Fikiria kila unachokijua na kukikumbuka kuhusu mabadiliko unayotaka yawe
katika maisha yako, halafu uone ukweli huu kama kweli nawe ni mmoja
kati ya watu wanaotaka mafanikio au uko nje ya mstari wa mafanikio na
pengine tu wewe hujijui.
Kama kweli unataka mafanikio, ni kwanini mara
kwa mara umekuwa ukisita au kuogopa kufanya... jambo ambalo lingeweza
kubadili maisha yako na kukuletea mafanikio mkubwa? Hili ndilo tatizo
walilonalo watu wengi wanahofia sana kufanya mabadiliko kwa namna moja
au nyingine hata kwenye yale malengo waliojiwekea wao wenyewe kuna
wakati huwa wanaogopa pia.
Kimaumbile, kila binadamiu anahofia mabadiliko, lakini hofu ya
mabadiliko inapozidi kuwa kubwa na kukuzuia kufanya mambo ya maana
kwako, hofu hii sasa hugeuka kuwa ni maradhi yanayokuzuia wewe
kufanikiwa. Hebu fikiria tena, ni mara ngapi umekuwa ukitaka kufanya
mabadiliko Fulani katika maisha yako, lakini umekuwa ukijikuta
ukishindwa kufanya hivyo kutokana na kuogopa kufanya vitu Fulani? Ni
mara ngapi umekuwa ukitaka kuingia kwenye biashara lakini umekuwa na
hofu nyingi zinakuzuia? Hivi ndivyo ilivyo mabadiliko huogopwa, wakati
mwingine bila sababu ya msingi.
Wengi wetu kutokana na kuogopa mabadiliko, hujikuta ni watu wa kutoa
sababu ambazo hata hazina mashiko zinazosababisha wao washindwe
kutekeleza malengo na mipango waliojiwekea. Utakuta mtu anakwambia
hawezi kufanya biashara ni kwa sababu hana mtaji, ukija kuchunguza
kidogo utagundua kuwa hiyo ni sababu ambayo amekuwa akiitoa kwa muda
mrefu, iweje kila siku mtu huyohuyo awe hana mtaji tu. Kama uko hivi una
hofu tu hata kwa vitu vidogo ambavyo ungeweza kuvifanyana , tambua kuwa
kuanzia sasa unaye adui mkubwa ndani mwako anayekuzuia kufanikiwa. Na
unapoogopa kufanya mabadiliko ambayo unaahitaji sasa ili ufanikiwe,
sahau kuhusu mafanikio katika maisha yako yote.
Tatizo kubwa utakalokuwa nalo linalosababishwa na hofu hii ya kuogopa
kufanya mabadiliko ni lazima utakuwa mtu wa kutaka mafanikio ya
harakaharaka. Watu wengi wenye mawazo ya kutaka kufanikiwa leoleo hata
kama wameanza biashara leo, wengi wao huwa wana hofu hii kubwa ya
mabadiliko ndani mwao, unaweza kufanya utafiti mdogo utagundua ukweli
huu ulio wazi. Hawa ni watu ambao kiuhalisia hawaijui wala kuiamini
subira ndani mwao, bali ni watu wakutaka mfumo wa maisha uwe ambao
unaanza leo biashara na wiki ijayo uwe tajiri ni kitu ambacho
hakiwezekani kabisa.
Hivi ndivyo walivyo watanzania wengi wanaogopa mabadiliko na kuamini
katika miujiza, sio katika wao wenyewe kutenda na kuona matokeo. Hebu
jaribu kukagua maisha ya walio wengi utakuja kugundua ukweli huu ni watu
wanaofikiria sana leo, sasa hivi, siyo baadaye. Hata malengo yao ni ya
karibu sana na hawataki shida, wanataka wafanye leo, wamudu leo na kila
kitu kimalizike leo. Sijui kesho watafanya kitu gani? Ukimwambia
mtanzania aanzishe mradi ili aje faidi baada ya miaka 10 kutoka sasa
kwanza atakushangaa, kisha atakucheka we hadi mbavu zimuume. Anataka leo
hata kama ni kwa miujiza.
Ndiyo maana wengi kati ya Watanzania hawana malengo, wanaishi tu na
kutawaliwa na hofu za mabadiliko. Kuweka malengo siyo sehemu ya maisha
yao, kwani malengo yanataka mtu mwenye subira, mtu anayeamini kwamba
maisha ni kuanguka na kusimama. Wanachojua kikubwa ni kulalamika na
kulaumu, kuponda na kukejeli, kwa sababu wao wamekata tamaa bila
kujijua. Ndiyo maana ni watanzania wanne tu kati ya kumi ambao wanafanya
kazi, wanatoka jasho na wanaweza kusubiri bila kukata tamaa, wengine
waliobaki wanasubiri ujanja ujanja tu ilimradi wafanikiwe hata kama ni
kwa kufanya uhalifu wa aina yoyote.
Ni watu ambao wanataka kuishi kihadithi, wawe na pete ambayo wanaweza
kuiamuru iwape wakitakacho na wakipate. Maisha ni ya kibunuasi- abunuasi
tu, watu hawa kwao mabadiliko ni kitu kigumu sana kwao na kinaogopwa
kweli. Kama unataka mafanikio ya kweli yawe kwako, unatakiwa kubadilisha
fikra za zako na kuamua kukubali kuwa mafanikio yanahitaji mabadiliko
makubwa sana ambayo wewe mwenyewe unatakiwa uyafanye kwa kujitoa hasa.
Acha kuwa na hofu zisizo na maana zinazokuzuia wewe usifanikiwe, chukua
hatua katika maisha yako, kuyafikia maisha unayoyataka.
0 comments:
Post a Comment