya mipango ili niweze kuachiwa kwa dhamana.

Lakini suala hilo lilionekana kuwa bado gumu sana, polisi hawakuhitaji kabisa kuwasikiliza maana hata pale walipojaribu kuuzunguka mbuyu kwa kuhonga pesa kwa baadhi ya askari wenye nguvu ili angalau nitoke nje kwa dhamana huku upelelezi ukiendelea waliambiwa wasiwe na haraka kwanza maana ishu yenyewe haikuwa ndogo.

Waliambiwa wapelelezi walikuwa wameivalia njuga kesi hiyo na suala la muhimu kama kweli nilikuwa sihusiki katika mipango ya kumuua Sheneiza ilikuwa ni kusali kwa nguvu zote ili msichana huyo aweze kupata nafuu hata azungumze ukweli mzima wa nini kilimtokea mpaka akawa anaandamwa na watu waliokuwa wanataka kupoteza maisha yake.

Rafiki zangu hawakuwa na namna ya kulazimisha kama walivyokuwa wanataka wao, walichofanya ilikuwa ni kuomba ruhusa ya kuzungumza na mimi japo kwa dakika chache tu. Kwa kuwa kuna chochote walikuwa wamekwishapenyeza kwa askari hao hilo halikuwa suala gumu sana, waliruhusiwa, nikatolewa mahabusu na kwenda kuzungumza nao.

“Haya yote yatakwisha, hutakiwi kujali kabisa baba, jipe moyo kila kitu kitakuwa sawa,” Raya aliniambia huku machozi yanambubujika kwa wingi.
“Asante Raya, ninaamini hivyo pia, Mungu atanisimamia na kila kitu kitakwenda sawa.” Nilimjibu.

“Hapa kaka ni muhimu kuomba kwa nguvu zote huyo mgonjwa maendeleo yake yawe mazuri ili aeleze ukweli mzima wa nini kimetokea, hicho pekee ndicho kinachoweza kukutoa kwenye hii hatia,” Justice aliniambia.

“Ndivyo askari walivyosema?”
“Ndiyo, mimi pia ninaunga mkono suala hilo maana hakuna njia nyingine ya kukunusuru.”
“Dah! Kwani Sheneiza amelazwa wapi?” Nilimuuliza Justice swali lingine.
“Yuko Mwananyamala hospitali lakini sijafahamu amelazwa katika wodi namba  ngapi.”
“Fuatilia kaka ufahamu pia na maendeleo yake maana huyo ndiyo kila kitu kwenye hili suala kama unavyosema. Lakini kuna kitu pia nilikuwa ninakifikiria ambacho tunaweza kuzungumza na askari polisi wazidishe ulinzi katika hospitali hiyo kutokana na hali halisi, hao watu wanaotaka kumuua wakigundua kuwa bado ni mzima lazima wataendelea kumuandama.”
“Hilo ni kweli kaka, niachie mimi, nitazungumza na mkuu wa kituo maana ni mtu mzuri, ametupokea vyema mimi na Raya.”

Baada ya kuzungumza mawili matatu na rafiki zangu hao ambao walionekana kuniunga mkono kwa kiasi kikubwa ikiwa ni pamoja na kunifariji katika matatizo yangu hayo yaliyokuwa yananisonga, nilirudishwa mahabusu na wao walikwenda kama tulivyozungumza kwa mkuu wa kituo na kumwambia juu ya kuongeza ulinzi kwenye Hospitali ya Mwananyamala.

Hatimaye siku hiyo ilimalizika nikiwa ndani ya kituo hicho cha polisi, siku iliyofuata majira ya asubuhi Raya alikuwa kituoni hapo kwa ajili ya kuniletea kifungua kinywa. Ukweli ni kwamba hakuna wakati niliyomuona Raya kuwa ni mtu wa muhimu kwangu kama wakati huo nilipopata matatizo.

Huko nyuma nilikuwa mtu wa kumchukulia poa sana kwa vitendo vyake vya kuonyesha kuwa ananipenda lakini wakati huo thamani yake niliiona na niliamini kweli mwanamke huyo alikuwa ananipenda kwa dhati.

Baadaye Raya aliondoka na mimi niliendelea kukaa kwenye chumba kile cha mahabusu ambapo mchana nikiwa sina hili wala lile nilishituka baada ya kumuona askari polisi akija kwenye nondo na kuita jina langu, nilipoitika alinichukua mpaka mapokezi nikapewa nguo zangu na kuambiwa nivae, baada ya kuvaa akanitaka nimfuate kuelekea nje, nilifanya hivyo na tulipoanza tu kutoka nje askari wengine watatu walioshika mtutu wa bunduki mkononi walitufuata nyuma tukaenda kuingia pamoja kwenye difenda.

Difenda hilo liliwashwa na kuanza kuelekea mahali ambapo sikuweza kupafahamu kwa mara moja, nilikaa kimya katikati ya askari hao bila kuzungumza neno lolote lile na safari ikazidi kupamba moto. Nilikuja kugundua kuwa huenda tunaelekea Mwananyamala Hospitali baada ya kuumaliza Mtaa wa Makumbusho na kushika barabara ya Mwananyamala, moyoni nilianza kugubikwa na maswali mengi, nilijiuliza kama ni kweli ninapelekwa katika hospitali hiyo ilikuwa ni kufanya nini?
Je, nini kitaendelea kwenye simulizi hii? Usikose next issue!

0 comments:

Post a Comment