Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli amefika nyumbani kwake katika kijiji cha
Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita kwa mara ya kwanza tangu
achaguliwe kuwa Rais, ambapo akizungumza na wananchi katika mkutano wa
hadhara uliofanyika katika uwanja wa shule ya sekondari Chato, ametoa
wito kwa kila mtanzania kuchapa kazi kwa juhudi ili nchi iondokane na
utegemezi wa misaada ya wafadhili ambayo... huambatana na masharti.
Dkt. Magufuli amesema jukumu kubwa
lililo mbele ya watanzania kwa sasa, ni kushikamana na kujisimamia
katika maendeleo ili kila mmoja ahakikishe anaongeza uzalishaji na
utendaji kazi mahali pake pa kazi.
"Kwa hiyo ni lazima tujisimamie sisi
wenyewe, na tukijisimama sisi wenyewe kwa kila mmoja kuwajibika mahali
alipo, kama ni mfanyakazi afanye kazi kwelikweli, kama ni mkulima afanye
ukulima wake kwelikweli, kama ni mfanyabiashara afanye biashara
kwelikweli, kama ni mfugaji afuge kwelikweli, kama ni mvuvi avue
kwelikweli, Tanzania hii tutavuka" Amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amesema serikali
yake imeamua kuchukua hatua kudhibiti nidhamu serikalini, kwa
kuhakikisha inawachukulia hatua watumishi wa umma wanaolisababishia
taifa upotevu mkubwa wa fedha, na ameahidi kuwa hatua hizo maarufu kwa
jina la "Kutumbua Majipu" zitaendelea kuchukuliwa hadi tatizo hilo
likomeshwe.
Dkt. Magufuli pia amekumbusha viongozi
wote wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala na
Wakurugenzi, kutekeleza wajibu wao ipasavyo na ameweka bayana kuwa
mahali popote ambapo hapatakuwa na ufanisi, kiongozi husika atakuwa
amedhihirisha kuwa hatoshi kuendelea na wadhifa aliopewa.
Rais Magufuli amewapongeza walimu kote
nchini kwa kufanya kazi nzuri ya kufundisha, licha ya changamoto ya
ongezeko kubwa la wanafunzi waliojiunga darasa la kwanza mwaka huu,
lakini ametaka Wazazi na kamati za shule kushirikiana na walimu
kuwasimamia wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
"Niziombe kamati za shule zote Tanzania
nzima, kama haziwezi kusimamia nidhamu ya wanafunzi shuleni, zile kamati
za shule zijiuzulu. Lakini pia kama wewe ni Mwalimu Mkuu, shule yako
kila siku inatoa divisheni ziro nyingi kila mwaka, sioni sababu ya wewe
kuendelea kuwa Mwalimu Mkuu" Alisisitiza Dkt. Magufuli.
Kuhusu tatizo la wafanyakazi hewa, Rais
Magufuli amesema uhakiki mdogo uliofanywa hivi karibuni, umebaini
wafanyakazi hewa 1,680 waliokuwa wakilipwa shilingi bilioni 1 na milioni
800, na kwamba ni matarajio kuwa uhakiki unaofanywa nchi nzima
utaisaidia serikali kubaini wafanyakazi hewa wengi zaidi na kunusuru
fedha nyingi zaidi za watanzania.
Ametolea mfano wa mfanyakazi mmoja wa
Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) ambaye alikuwa akilipwa mishahara ya watu
17, na kueleza kuwa mfanyakazi huyo atafikishwa mahakamani.
Pia Rais Magufuli amesema serikali yake
imejiandaa kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kupunguza kodi kutoka
asilimia 11 ya sasa hadi asilimia 10 au 9 kuanzia bajeti ijayo, lakini
amesema kwa wale wanaolipwa mishahara mikubwa ambayo inafikia hadi
shilingi milioni 40, itapunguzwa na kuweka kima cha juu cha mshahara
usiozidi shilingi milioni 15.
0 comments:
Post a Comment