Mzee Khamesse: Kutokana na kuwepo kwa taarifa za Paul Makonda kulelewa katika familia
ya aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Seleman Khamesse, JAMHURI limefika
nyumbani kwa Mzee Khamesse, katika eneo la Nyamanoro, jijini Mwanza na
kufanya mahojiano;
JAMHURI; Kuna taarifa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewahi kuishi nyumbani kwako. Je, ni kweli?
KHAMESSE; Ni kweli Daudi alikuja kwangu akiwa darasa la tano akitokea
kijijini kwao, Koromije na kisha...
kuishi hapa na familia yangu.
kuishi hapa na familia yangu.
JAMHURI; Mbona unasema uliishi na Daudi wakati nimekuuliza kuhusu Paul Makonda?
KHAMESSE; Ni kweli nimesema Daudi kwa sababu namfahamu kwa jina hilo.
Amekuja kwangu akitokea kwa wazazi wake waliokuwa wakiishi Koromije, na
jina lake ni Daudi Albert Bashite.
Wakati shangazi yake ambaye ni mke wangu mdogo (Mama Khamesse) anamleta
hapa alikuwa akitumia jina hilo na hata alipopelekwa shule alikuwa
akitumia jina la Daudi Bashite wakati anasoma Shule ya Msingi Nyanza.
Hata wakati anakwenda kuanza shule Pamba Sekondari alienda kwa jina la Daudi Bashite.
JAMHURI; Una uhusiano gani na Daudi?
KHAMESSE; Daudi ana uhusiano na mke wangu mdogo Bernadeta maarufu kama
Mama Khamesse. Mama ndiye aliyemleta hapa kwani ni shangazi yake anaweza
kukwambia zaidi kuhusu hilo.
JAMHURI; Tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na kisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam mmekuwa mkiwasiliana?
KHAMESSE; Hatuna mawasiliano kwani tangu ateuliwe amewahi kufika nyumbani kwangu hapa tulipo mara mbili tu, tena alikuja usiku.
Mara ya kwanza alikuja saa saba usiku, hakuingia ndani aliishia nje
akaongea na vijana wenzie akaondoka. Mwaka jana mwezi wa Ramadhan
alikuja saa tano usiku akiwa amesindikizwa na vijana wawili hakuingia
ndani aliishia nje akaongea na vijana wenzie, kwa vile nilikuwa sijalala
tulisalimiana akanipatia mawasiliano yake kisha akaondoka.
Ukweli ni kwamba hatuna mawasiliano, kutokana na kwamba haoneshi
kuhitaji kuwasiliana kwani namba alizonipatia nikipiga hapokei, hata
nilipotuma ujumbe hakukuwa na majibu.
Ila wasiliana na shangazi yake anaweza kukueleza zaidi maana mie sikukaa
naye sana kutokana na majukumu yangu yaliyokuwa yakinikabiri wakati
huo. Pamoja na kwamba alikuwa akiishi nyumbani kwangu.
Ramadhani Khamesse
Ramadhani ni mtoto wa Mzee Khamesse, ambaye alikuwa akisoma shule moja
na Paul Makonda, amesema kwamba amesoma na kuishi na Makonda katika
kipindi chote alichokuwa nyumbani kwao.
“Tulikuwa naye shule moja ya Nyanza, na jina lake ni Daud Albert
Bashite. Dada yangu, mimi, huyu Daudi tulikuwa tunalala naye chumba
kimoja hivyo namfahamu. Pia tulikuwa rika moja hivyo hata michezo yetu
ilifanana ingawa tulikuwa tunatofautiana baadhi ya tabia,” amesema
Ramadhan.
Akimuelezea Makonda amesema anajua kuishi na watu pale anapohitaji jambo
lake lifanikiwe kwani alikuwa anajua kunyenyekea kwa walimu ingawa
alikuwa na tabia ya kubagua marafiki hasa wale ambao familia zao
zilikuwa duni. “Alikuwa ni rafiki wa wenye uwezo,” amesema.
Pia ameeleza kwamba baada ya kujiunga na masomo ya jioni Pamba Sekondari
alihamia kwa ndugu yake mwingine anayefahamika kwa jina la Mwana
Zakhia.
Kuhusu mawasiliano kati yao, amesema ingawa wamekua pamoja hakuna
mawasiliano yoyote kati yao kutokana na Makonda kumpatia namba ambazo
hata akipiga simu hazipolewi.
“Alikuja hapa mara mbili usiku tukazungumza mambo mengi ikiwa ni pamoja
na kukumbushana maisha tuliyoishi. Zaidi ya hapo hatuna mawasiliano
kabisa zaidi ya kumsikia na kumuona kupitia vyombo vya habari na
mitandao ya kijamii,” amesema Ramadhani.
Mama Khamesse
JAMHURI lilifika nyumbani kwa Mama Khamesse Lumara na kufanya mahojiano;
JAMHURI: Una uhusiano gani na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam?
MAMA KHAMESSE: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni ndugu yangu kwani baba
yake, Mzee Albert Bashite ni binamu yangu. Kwa hiyo Daudi ananiita mimi
shangazi.
JAMHURI: Unaweza kunisaidia jila lake ni Daudi au Paul Makonda?
MAMA KHAMESSE: Mimi ninamfahamu kwa jina la Daudi Albert Bashite. Na
hata wakati nampeleka kuanza shule katika shule ya mshingi Nyanza
aliandikishwa kwa jina la Daudi Bashite.
JAMHURI: Ilikuwaje ukaanza kuishi naye?
MAMA KHAMESSE: Mama yake alikuja kuniomba mtoto wake aje kuishi na
kusomea kwangu. Ukweli sikuona sababu za kumkatalia. Nilimkubaliana na
kumpokea kisha ‘kumfanyia mpango wa kujiunga’ na shule ya Nyanza ambapo
aliingia darasa la tano mpaka alipomaliza darasa la saba.
JAMHURI: Alipomaliza darasa la saba matokeo yake yalikuwaje?
MAMA KHAMESSE: Ukweli ni kwamba hakubahatika kufaulu ili kujiunga na
kidato cha kwanza hivyo alilazimika kuanza kusoma masomo ya jioni katika
shule ya sekondari ya Pamba.
Lakini hakuweza kukaa nyumbani kwangu kwa kipindi kirefu baada ya kuanza
kusoma Pamba kutokana na sababu ambazo siwezi kukuelezea, kwani
nilimuita mama yake tukazungumza kisha akamchukua na kumuhamishia kwa
ndugu mwingine ambaye ni baba yake mdogo na Daudi.
Hata hivyo, wakati shangazi yake akigoma kutaja chanzo cha Makonda
kuondoka kwa Mzee Khamesse, habari za uhakika ambazo familia ya Khamesse
haikuthibitisha wala kukanusha zinasema Makonda alikuwa anachezea
bunduki ya Mzee Khamesse risasi ikafyatuka na kupasua paa.
“Mzee Khamesse alisema huyu mtoto andoke haraka. Alisema kama amechezea
bunduki yake kuna hatari anaweza akaua watoto wake kwa risasi kupitia
michezo yake isiyokubalika,” kinasema chanzo chetu.
Mtu aliyeko karibu na Makonda amekiri lilitokea tukio hilo, ila akasema:
“Hiyo ilikuwa michezo ya watoto. Mbona wengi tumemwaga uji wa mgonjwa?
Ni hawa watu wa dawa za kulevya tu wanaochochea hata hayo mambo madogo.”
JAMHURI: Je, alimaliza masomo yake ya sekondari na kuhitimu?
MAMA KHAMESSE: Mh! Hapo kwenye kumaliza sekondari siwezi kukueleza
lolote maana ni kautata kidogo kwani sikumbuki kitu kama hicho.
Ila ninachofahamu ni kwamba alianza kufanya kazi ya ukondakta wa
daladala kwenye mabasi ya baba yake mdogo ambaye kwa sasa ni marehemu
anayefahamika kwa jina la Mabina.
Baada ya muda kupita nilisikia kuwa amejiunga na Chuo cha Uvuvi Nyegezi,
jijini Mwanza, na baadaye nikasikia yuko chuo huko Mbegani, Bagamoyo
anasoma.
Lakini muda haukupita sana ndipo nikasikia kuwa amekuwa muhubiri hivyo alikuwa akihubiri injili na alikuwa akisafiri sana.
JAMHURI: Katika kipindi chote hicho uliwahi kusikia kuwa amebadili jina na kuitwa Paul?
MAMA KHAMESSE: Hapana nilikuwa sijawahi kusikia akiitwa jina zaidi ya
tunalolifahamu wanafamilia la Daud Bashite. Na siku zote namfahamu kwa
jina hilo hilo ingawa nilikuja kushangaa kuona kwenye luninga wakati
yuko Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) alipotambulishwa kwa jina la Paul
Makonda.
Nilishangaa jina nikadhani wamekosea, lakini kila siku zinavyokwenda
niliendelea kumuona kwenye luninga akitambulishwa kwa jina la Paul
Makonda huku akiwa ni Daud Bashite ninayemfahamu.
JAMHURI: Hili jina la Makonda unadhani amelitoa wapi?
MAMA KHAMESSE: Jina hili la Makonda ni jina ambalo lipo katika ukoo,
upande wa babu na bibi zake, hivyo sio jina jipya katika ukoo. Lakini
suala la yeye kuanza kuitwa hivyo labda yeye binafsi au wazazi wake
wanaweza kulisema hilo.
Ndugu
Mmoja wa ndugu zake wa karibu (jina linahifadhiwa) amesema kwamba Daudi
alishindwa kuendelea kuishi nyumbani kwa shangazi yake (Mama Khamesse)
kutokana na tabia ya kupenda kuwa karibu na marafiki wenye uwezo mkubwa
jambo lililokuwa linamnyima uhuru kwani alikuwa na tabia ya kuhamia huko
na kutorudi nyumbani.
“Daudi alikuwa anaweza kutoka nyumbani kwao Nyamanoro akahamia nyumbani
kwa rafiki zake baada ya siku kadhaa akarudi nyumbani tena kwa shangazi
yake. Tabia hii ilimkera Mama Khamesse ikamlazimu kuwasiliana na wazazi
wake ambao walimuondoa hapo na kumpeleka kwa ndugu mwingine,” amesema.
Amesema Mzee Albert Bashite alibahatika kuzaa watoto wawili tu ambao ni
Daudi na mdogo wake wa kike ambaye hata hivyo alifariki akiwa mdogo,
hivyo Daudi ni mtoto wa pekee wa Mzee Daudi Bashite na Susan Daud
Malagila. Jina la Daudi alilithi kutoka kwa babu yake mzaa mama.
Shule ya Msingi Nyanza
JAMHURI lilifika Shule ya Msingi Nyanza na kukutana na Mwalimu Mkuu
ambaye alikataa kujitambulisha kwa jina kwa madai kuwa hawezi kuzungumza
chchote mpaka atakapopata kibali kutoka kwa wakubwa wake.
JAMHURI: Mimi ni Mwandishi wa Habari kutoka Gazeti la JAMHURI. Nimefika
kwako kupata ufafanuzi kuhusiana na taarifa za Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam kusoma katika shule yako ya Nyanza.
Mwalimu Mkuu: Siwezi kuzungumzia suala lolote linalohusu jambo hilo.
Unatakiwa kuwa na kibali kutoka Ofisi ya Mkoa, nenda kwa RAS (Katibu
Tawala wa Mkoa), RAS akishatoa kibali kitatakiwa kuthibitishwa na DAS
(Katibu Tawala wa Wilaya), kisha utakipeleka kwa Afisa Elimu Wilaya,
ambaye naye atakithibitisha na kukuelekeza kwa Mkurugenzi wa Wilaya
ambaye atakupatia kibali cha kuja nacho hapa shuleni niweze kukujibu
maswali yako.
Hapa unataka data (takwimu), na taratibu za kupata data unazifahamu. Hivyo siwezi kabisa kukusaidia chochote. Karibu tena.
JAMHURI limefanya mahojiano na mmoja wa walimu shuleni hapo (jina
linahifadhiwa) ambaye amethibitisha Daudi Bashite kusoma katika shule ya
Nyanza.
“Nashangaa hili jambo kukuzwa kiasi hiki! Hili suala lipo wazi kabisa,
Daudi au Makonda kama anavyoitwa alisoma hapa na huyo Mwalimu Mkuu wa
Nyanza, Jovenary anaweza kuwa anafahamiana naye kama hakumtangulia
darasa kwani naye alisoma hapa hapa. Picha unayoiona kwenye mitandao
Daudi aliipigia palee kwenye ngazi,” amesema Mwalimu huyo.
Source: Jamhuri.
0 comments:
Post a Comment