Pages

Subscribe:

Saturday, June 25, 2016

HADITHI: NYUMA YA MACHOZI (sehemu ya nane) 08


MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
ILIPOISHIA:
Toka aolewe na Deus hakuwahi kwenda sehemu za starehe zaidi ya kwenda kwenye dhifa ya kiserikali. Lakini mashoga zake walimweleza raha wanazozipata wanapokwenda kwenye kumbi za starehe hata kwenye vikundi vya taarabu. Moyoni alijisemea: Leo mjanja lakini ipo siku utanijua mimi na yeye nani zaidi.”
SASA ENDELEA...
Kilole akiwa na mpango mzito moyoni mwake ambao aliujua yeye na Mungu wake, ili kuufanikisha alionesha ukaribu na mpenzi wa Kinape kitu kilichomziba macho Kinape kwa kuamini...
Kilole amekubaliana na alichomueleza *****

Maisha yaliendelea kama kawaida kwa Kilole naye kumtembea mchumba wa Kinape kuonesha ukaribu. Hali ile iliongeza mapenzi kwa Kinape kuona hali ipo shwari bila kujua kuna bomu zito limepangwa dhidi yake ya kulisambaratisha penzi lake. Wakati huo Kinape alikuwa katika hatua za mwisho kumpeleka happy kijijini kutambulishwa kwa wazazi wake. Kilole alipanga kutekeleza mpango kabla ya Kinape hajampeleka Happy kijijini, aliamini kama atachelewa itakuwa vigumu kuutekeleza mpango wake. Matumaini ya kutekeleza mpango wake yalikuwa makubwa baada ya kupewa na taarifa na mumewe ana safari ya kikazi nje ya nchi kwa siku tano. Siku ilipofika ya mumewe kusafiri ilikuwa tofauti na siku zote, Kilole alionesha kumhitaji mumewe kuliko kipindi chochote kilichopita.

“Mke wangu siku tano si nyingi,” Deus alimtuliza mkewe aliyekuwa akilia.
“Kwako si nyingi lakini kwangu naona kama miaka mitano,” Kilole alidondosha machozi ya uongo.
“Najua basi nitajitahidi safari nyingine tusafiri pamoja.”
“Itakuwa afadhari.”

“Kinape kuwa karibu na shemeji yako hata ukiwa mbali na nyumbani mpigie simu ili asipate upweke.” Deus alimweleza rafiki yake.
“Deus si mpo kwenye Facebook twitter instagram usiku tumieni kuliwazana ili usijione mpo mbali mbali,” Kinape alitoa wazo ili ajiweke mbali na Kilole.
“Na kweli mke wangu, kila baada ya kazi nitakuwa pamoja na wewe katika kuchati.”
“Lakini si sawa na wewe kuwa pembeni ya ubavu wangu,” Kilole alilia wivu wa uongo. 

“Basi mke wangu niombee niende salama nirudi salama, si unajua kazi zetu.”
“Na ukirudi utimize ahadi ya kuninunulia gari langu,” Kilole alisema kwa sauti ya kideka. 

“Kila kitu kipo tayari, subiri nikufanyie Surprise.”
“Waawoo mpenzi wangu.” Kinape alijikuta akifurahi furaha ya kweli baada ya kuona ndoto yake ya siku moja kuendesha gari lake mwenyewe inatimia. Alimkumbatia mumewe na kumtakia safari njema. 

“Dear usafiri salama na urudi salama, ukiwa mbali kumbuka umeniacha kama kinda la ndege linalomsubiri mama yake aliyekwenda kutafuta chakula.”
“Hilo nalijua, nataka mpenzi wangu na mwanangu muishi maisha nusu ya peponi.” “Asante mume wangu.

” Kilole aliagana na mumewe na kurudi nyumbani na Kinape katika gari moja, wakiwa njiani Kinape alimchokoza.
“Ona ulitaka kupoteza bahati yako bure, haya ndiyo mapenzi unayotakiwa kuyapigania.”

“Kinape yale yalikwishapita achana nayo.
” Walirudi wote mpaka nyumbani, walipofika Kinape hakukaa aliaga na kwenda kuonana na mpenzi wake kitu ambacho Kilole hakupenda kukisikia.
*****
Kilole akiwa peke yake aliamini mpango alioupanga Kinape hawezi kuruka, alichukua simu yake na mkononi na kutafuta jina la mtu, kisha alipiga na kuiweka sikioni kusikiliza. Baada ya kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo Sisiter.”
“Haloo Jimmy.”
“Ndiyo Sister lete stori, naona leo umenikumbuka.”
“Mambo mengi mtu wangu, upo pande zipi?”
“Ndiyo nafika kijiweni, ulikuwa unasemaje? Najua wito wako lazima nidake vumba nene.”
“Unaweza kuja nyumbani mara moja?”
“Hakuna tatizo.” “Basi njoo mara moja.”
“Okay, nakuja.” 

Kilole alikata simu na kutabasamu mwenyewe huku akijisemea moyoni: “Kinape hana ujanja japo mjini aliwahi lakini mimi ndiye mwisho wa matatizo lazima arudi mikononi mwangu na uchumba wake ubakie hadithi.”

Kengele ya mlangoni ilimuondoa kwenye mawazo na kumfanya ananyuke kwenda kufungua.
“Ooh! Jimmy, karibu.”
“Asante Sister.”
Baada ya Jimmy kuingia alikaa kwenye kochi la watu watatu, Kilole alikaa kwenye kochi la mtu mmoja. Kwa vile Jimmy alikuwa mbali na Kilole, alimuomba asogee kochi la karibu.

“Jimmy, njoo ukae kwenye kochi hili.”
Jimmy alinyanyuka na kwenda kukaa karibu yake, Jimmy alionekana mtu mwenye wasiwasi sana.
“Jimmy mbona hivyo?” 

“Mmh! Jinsi tulivyokaa mumeo akitokea inaweza kuwa msala.” “Kwani hajui kama wewe mpiga picha?”
“Anajua, lakini naona kama tumekaa karibu sana.”
“Wasiwasi wako kwanza mume wangu kasafiri.”
“Na mdogo wake?”
“Ametoka na hawezi kurudi sasa hivi.”
“Haya sister nipe dili basi.” 

“Kuna kazi nitakupa uifanye, ukiifanya vizuri nitakupa pesa nzuri sana ambayo hukuwahi kuipata toka ulipoanza kazi ya kupiga picha.” “Kazi gani hiyo dada?”
“Ya kupiga picha.”
“ Mmh! Ni kazi ipi, mbona kama naona kama si ya kawaida?”
“Ni kweli, hii itakuwa siri yako na malipo yatakuwa mazuri.”
“Kazi hiyo itakuwa lini?”
“Ikiwezekana leo hii.”
“Poa basi ikiwa tayari nishtue.”

“Jimmy, naomba usifanye kazi yoyote kuanzia sasa hivi, nitakulipa pesa ya usumbufu na kazi ikikamilika nitakupa fedha nzuri sana.”
“Hakuna tatizo sister, nakuamini dada yangu wa ukweli.” “Nisubiri,” Kilole alinyanyuka na kwenda chumbani, baada ya muda alirudi na elfu 50 na kumpa Jimmy.
“Hii ya usumbufu, ya kazi bado.”

“Asante Sister.” Jimmy alipokea na kutoka akimwacha Kilole akifurahia mpango wake, alichukua simu yake na kumpigia Kinape. Baada ya simu kuita kwa muda Kinape upande wa pili aliipokea. 

“Haloo Shemu.”
“Kinape upo wapi?”
“Nipo na mke mwenzio hapa.”
“Waawoo! Nimeipenda hiyo,”
. “Kweli?” Kinape alimuuliza.
“Kweli, inafurahisha, mmeonesha jinsi gani mnavyo pendana.” “Ndiyo shemeji yangu, una lipi tena?”

“Nimesahau kukujulisha kuwa leo ni siku yangu ya kuzaliwa.” “Wawooo, mbona hukuniambia mapema nikuandalie zawadi?” “Nilipitiwa lakini jioni kutakuwa na sherehe fupi ya kifamilia.” “Hakuna tatizo nitakutafutia zawadi nzuriii shemeji yangu.” “Nitashukuru, uje na Happy.”
“Hakuna tatizo.” 

Baada ya kuzungumza na Kinape, alimpigia simu mtengeneza keki ili amuandalie keki ya birthday, ambaye aliwahi kumtengenezea mwanaye alipotimiza mwaka mmoja.
“Sakina ninaweza kupata keki ya birthday?”
“Lini shoga?”
“Leo hii jioni.”
“Jamani! Mbona haraka, ya nani?”
“Yangu mwenyewe.”
“Jamani shoga! Mbona hukunialika?”
“Kwani mimi? Shemeji yako ndiye kasema akirudi jioni akute keki, mwenyewe nilikwisha sahau kama leo siku yangu ya kuzaliwa,” Kilole aliunda uongo unaofanana na kweli. “Kwa hiyo jina lako ni lilelile?”
“Lipi hilo?”
“La Kilole?”
“Hilohilo mpenzi.”

“Basi hakuna tatizo nipe saa mbili kila kitu kitakuwa tayari.” “Nitashukuru.” Baada ya kuachana na mtengeneza keki, alikumbuka kitu muhimu kilichotakiwa kiwepo pale ili kufanikisha mpango wake. Alimpigia simu mpiga picha, simu iliita kwa muda kisha ilipokelewa upande wa pili.

“Oya, sister mambo tayari?”
“No, kuna kitu nataka kukutuma kabla ya kazi yetu.”
“Kitu gani hicho?”
“Eti kete ya unga shilingi ngapi?”
“Unga upi?”
“Kokeni, sijui heloin.”
“Una maanisha madawa ya kulevya?”
“Ndiyo.”
“Mmh! Ya nini?”
“Jimmy, utajua baadaye.”
“Sijajua bei yake, lakini sidhani kama inazidi elfu tano kwa kete.” “Basi njoo uchukue fedha ukaninunulie kete mbili.”
“Sister unajidunga nini?”
“Jimmy, kazi itakushinda.”
“Basi Sister nakuja.”

Baada ya muda mfupi alifika na kupewa elfu ishirini akanunue kete mbili za unga. Alitoka na kumwacha Kilole akiendelea na maandalizi ya mipango yake ambayo ilikuwa siri yake na Mungu wake. 

Alimtuma mlinzi kununua vinywaji ambavyo alivijaza kwenye friza, kila kitu kilikwenda kama kilivyopangwa. Kilole baada ya kuridhika na mipango yake kwenda vizuri alijiandaa kuisubiri keki ili akamilishe zoezi lake.

Baada ya saa mbili kama alivyoahidia alijulishwa kuwa keki tayari, kwa vile hakutaka kutoka alimuomba mpelekewe. Sakina alimletea keki baada ya nusu saa, wakati huo mpiga picha alikuwa amefika na kumpa kete mbili za unga.

“Asante Jimmy, kwa kazi hii nitakupa posho elfu kumi, ila kuna kazi nyingine unatakiwa kuifanya.”
“Ipi hiyo?”
“Nitakupa namba hii nikikubip ipige, akipokea mwambie anatakiwa kwao haraka sana kuna matatizo.”
“Sawa.”
“Hakikisha unakaa mkao wa kazi usicheze mbali nakutegemea wewe ndiye steling wa picha.”
“Hakuna tatizo sister.”
“Jimmy ukiifanya kazi kwa ufanisi nitakupa laki mbili.”
“Utani huo sister!”
“Sina utani kwa jambo nitakalo kuahidi.”
“Sawa, wacha nikuache uendelee na mambo mengine.”
Jimmy aliondoka na kumuacha Kilole akitengeneza nyumba kwa ajili ya sherehe ya kutengeneza ya birhtday yake. Sebule aliipamba na kupambika ikawa katika muonekana wa kupendeza.
Itaendelea

1 comments:

Unknown said...

iko poa sana kijan

Post a Comment