Pages

Subscribe:

Wednesday, August 16, 2017

Story: SIKU SABA KUZIMU (Sehemu Ya Nane) 08


ILIPOISHIA:
“Please nakuomba tuonane usiku huuhuu, baba na mama wamesafiri tangu juzi, niko mwenyewe tu, nahisi haupo sawa na nahitaji kukusaidia, niambie nikukute wapi, nakuja na bodaboda sasa hivi,” alisema Raya, nikashusha pumzi ndefu.

SASA ENDELEA…
Nilishindwa nimjibu nini Raya, ni kweli nilikuwa kwenye matatizo makubwa na nilihitaji mtu wa kunisaidia lakini nilipomfikiria Raya, nilijikuta nikikosa...
majibu. Nilikumbuka jinsi msichana huyo alivyokuwa anajitoa kwa ajili yangu, akihitaji ukaribu wangu tu.

Watu wengi walikuwa wakihisi kwamba huenda tupo kwenye uhusiano wa kimapenzi lakini haikuwa hivyo, nilimchukulia kama rafiki wa kawaida tu ingawa hata yeye alikuwa akiwaambia marafiki zake kwamba mimi ndiyo mumewe mtarajiwa.

Mara kwa mara alikuwa akinilazimisha sana aje nyumbani kwangu lakini nikawa nampiga chenga sana na hata akija, nahakikisha sipo peke yangu, namuita rafiki yangu Justice au Prosper kisha tunajumuika wote. Japokuwa alikuwa akionesha waziwazi anavyonipenda, nilikuwa namchukulia kama rafiki tu na sikutaka kabisa uhusiano wetu uvuke zaidi ya hapo.

Hata hivyo, hakuwahi kuchoka, naye akawa ananialika mara kwa mara niende nyumbani kwao lakini sikuwa tayari kwa hilo. Nilijiwekea mipaka kati yetu na kamwe sikutaka tuivuke zaidi ya kuwa marafiki wa kawaida. Japokuwa nilikuwa najua kwamba namkera sana Raya kwa misimamo yangu lakini sikujali.

“Mbona hunijibu Jamal? Au hutaki nije?” swali hilo la Raya ndilo lililonizindua kutoka kwenye lindi zito la mawazo. Nilishasahau kwamba nazungumza na simu, nilizama kwenye mawazo ya kumfikiria Raya na kushindwa kuamua nini cha kufanya kwa wakati huo.

“Ok… ok… njoo hapa jirani na kituo cha polisi Mabatini, nakusubiri,” niliamua kukubali kwani sikuwa na ujanja mwingine, akakata simu. Mitaa yote ilikuwa kimya kabisa usiku ule, kelele pekee zilizokuwa zinasikika ni za vyura waliokuwa wakikoroma, wenyeji wa Kijitonyama watakuwa wananielewa vizuri kwani maeneo hayo hasa nyakati za mvua, huwa kunakuwa na vyura wengi wanaopiga sana kelele nyakati za usiku.

Nilisogea pembeni ya barabara na kusimama, nikawa namsubiri Raya ambaye hata dakika kumi hazikupita, akawasili akiwa kwenye bodaboda. Alishtuka sana kwa hali aliyonikuta nayo, mkononi nikiwa bado nimeshikilia mfuko wa chipsi nilizokuwa nimeenda kununua kwa ajili ya kula na Shenaiza.

“Jamal! What’s wrong with you?” (Jamal! Umepatwa na nini) alisema Raya huku akinisogelea, akionesha dhahiri alivyokuwa na shauku ya kutaka kujua kilichonitokea. Nilimjibu kwa kifupi kwamba ni stori ndefu na nipo kwenye matatizo makubwa.

“Twende tukaongelee nyumbani, it’s not safe out here in this dark hours (siyo salama hapa nje muda huu wa giza) alisema Raya huku akinipokea ule mfuko wa chipsi, akanitaka tupande ‘mshikaki’ kwenye bodaboda iliyomleta. Huo ulikuwa mtihani mwingine kwangu lakini sikujali sana.

Alitangulia yeye, akakaa kwa mtindo wa kujibinua, nilijua anafanya vile kwa lengo gani. Na Mimi nikapanda na kukaa nyuma yake, tukawa tumesogeleana sana kiasi cha miili yetu kugusana.

Hata hivyo, sikupatwa na hisia zozote kwani akili zangu hazikuwa hapo muda huo, nilikuwa nikiendelea kuwaza kuhusu hatima ya Shenaiza kule nyumbani kwangu. Dakika chache baadaye, tuliwasili nyumbani kwa akina Raya.

Kama alivyonieleza kwenye simu, kweli wazazi wake hawakuwepo, akanikaribisha mpaka sebuleni kwao, akafunga milango na mageti yote kisha akataka nimueleze kilichotokea. Tayari saa ya ukutani ilikuwa ikionesha kwamba ni saa saba za usiku.

Ilibidi nimueleze Raya ukweli wa kila kitu. Kwanza alinishangaa sana na kuniuliza nilipata wapi ujasiri wa kwenda kumtorosha hospitalini mtu ambaye ndiyo kwanza nimejuana naye siku hiyohiyo. Akazidi kunishangaa kwamba kwa nini sikumlazimisha msichana huyo anieleze ukweli wa kilichosababisha akajeruhiwa kiasi hicho na zaidi akaendelea kunilaumu kwa nini nimempeleka nyumbani kwangu, tena usiku ule.

“Mimi kila siku nikikwambia nije kukutembelea kwako unakuwa na visingizio lukuki, hata nikija hutaki tukae wawili tu lakini huyo umeweza kumuingiza kwako, tena usiku, kwa nini Jamal?” Raya alianza kulia kwa wivu.

“Naomba tuachane na hayo kwanza Raya, hebu tulimalize hili lililopo mbele yetu,” nilisema kwa upole kwani japokuwa alikuwa akisumbuliwa na wivu, kuna mambo ya msingi kabisa aliyoyaongea ambayo hata mimi nilipofikiria vizuri, niligundua kwamba nilikosa umakini katika kulishughulikia suala hilo.

Tukaanza kujadiliana nini cha kufanya ambapo aliniambia kwa sababu muda umeshaenda sana na nimeshatoa taarifa polisi, kwa usalama nilale hapohapo nyumbani kwao mpaka asubuhi ndiyo tutajua nini cha kufanya.

Sikuwa na cha kufanya, pamoja na ujanja wangu wote nikawa nimenasa kwenye tundu bovu, Raya akainuka na kuniandalia chakula kilichokuwa kimesalia, akaniambia zile chipsi nilizoenda kununua nizitupe kwani zinaweza hata kuwa zimewekwa sumu, nikakubaliana naye.

Ilibidi nijilazimishe tu kula kwani bado nilikuwa nikisumbuliwa sana na mawazo, nikala huku Raya akijitahidi kunichangamsha na kuniambia nichukulie kila kitu kilichotokea kuwa ni mipango ya Mungu.

“Huenda Mungu amesikia kilio changu cha siku nyingi cha kutaka uje kwetu,” alisema na kucheka mwenyewe, nikatabasamu kiaina kwani bado moyo wangu ulikuwa na hofu kubwa mno. Baada ya kumaliza kula, alinipeleka kuoga kisha kinarudi pale sebuleni.

“Si tunalala wote kitanda kimoja?” alisema Raya, kauli iliyonishtua sana kwa sababu niliona haiwezi kuwa tabia njema kwa mimi kulala naye kitanda kimoja wakati hakuwa mpenzi wangu, na pia tukiwa nyumbani kwao. Nikamkatalia katakata!
“Basi usijali, wewe utalala chumbani kwangu halafu mimi nitaenda kulala chumba cha wageni,” alisema akionesha kupoteza furaha. Nilimwambia yeye akalale chumbani kwake kama kawaida halafu mimi nikalale huko kwenye chumba cha wageni, akawa hataki, tukabishana kidogo lakini baadaye alikubali.

Akanipeleka mpaka kwenye chumba cha wageni huku mara kwa mara akinishika mwilini, niliamua kujikausha kwani nilijua endapo nitamchekea tu, usiku huo hautaisha salama, lazima tutaangukia dhambini.

Kwa jinsi nilivyokuwa nimechoka kwa pilikapilika za siku nzima, nilipoingia tu chumbani na Raya kutoka, nilivua nguo na kubaki na bukta tu, nikajilaza kitandani ambapo muda mfupi baadaye, nilipitiwa na usingizi mzito.

Nilipokuja kuzinduka, nilishtuka mno baada ya kugundua kuwa sikuwa nimelala peke yangu bali kuna mtu mwingine, tena wa jinsia ya kike, na kibaya zaidi, hata ile bukta yangu niliyolala nayo, ilishavuliwa. Nilikurupuka kwa kasi lakini yule mtu aliyelala pembeni yangu akanituliza na kuniambia nisiogope.

“Mungu wangu,” nilisema baada ya kugundua kuwa kumbe alikuwa ni Raya, tena naye akiwa mtupu kabisa, akaniambia kwamba alikuwa anaogopa kulala peke yake na ndiyo maana amekuja kulala na mimi.

Sikupata hata muda wa kujibu chochote, Raya akanikumbatia kwa nguvu mwilini na kuanza kunibusu sehemu mbalimbali za mwili wangu, japokuwa sikuwa tayari kwa alichokuwa anakitaka, nilijikuta kwenye wakati mgumu mno, kwani ukichanganya joto la mwili wake na uzuri aliokuwa nao, ukizingatia kwamba tulikuwa wawili tu, nilijikuta nikishindwa cha kuamua, ‘Jamal’ wangu naye akaanza usumbufu.

Itaendelea...

0 comments:

Post a Comment