Pages

Subscribe:

Monday, December 25, 2017

Story: MPAKA KIELEWEKE (Sehemu Ya Kwanza) 01

Image result for salem village
SEHEMU YA KWANZA
Nilikuwa nimeongozana na mke wangu tukitokea dukani eneo lile la ugenini. Nikiwa ‘busy’ kwenye simu yangu huku nikiongea na mke wangu ambaye alikuwa nyuma yangu akinisemesha hili na lile.

Mara nikagundua hali isiyo ya kawaida, mke wangu alikuwa kimya ghafla. Nikageuka haraka kutaka kujua nini kilimfanya awe kimya namna ile, lakini cha ajabu sikumuona mke wangu. “Khaaa...
!! kabaki wapi huyu mwanamke?” nilijikuta nikiuliza kwa sauti ilhali nilijua fika kuwa nilikuwa peke yangu eneo lile lenye kiza cha kutosha.

Uamuzi nilioufikia haraka ni kurudi nyuma kujaribu kumtafuta huku nikimpigia simu kwa maana nakumbuka alitoka nyumbani na simu yake. Kitu cha ajabu simu yake iliita nyuma yangu baada ya kuwa nimetembea hatua chache tu. Niligeuka nikaufuata muito ule wa simu ambao nilikuwa nikiujua kuwa ni wa simu ya mke wangu.

Kweli ilikuwa simu ya mke wangu ikiwa pale chini ikiendelea kuita.
Nilishikwa na bumbuwazi kwa sekunde chache nisijue hata cha kufanya, kisha nikaiokota ile simu na kuanza upya safari ya kurudi eneo lile la madukani kujaribu kuona kama naweza kumuona mke wangu.

Nilitembea huku nikiangaza huku na huko nikiamini pengine ningemuona mke wangu lakini mpaka nafika eneo lile la maduka sikuwa nimemuona.

Nikajaribu kuvuka eneo lile na kuangalia maeneo ya mbele zaidi ila sikumuona. Akili ikaniambia labda atakuwa amekwenda nyumbani, nikakimbia mpaka nyumbani ila mlango ulikuwa umefungwa kama ambavyo tuliuacha, mke wangu hakuwepo na funguo alikuwa nazo yeye. Sikuwa na sehemu nyingine ya kumuangalia kwa maana tulikuwa hata hatujazoeana na majirani.

Moja kwa moja nikaenda mpaka duka lile ambalo tulikuwa tumenunua bidhaa dakika chache zilizopita kwani ndilo duka pekee ambalo tulikuwa tukinunua kwa muda wote wa siku tatu tangu tuhamie mji ule. Hata muuzaji wa duka lile tulikuwa tumeanza kuzoeana hivyo sikuwa na mtu mwingine wa kumfuata wakati ule zaidi yake.
“Samahani Mangi” Nilianza kumsemesha mara baada ya mteja aliyekuwa akimuhudumia
kuondoka.

“Aisee mke wangu hajafika hapa?” niliuliza nikilingojea jibu kwa hamu huku nikitamani awe na chochote cha kusema ambacho kingesaidia kumpata mke wangu kwa maana hofu kubwa ilikuwa imeniingia tayari.

Mangi alionekana kunishangaa kidodgo kisha akauliza “Wewe si umeondoka hapa na mke wako hata dakika kumi hazijaisha?” kufika hapo nikachoka kabisa na kujikuta nikikaa kwenye benchi ambalo lilikuwa nnje pale dukani. Mwili wangu ulikuwa ukitetemeka kiasi ambacho kilimshangaza Mangi ambaye wakati huo alikuwa akijaribu kunisemesha lakini hata sikumbuki alikuwa anaongea nini kwa maana akili yangu hata haikuwa pale na wala sijui ilikuwa wapi.

Kugutuka nilimuona Mangi akiwa amesimama mbele yangu pamoja na watu wengine ambao walionekena kuwa wenyeji wa eneo lile wakitaka kujua nini kilikuwa kimetokea.

Usikose Sehemu ya Pili.

0 comments:

Post a Comment