ILIPOISHIA JANA
Nilimaliza kuzungumza, ikawa zamu ya mganga kusema: “Nimekusikia mwanangu… kinachokusumbua ni mzimu wa huyo marehemu ambaye hakufurahishwa na kitendo kichafu ulichokifanya mahali alipolala. Hakuna tiba nyingine ila kwenda kuomba radhi katika kaburi lake.”
ENDELEA NAYO
Kwa kuwa lengo langu lilikuwa kupata tiba, nilikubaliana na maneno ya mganga, Alifurahi, akanitaka...
nilale ili kesho twende katika makaburi yale.
Asubuhi ilifika. niliamshwa na jogoo aliyewika kwa maringo, ‘kokorikoo.’ Msichana mdogo aliingia ndani ya chumba nilicholala bila kubisha hodi. Mkononi alishika kikombe cha uji, alinipatia nikaanza kuunywa taratibu. Uji wenyewe haukuwa na sukari, nilinusa mara tatu nikaachana nao.
“Haya kijana haraka twende!” alisema mganga. Nikatii maagizo yake!
Baada ya kusafiri kwa muda mfupi, hatimaye tulifika mjini Chisanza. Tulishuka karibu na eneo lijaalo vilevi na vimwana ufikapo usiku, ni katika eneo hili ndipo nililizua balaa la kufukuzwa na mtu wa ajabu.
Kwa kuwa ilikuwa asubuhi, tuliwaona walevi wakifunga sherehe ya mvinyo tayari kurudi nyumbani. Wengi walionekana kuwa na majuto baada ya kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa mambo ya hovyo.
Japo mganga alikuwa mzee, hatua zake zilikuwa kali kama kijana mdogo anayewahi michezoni. Alitembea bila kuchoka. Nilishangaa ukakamavu wake, kwani japokuwa alibeba kapu lililojaa manyanga na kila aina ya ulozi, hakutetereka, alichapa mwendo haraka.
“Kaburi lenyewe liko wapi?” mganga aliuliza mara baada ya kuwa tumeyafikia makaburi yale.
“Ngoja tulitafute… nakumbuka liliandikwaaaa….” nilijiumauma, sikukumbuka jina la kaburi lile na makaburi yalikuwa mengi.
Japo jina nililisahau, niliendelea kutafuta nikiamini kuwa nikiliona nitakumbuka. Tulizunguka kwa muda wa dakika tano, jicho langu likatua katika kaburi lililoandikwa, ‘KIMOTA S. SAMIKE’, nikamwambia mganga, “simama ni hapa.”
Mganga alisimama akashusha vifaa vyake vya kutendea kazi. Alitoa matunguli kutoka katika kikapu kikubwa alichobeba. Akasimama juu ya kaburi huku akisema maneno ambayo sikuyaelewa.
Wakati mganga akiendelea kufanya manyanga yake, yule mtu wa ajabu aliibuka ghafla hata sikujua alipotokea. Mkononi alishika upanga wake, na kama ilivyo siku zote, usoni palikuwa na kiza kinene!
Mganga alikimbia kama swala, niliona rubega yake ikipepea, nilikimbia kuelekea alikoelekea mganga, lakini kasi ya mganga ilikuwa kali na sikuweza kumpata, alikunja kona zake na mi’ nikakunja zangu. Mwisho kila mtu alimpoteza mwenzake, nikabaki nikikimbia peke yangu.
0 comments:
Post a Comment