Pages

Subscribe:

Saturday, December 30, 2017

STORY: MPAKA KIELEWEKE (Sehemu Ye Tatu) 03

Image result for salem village
Nilisogea mpaka zilipokua zile nguo nikazikagua na kugundua kweli zilikuwa nguo za mke wangu, tena zote mpaka za ndani. Niliogopa sana na kuanza kuhofia ambacho kilikuwa kimempata mke wangu kipenzi. 
Wakati naendelea kumulika nikaiona na funguo ambayo ndio chanzo hasa cha mimi kwenda eneo lile wakati ule, nikaiokota pamoja na nguo za mke wangu na kuanza...
safari ya kuelekea nyumbani.
Nilifika nyumbani nikafungua mlango na kuingia ndani kisha nikajilaza chali kitandani, nilikuwa nimechoka sana kuanzia mwili mpaka akili, nikachukua simu yangu na kupiga namba za baba yangu, niliamini ni mtu pekee ambaye angeweza kunifaa kwa wakati ule kama ambavyo amenifaa mara zote ninapohitaji msaada wake wa kimawazo…

Simu ile iliita kwa muda lakini haikupokelewa, nikaangalia saa na kugundua ilikuwa saa sita na robo usiku, bila shaka atakuwa usingizini na mara zote huiweka simu yake silent anapolala.
Niliachana na kupiga simu nikajaribu kulala lakini haukuwa usingizi wa maana, akili yote ilibaki macho ikijaribu kuvuta upya taswira ya tukio zima ambalo lilikuwa limetokea…
Nilijikuta nikiamini tukio lile lilikuwa likihusika na masuala ya kishirikina, mambo ambayo sikuwa na uzoefu nayo hata kidogo, niliishia kuyasikia tu kwa watu.
Hali ikawa hivyo usiku kucha, kila saa nikijaribu kuangalia saa yangu nikitamani kuche nianze hatua za kumtafuta mke wangu…
Saa ilionesha kuwa ilikuwa saa 11 na dakika 5 alfajiri, simu yangu ikiwa inaita, nilikurupuka haraka nikaichukua na kumuangalia mpigaji, alikuwa ni baba yangu, ambaye nadhani ndio alikuwa anaamka na kukuta “missed call” yangu ile ya usiku mnene. Nilipokea haraka haraka na kuanza kuongea na baba ambaye moja kwa moja alijua kuna tatizo kutokana na kumpigia muda ule ambao si muda wa kupeana salamu za kawaida.
Nilimuelezea baba kila kilichokuwa kimetokea naye akashangazwa sana na hali ile, alikaa kimya kwa muda, nadhani alikosa chochote cha kusema kisha akaongea.
“Jikaze mwanangu, kukicha nenda kwa huyo mzee ukaone kama atakuwa na msaada wowote, mimi nitaondoka na basi la kwanza hapa nadhani majira ya saa saba mchana tutakuwa pamoja” Tukaagana, akakata simu nami nikajiinua kutoka pale kitandani ambapo sikuweza kupata usingizi usiku kucha.
Nikaingia bafuni, nikajimwagia maji ili kuchangamsha mwili tayari kwa kwenda kwa mzee Miale, wakati nikiwa nakoga nikajiuliza kwanini sikuwa nimeripoti tukio lile katika kituo cha polisi, nikajiona nilikuwa mzembe hivyo nikaoga haraka haraka kisha nikatoka na kuvaa, safari ya kuelekea kituo cha polisi ikaanza kwa kutumia pikipiki yangu, wakati huo ilikuwa ni majira ya saa 12 za asubuhi nikaamini nitawahi kurudi na kwenda kwa Mzee miale kwa wakati.
Nilifika kituoni nikajitambulisha na kuelezea kilichotokea, askari walichukua maelezo yangu wakayaandika na kuniruhusu kuondoka, nilishangazwa kuona hawakulichukulia jambo lile kama jambo kubwa sana, sasa niliamini tukio langu halikuwa la kwanza katika jamii ile. Nikaondoka na kuelekea kwa mzee Miale.
Nilifika nikapokelewa na mzee ambaye umri wake ulionekana kuwa si chini ya miaka 70, ambaye nilimkuta amekaa peke yeke kwenye kiti cha kizee pale nje.
usikose sehemu ya nne

0 comments:

Post a Comment