Thursday, March 30, 2017
NILIACHA USISTER NIKAWA MCHAWI 09
“Mwezi huu hauwezi kupita. Sawa tumekusikia. Sasa atakuwa nani?” Nilimwona bibi akigeukageuka kunitafuta niliposimama, nikashangaa ni kwa nini bibi anitupie macho mimi wakati nimeshakuwa mchawi mwenzao? Je, anataka kunitaja nini?” nilijiuliza hivyo huku miguu ikinichezacheza kwa wasiwasi.
SASA ENDELEA…
“ Kuna mjukuu wangu ndiyo namtegemea,” alisema bibi. “Kuna mjukuu wako ndiyo unamtegemea, yuko hapa? Maana naona unaangazaangaza sana kwa wenzako.” Mimi nilizidi...
kutetemeka huku moyoni nikisema kama wachawi wako hivyo hawana maana, inakuwaje mchawi amtoe sadaka mchawi mwenzake? Basi kama ni hivyo bibi alitakiwa kumtaja mama ambaye ni mwanaye.
Pia niliwaza kwamba kama bibi atafikia hatua ya kunitaja mimi basi nitahakikisha nafanya fujo pale pasikalike maana hawawezi kuniingiza kwenye njia ya kifo huku naona. “Hapa hayupo, yupo dada yake ambaye ni mwenzetu,” alisema bibi na kunifanya nipumue kwa urahisi sasa.
“Una uhakika mwisho wa mwezi ukifika atakuwa wetu?” aliuliza yule mkuu kwa sauti yenye wasiwasi na maelezo ya bibi lakini kabla bibi hajajibu, mama alisikika akisema: “Naomba nikae na mama pembeni tuangalie jinsi ya kumpata wa kumlipa nyama badala ya huyo mwanangu. ” Mkuu alikataa, akasema kama wanataka kuongea watumie nafasi ileile pale na wengine wasikie ili iwe mafunzo kwa wote kama kuna kikwazo. Mama akasema sawa, akapaza sauti yake na kusema: “Mimi safari hii siko tayari kumaliza damu yangu.
Nilimtoa kaka, mwanangu wa wa pili, nikamtoa mume wangu halafu huyu mama anataka kutoka kwenye nyumba yangu tena, siko tayari.” “Haya bi Mtiwati jitetee.” “Kwa kuwa mwenye mtoto amegoma mimi ni mjukuu tu basi namtoa mwanangu wa Morogoro yeye ndiyo awe nyama. ” Wachawi wakapiga makofi kuonesha furaha yao ya hali ya juu. Lakini mimi sikupiga makofi. Nilikuwa najiuliza kwamba huyo mtoto wake mwenyewe anayemsema bibi ameathirika na huu ugonjwa hatari wa Ukimwi na dalili zote anazo anatumia dawa, sasa ina maana wachawi wanakula kila kitu? “Mtiwati kwa nini hujapiga makofi?” mkuu aliniuliza.
“Nina wasiwasi.” “Upi?” “Nitamuuliza mama baadaye.” Niliposema nitamuuliza mama baadaye wote wakacheka sana, tena sana, halafu kicheko kile cha kebehi fulani hivi. Mkuu akasema: “Hapa hakuna kitu cha mama. Kila kitu ni cha umoja, kwa jambo lolote lile lazima tulijue wote na kulijadili wote, hebu sema kwa nini umesema utamuuliza mama, ni kitu gani hicho?” Wakati najuta moyoni kwa nini nilisema vile, mchawi mmoja alinisogelea akaniambia: “Usiposema utapata adhabu kubwa, sema ukweli ulilotaka kusema. ” “Haya umepewa elimu hapo, sema sasa,” alisema mkuu.
“Huyo mtoto wa bibi ni mwathirika wa Ukimwi, sasa ina maana wachawi wanakula nyama za kila binadamu hata mgonjwa?” niliuliza huku nikijua nimeuwasha moto kwa bibi maana nimefichua siri yake nyingine. Wachawi wakacheka wote, nikashangaa kwa nini wacheke wakati ni kashfa.
“Mtiwati kwetu wachawi hakuna binadamu mgonjwa, hata kama ana TB kwetu ni halali tu, tena ananoga sana.” “Mh,” niliguna. Kuna siri nyingine nilitaka kuisema lakini nikaacha nikajua ndiyo itakuwa mbaya zaidi nayo ni huyo mtoto aliyemsema bibi, si wake ni mdogo wake lakini pale alitambulisha kama wake. “Sasa nendeni mkawatese wakubwa. Wewe Mtiwati leo nataka tukupeleke ulikokuwa ili ukawatese wenzako, uko tayari?” mkuu alisema na kuniuliza.
“Niko tayari.” Palepale mama alinifuata, akanishika mkono tukatembea hadi katikati ya wachawi wengine, akanishika kichwani kisha akanipiga kofi la kawaida, kufumba na kufumbua tulikuwa Iringa kwenye makazi ya masista wenzangu, tena chumbani. “Mmmm…mmmmm…mmmmm,” mama alitoa huo mguno. Ulifanana sana na miguno ya njiwa kama kuna wanaowajua wale ndege wanaitwa njiwa.
Automatiki na mimi nikajikuta naguna vilevile kama mama na kama njiwa: “Mmmm…mmmm….mmmm.” Mama akaniangalia kisha akanionesha ishara kwamba nimwamshe sista mmoja pale. Tulikuwa tumesimama ukutani, nikanyoosha mkono na kumwita sista mmoja huku na yeye akiamka polepole mpaka akafika hatua ya kukaa kitandani. Mikono aliifunga kifuani pake kama muumini anapofunga sala. Niliendelea kumwita kwa mikono nikiivutia kwangu kuanzia mbele, naye akashuka kitandani polepole kuja usawa wangu. Kwangu ilizidi kuwa elimu ya ajabu saba, kumwita aliyelala halafu anaamka na kukujia.
Lakini ilitaka ujasiri wa hali ya juu kwani wakati anatoka kitandani alinitazama nikahisi amenijua na anaweza kuniita kwa sauti ya juu. Niliendelea kumwita hadi akatoka kabisa kitandani nikamfanyia mikono kwa ishara ya kumsimamisha, yaani alipo asitembee kunisogelea bali asimame palepale, akasimama. Je. kilifuatia nini? Usikose kufuatilia mkasa huu wiki ijayo.
Nikamwangalia mama kama kuna hatua nyingine, mama akaniashiria nimchape makofi. Nikainua mkono mmoja na kumchapa makofi kwa mbali kwa shavu lake la kulia, akashtuka na kujishika shavu hilo huku akifuta kwa mkono kuonesha kwamba ameumia, nikafanya vile na mkono wa kushoto, akayumbia kulia kwangu kuonesha kwamba kofi lilimpata.
Kisha nikatumia akili zangu sasa, nikaifanya mikono kwa ishara ya kumzungusha, akaanza kuzunguka ndani ya chumba kutoka sehemu moja kwenda nyingine akiwa hajitambui kwa lolote. Nikamsimamisha, akasimama wimba huku mikono ameikunjia kifuani. Nilimyooshea mikono sista mwingine pale kitandani, naye akaamka kwanza. Halafu likafuata zoezi la kuinuka na kukaa, ndipo likaja zoezi la kutoka kitgandani kunifuata nilipo. Sista huyu ni yule ambaye aliwahi kukemea wakati mimi naandamwa na maajabu ya kichawi, kwa hiyo nilikuwa namwogopa kwani niliamini angeweza kunishinda lakini nilipomwona anaamka na kunijia nikasema moyoni hana kitu.
Alikuwa anakaribia kuweka mguu wa kwanza chini nikashtuka kumsikia akisema ‘asante Yeu’ kisha mama akanishika kichwani haraka na kufumba na kufumbua tukawa tumesimama nje ya jingo. Mimi nilijiona kawaida lakini mama alikuwa akihema sana. “Mama kuna nini kwani?” nilimuuliza kwa sauti ya chini na ya woga. “Mwanagu hatari.” Je, bibi kizee huyo mchawi anamtaja Benadeta?
Labels:
HABARI & UDAKU,
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment