Monday, October 16, 2017
BILIONEA KUTOKA OMAN ATANGAZA NIA YA KUINUNUA CLUB YA SIMBA
Bilionea kutoka Oman ameonyesha nia ya kutaka kuwekeza Simba kwa kutaka kujitosa katika mchakato wa kununua hisa za klabu hiyo ili awe sehemu ya umiliki wa timu hiyo kwa asilimia 50.
Kutokana na hali hiyo, hali ya mambo hivi sasa ndani ya Simba ni mshikemshike baada ya zoezi la mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kuanza hivi...
karibuni.
Mchakato wa bilionea huyo kutia mguu katika kutaka kununua hisa hizo za kuimiliki Simba, unafanyika kwa siri kubwa na hata kamati inayoshughulikia mabadiliko hayo haiwezi kufahamu kwani bado haijakutana kuwajua walioweka nia.
Nia ya bilionea huyo wa Oman kutaka kujitosa Simba, inaonekana kama kuleta upinzani kwa mwanachama aliyekuwa anapewa nafasi kubwa ya kununua hisa hizo mfanyabiashara Mohamed Dewji ‘Mo’.
Mo yeye yupo tayari kutoa Sh bilioni 20 lakini bilionea huyo wa Oman anaonekana kutaka kutoa kiasi kikubwa cha fedha zaidi ya hizo anazotaka kutoa Mo.
Mchakato wa bilionea huyo kutaka kununua hisa hizo unafanywa siri kubwa kwani hata baadhi ya watu wa familia yake hawataki ijulikane kwa hivi sasa kwanza wakikataa kuzungumzia mchakato mzima.
Bilionea huyo ambaye kwa sasa jina lake tunalihifadhi anaonekana anataka mambo yake yaende kimyakimya bila ya kutaka kujulikana kwanza, halafu baadaye ndipo awekwe wazi.
Mmoja wa ndugu wa karibu wa bilionea huyo alilikatalia gazeti hili kuhusu mpango huo wa ndugu yake kutaka kununua hisa hizo za Simba lakini mmoja wa mabosi wa Simba amethibitisha.
Bosi huyo alisema; “Kuna bilionea mmoja ameonyesha kuwa na nia ya kutaka kununua hisa za kuimiliki Simba, huyu mambo yake yanaenda kwa siri sana ili tuweze kufanikiwa.
“Huyo bilionea kutoka Oman anamiliki visima vya mafuta pia ana uhusiano mzuri na klabu yetu kupitia kwa kijana wake na yupo tayari kuwekeza zaidi ya Sh bilioni 20 ambazo Mo anataka kuwekeza.
“Hatuwezi kumtaja bilionea huyo kwa sasa kwani tunahofia kuvuruga hali ya mambo wakati zoezi hili la mabadiliko likiwa hatua za kwanza kabisa.”
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusiana na hilo, Kaimu Makamu wa Rais wa Simba, Idd Kajuna alisema: “Ni nani aliyewaeleza taarifa hizo? Sina taarifa yoyote kuhusiana na watu hao.”
Mmoja wa watu wa kamati ya mchakato wa mabadiliko hayo aliliambia Championi Jumamosi: “Ni ngumu kujua kama huyo bilionea ameomba au la kwa maana, hizo tenda hazijafunguliwa.
“Zitakapofunguliwa tutajua hayo yote, ila mtu anaweza kuwa na nia halafu akamweleza mwenzake hiyo inawezekana lakini kwetu kwa sasa hatuwezi kuwa na jibu la moja kwa moja.”
Alipoulizwa kuhusu tetesi za mfanyabiashara Said Salim Bakhresa kutaka kununua hisa hizo, alisema: “Bakhresa hawezi kununua hisa za Simba kwani kanuni zinambana, yule tayari ana timu ligi kuu na kanuni haziruhusu mmiliki mmoja kuwa na timu mbili ligi kuu.”
Hata hivyo, bado nafasi kubwa ya kumiliki hisa za Simba anapewa Mo ambaye ameonyesha kuwa bega kwa bega na timu kwa muda mrefu, lakini kamati itakapofungua tenda lolote laweza kutokea endapo kuna mtu ataweka fedha zaidi ya Sh bilioni 20 za Mo.
Labels:
HABARI & UDAKU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment