Wednesday, August 16, 2017
Story: KAHABA KUTOKA CHINA (Sehemu Ya Kumi Na Mbili) 12
Bwana Shedrack bado alionekana mwenye hasira nyingi. Kila siku hasira zake zilikuwa juu ya Irene ambaye alionekana kuwa chanzo cha kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea, kile cha kumfanya Irene aondoke nyumbani hapo. Kila siku, Bwana Shedrack alikuwa akitafakari namna ya kumpata Irene na kisha kutekeleza kile ambacho alikuwa amekipanga katika kipindi kile.
Irene akaonekana kuwa sababu ya kuiondoa amani ndani ya nyumba yake, Irene ndiye akaonekana kuwa sababu ya kumfanya Rose atorokea ndani ya nyumba ile, na kwa...
sababu huyo ndiye alionekana kusababisha hayo yote, haikuwa budi kumuua, kumuua mtu kama huyo kwake wala halikuonekana kuwa dhambi, kwani alimuona Irene kuwa kama gugu ambalo liliota ndani ya shamba la mchicha na hivyo lilitakiwa kukatwa ili lisiweze kuleta matatizo kwa wengine.
Kwa sababu katika kipindi hicho alikuwa na hasira kali, akajua fika kwamba Irene alikuwa makini kwa kila akifanyacho. Msichana huyo asingeweza kutulia kwa kujua kwamba Bwana Shedrack alikuwa na hasira juu yake. Ni lazima angekuwa akiishi katika maisha ya kujificha jificha na hivyo kumfanya Bwana Shedrack kutokumpata kabisa. Uamuzi ambao aliufikia bwana Shedrack ni kujifanya amesahau huku hasira zake zikiendelea kuwa kali kila siku.
Kuna kitu kingine kikaonekana kuibuka katika wakati huo. Lawama nyingi zilikuwa zikipelekwa kwake kutoka kwa Bwana Edward na familia yake kutokana na kusababisha Rose aondoke nyumbani pale na wakati alikuwa na ujauzito wa Peter.Lawama zile ndizo ambazo zilikuwa zikimtia hasira Bwana Shedrack na kujiona kama alikuwa akichelewa kutimiza kile ambacho aliuahidi moyo wake, kumuua Irene kwa gharama zozote zile.
“Yeye kuondoka si tatizo. Tatizo ni mjukuu wangu tu. Ningependa kumuona mjukuu wangu ili nione anafanana vipi na mwanangu pamoja na mimi” Bwana Edward, baba yake Peter alimwambia Bwana Shedrack ambaye alikuwa amekaa kimya kwa kipindi kirefu.
“Usinilaumu sana kama mimi ndiye niliyesababisha hilo” Bwana Shedrack alimwambia Bwana Edward.
“Sasa nani kashababisha kama sio wewe?”
“Kuna malaya mmoja ndiye aliyesababisha haya yote. Yaani unavyoona Rose kaondoka nyumbani, jua kwamba yeye ndiye aliyesababisha haya, unapoona kwamba hauwezi kumuona mjukuu wako, basi jua kwamba huyu malaya ndiye aliyesababisha hayo” Bwana Shedrack alimwambia Bwana Edward.
“Kivipi?”
“Usitake kujua kivipi ila wewe jua hivyo tu” Bwana Shedrack alijibu.
“Hebu nisikilize. Kama kuna mtu kasababisha hayo, kwa nini tusimuue? Kwa nini amejaribu kucheza na watu kama sisi halafu sisi tusimuonyeshee kwamba sisi ni watu wa aina gani? Au mwenzangu umelifurahia hili?” Bwana Edward alimuuliza Bwana Shedrack.
“Hapana. Sijalifurahia hata kidogo”
“Kwa hiyo hapa kitu cha msingi ni kufanya jambo moja tu, kumuua huyo mtu ili kila kitu kiwe kama zamani na nina matumaini kwamba kama tukifanikisha jambo hilo basi itakuwa imeturahisishia sana. Au wewe unaonaje?” Bwana Edward alimwambia Bwana Shedrack na kisha kumuuliza.
“Sawasawa. Hakuna tatizo”
“Ila unapafahamu anapokaa katika kipindi hiki?”
“Alikuwa akikaa hostel”
“Mpaka sasa hivi au?”
“Bado sijajua kwani siku ambayo nilikwenda kumuulizia hakuwepo, nafikiri alinikimbia” Bwana Shedrack alisema.
“Kwa hiyo siku hiyo alijua kama ungefika mahali hapo?”
“Yeah! Nadhani Rose alimpigia simu na kumtaarifu”
“Hakuna tatizo. Acha tujifanye kama tumemsahau vile. Au wewe unaonaje?”
“Hilo neno. Na tayari sasa hivi ushapita mwezi mzima tangu nisahau”
“Basi hakuna neno kama tutampa mwezi mwingine wa kuzidi kuvuta pumzi ya dunia hii”
Siku hiyo wakakubaliana kwamba ilikuwa ni lazima Irene auawe kwa ajili ya kurekebisha kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea. Bwana Edward alikuwa kama mtu wa kufuata mkumbo katika tukio zima la kumtaka Irene kuuawa, alichokuwa akikijua yeye ni kwamba Rose alikuwa ametoroka nyumbani, kaelekea wapi? Na kwa sababu gani alikuwa ametoroka? Hivyo wala hakujua, alichokuwa akikitaka ni kuona Irene akiuawa kwa sababu tu aliambiwa kuwa chanzo cha Rose kutoroka nyumbani.
Kila siku Peter hakuonekana kuwa na furaha kabisa, hakuamini kama mpenzi wake, Rose alikuwa ametoroka nyumbani kwao na kwenda sehemu ambapo wala hakupafahamu. Mawazo yalikuwa yakimuandama moyoni mwake, akakosa amani, furaha yote ikaonekana kumpotea katika kipindi hicho. Kitu ambacho alikuwa akikifikiria zaidi kilikuwa ni mimba ambayo aliamini kwamba alikuwa amempa Rose, aliamini kwa asilimia mia moja kwamba mimba ile ilikuwa yake.
Kila siku alikuwa akitamani kukaa na Rose, kuilea mimba ambayo wala haikuwa yake na mambo mengine kusonga mbele. Kitendo cha Rose kutoroka nyumbani kwao kiliendelea kumuumiza kupita kawaida, ndoto za kuishi na Rose zikaonekna kupotea kabisa moyoni mwake. Kiu ikaonekana kumkaba, kiu ya kutaka kuliona tumbo la Rose ikaonekana kumshika kupita kawaida.
Alipoletewa taarifa kwamba nyuba ya kila kilichotokea kulikuwa na mtu fulani ambaye huyo alikuwa chanzo cha kila kitu, akaunga mkono mpango ambao ulikuwa umewekwa kwa ajili ya mtu huyo kuuawa. Kila mmoja katika familia yao akakubaliana na Bwana Edward ambaye alionekana kuwa na hamu kubwa zaidi ya kutaka kummaliza mbaya aliyeleta masikitiko moyoni mwa kijana wake, Peter.
Mipango ikapangwa na baada ya mwezi mwingine kupita, hapo wakaonana na kisha kuanza kupanga mipango ya mauaji zaidi. Kwanza ilitakiwa Irene kutekwa na kupelekwa sehemu ambayo isingekuwa na watu na kisha kumuulia huko kama kisasi.
Japokuwa Peter hakuwa amehusika hata katika tukio moja la hatari, lakini siku hiyo nae alikuwa mmoja wa wahusika ambao walitakiwa kufanya ile kilichotakiwa kufanywa kwa wakati huo.
Bwana Shedrack akawaambia mahali ambapo Irene alikuwa akipatikana, alikuwa akiishi katika jengo la hosteli moja iliyokuwa Sinza Makaburini. Hilo likaonekana kutokutosha kabisa kitu ambacho akawapa mpaka picha ili kila kitu kiwe rahisi.
“Kwa hiyo tutaanzia wapi?” Bwana Shedrack aliuliza.
“Tunamtumia Peter, yeye ndiye atakayefanya asilimia kubwa ya kazi yetu” Bwana Edward aliwaambia.
Peter ndiye alionekana kutakiwa kufanya asilimia kubwa juu ya kazi ambayo ilikuwepo mbele yao katika kipindi hicho, yeye ndiye ambaye alitakiwa kuhakikisha anamchukua Irene na kisha kumuingiza ndani ya gari na kuelekea nae sehemu kwa ajili ya kumuua tu. Hilo wala halikuonekana kuwa tatizo sana, kwa sababu kila kitu kilikuwa katika mipango, kazi ikaonekana kukamilika ndani ya siku kadhaa.
“Kuna jingine la kuongezea” Bwana Shedrack aliwaambia.
“Lipi?”
“Huyu malaya ni msagaji” Bwana Edward aliwaambia.
“Unasemaje?”
“Huyu malaya ni msagaji. Kumbuka hilo Peter” Bwana Shedrack aliwaambia jambo ambalo likawafanya kugundua baadhi ya sababu iliyomfanya Bwana Shedrack kumchukia Irene.
“Hakuna neno” Peter alijibu.
Pamoja na wote wawili kusoma katika shule ya St’Marys lakini wakati mwingine Lee na Lydia walikuwa wakipelekwa katika shule ya Kichina ya Sheng Shun iliyokuwa Posta ya zamani kwa ajili ya kujifundisha lugha ya Kichina. Bado ukaribu wao ulikuwa mkubwa sana kana kwamba wote walikuwa wachina au watanzania.
Kwa Lee, bado alikuwa mvulana ambaye alipenda sana kuongea na utundu mkubwa ambao ulikuwa ukiwakasirisha sana hata walimu wa kichina katika kipindi ambacho alikuwa akienda pamoja na Lydia katika shule hiyo. Kila walipokuwa wakiweka mishumaa katika sehemu ambayo kulikuwa na mungu wao, buddha, mishumaa ile ilikuwa ikizimwa na Lee ambaye alikuwa akiingia kisiri ndani ya ukumbi ule wa ibada.
Lee akaonekana kukera kupita kawaida, walimu walikuwa wakiuchukia sana utundu wake lakini kamwe hawakuweza kumchukia yeye. Kikafika kipindi ambacho Lee akaonekana kutokusikia hali ambayo ikawafanya kuanza kumfunga kamba miguuni na kisha kamba ile ngumu kuifunga katika bomba moja kubwa darasani humo.
Kwa kitendo hicho, kidogo kikaonekana kusaidia, Lee akawa anatulia darasani na kusoma kama alivyokuwa akisoma Lydia ambaye bado alikuwa katika hali ya ukimya kupita kawaida. Hao walikuwa watoto wawili ambao walikuwa wakiishi pamoja kama ndugu ambao walizaliwa tumbo moja.
Maisha yaliendelea zaidi, kila siku dereva alikuwa akiwafuata shuleni hapo na kisha kuwachukua na kurudi nao nyumbani. Hilo ndilo lilikuwa jukumu lake ambalo alitakiwa kulifanya kila siku, jukumu la kuhakikisha kwamba Lee na Lydia wanafuatwa shuleni na kuletwa nyumbani kama kawaida.
Katika siku ya leo, derava alionekana kuchoka kupita kawaida, ni kweli aliambiwa awafuate Lee na Lydia shuleni lakini hakuwa akijisikia vizuri kabisa kwa sababu alikuwa akiumwa. Bi Lucy wala hakuonekana kujalia, alichokifanya ni kuwasiliana na uongozi wa shule ile ya Kichina ambayo walikuwa wakiingia mchana baada ya kutoka St Marrys na kisha kuwaambia kuhusiana na hali ambayo ilikuwa ikiendelea kwamba dereva asingeweza kufika, hivyo Lee na Lydia walitakiwa kupanda ndani ya basi la shule pamoja na wanafunzi wengine.
Baada ya kutoa taarifa hiyo, akaendelea na kazi zake kama kawaida huku akiongea na Rose ambaye alionekana kuwa kama ndugu kwake. Kila mmoja katika kipindi hicho alikuwa na hamu ya kitu kimoja tu, kuwaona watoto wao wakifika nyumbani hapo salama kama ilivyokuwa siku nyingine. Siku hiyo ikaonekana kuwa tofauti sana, muda ambalo gari la shule lilitakiwa kufika katika nyumba za watoto wote, siku hiyo likaonekana kuchelewa kufika ndani ya nyumba hiyo kwani muda wa mwisho ilikuwa ni saa kumi na moja lile limekwisharudi shuleni.
Kila mmoja akaonekana kuwa na wasiwasi, hawakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea. Alichokifanya Bi Lucy ni kuanza kuelekea ilipokuwa simu yake ya mezani kwa lengo la kupiga simu shuleni na kuulizia ni kitu gani kilikuwa kimetokea mpaka basi la shule kuchelewa kufika mahali hapo.
Huku akiifuata simu ile, mara ikaanza kuita, akaongeza mwendo kidogo na kisha kuipokea. Rose hakutaka kubaki kule jikoni alipokuwa, alichokifanya ni kuanza kuelekea kule sebuleni na kisha kuanza kumwangalia Bi Lucy ambaye alikuwa akiongea na mtu simuni.
Kadri sekunde zilivyozidi kusonga mbele, Bi Lucy akaonekana kubadilika, uso wake ukaanza kuingiwa na majonzi na mwisho wa siku machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake jambo ambalo lilimshtua sana Rose. Bi Lucy akaonekana kushindwa kuvumilia, akauachia mkonga wa simu na kisha kuchuchumaa, akaanza kulia kama mtoto jambo ambalo lilimfanya Rose kushtuka zaidi na kumsogele na kumuuliza ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea.
Bi Lucy alikuwa akiendelea kulia kama kawaida jambo ambalo lilimfanya Rose kugudua kwamba simu ambayo ilikuwa imeingia kipindi kichache kilichopita ilikuwa ni simu mbaya ambayo ilimsababishia kulia kwa uchungu mkali namna ile. Rose akabaki akimbeleza huku akitaka kujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea lakini Bi Lucy hakunyamaza zaidi ya kuendelea kulia.
Kichwa cha Rose katika kipindi hicho kilikuwa kikifikiria kuhusiana na taarifa ya msiba ambayo alikuwa amepewa katika simu ile, nae akajikuta akianza kulengwa na machozi. Hali ile iliendelea kwa dakika mbili, Bi Lucy akanyamaza na kisha kumwangalia Rose usoni, alionekana kusikitka sana huku dhahiri akionekana kuwa na jambo moyoni mwake.
“Kuna nini?” Rose alimuuliza Bi Lucy ambaye alikuwa akiendelea kumwangalia Rose usoni kwa masikitiko.
“Taarifa mbaya kutoka shuleni” Bi Lucy alijibu huku akiyafuta mahozi yaliyokuwa yakimtoka.
“Taarifa gani?”
“Twende shuleni” Bi Lucy alimwambia Rose huku akisimama.
Mpaka katika kipindi hicho tayari Rose akaonekana kugundua kitu kwamba kulikuwa na uwezekano kwamba basi la shule ambalo walikuwa wakilitumia wanafunzi wa shule ya ile iliyokuwa ikifundisha kichina lilikuwa limepata ajali. Hapo ndipo ambapo Rose akaanza kumfikiria mtoto wake, Lydia, bila kutarajia nae machozi yakaanza kumtoka kwa kuona kwamba kama basi litakuwa limepata ajali basi Lydia atakuwa amekufa na kama kanusurika basi atakuwa mahututi.
Walipotoka nje ya nyumba ile, wakachukua gari lao ambalo kulikuwa na dereva ambaye alitakiwa kuwafikisha popote pale walipokuwa wakitaka kwenda. Ndani ya gari, kila mmoja alikuwa kimya, Bi Lucy alionekana kama alikuwa kitu moyoni, kitu ambacho alikuwa akitamani sana kumwambia Rose lakini hakutaka kufanya hivyo, alikuwa kimya huku akisubiri mpaka katika kipindi ambacho wangeingia shuleni hapo.
Walichukua muda wa dakika thelathini wakawa wamekwishafika katika eneo la shule hiyo ambapo wakateremka na kisha kuanza kuelekea ofisini. Polisi kadhaa walikuwepo katika eneo la shule ile huku wakihakikisha kwamba ulinzi bado ulikuwa ukiendelea kuwekwa katika eneo lile.Wakaelekea mpaka ofisini, mkuu wa polisi wa kitu cha Osterbay alikuwa akimhoji mwalimu mkuu wa shule hiyo.
Hawakuongea kitu chochote kile mpaka mahojiano yalipokwisha na ndipo wakawageukia Bi Lucy na Rose ambao walikuwa wamekwishafika ndani ya eneo hilo.
Hata kabla ya kuongea kitu chochote kile, polisi yule akaanza kuwaangalia kwa zamu na kisha kutoa kalamu yake iliyokuwa mfukoni.
Huku wakiendelea kuwepo mahali hapo, Lee akatokea na kisha kuanza kumfuata mama yake, alipomfikia, Bi Lucy akamkumbatia kwa furaha, hakuamini kama mtoto wake angekuwa hai katika kipindi hicho. Rose hakuonekana kuwa katika hali nzuri, maswali kibao yakaanza kumiminika kichwani kwake kwamba kama Lee alikuwa hai na alikuja kumkumbatia mama yake, Lydia alikuwa wapi? Kila alichokuwa akijiuliza, alikosa jibu na moyo wake kuendelea kuwa na wasiwasi zaidi.
“Kuna utekaji umetokea” Polisi yule aliwaambia huku akionekana kuwa katika hali ya majonzi.
“Utekaji?” Rose aliuliza kwa mshtuko
“Ndio. Basi la shule lilivamiwa na watu wasiojulikana na kisha mtoto mmoja mwenye ngozi nyeusi, mtoto pekee mweusi kwenye basi hilo kutekwa na watu hao waliouwa na bunduki” Polisi yule alisema maneno ambayo yalionekana kumshtua Rose.
Rose akashindwa kuvumilia, bila kupenda, machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake. Kati ya watoto wote sitini ambao walikuwa wakipandishwa ndani ya basi na kisha kurudishwa nyumbani, ni mtoto wake tu ndiye hakuwa mchina, hiyo ilimaanisha kwamba ni mtoto wake ndiye ambaye alikuwa ametekwa na watu hao.
“Lydia…!” Rose alisema huku akiendelea kulia.
“Yeah! Ni mtoto wa kike. Jina lake ni hilo hilo, Lydia. Ila katika hayo yote, tayari polisi wamekwishaanza kufanya kazi yao kwa hiyo hautakiwi kuhofia kitu chochote kile” Polisi yule alimwambia Rose.
Maumivu ambayo yalikuwepo moyoni mwake katika kipindi hcho yalikuwa makubwa kupita kawaida, kitendo cha mtoto wake kutekwa na watu wasiojulikana kilionekana kumuumiza kupita kawaida. Hakujua ni mtu gani ambaye alikuwa amemteka mtoto wake, hakujua ni mtu gani ambaye alikuwa nyuma ya kila kitu kilichokuwa kimetokea.
Rose akaanza kulia mfululizo huku akifarijiwa lakini katika kipindi kile faraja zile hazikuonekana kusaidia hata mara moja kwa sababu hazikuweza kubadilisha kitu chochote kile zaidi ya ukweli kubaki pale pale kwamba Lydia alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana. Walichokifanya polisi ni kumuita dereva pamoja na jamaa yake ambaye alikuwa nae ndani ya basi lile na kisha kumtaka kuelezea.
“Wakati tumefika hapo General Tyre, kuna watu walitusimamisha, hatukutaka kusimama kwa sababu hatukuwa tukiwafahamu na wala hawakuwa polisi. Nikazidi kuendesha gari kama kawaida. Tulipofika Macho, kulikuwa na kijifoleni cha daladala kadhaa, tukashangaa kuwaona wale watu wakiwa wamelisogelea gari letu, tena huku wakiwa wametoka katika gari yao ndogo na kisha kunifuata. Walichonitaka ni kumwambia utingo wangu afungue mlango, nilitaka kubisha, na alijua kwamba ningefanya hivyo, akanitolea bunduki, sikuwa na ujanja, nikamwambia utingo afungue mlango” Dereva alielezea huku akionekana kuwa na uchungu.
“Ikawaje bada ya hapo?” Polisi yule aliuliza.
“Vijana wawili wakaingia ndani huku wakiwa na bunduki, wakabaki wakiangalia huku na kule, walipomuona yule mtoto mweusi, wakamfuata, wakambeba juu juu na kisha kutoka nae nje ya basi lile” Dereva aliendelea kuelezea.
“Ikawaje sasa baada ya kuondoka nae? Walielekea nae wapi?”
“Walimpakiza ndani ya gari lao na kisha kuondoka nae” Dereva aliwaambia.
“Waliondoka nae upande gani?”
“Ule unaoelekea Coco Beach. Ila sijajua baada ya hapo walielekea wapi japokuwa kwa mbali niliwaona wakikata kwenye barabara ya kulia kwa kuacha lami pale katika hospitali ya CCBRT na kisha kuchukua barabara ya vumbi upande wa kulia, bila shaka walikuwa wakienda mpaka barabara ya Mwinyi kuendelea na safari yao” Dereva Wa basi la shule alisema.
Polisi wakachukua maelezo yake na kisha kutaka kuwa karibu nao zaidi kwa ajili ya maelezo mengine ambayo yangehitajika kutoka kwake huku uchunguzi zaidi ukiendelea kufanyika juu ya utekaji ambao ulikuwa umefanyika ndani ya jiji la Dar es Salaam. Taarifa za utekaji ule zikazidi kuenezwa katika vituo vingine ndani ya jiji la Dar es Salaam, Kibaha pamoja na Bagamoyo huku baadhi ya wananchi wakipewa taarifa juu ya utekaji huo.
Waandishi wa habari walipozipata taarifa hiyo, kwanza wakaanza kuelekea katika makao makuu ya polisi yaliyokuwa Posta karibu kabisa na kituo cha treni ziendazo mkoani Kigoma na Mwanza na kisha kuanza kuzungumza na Kamanda mkuu wa polisi mkoa, Bwana Suleimani Rashidi ambaye alidhibitisha juu ya utekaji ambao ulikuwa umefanyika.
Taarifa zikapelekwa katika vituo vya habari ambapo moja kwa moja taarifa ile ikaanza kutangazwa. Kwa kila mwananchi ambaye aliisikia taarifa ile alionekana kushtuka, taarifa ile ilikuwa na mshtuko kutokana na matukio ya utekaji kutokufanyika ndani ya jiji la Dar es Salaam tena mbaya zaidi likiwa limefanyika kwa mwanafunzi mmoja ambaye alikuwa akitoka shuleni.
Watu wakaonekana kukilaani kitendo kile ambacho kilikuwa kimetokea, malalamiko mengi ya wananchi yakaanza kusikika katika kila sehemu ambazo walikuwa wakihojiwa na waandishi wa habari kuhusiana na habari hiyo ambayo tayari ilikuwa imesambaa ndani ya jiji la Dar es Salaam na hivyo kuanza kulitikisa jiji hilo. Kila mmoja alionesha kukasirikia kitendo ambacho kilikuwa kimefanyika juu ya utekaji ambao ulikuwa umefanywa, kila mmoja akaonekana kuukasirikia ulinzi wa polisi ambao walitakiwa kuuweka katika kila kona.
Katika kipindi hicho, hakikuwa kipindi cha kupeana lawama tena, tayari polisi pamoja na wapelelezi walikuwa wamekwishaingia katika kazi ya kutaka kujua ni mtu gani ambaye alikuwa amehusika na utekaji ambao ulikuwa umefanyika, utekaji ambao ulianza kuwa gumzo ndani ya jiji la Dar es Salaam huku taarifa ile ikizidi kusambaa kama upepo ndani ya nchi nzima ya Tanzania.
“Kwanza inabidi tujue vitu fulani juu ya mtekaji ambaye amemteka mtoto ila kama tukiingia kichwa kichwa, hatutofanikiwa hata kidogo” Mkuu wa kituo kikubwa cha polisi cha Osterbay jijini Dar es Salaam, Bwana Amri aliwaambia polisi wenzake.
“Unavyoona kipi kifanyike mkuu?” Polisi mmoja alimuuliza.
“Mahojiano ni kitu muhimu sana, kama tutafanya mahojiano na mzazi wa mtoto yule basi tunaweza kupata japo hatua ya kuanzia” Bwana Amri aliwaambia.
“Hakuna tatizo mkuu. Tutafanya kama ulivyoshauri:
Hakukuwa na kitu cha kupoteza katika kipindi hicho, kile ambacho kilikuwa kimeshauriwa na Bwana Amri ndicho ambacho kilitakiwa kufanyika kwa haraka sana. Polisi wawili waliokuwa katika kitengo cha upelelezi, Deogratius Mariga na Dickson Zemba wakaondoka mahali hapo mpaka Masaki, sehemu alipokuwa akiishi Bi Lucy pamoja na Rose.
Katika kipindi chote hicho, Rose alionekana kuwa na majonzi kupita kawaida, kitendo kilichokuwa kimetokea cha kutekwa kwa mtoto wake kilionekana kumuumiza kupita kawaida. Muda mwingi alionekana kuwa na mawazo, machozi hayakukoma kutiririka mashavuni mwake, alionekana kuumia, tabasamu zuri ambalo lilikuwa likiutengeneza uso wake mara kwa mara na kumfanya kuvutia katika kipindi hicho halikuonekana tena.
Vijana wale wakaanza kumwangalia Rose ambaye alikuwa amekaa katika kochi lililokuwa mbele yao huku pembeni yake akiwepo Bi Lucy ambaye alikuwa akitumia muda mwingi kumfariji japokuwa faraja zake hazikuweza kuleta mabadiliko yoyote yale, bado Rose alionekana kuwa na majonzi tele moyoni mwake.
“Koh koh koh” Mariga akakohoa kama ishara kwamba alikuwa akitaka kuongea kile ambacho kilikuwa kimewafanya kuwa mahali pale katika kipindi kile.
“Kuna mambo machache tunahitaji kufahamu kutoka kwako, mambo ambayo yatatufanya tufahamu ni wapi pa kuanzia, tunahitaji ushirikiano wako katika hili” Mariga alimwambia Rose ambaye bado alionekana kuwa katika hali ya majonzi. Akaitikia kwa kutikisa kichwa juu na chini.
“Unaweza kutuambia mzazi wa baba huyu ni nani?” Lilikuwa swali la kwanza ambalo lilitoka kwa Mariga, swali ambalo likamfanya Rose kukaa kimya kwa muda kama mtu aliyekuwa akifikiria jibu la kutoa.
Labels:
HABARI & UDAKU,
LOVE & STORY
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment